MWANAMITINDO na muigizaji mahiri wa filamu nchini, Ummy Wenceslaud 'Dokii' amesema kauli yake ya kutaka kuwania ubunge siyo ya utani na kwamba ‘hajambeep’ yeyote bali amedhamiria kweli 2015 kuingia bungeni.
Akizungumza na MICHARAZO, Dokii alisema tofauti na wasanii wenzake ambao wamekuwa wakitangaza nia ya kujitosa kwenye siasa kisha kuishia njiani yeye hatanii na kwamba uchaguzi ujao atakuwa miongoni mwa wanawake watakaowania ubunge jimboni.
"Sitanii na wala ‘simbeep’ mtu, nimenuia kabisa kujitosa kwenye mbio za uchaguzi wa 2015, nautaka ubunge wa Kilosa na ninaamini ninaweza nikipewa nafasi na chama changu cha CCM," alisema Dokii.
Dokii ambaye pia ni muimbaji muziki, alitangaza nia yake hiyo wiki mbili zilizopita, lakini baadhi ya mashabiki wake wanadhani ni kauli kama zilizowahi kutolewa na wasanii mbalimbali akiwamo JB, King Majuto, Steve Nyerere, Shilole na wengine lakini wasioaminika kama watajitosa kwenye uchaguzi huo.
Katika bunge la sasa linaloelekea ukingoni wapo wasanii kadhaa walitwaa viti vya ubunge akiwamo mmoja wa waasisi wa Bongofleva nchini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' ambaye ni Mbunge wa Mbeya-Chadema, huku muimbaji Vick Kamata akiwa Mbunge-CCM Viti Maalum.
No comments:
Post a Comment