Awadh Juma (kushoto) akipambana katika NMJ-2 jana ambapo Simba ilishinda mabao 2-0, moja likifungwa naye |
Awadh Juma alivyokuwa akishughulika jana wakati wa pambano la NMJ-2 |
Awadh Juma alivyomtesha Kaseja katika NMJ-1 |
Awadh Juma akiwa na Jonas Mkude |
Maniche alisema lililomsisimua zaidi ni kitendo cha kumzidi ujanja kipa bora nchini na Afrika Mashariki, Juma Kaseja.
Kiungo mshambuliaji huyo alifunga bao la tatu lililo gumzo kwa sasa na lililomletea kizaazaa kipa Kaseja akisakamwa akidaiwa 'aliiuza' Yanga kwa klabu yake ya zamani.
wakati mashabiki wakiamini labda alibahatisha tu kwenye mchezo huo, Maniche kwa mara nyingine tena amedhihirisha kuwa ana bahati ya michuano hiyo ya Nani Mtani Jembe baada ya jana kufunga bao la kuongoza la Simba lililoisaidia kupata ushindi wa pili mfululizo dhidi ya Yanga.
Mchezaji huyo alifunga bao la kwanza katika dakika ya 31 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa kizembe na kipa Deogratius Munishi 'Dida' na yeye kuukwamisha kulia mwa lango ya Yanga lililokuwa likimdokolea macho.
Bao hilo lilitokana na mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa kiufundi na Mganda Emmanuel Okwi na kuchangia kummsha hamasa ya vijana wa Msimbazi walioandika bao la pili dakika chache kabla ya mapumziko kupitia kwa Elias Maguli aliyeuwahi mpira wake wa kichwa uliogonga besela na kurudi kwake.
Maniche aliyemtetea Kaseja baada ya kumtungua mwaka jana, alisema amefurahi sana kufunga tena kwenye michuano hiyo na kusaidia Simba kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Alisema kuwa kujiamini na kuwa katika kikosi bora chini ya kocha Patrick Phiri ndiyo siri ya ushindi wa timu yao na sababu ya yeye kuendeleza kuwaliza Yanga.
Mchezaji huyo anadai alichofanya katika mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe, ni sehemu tu ya ujuzi alionao katika soka na kuwaahidi wadau wa Simba kusubiri kupata mambo makubwa wakati ngwe Ligi Kuu Tanzania Bara itakapoendelea tena kuanzia Desemba 26.
Kiungo huyo aliyezaliwa miaka 22 visiwani Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya saba wa familia yao anasema angependa kufanya makubwa katika ligi ili aweze kupata nafasi ya kujitangaza katika soka la kimataifa kupitia Simba.
Nyota huyo wa zamani wa klabu za Jang'ombe, New National, Leba, Tanzania Soccer Academy (TSA) kabla ya kutua Mtibwa Sugar miaka mitatu iliyopita, anasema anatamani kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Maniche anayependa kula ndizi kwa nyama na juisi halisi ni shabiki mkubwa wa klabu za Barcelona na Manchester United.
Juu ya pambano analokumbuka kichwani mwake ni lile la Zanzibar Heroes dhidi ya Sudan katika michuano ya Chalenji ya mwaka 2009.
"Naikumbuka mechi hiyo kwa vile ilikuwa ya kwanza kwa michuano ya Kombe la Chalenji," anasema.
Mchezaji huyo anayetaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kurekebisha mfumo wa ligi na kuongeza mashindano mengi ili kuwapa nafasi wachezaji kukuza viwango vyao.
"Kuwepo kwa michuano mingi kama ile ya Super8 itawasaidia wachezaji, pia mfumo wa ligi ubadilishwe kwani unafanya wachezaji wawe mapumziko muda mrefu bila sababu," anasema.
Maniche aliyevutiwa na kiungo nyota wa zamani wa Tanzania, Shekhan Rashid, japo kwa sasa anamzimia kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, anasema kubadilishwa mfumo wa soka nchini ni 'muarobaini' wa mafanikio ya Taifa Stars.
Anasema Stars inaangushwa na mambo madogo ambayo yakirekebishwa huenda ikaifanya timu hiyo ikatamba kama mataifa mengine, huku akiwataka wachezaji wenzake kujituma na kuzingatia nidhamu na miiko ya soka.
Juu ya tukio la furaha Awadh anasema ni kitendo cha kusajiliwa na Simba na anahuzunishwa na tukio la ajabu lililowahi kumpata wakati akiwa uwanja wa Ndege kuelekea Thailand kucheza soka la kulipwa bada ya pasi yake ya kusafiria kushindwa kusoma kwenye mitando na kukwama kuondoka.
"Yaani ni kama miujiza, nilifaulu majaribio yangu ya soka la kulipwa Thailand, nikarejea kusubiri kutumiwa tiketi nikaanze kuitumikia, siku ikawadiwa tiketi ikaja sasa nikiwa uwanja wa ndege amini usiamini pasipoti yangu iligoma kusoma na kukwama safari," anasema.
"Mpaka leo nashindwa kujua ilitokana na nini, ila sijakata tamaa Mungu atanisaidia nitatimiza ndoto za kucheza soka la kulipwa," anaongeza.
Awadh Juma Issa, alianza kucheza soka la chandimu tangu akisoma Shule ya Msingi Jang'ombe na kuendelea wakati akiwa Sekondari ya Mtakuja aliposoma hadi kidato cha pili na kuhamia Makongo baada ya kumvutia Kanali Mstaafu Idd Kipingu kupitia michuano ya shule visiwani Zanzibar.
Kabla ya kuja Makongo alishaanza kung'ara katika soka kupitia Jang'ombe, New National na Leba Fc, na alipokuwa Makongo alichaguliwa TSA kabla ya Mtibwa kumchukua na hivi karibuni kutua Simba.
No comments:
Post a Comment