Azam Fc watakaokuwa ugenini nchini Sudan |
Yanga wao watakuwa vitani nchini Botswana |
Azam waliondoka jana kuelekea Sudan watakuwa na kibarua kizito mbele ya wenyeji wao El Merreikh waliowafumua kwenye uwanja wa Chamazi, mabao 2-0 wakati Yanga wenyewe waliondoka alfajiri ya leo wakiwa na morali mkubwa baada ya ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Maafande wa BDF XI ya Botswana watakaorudiana nao Jumamosi.
Yanga waliowaacha baadhi ya nyota wake akiwamo Mbrazil, Andrey Coutinho kutokana na kuwa majeruhi, imeenda Botswana wakiwa na amani kutokana na mwenendo mzuri wa timu yao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ikipata ushindi mfululizo na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi nne mbele zaidi ya watetezi Azam ambao mechi zao mbili za mwisho waliambulia sare tupu.
Uongozi wa Yanga kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Jerry Muro amesema Yanga inaenda ugenini ikiwa imepania kusonga mbele licha ya kutambua pambano lao litakuwa gumu kwa vile BDF watakuwa nyumbani na wana hasira ya kufungwa mabao 2-0.
Muro alisema vijana wake wote 20 waliopo kwenye msafara wao wameapa kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ugenini ili kusonga mbele ya kuvaana ama na Sofapaka ya Kenya au Platnum ya Zimbabwe ambao walishinda mabao 2-1 katika mchezo baina yao wiki mbili zilizopita mjini Nairobi.
Upande wa Azam kupitia Meneja wake, Jemedari Said, alisema kuwa wanaenda Sudan wakiwa na nia ya kukamilisha malengo yao ya kufuzu raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jemedari, nyota wa zamani wa Majimaji-Songea na klabu nyingine alisema kuwa Azam wanaenda Sudan wakitambua kuwa watakabaliwa na mechi ngumu kwa vile El Merreikh siyo timu ya kubezwa hata kama waliwafunga mabao 2-0 katika mechi ya kwanza nyumbani.
Meneja huyo aliongeza kuwa Azam inayoiwakilisha Tanzania kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka miwili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho, imepania kufika mbali kwenye michuano hiyo ili kufuta dhana kwamba timu za Tanzania ni wasindikizaji tu katika michuano ya kimataifa.
Mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, watashuka dimbani keshokutwa, watahitaji sare ya aina yoyote ili kujihakikisha kusonga mbele na kukutana na ama timu ya Lydia Ludic B.A ya Burundi au Kabuscorp do Palanca ya Angola ambazo zilishindwa kufunga katika mechi mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyochezwa nchini Burundi.
Wawakilishi wengi wa Tanzania visiwani, KMKM waliofungwa mabao 2-0 na Al Hilal na POlisi Zanzibar walifumuliwa mabao 5-0 na Maunama ya Gabon watashuka dimbani mwishoni mwa wiki kukamilisha ratiba ya mechi zao za michuano hiyo ya kimataifa ya Afrika.
Mabingwa wa Zanzibar, KMKM watahitajika kuwafunga wa Sudan mabao 3-0 ili kufuzu, huku Polisi wakihitajika kushinda mabao 6-0 kitu kinachoonekana kuwa ndoto ikizingatiwa wawakilishi wa Zanzibar hawajawahi kuvuka raundi ya awali tangu nchi hiyo ilipotambuliwa rasmi na Shirikisho ya Soka Afrika (CAF) mnamo Desemba mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment