STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 25, 2015

Mwili wa Christopher Alex hatimaye wapumzishwa Dodoma

IMG-20150224-WA0007
Makazi ya milele ya Christopher Alex
Na Rahma Junior, Dodoma
MWILI wa kiungo nyota wa zamani wa timu ya Simba, Christopher Alex, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma, umezikwa jana kwenye makaburi ya Nkuhungu.
Mwili wa Alex ulifanyiwa ibada ya maziko nyumbani kwa mama yake Massawe, Martha Matonya chini ya  Mchungaji wa Kanisa la Anglikan, Parishi ya Chamwino, Mch. David Matonya na ilihudhuriwa wa mamia ya waombelezaji, wakiwamo waliokuwa wachezaji wenzake kwa nyakati tofauti.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kumsindikiza marehemu Alex ni Ulimboka Mwakingwe, Boniface Pawasa, Kelvin Mhagama, Amani Mbarouk, Juma Kaseja na Juma Ikaba aliyecheza naye kwenye timu ya CDA-Dodoma, ambaye sasa ni kocha wa timu hiyo.
Klabu ya Simba iliwakilishwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa timu hiyo, Ally Sulu, ambaye pia alizungumzia malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya waombolezaji kwamba klabu zimekuwa na kawaida ya kuwatelekeza wachezaji pindi wanapokuwa wamemaliza kuzitumikia.
Naye Pawasa, alisema siyo tu klabu vya mpira wa miguu bali Watanzania wengi wanafurahia mtu akiwa mchezaji, anapomaliza muda wa kucheza na ikatokea ameugua au kupatwa majanga, wanamtelekeza.
“Wasanii wengine mathalani wa filamu wanashuhudiwa wakisaidiwa hata wanapokuwa kwenye matatizo ya kujitakia. (Tulipaswa kumjali) Alex alifunga penalti ya mwisho katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya timu ngumu ya Zamalek ya Misri mwaka 2003,” alisema Pawasa.
Marehemu Christopher Alex atakumbukwa kwa kufunga penati ya mwisho iliyowavua ubingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika Zamalek mwaka 2003 na kuvunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Yanga katika michuano hiyo tangu 1998 walipotinga hatua ya makundi kwa timu za Tanzania.
Simba ilishinda nyumbani bao 1-0 kabla ya kufungwa idadi kama hiyo katika mechi ya marudiano nchini Misri na kufikia hatua ya kupigiana penati na Sinmba kufuzu.

No comments:

Post a Comment