STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 6, 2017

Mahrez ndiye Baba lao Afrika, Onyango amrithi Samatta


Mahrez akiwa na tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Afrika 2016
Akiwa kazini Leicester
Kipa Dennis Onyango wa Uganda aliyemrithi Samatta
RIYAD Mahrez amembwaga straika wa kimataifa wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang katika kinyang'anyiro cha Tuzo za Mchezaji Bora wa Afrika 2016 baada ya Mualgeria huyo kunyakua tuzo hiyo kwa mara ya kwanza.
Tuzo hizo za Wanasoka waliofanya vema kwa mwaka 2016 zilifanyika usiku wa kuamkia leo mjini Abuja, Nigeria na kusindikizwa na burudani toka kwa wasanii mbalimbali akiwamo Diamond Platinumz na Rayvan.
Mahrez anayekipiga Leicester City ametwaa tuzo hiyo kwa kupigiwa kura 361 akimzidi Aubameyang aliyekuwa akitetea tuzo hiyo aliyevuna pointi 313 na Sadio Mane wa Senegal akiambulia nafasi ya tatu na pointi 186.
Hiyo ni tuzo ya pili Afrika kwa Mahrez kwani hivi karibuni alitwaa tuzo ya Mwanasoka wa Afrika wa BBC 2016.
Mahrez na tuzo yake ya BBC

Kwa upande wa Mchezaji Bora wa Afrika Wanaocheza barani humu, nafasi hiyo ilitwaliwa na kipa Dennis Onyango aliyewafunika washindani wake, Khama Brilliat anayecheza naye Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Rainford Kalaba wa TP Mazembe.
Mganda huyo ametwaa tuzo hiyo akimpokea Mtanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta aliyeitwaa mwaka jana nchini humo akiwa na klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.
Uganda iliendelea kutisha baada ya timu yao ya taifa, The Cranes kushinda tuzo ya Timu Bora ya Taifa, huku Mamelodi Sunsdowns ikiwa Klabu Bora ya Mwaka ya Afrika na Kocha wa klabu hiyo Pitso Mosimane akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka.
Tuzo nyingine zimeenda kwa Kelechi Iheanacho kama Mchezaji Mwenye Kipaji na Alex Iwobi anayeichezea Arsenal akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Afrika, wote hao wanatokea Nigeria, huku Mwanasoka Bora wa Kike nafasi ikienda kwa Asisat Ashoala kutoka Nigeria.
Tuzo ya Gwiji wa Afrika ilienda kwa wakali wawili wa zamani wa Laurent Pokou wa Ivory Coast na Emilienne Mbango wa Cameroon, huku timu ya wanawake ya Nigeria ikishinda kuwa Timu Bora ya Soka la Wanawake.
Mwamuzi Bakary Gassama wa Gambia alipiga 'hat trick' ya kuwa Mwamuzi Bora wa Afrika kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo pia mwaka 2014 na 2015 kabla ya jana usiku mjini Abuja, Nigeria kutwaa tuzo hiyo tena naye  Rais wa Shirikisho la Soka la Guinea Bissau, Manuel Lopes Nascimento alitwaa tuzo ya Kiongozi Bora wa Soka wa barani Afrika.

Orodha ya Washindi wa Tuzo za CAF 2016

Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka
Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)

Mchezaji Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika
Dennis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)

Mchezaji Bora wa Kike wa Mwaka
Asisat Oshoala (Nigeria & Arsenal)

Chipukizi Mwenye Kipaji cha Aina Yake
Kelechi Iheanacho (Nigeria & Manchester City)

Chipukizi Bora wa Mwaka
Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)

Kocha Bora wa Mwaka
Pitso Mosimane (Mamelodi Sundowns)

Klabu Bora ya Mwaka
Mamelodi Sundowns

Timu Bora ya Taifa ya Mwaka
Uganda The Cranes

Timu Bora ya Taifa ya Wanawake
Nigeria

Mwamuzi Bora wa Mwaka:
Bakary Papa Gassama

No comments:

Post a Comment