Simon Msuva |
Hekaheka wakati wa pambano la Simba na Yanga Oktoba 1, 2016 lililoisha kwa sare ya 1-1. |
Tena aliyeiopiga bao ni kijana mmoja mfupi hivi, ambaye amekuwa akipata wakati mgumu mbele ya mashabiki wa Jangwani kila Yanga inapocheza jijini Dar es Salaam. Mashabiki wasio na ustaarabu wala kuheshimu mchango wa nyota wao, Simon Msuva wamekuwa wakimtusi na kumtolea kejeli winga huyo, lakini ukirejea kwa kile anachjokifanya uwanjani utajua Msuva ni nani!
Winga huyo anayeongoza orodha ya ufungaji bora katika Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa sambamba na Amissi Tambwe anayecheza naye pale Jangwani na Shiza Kichuya wa Wekundu wa Msimbazi ni balaa.
Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Msuva ameifanyia mbaya Simba hata kama ya kukutana nao baada ya kufunga mabao manne ambayo ni moja zaidi ya iliyonao wapinzani wao hao kutoka Mtaa wa Msimbazi.
Katika mechi mbili tu za Kombe la Mapinduzi, Msuva amefunga mabao hayo, huku kikosi kizima cha Simba kikiwa kimecheza mechi tatu mpaka sasa, lakini kikiwa na mabao matatu tu, yaliyofungwa na Mzamiru Yassin mawili na Juma 'Ndanda' Liuzio.
Kwa lugha nyepesi unaweza kusema kuwa Msuva ameibwaga Simba kwa mabao 4-3 hata kabla timu yake na Wekundu wa Msimbazi hazijashuka uwanjani wikiendi hii kusaka tiketi ya kukutana ama kukwepana pale Unguja.
Msuva alianza kwa kufunga mabao mawili walipoikamua Jamhuri ya Pemba kwa mabao 6-0, kabla ya kuongeza mengine walipoizamisha Zimamoto na kama sio kukosa umakini katika mechi hiyo ya pili jamaa angetupia hat trick kwani alipata nafasi ya kupiga penalti, lakini akashindwa kukwamisha kimiani.
Bila ya shaka mashabiki wa Simba kokote walipo kwa sasa watakuwa wanajiuliza itakuwa vipi kama chama lao litakutana na Yanga katika michuano hiyo kwa mziki mnene iliyonayo wapinzani wao hao.
Katika mechi yao ya pili, Yanga iliwakosa washambuliaji wake wote wa kati baada ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe kutocheza kabisa, lakini katika mechi yao ya kesho dhidi ya Azam huenda majembe hayo yakawepo.
Simba kwa upande wao makali yake kwa sasa yanabebwa na viungo wake wajanja, Mzamiru, Mohammed Ibrahim na Pastory Athanas, huku wakipigwa tafu na Liuzio ambaye katika mechi ya tatu ya Simba dhidi URA Uganda alianza sambamba na Laudit Mavugo ambaye amekuwa na hali mbaya klabuni.
Je, Msuva ataendelea kuikimbiza Simba ama Simba itatafuta upenyo wa kuukacha mziki wa Jangwani na kusubiri kujua majaliwa yao kwenye fainali ya michuano hiyo Januari 13? Tusubiri tuone.
No comments:
Post a Comment