STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 15, 2017

Carzola majanga matupu Arsenal, nje wiki 10 zaidi

MAJANGA. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anahofu kiungo wake nyota Santi Cazorla anaweza kukaa nje ya uwanja kwa wiki 10 zaidi kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu yanayomsumbua.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amekuwa nje ya uwanja toka Oktoba baada ya kucheza mechi 11 katika mashindano yote msimu huu. Lakini Cazorla mwenye umri wa miaka 32 sasa anategemewa kuendelea kukaa nje zaidi kutokana na majeruhi kupona taratibu kuliko ilivyotegemewa awali.
Wenger alisema Cazorla bado hajaanza hata kukimbia hivyo hadhani kama atarejea uwanjani hivi karibuni.

Imeelezwa huenda Wenger akafanya mpango wa kusajili mbadala wake.
Klabu hiyo jana Jumamosi ilivaana na Swansea City na kupata ushindi wa mabao 4-0 ugenini katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

PSG yaingia vita ya kumnasa Depay wa Man United

Memphis Depay
PSG nayo imoooo! Klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, imedaiwa nayo kuingia kwenye mbio za kumwania winga wa Manchester United, Mholanzi Memphis Depay.
Meneja wa United Jose Mourinho tayari ameshamwambia winga huyo kutafuta timu nyingine, huku Everton na Olympique Lyon zote zikitajwa kumtaka.
PSG walikaribia kumsajili Depay kabla hajakwenda Old Trafford kwa kitita cha Pauni milioni 25 mwaka 2015, lakini sasa wanaonekana kumhitaji tena mchezaji huyo ambaye hajacheza katika kikosi cha United toka Novemba mwaka jana. United inataka kitita cha Paundi milioni 15 kwa Depay baada ya kukataa ofa ya Paundi milioni 10 iliyotolewa na Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Breaking News: Mwili wa Amina kuletwa, kuagwa Dar kesho

Na Mwandishi Wetu

HABARI zilizotufikia muda huu, zinasema kuwa mwili wa Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Uhuru Wikiendi, Burudani na Mzalendo, Amina Athuman unatarajiwa kurejeshwa Dar es Salaam kesho asubuhi kwa boti kutoka Zanzibar. Msemaji wa Familia ya Marehemu, Athumani Kazukamwe, amesema jioni hii kuwa, mwili wa Amina utasafirishwa kutoka Zanzibar saa moja asubuhi kwa boti na unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kati ya saa tatu na saa nne asubuhi.
Kazukamwe, ambaye ni baba mkubwa wa mume wa marehemu, amesema mazishi ya Amina yamepangwa kufanyika keshokutwa Jumanne katika makaburi ya Soni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Amesema awali, upande wa mume wa marehemu ulitaka mazishi hayo yafanyike kesho Dar es Salaam, lakini baada ya majadiliano na familia ya marehemu, waliafikiana mazishi yakafanyika Tanga.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia ya marehemu, taratibu za kuuaga mwili wa Amina zitafanyika papo hapo bandarini na mara baada ya kumalizika, utasafirishwa kwa basi maalumu la kukodi kupelekwa Tanga.
Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL, Ramadhani Mkoma, amethibitisha mazishi ya marehemu Amina kufanyika Tanga.
Ramadhani amesema amepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu hakutarajia iwapo Amina angetangulia kuondoka duniani katika umri mdogo.
Amesema Amina ameacha pengo kubwa kwa sababu alikuwa mmoja wa wanahabari wa UPL waliokuwa wakifanyakazi kwa kujituma, aliipenda kazi yake na ilikuwa mwiko kwake kusukumwa kutimiza wajibu wake.
Amesema kazi aliyoifanya wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo alitumwa kuandika habari zake, ni uthibitisha wa wazi wa utendaji mzuri aliokuwa nao.
Amesema hawana la kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu kwa kuwa kila alipangalo, hakuna anayeweza kulipangua. Amewataka wafanyakazi wa UPL kumuenzi Amina kwa kuiga utendaji wake wa kazi.

Mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu ang'ara India Marathon

Simbu (wa pili kushoto) akipozi na washindani wake baada ya kutwaa nafasi ya kwanza wa Mbio za kimataifa za India Marathon 2017
Na Lasteck Alfred
MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, ameibuka mshindi kwenye mbio ndefu za Mumbai Marathon  2017, akifanikiwa kumpiku Mkenya Joshua Kipkorir na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.
Mashindano hayo yajulikanayo kama Standard Chartered Mumbai Marathon huwa yanafanyika kila Jumapili ya tatu ya Januari katika jiji la Mumbai, India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kwa idadi ya washiriki.
Simbu, aliyedhaminiwa na kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika 2:09:28 muda ambao ni mzuri sana kwa mbio za aina hiyo.
Akizungumzia ushindi wake, Simbu alisema ushindi huo umesababishwa na maandalizi mazuri aliyoyafanya.
Alisema anauchukulia ushindi huo kama changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu. Amesisitiza kuwa ushindi huo sio wake pekee yake au Multichoice ambao ndio wathamini wake, bali ni ushindi wa Taifa zima.
Kwa upande wa Serikali,  Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: "Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania."
Kwa upande wake Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema Multichoice imefurahishwa sana na matokeo hayo na kwamba wataendela kumdhamini Simbu kwa mujibu wa makubaliano yao, ili kuhakikisha anaendelea kufanya vyema na kuliletea taifa sifa kubwa.
“Tulichukua jukumu la kumdhamini simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.
Alisema Mshana na kuongeza “Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”
Katika mbio hizo, waigizaji maarufu wa Bollywood John Abraham and Neha Dhupia walikuwepo kuleta amsha amsha kwa washiriki. Alphonce anatarajiwa kurejea nyumbani leo Jumatatu.

Beki Mholanzi akichonganisha Chelsea na Man United

Beki Stefan De Vrij
LAZIMA kieleweke. Klabu za Chelsea na Manchester United zimedaiwa kuingia vitani kwa ajili ya kusaka saini ya beki wa Lazio, Stefan De Vrij.
Duru za kisoka zinasema kuwa, Chelsea imejipanga kupambana na Man United katika kipindi cha kiangazi kwa ajili ya kumwania beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na Mashetani Wekundu.
Chelsea inadaiwa nao wako tayari kuingia katika kinyang’anyiro hicho, huku klabu yake ya Lazia imeondoa uwezekano wa kumuuza beki huyo katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Hatua hiyo imetoa mwanya kwa klabu hiyo kuweka kitita cha Euro milioni 40 kwa timu itakayomhitaji majira ya kiangazi, ambapo klabu yoyote kati ya Man United ama Chelsea wakituliza kichwa inaweza kueleweka kwao kwa beki huyo.

Simanzi! Mwandishi Amina Athuman hatunaye, Malinzi amlilia

Amina Athuman enzi za uhai wake
Na Alfred Lucas
SIMANZI. Mwandishi wa habari wa michezo wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Amina Athuman amefariki dunia asubuhi ya leo Jumapili na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi.
Malinzi ametuma salamu hizo kwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kutokana na kifo hicho cha Amina, aliyekuwa visiwani Zanzibar kuripoti michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika juzi Ijumaa.
Katika salamu hizo ambazo pia zimeenda kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto; Rais Malinzi ameelezea kushtushwa kwake kwa taarifa za kifo cha ghafla cha Amina.
“Niseme tu wazi kuwa tangu kuanza kwa michuano ya Mapinduzi, nimekuwa nikifuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanahabari. Huwa pia sikosi magazeti ya Uhuru na Mzalendo na kuona byline (jina la mwandishi) ya Amina. Mpaka matokeo ya fainali zilizofanyika Januari 13, mwaka huu.
“Sasa asubuhi hii nimepata taarifa za kifo chake, ama kwa hakika zinasikitisha. Ni kifo cha ghafla, ninavyomfahamu binti huyo ni mchapakazi hodari na mfano uko wazi kwani katika hali ya ujauzito alikuwa hakosi kufuatilia habari,” amesema Rais Malinzi.
Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia ya marehemu Amina, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
“Binafsi naona ni kama askari aliyefia vitani. Naweza kumwita ni shujaa, lakini ndivyo hivyo tena, huwezi kupingana na mipango ya Mungu, nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, naomba wenzangu pia muwe na subira wakati huu mgumu ambao tasnia na Kampuni ya Uhuru Publications imepoteza mwanahabari mahiri.
Taarifa zinasema Amina alifariki dunia leo Jumapili Januari 15, 2017 akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazimmoja, iliyoko Zanzibar mara baada ya kujifungua jana kwa mtoto ambaye pia alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo pamoja na gazeti la Burudani linalochapisha mahsusi habari za michezo na sanaa kabla ya hapo aliwahi pia kufanya kazi kampuni na Business Times Limited. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Amina Athuman Mahala Pema Peponi. Inna Lillah wa Innaa Ilaihi Rajaajiuun.

Friday, January 13, 2017

Msuva, Manula, Mwanjali noma sana Ma[pinduzi 2017


Add caption
Na Rahma White
SIMON Msuva amefanikiwa kunyakua tena tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya mabao yake manne aliyofunga kwenye mechi mbili za awali za Yanga kushindwa kufikiwa na mchezaji yeyote.
Mwaka 2014 winga huyo alinyakua pia tuzo hiyo kwa idadi kama hiyo wakati Yanga ikiwa imeaga mashindano hatua ya robo fainali kwa kuchapwa bao 1-0 na JKU.
Kipa Aishi Manula wa Azam ambaye hakuruhusu wavu wake kuguswa hata mara moja kama alivyofanya kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2015, alitangazwa kuwa Kipa Bora wa michuano ya mwaka huu ya Mapinduzi, huku beki wa Simba, Method Mwanjali akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mashindano na Said Mohammed wa Taifa akitangazwa Mchezaji Bora Chipukizi.
Mwamuzi Mfaume Ali alitwaa tuzo ya Mwamuzi Bora na kila mmoja kati ya walionyakua tuzo hizo alitwaa kitiota cha Sh 1 milioni moja.
Tuzo hizo na zawadi kwa washindi wote wa michuano ya msimu huu wa 11 ya Kombe la Mapinduzi walikabidhiwa zawadi zao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein aliyekuwa mgeni rasmi.
Azam ndio mabingwa wapya wa michuano hiyo iliyoanza Desemba 30 mwaka jana kwa kuilaza Simba kwa bao 1-0.

AZAM NDIO MABINGWA WAPYA WA KOMBE LA MAPINDUZI 2017

PAMBANO la fainali ya Kombe la Mapinduzi 2017 limeisha kwa Azam kutwaa taji kwa mara ya tatu bila kupoteza pambano lolote wala kufungwa bao hata moja baada ya usiku huu kuichapa Simba kwa bao 1-0.
Bao pekee la Azam liliwekwa kimiani dakika ya 13 na Himid Mao 'Ninja' na kuifanya Azam kuweka rekodi ya aina yake katika michuano hiyo ikifanikiwa kuzilaza Simba na Yanga kwa hatua tofauti na kubwa kutoruhusu bao lolote katika michuano hii ya 11 iliyochezwa Uwanja wa Amaan.
Azam ilionekana tangu mapema kuibana Simba ambayo ilicharuka dakika za mwishoni mwa washambuliaji wake Juma Liuzio, Pastory Athanas na Laudit Mavugo wakikosa mabao ya wazi.

Zimeongezwa dakika nne

ZIMEONGEZWA dakika nne kabla ya pambano la fainali tya Kombe la Mapinduzi 2017 kati ya Simba na Azam kumalizika na Azam inaelekea kuweka rekodi ya kutwaa taji lao la tatu katika fainali tatu ilizowahi kucheza katika michuano hiyo.
Kama itatwaa itakuwa inalingana na Simba ambayo ilikuwa imetwaa mataji matatu katika fainali zao tano za mwanzo kabla ya leo inayoelekea mwishoni. Azam 1 Simba 0.

Mudathir Yahya kabadili mchezo

KUINGIA kwa Mudathir Yahya kwa upande wa Azam kumefanya timu hiyo kubadilika kabisa, tofauti na kipindi cha pili kilipoanza ambapo Simba walitawala kwa sehemu kubwa ya mchezo na kuonekana kama itasawazisha bao. Bao bado 1-0 Azam ikiwa mbele.

Dakika ya 75 bado 1-0 Azam ikiongoza

DAKIKA ni ya 75 matokeo bao ni 1-0, Azam ikiongoza na timu zimefanya mabadiliko, Joseph Mahundi katoka kumpisha Frank Domayo, Mudathjiri Yahya kampokea Yahya Mohammed, huku Simba ikimtoa Mzamiru Yahya na kumuingiza Pastory Athanas. 

Pambano limeanza tena kule Amaan

PAMBANO la Simba na Azam, limeanza tena kwa ngwe ya dakika 45 za mwisho, matokeo yakiwa bado ni bao 1-0, azam wakiwa mbele.

Kocha Antonio Conte atwaa tuzo nyingine England

Kocha Conte

Zlatan na tuzo yake
KOCHA wa Chelsea, Mtaliano Antonio Conte ametwaa tuzo kwa mara nyingine ya kuwa Kocha Bora katika Ligi Kuu ya England kwa mwezi Desemba.
Hiyo ni tuzo ya tatu mfululizo ambayo Kocha hjuyo ameitwaa ikiwa ni rekodi katika ligi hiyo. Conte alipewa tuzo hiyo leo ikiwa ni mara ya tatu baada ya Oktoba na Novemba pia kuibeba.
Wakati huo huo, straika wa Man United, Zlatan Ibrahimovic amenyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi huo wa Desemba mwaka jana.

Farid Mussa apata leseni, ila apelekwa timu B Hispania

Na Mahmoud Zubeiry
HATIMAYE winga chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Farid Malik Mussa amepewa leseni ya Mamlaka ya Shirikisho la Soka Hispania (RFEF) aanze kuchezea nchini humo na klabu yake, Deportivo Tenerife imempangia kuanza kuchezea kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo kwa simu kutoka Tenerife, Farid amesema kwamba amepangiwa kuanza kuchezea kikosi cha U23 ili kupata uzoefu kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza kinachocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini humo, maarufu kama Segunda.

Farid Mussa na mmoja ya wachezaji wenzake wa timu yake mpya
“Nimepatiwa leseni na tayari nimepelekewa Tenerife B ili nikapate uzoefu kwanza na Jumamosi (leo) natarajia kucheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya timu inaitwa Vera,”alisema Farid.
Farid amejiunga na klabu hiyo ya Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, visiwa vya Canary Desemba kwa mkopo wa muda mrefu wa msimu kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.
Azam FC imemtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum baada ya winga huyo kufuzu majaribio katika klabu hiyo Aprili mwaka jana alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
Na ilimchukua wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo.
Bin Zubeiry

Sasa ni mapumziko Azam 1, Simba 0

Kotei akithibitiwa na mabeki wa Azam wakiongozwa na Gadiel Michael (2)
Mashabiki wa Azam
DAKIKA 45 za kwanza za fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ni mapumziko wakati Azam ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Simba. Kwa wastani pambano lilikuwa fifte fifte, licha ya Azam kukosa bao la pili baada ya kichwa cha Bocco kushindwa kuingia kimiani dakika moja kabla ya mapumziko.

Kazimoto katoka, Mavugo achukua nafasi yake

DAKIKA tatu kabla ya mapumziko, Simba inamtoa Mwinyi Kazimoto na kumuingiza Laudit Mavugo. Kazimoto kajitonesha enka yake ya mguu na benchi la Msimbazi limeamua kumtoa.
Azam wakikosa bao muda mfupi uliopita. Sure Boy akishirikiana na John Bocco. Azam 1 Simba 0.

Dak 33, Azam bado ipo mbele kwa bao 1-0

SIMBA wanafanya kosa kosa nyingi langoni mwa Azam, ikiwa dakika ya 33 sasa matokeo yakiwa bado 1-0 Azam ikiongoza.

Dakika 21, Azam 1 Simba O

PAMBANO bado kali kwelikweli kila timu ikishambulia, ikiwa dakika ya 21 sasa mabao bado 1-0. Azam ikiongoza.

Himid Mao anaiandikia Azam bao tamu la

HIMID Mao 'Ninja' anaiandikia Azam bao dakika ya 13 kwa shuti kali la Dar mpaka Moro, lililomuacha Kipa Agyei ashindwe kuokoa.
Azam 1 Simba 0

Pambano la Simba na Azam limeanza

PAMBANO la fainali za Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Azam limeanza kama dakika 10 zilizopita na Wekundu wa Msimbazi wanafanya mashambulizi makali langoni mwa Azam.
Kichuya ameonekana msumbufu kwa mabeki wa Azam, lakini bado Simba wamekosa plan ya kupata bao mapema.
Azam wameonekana kuimarika na wamejaribu kama mara mbili kumpima Daniel Agyei, lakini milango imekuwa migumu. Micharazo itaendelea kukuwaletea dondoo za mchezo huu.

Azam yaivaa Simba kuitemi, Himid Mao ndani, Domayo anasubiri

Kikosi cha Azam, hapo Domayo tu ndio yupo nje kumpisha Himis Mao 'Ninja'
Na Rahma White
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Azam imemjumuisha kikosi Himid Mao 'Ninja', wakati wakijiandaa kuvaana na Simba muda mchache kwenye pambano la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 litakalochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Sehemu kubwa ya kikosi hicho ni kile kile kilichoizamisha Yanga na Taifa Jang'ombe kwenye nusu fainali kwani golini atasimama Aishi Manula, akisaidiwa na Shomari Kapombe na Gadiel Michael, huku kati wakiwamo Aggrey Morris na Yakubu Mohammed, wakati kati kuna majembe kama Himid Mao na Shephan Kingue, huku pemeni wakicheza Salum Abubakar 'Sure Boy' na Joseph Mahundi wakati safu ya ushambuliaji itaongozwa na Nahodha, John Bocco 'Adebayopr' akisaidiana na Yahya Mohammed.

Akiba: Mwadini Ali, David Mwantika, Frank Domayo, Mudathir Yahya, Enock Atta-Agyei, Samuel Afful na Shaaban Idd.

Majembe ya Simba yatakayoivaa Azam usiku huu, Kazimoto ndani

Na Rahma Junior
KOCHA wa Simba amekitoa hadharani kikosi chake kitakachoivaa Azam muda mchache kwenye pambano la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 litakalochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Sehemu kubwa ya kikosi hicho ni kile kile kilichoizamisha Yanga kwenye nusu fainali kwani golini yupo, Mghana Daniel Agyei kama kawa akilindwa na mabeki wa pembeni Janvier Bokungu na Mohammed Hussein 'Tshabalala' huku kati wakiwamo Abdi Banda na Method Mwanjali.
Jonas Mkude, Muzamir Yassin na James Kotei wakisimama kati, huku mshambuliaji akiwa Juma Liuzio 'Ndanda' na mawinga wakiwa ni Shiza Kichuya na Mkongwe, Mwinyi Kazimoto.


Akiba: Manyika Peter, Hamad Juma, Novaty Lufunga, Said Ndemla, Jamal MNyate, Pastory Athanas na Laudit Mavugo.

Kocha Lyon anamtaka Depay hata leo hii

Depay
KOCHA wa klabu ya Olympique Lyon, Bruno Genesio amefichua kuwa straika wa Man United, Memphis Depay ni moja ya vipaumbele vyake katika usajili wa Januari.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi inaelezwa kuwa, huenda akaondoka klabu hapo mwezi juu kwenda katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ingawa inadaiwa kikwazo ni dau la Pauni 13 milioni lililotajwa kutaka kulipwa na Lyon.
Mabosi wa Mashetani Wekundu wanataka kumuuza mchezaji huyo kwa Pauni milioni 15.
Hata hivyo, Kocha Genesio amefichua juu ya kumhitaji mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kwa kusema; "Depay ni kipaumbele changu."
"Ni mchezaji aliyekamilika kwa kila kitu na atatufaa kuziba nafasui ya (Rachid) Ghezzal, iwapo mchezaji huyo ataamua kuondoka Lyon," aliongeza Genesio.
Depay amekuwa hana nafasi ndani ya kikosi cha Kocha Jose Mourinho, huku ikielezwa 'ubishoo' ndio unaomponza, hivyo njia pekee ya kuokoa kipaji chake ni lazima apate timu ya kuichezea na Lyon inasisitiza inamtaka.

Nani kubeba taji la Mapinduzi Cup 2017?

Na Rahma White
LIMEBAKI kama saa moja na ushei tu kabla ya Simba na Azam kumaliza ubishi kwenye pambano la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 litakalopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Simba inacheza fainali yake ya sita katika msimu huu wa 11 wa michuano hiyo, ilihali Azam itakuwa ni ya tatu, lakini ikiwa na rekodi ya kusisimua ya kuingia fainali chache lakini haijawahi kuacha taji.
Iliingia mwaka 2012 na 2013 na mara zote likabeba taji mbele ya Jamhuri ya Pemba na KCCA, wakati Simba katika fainali zake tano za awali imetwaa mara tatu ikiwa klabu yenye historia ya kutwaa mara nyingi taji hilo.
Licha ya rekodi hizo za kusisimua kwa wababe hao wa Ligi Kuu Bara, bado timu yoyote itakayocheza vema na kutumia kwa ufanisi dakika 90 inaweza kubeba taji na kuhitimisha siku 15 za michuano hiyo iliyoanza Desemba 30, 2016.
Makocha na wachezaji wa timu zote wamekuwa wakitambiana tangu walipofahamu watakutana kwenye mchezo huo utakaoanza majira ya Saa 2:15, lakini ukweli ni kwamba lolote linaweza kutokea usiku huu visiwani humo.
Simba inayotarajiwa kupanga kikosi karibu chote kilichoitoa nishai Yanga kwa kuifunga kwenye nusu fainali, inaivaa Azam ikiwa haijkapoteza mechi yoyote ila imeruhusu bao moja wavuni wake, tofauti na Azam ambayo haijafungwa kabisa.
Mbali na mashabiki usiku kutaka kushuhudia timu ipi itakuwa bingwa mpya wa michuano ya mwaka huu, pia fainali hizo zitakuwa na utamu mwingine wa kujua wachezaji gani watakaonyakua tuzo za Ufungaji Bora, Kipa Bora, Mchezaji Bora Chjipukizi na Mchezaji Bora wa michuano.
Mpaka sasa tuzo ya Mfungaji Bora ni kama inarudi tena kwa Simon Msuva aliyetwaa mwaka 2014 akiwa na mabao manne sawa na aliyonayo msimu huu, licha ya timu yake ya Yanga kutolewa.
Wachezaji waliokuwa wakimfukuzia winga huyo mchachari, Bokota Labama wa URA Uganda ma Abdulsamad Kassim wa Jang'ombe Boys timu zao zimeaga michuano, japo Laudi Mavugo mwenye mabao mawili anaweza kumvurugia.
Kipa Bora nafasi ipo wazi kwa Aishi Manula wa Azam ambayo mpaka timu yake ikiivaa Simba, hajaruhusu bao lolote na akiwa ameonyesha kiwango cha hali ya juu, huku Daniel Agyei wa Simba naye aliyeibuka shujaa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Yanga kwa kuokoa penalti mbili za Deo Munishi 'Dida' na ile ya Haji Mwinyi anaweza kujikuta akibeba, iwapo Simba itafanya yake usiku huu.
Kwenye tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ni vigumu kufahamu kwa sasa kwa sababu kuna vijana wengi walioonyesha makali akiwamo Enock Atta-Agyei wa Azam ambaye ndio kwanza anamiaka 18, lakini amepiga soka la nguvu Zanzibar.
Bila shaka ni suala la kusubiri kujua mambo yatakuwaje na MICHARAZO MITUPU litakuletea hatua kwa hatua ya pambano hilo mpaka mwisho wa fainali hiyo, usiache kuperuzi blog yako makini upate uhondo.

Kijeba cha Congo chazingua, CAF chapigwa mkwara

Na Alfred Lucas, TFF
BADO hakijaeleweka. Lile sakata la kijeba cha timu ya taifa ya vijana ya Congo, Langa Lesse Bercy, halijatafutiwa ufumbuzi mpaka sasa, ila safari hii Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limetoa nafasi ya mwisho kwa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT) kumpeleka mchezaji huyo  jijini Libreville, Gabon ili apimwe kipimo kipya cha MRI ili kutambua umri wake.
CAF limetaka FECOFOOT kumpeleka mchezaji huyo huko Libreville, Gabon ndani ya siku 10 zijazo kuanzia jana Januari 12, 2017.
CAF limepata kumwita mchezaji huyo mara mbili mwaka jana, na FECOFOOT imeshindwa kumpeleka kwa sababu mbalimbali wanazozijua FECOFOOT.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, vijana waliohitajika kucheza ni wale wenye umri wa chini ya miaka 17.
Langa Lesse Bercy, amelalamikiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba amezidi umri hivyo kuhitajika kumpeleka kwani hakustahili kucheza hatua ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Fainali za vijana zinatarajiwa kufanyika katika nchi nyingine itakayotangazwa hapo baadaye baada ya Madagascar kuondolewa kuandaa fainali hizo baada ya kubainika kutokamilisha baadhi ya taratibu.
Hii inatokana na ripoti ambayo CAF wameipata kutoka kwa wakaguzi wa maandalizi ya fainali hizo. CAF imefungua kandarasi ya kwa nchi wanachama wengine kuandaa fainali hizo. Mwisho wa kupokea maombi ni Januari 30, mwaka huu.
Kadhalika Kamati ya Utendaji ya CAF, imemteua Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Chilla Tenga kuwania nafasi ya uwakilishi katika Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).
Katika nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Tenga atachuana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
Wengine waliopitishwa kuwania nafasi ya uwakilishi katika Kamati ya Utendaji ya FIFA kutoka nchi za Afrika ni Tarek Bouchamaoui wa Tunisia ambaye anaingia kwenye kundi la nchi zinazozungumza lugha za Kiarabu, Kireno na Kihispaniola.
Kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa wamo Constant Omari Selemani wa DR Congo na Augustin Sidy Diallo wa Cote d’Ivoire wakati nafasi nyingine za wazi ihuhusisha mwanamke mmoja, wamo Almamy Kabele Camara (Guinea), Chabur Goc (South Sudan), Danny Jordaan (Afrika Kusini), Hani Abo Rida (Misri)  na Lydia Sekera (Burundi).