STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 31, 2012

Majeraha yamzuia Cheka kurudiana na Mmalawi

Bondia Francis Cheka 'SMG'


BINGWA anayeshikilia mataji manne tofauti likiwemo la IBF, bondia Francis Cheka 'SMG' hataweza kupambana kwa mara nyingine tena na Mmalawi, Chiotra Chimwemwe kutokana na kuumia katika pambano lao la kwanza lililochezwa jijini Arusha wiki iliyopita.
Cheka na Chimwemwe walitarajiwa kuvaana mjini Addis Ababa, Ethiopia katika pambano maalum la kusindikiza mkutano wa Viongozi Wakuu wa nchi za Afrika, Januari 26.
Mabondia hao wangepigana kuzindikiza pambano la kimataifa kati ya Oliver McCall wa Marekani dhidi ya Sammy Retta wa Ethiopia kuwania ubingwa wa uzito wa juu IBF (IBF AMEPG).
Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi, alisema nafasi ya Cheka imechukuliwa na mkali mwingine nwa ngumi za kulipwa nchini katika uzito wa juu, Alphonce Mchumiatumbo, ingawa haijafahamika atapigana na nani.

Ngowi alisema mapambano mengine siku hiyo ya Januari 26 ni pamoja na lile la Mkenya, Daniel Wanyonyi dhidi ya Issac Hlatswayo wa Afrika Kusini watakaowania ubingwa wa IBF AMEPG uzito wa Welterweight
Pambano jingine litawakutanisha Manzur Ali wa Misri dhidi ya Harry Simon wa Namibia watakaowania taji la IBF AMEPG uzito wa Light heavyweight.

Minziro atamba Yanga moto ule ule

Fred Minziro (kulia) katika moja ya majukumu yake uwanjani

KOCHA Msaidizi wa klabu ya Yanga, Fred Felix Minziro, ametamba kwamba moto waliomalizia nao kwenye duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo watakaoanza nao katika duru lijalo, huku akisisitiza lazima Yanga iwe bingwa 2012-2013.
Aidha kocha huyo ametamba kwamba timu yao imejipanga ili kuhakikisha wanatetea taji lao la Kombe la Kagame katika michuano itakayofanyika hivi karibuni nchini Rwanda.
Akizungumza na MICHARAZO kabla ya kupaa na timu kwenda Uturuki, Minziro, beki wa kimataifa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema ubora wa kikosi alichonacho na namna  wanavyojiandaa, inampa imani ya kuamini kwamba Yanga itawavua ubingwa wa ligi watani zao, Simba msimu huu.
Minziro, alisema Yanga itaendeleza moto ule ule waliomalizia nao duru la kwanza la ligi hiyo iliyowatoa nafasi za kati mpaka kileleni ikiwaengua waliokuwa vinara Simba na Azam, ili mwisho wa msimu klabu yao iwe mabingwa wapya wa Tanzania.
"Hatudhani kama tutaanza kinyonge kama ilivyokuwa katika duru la kwanza, tupo katika maandalizi kabambe ili kuhakikisha tunaendeleza moto na kasi yetu ili kurejesha taji tuliloporwa na watanbi zetu, Simba," alisema Minziro.
Minziro, alisema japo anatambua duru lijalo litakuwa lenye ushindani mkubwa, lakini wao wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanafanya vema, huku akisisitiza kuwa maandalizi yao yanalenga pia kwenda kutetea taji lao la Kombe la Kagame njini KIgali.
"Macho na akili zetu zote tumezielekeza kwenye duru la pili la ligi pamoja na michuano ya Kagame, tungependa kwenda kutetea taji ugenini, tunajiamini na wachezaji wana ari kubwa ya kufanya hivyo," alisema Minziro.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 29, tano zaidi ya Azam waliopo nafasi ya pili na sita zaidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya tatu, ilitwaa taji hilo la Kagame Julai, 2012 kwa kuilaza Azam mabao 2-0 katika mchezo fainali zilizochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mtanzania kuwania taji la Jumuiya ya Madola


BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Fadhili Majia ameteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) kupigana na Isaac Quaye wa Ghana kuwania nafasi ya kupigana na bingwa Kevin Satchell wa Uingereza.
Mabondia hao wanatarajia kupigana katika pambano hilo la uzani wa Fly Februari 22 mwakani kwenye mji wa Accra, Ghana ambapo mshindi wa mechi hiyo ya mchujo atapata fursa ya kupigana na Satchell anayeshikilia taji hilo la Jumuiya ya Madola.
Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Onesmo Ngowi ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa CBC, alisema wajumbe wa bodi hiyo walimpigia kura Majia baada ya yeye kulipendekeza na hiyo kuibuka kidedea.
Ngowi, alisema hiyo itakuwa ni mara ya kwanaa kwa Majia kuwania mkanda huo wa Jumuiya ya Madola ambao huziunganisha nchi zote zilizotawaliwa na Uingereza.
"Bondia Mtanzania Fadhil Majia amepeta fursa ya kuteuliwa kucheza mechi ya mchujo dhidi ya Mghana, Isaac Quaye Februari 22, 2013 ili kuwania nafasi ya kupigana na bingwa wanayeshikilia taji la CBC, Kevin Satchell wa Uingereza," alisema Ngowi.
Katika hatua nyingine, Ngomi alisema CBC, imepitisha azimio la kuruhusu ubingwa wa baraza hilo katika Bara la Afrika.
Ubingwa huo utakuwa unajukikana kama 'CBC Africa Zone' na tayari wapo mabondia kadhaa wa nchi za Afrika ya Magharibi ambao wameshandaa mapambano mwakani.
"Napenda kuwahamasisha mapromota wa Tanzania kuchangamkia fursa hizi adimu na kuandaa mapambano ya ubingwa wa 'CBC Africa Zone' kwa manufaa ya mabondia wetu," alisema Ngowi ambaye pia ni Rais wa IBF Afrika/USBA.
***

Julio afichua siri Msimbazi


KOCHA msaidizi wa timu ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys, Jamhuri Kihwelo 'Julio', aliyerejeshwa Msimbazi kama kocha msaidizi, amefichua siri ya wachezaji wa Simba akidai wengi wao wana matatizo ya kutokuwa na pumzi na stamina ya kutosha.
Julio, alisema kutokana na kupewa jukumu la kuwanoa vijana hao kama kocha wa viungo wa Simba atarekebisha tatizo, ili timu yao iweze kufanya vema katika duru lijalo la ligi kuu pamoja na uwakilishi wa nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Beki huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema pamoja na mambo mengine yaliyoiponza Simba kwenye duru lililopita, amegundua tatizo kubwa kwa kikosi hicho ni kukosekana kwa stamina na pumzi za kutosha kwa nyota wa timu hiyo.
Alisema kutokana na kubaini tatizo hilo, amejipanga kuwanoa wachezaji hao ili wawe 'ngangari'.
Julio alisema anadhani tatizo hilo ndilo lililoigharimu Simba kwenye duru la kwanza kwa wachezaji wake kushindwa kumudu dakika zote 90 za mchezao badala yake kuonekana tishio dakika 45 za kwanza na kuwa 'urojo' dakika 45 za pili na kupata matokeo mabaya.
"Nimegundua wachezaji wengi wa Simba wana tatizo la pumzi na stamina, hivyo nitajitahidi kurekebisha tatizo kabla ya kuanza kwa duru la pili la ligi ili vijana wawe ng'ang'ari," alisema.
Julio amerejeshwa Msimbazi sambamba na aliyekuwa kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Moses Basena ili kumsaidia kocha mpya wa klabu hiyo, Patrick Liewig  anayechukua nafasi ya Mserbia , Circokiv Milovan aliyetupiwa virango Simba.
Kwa sasa Julio na vijana wake wanaendelea kujifua kwa mazoezi ya ufukweni wakati wakisubiri kuanza kufanya mazoezi ya uwanjani mara atakapowasilia kwa Mfaransa Liewig, aliyepewa mkataba wa muda mrefu ili 'kupimwa' kiwango chake.

Kocha wa Simba sasa kutua leo Yanga wafika salama Uturuki


UONGOZI wa Simba umedai kuwa kocha mpya wa timu yao, Mfaransa Patrick Lieweg atawasili kwenye Uwanja wa Kiamataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) leo saa 7:15 mchana akitokea mjini Baho, Ufaransa.
Ujio wa kocha huyo umekuwa wa danadana tangu ilipotangazwa awali angetua Desemba 27, lakini safari hii uongozi umethibitisha kuwa atatua leo mchana bila kupepesa macho.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alisema kuwa kocha huyo atatua kurithi mikoba ya aliyekuwa kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic, ambaye wamelazimika kumfungashia virago baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Kulikuwa na tatizo la usafiri wa ndege katika nchinnyingi za Ulaya kipindi hiki cha bararidi kali barani humo ndiyo maana alikuwa anakosa ndege za kumleta Tanzania,” alisema Rage.
Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, walilazimika kuvunja mkataba na Cirkovic kutokana na kilichodaiwa na uongozi wa klabu hiyo kuwa kocha huyo alikuwa ‘anaikamua’ kiasi kikubwa mno cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kuvunja mkataba na kocha huyo aliyewapa ubingwa msimu uliopita, ‘Wekundu wa Msimbazi’ tayari wameingia mkataba na makocha wawili wapya, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Mganda Mosses Basena.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, baada ya kutua kwa Lieweg, uongozi wa klabu hiyo utatangaza mfumo mpya wa benchi la ufundi la timu yao.
Katika hatua nyingine msafara wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga umefika salama nchini Uturuki na unatarajiwa kuanza programu zao nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, kikosi hicho kilifika salama jana asubuhi na leo kilitarajiwa kuanza kujifua kabla ya kuanza kucheza mechi kadhaa za kirafiki na wenyeji wao zikiwa maalum kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na utetezi wao wa Kombe la Kagame litakalofanyika nchini Rwanda.

Golden Bush, Wahenga kuuaga mwaka Tp Afrika


TIMU ya soka ya Golden Bush jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Wahenga Fc katika pambano maalum la kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2013.
Pambano la timu hizo mbili zinazoundwa na wachezaji nyota wa zamani nchini, litafanyika kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza Dar es Salaam kuanzia majira ya jioni.
Timu hizo zitakutana katika pambano hilo huku zikiwa na kumbukumbu ya kukutana hivi karibuni kwenye dimba la uwanja huo.
Wahenga wanakumbuka kipigo cha mabao 4-2 ilichopewa na wapinzani wao siku chache baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika michezo iliyochezwa hivi karibuni.
Golden Bush inayomilikiwa na mmoja wa wanachama wa zamani wa Friends of Simba, Onesmo Wazir 'Ticotico', itashuka dimbani leo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 iliyopata siku ya Jumamosi dhidi ya vijana nwa Chuo Kikuu.
Ticotico aliyeshindwa kuonyesha makeke yake katika pambano la Jumamosi kutokana na kuumia dakika 9 tu baada ya pambano hilo kuanza, alisema anaamini leo akijaliwa atashuka dimbani kuwaongoza wenzake kuendeleza 'dozi' yao ya mabao manne iliyokuwa inaitoa kabla ya kutibuliwa na vijana hao wa Chuo Kikuu.
"Nilikamia mechi ya Jumamosi, lakini nikashindwa kwa kuumia mapema, ila Jumatatu (leo) naweza kushuka dimbani kuwavaa wahenga," alisema Ticotico.
Katika mechi yao ya Jumamosi, Golden Bush ilipata mabao yake kupitia nyota wa zamani wa Yanga, Moro United na Prisons Mbeya, Herry Morris na Omar Msangi na inatarajiwa kushuka dimbani leo ikiwa na nyota wake kama Steven Marashi, Yahya Issa, Salum Swedi 'Kussi', Said Swedi 'Panucci', Herry Morris, Athuman Machuppa, Machotta, Majaliwa, Omar Msangi, Ticotico, Katina Shija na wakali wengine.
Wahenga wenyewe inatarajiwa kuwa chini ya nyota wa zamani wa Majimaji, Simba na Taifa Stars, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio'.


Lampard aipaisha Chelsea


Frank Lampard akishangilia moja ya mabao yake aliyofunga jana


LONDON, England
FRANK Lampard alionyesha thamani yake kwa  Chelsea baada ya kufunga magoli mawili ‘makali’ yaliyoipa ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Everton jana na kukwea hadi katika nafasi yake ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Huku kukiwa na uvumi mwingi kuhusiana na hatma yake ndani ya Chelsea, alionyesha kiwango cha juu na kufunga mabao yote huku goli la Everton likifungwa na Steven Pienaar.
Ushindi wan ne mfululizo wa Chelsea chini ya kocha Rafael Benitez umeiinua hadi kubakiza pointi nne tu kabla ya kuifikia Manchester City inayoshika nafasi ya pili, huku Chelsea ikiwa na mechi moja mkononi.
-----

Mhasibu Simba aporwa mamilioni ya fedha Sinza

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage


ZAIDI ya Sh. milioni 10 za klabu ya Simba zimeporwa baada ya Mhasibu wa klabu hiyo, Erick Sekiete (28) kudai kuvamiwa na majambazi sita katika mtaa wa Sinza kwa Remmy na kuporwa kiasi hicho cha pesa juzi saa 3:20 usiku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa Sh. milioni 7.59 na dola za Marekani 2,000 ambazo Simba walizipata baada ya makato ya mapato ya mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuchapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Simba ilipata mgawo wa Sh. milioni 10.6 na dola za Marekani 2,000 (Sh. milioni tatu) kutokana na mapato ya kiingilio cha mechi yao dhidi ya Tusker. Baada ya makato, walibakiwa na Sh. milioni 7.59 ambazo Sekiete alikabidhiwa,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Sekiete na mwenzake Stanley Phillipo (23) ambaye alidaiwa kuwa ni mwanafunzi, walipanda kwenye gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS lililokuwa likiendeshwa na Said Pamba na kwamba walipofika eneo hilo, dereva aliwashusha na kwamba wakaanza kutafuta teksi.
Aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya kushushwa, Sekiete na Philipo waliamua kuvuka upande wa pili wa barabara ya iendayo Kijitonyama ili wachukue teksi lakini ghafla  walilitekwa na watu sita walioshuka kutoka kwenye pikipiki tatu.
“Mmoja wa watu walioshuka kwenye pikipiki alikuwa na bastola... alifyatua risasi hewani wakati wenzake wakipora begi lenye fedha kutoka kwa mhasibu,” alisema Kenyela.
Aliendelea kufafanua kuwa wakati watu hao wakimnyang’anya begi Sekiete walikuwa wakitamka maneno ya kejeli kwa uongozi wa Simba.
Aliyanukuu maneno hayo kwa kusema; “Mnafungwa halafu mnazingua, na kwa kuwa viongozi wenu wanakula pesa za klabu, nasi hizi tunaziiba.”
Kamanda Kenyela alisema kuwa baada ya watu hao kupora fedha hizo, walitokomea kusikojulikana na hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu akiwamo Sekiete kuhusiana na tukio hilo.
Watu wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni ni Pamba na Philipo ambao walikuwa pamoja na Sekiete kwenye gari.
“Sisi (Jeshi la Polisi) tulishaonya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha bila ulinzi, tunawashikilia watu hawa watatu kwa sababu huenda walipanga kuiba fedha hizo,” aliongeza.
“Mazingira ya kuporwa kwa fedha hizo yanatia shaka huenda kuna kitu kilikuwa kimepangwa ili fedha hizo ziibwe. Iweje mtu akahifadhi nyumbani kwake kiasi kikubwa cha fedha kama hicho?” alihoji Kamanda Kenyela.
“Kwa sasa mtu yeyote atakayeripoti kuporwa fedha kiasi kikubwa kama hiki na alikuwa akisafirisha pasipo na ulinzi, tutaanza naye.
“Tunawashikilia wawa watatu kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo. Tunaomba ushirikiano kutoka watu wenye taarifa juu ya waliohusika na tukio hili.”
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alinukuliwa jana akidai amesikitishwa na taarifa za kuporwa kwa fedha za klabu yao.
“Mhasibu wetu anaishi Sinza. Alizichukua zile fedha za klabu akazihifadhi nyumbani kwake ili leo (jana) azipeleke benki,” alisema Rage.


Masawe Mtata ana Love position

MCHEKESHAJI mahiri wa kipindi cha 'Ze Comedy Show', Rogers Richard a.k.a. Masawe Mtata, amefyatua filamu mpya iitwayo 'Love Position', akijiandaa pia kupakua nyimbo mpya kwa ajili ya albamu yake ijayo.
Msanii huyo anayefahamika pia kwa jina la Dokta Kicheko, alisema tayari filamu hiyo ya kimapenzi ipo mtaani baada ya kuitoa wiki iliyopita akiwa ameigiza na wasanii kadhaa wenye majina na chipukizi.
Masawe Mtata, alisema filamu hiyo ya 'komedi' imekuja wakati akiwa katika harakati zake za kupakua albamu mpya ya muziki wa kizazi kipya baada ya kutamba na nyimbo kadhaa ukiwemo wa 'Siwezi Kulala'.
"Nimekamilisha na kuiachia filamu yangu mpya iitwayo 'Love Position', huku nikiwa mbioni kukamilisha albamu yangu ya tatu itakayokuwa na nyimbo nane," alisema.
Msanii huyo alisema albamu hiyo inakuja baada ya awali kutamba na albamu za 'Say Ye' au 'Unanipenda Mimi' na 'Mirinda Nyeusi' iliyofahamika pia kama 'Kicheko.com'.
Mchekeshaji huyo, alisema wakati filamu yake hiyo mpya ikiendelea kupokelewa na mashabiki wake, pia anajipanga kuandaa kazi nyingine mpya ili iwe kama 'funguo' kwa mwaka 2013 alioutabiri utakuwa na ushindani mkubwa kisanii nchini.

Saturday, December 29, 2012

RIDHIWANI APONDA MFUMO UENDESHAJI YANGA ADAI AFADHALI WA SIMBA

Ridhiwani akihutubia Waandishi asubuhi ya leo Kiromo Hotel

Na Mahmoud Zubeiry, Bagamoyo
MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, amesema mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ni mbovu kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo huo.
Kikwete alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa Simba SC, ambao desturi yao ni kuchangishana.
“Nilijaribu kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa wanachangishana,”alisema.
Ingawa hakumtaja mtu ambaye mfuko wake unategemewa Yanga, lakini wazi ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
Kwa ujumla katika hotuba yake, Kikwete alisema haridhishwi na mfumo wa uendeshwaji wa soka ya Tanzania na kwamba unahitaji mabadiliko.
Kikwete aliushauri uongozi wa TASWA upiganie nafasi ya uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kusisitiza juu ya umuhimu wa waandishi nchini kutambua haki zao.
Lakini pia Kikwete aliwaasa waandishi kuepuka uandishi wa kinazi wa Simba na Yanga na badala yake kuzama ndani zaidi katika kuripoti, sambamba na kuripoti michezo yote, badala ya kuegemea kwenye soka pekee.
“Vyombo vya habari lazima viwe na wataalamu tofauti wa kuripoti michezo tofauti, huyu akiegemea kwenye soka, mwingine aegemee kwenye mchezo mwingine, ili kuhakikisha tunafikisha ujumbe vema kwa jamii,” alisema mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo alisema kwamba ipo haja ya TASWA kuendesha semina kadhaa za kuelimisha Waandishi wa Habari kuweza kuripoti michezo mbalimbali nchini.  
Aidha, katika mkutano huo, wanachama walielimishwa kuhusu uanzishwaji wa Saccos na kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa chama cha ushirika wa akiba na mikopo kwa Taswa. Walipendekezwa wajumbe waunde timu ya mpito.

CHANZO:BIN ZUBEIRY

KOCHA  SIMBA KUTUA LEO KUSHUHUDIA MECHI YAO NA TUSKER


KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kuwasili leo nchini na atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili nchini juzi, lakini ilishindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege na sasa mashabiki wa timu hiyo wamtarajie leo.
Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, Patrick Liewig na ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kuelekea mchezo wa leo, Simba itamenyana na Tusker FC ambayo ilianza vema ziara yake nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumatano.
Simba SC na Tusker zinatarajiwa kukutana pia kwenye Kundi la Mapinduzi visiwani Zanziabr hivi karibuni, kwani zimepangwa kundi moja, A pamoja na Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Aidha, katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini Kenya, Tusker.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi (10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na zawadi nyinginezo.

Masai Nyota Mbof adai 2012 ulikuwa nomaa!

Masai Nyota Mbof

MCHEKESHAJI anayejitosa kwenye fani ya muziki nchini, Gilliad Severine 'Masai  Nyota Mbofu', amesema mwaka 2012 utakabaki kuwa wa mchungu kwake kutokana na matukio ya kusikikitisha yaliyotokea ndani ya mwaka huo.
Masai anayejiandaa kufyatua wimbo mpya wa 'Masai ya Wapi' akishirikiana na rapa Kalidjo Kitokololo, alisema vifo na kuugua kwa baadhi ya nyota wa sanaa nchini ndiko kunamfanya ashindwe kuusahau mwaka huo.
Alisema kwa kumbukumbu zake tangu Januari mpaka Desemba fani ya sanaa imekuwa  haina nafuu kutokana na kuandamwa na matatizo ikiwemo vifo, ajali na kuugua kwa wasanii wakiwemo waigizaji wa filamu, wachekeshaji na wasanii wa muziki tofauti.
"Kwa kweli pamoja na kumshukuru Mungu kukaribia kuumaliza mwaka 2012, lakini ni vigumu kuusahau kwa jinsi ulivyokuwa mchungu kwangu na wadau wa sanaa  nchini kwa matukio yaliyotokea miezi yote 12," alisema.
Alisema hata hivyo anamuomba Mungu awalinde wasanii na kuufanya mwaka 2013 uwe wa neema, furaha na mafanikio huku akiwasihi wasanii wenzake kumcha Mungu na kuishi kinyenyekevu ili kutomuudhi Muumbaji wao.
"Tunaomba tuuingie mwaka 2013 kwa amani na utulivu na kujipanga upya kwa 2013 ila muhimu tunapaswa kumrudia Mungu ili atupe baraka zake," alisema Masai anayetamba  na wimbo wa 'Rungu na Mukuki'.
Japo Masai hakuyataja matukio yaliyomtia simanzi, ila vifo vya wasanii kama Mzee Kipara, Steven Kanumba, Mlopero, Sharo Milionea, John Stephano, Mariam Khamis na  kuugua kwa akina Vengu, Mzee Small, Sajuki na ajali kadhaa zilizowatokea wasanii   nchini ni kati ya matukio makubwa yaliyojiri ndani ya mwaka 2012.

Morris, Machuppa, Kussi waibeba Golden Bush


NYOTA wa zamani wa timu za Simba na Yanga, Herry Morris, Athuman Machuppa na Salum Swedi 'Kussi' leo waling'ara 'mchangani' baada ya kuibeba timu ya Golden Bush kwa kuiwezesha kuinyuka timu ya vijana ya Chuo Kikuu kwa mabao 3-2 katika pambano la kirafiki lililochezwa jijini Dar es Salaam.
Morris aliyewahi pia kuzichezea timu za Prisons Mbeya na Moro United, aliifungia Golden Bush mabao mawili katika pambano hilo maalum la kuagia mwaka 2012 lililochezwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu.
Kivumbi uwanjani kati ya pambano la Chuo Kikuu na Golden Bus Veterani.

Kikosi cha Golden Bush, kikijiandaa kuingia uwanjani kuumana na Chuo Kikuu leo asubuhi kwenyue uwanja wa Chuo Kikuu, Dar es salaam.

Hatari langoni mwa timu ya vijana ya Chuo Kikuu, walipokuwa wakiumana na Golden Bush Veterani asubuhi ya leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu, Dar es Salaam. Golden Bush waliibuka washindi wa mabao 3-2.


Katika pambano hilo lililochezeshwa vema na nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', Golden ilishuka dimbani na wakali kama Said Swedi 'Pannuci', Athuman Machuppa, Yahya Issa, Steve Marashi, Ben Mwalala, Salum Swedi, Katina Shija na wakali wengine waliotamba Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo kikosi hicho kilichompoteza 'nahodha' wake, Onesmop Wazir 'Ticotico' aliyeumia dakika ya tisa tu ya mchezo huo ilijikuta ikitanguliwa kufungwa kwa bao 'tamu' lililopachikwa wavuni na nyota wa Chuo Kikuu, Wonder katika dakika ya 13.
Bao hilo lilisawazishwa katika dakika ya 21 na nyota wa mchezo huo, Katina aliyetoa pande murua kwa Morris aliyefunga kwa shuti kali na baadae Omar Mgonja akaiongezea Golden bao la pili dakika ya 38.
Dakika mbili kabla ya mapumziko Chuo Kikuu ilifunga bao la pili na la kusawazisha kupitia tena kwa Wonder baada ya kuwatoka mabeki wa Golden waliokuwa chini ya Salum Kussi, Yahya Issa na Majaliwa na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 2-2.
Kipindi cha pili kilianza kwa Golden kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na kuongeza kasi yao ya mashambulizi na kujipatia bao la tatu na la ushindi lililofungwa tena na Morris katika dakika ya 63 kwa mkwaju mkali wa karibu.

Mmoja wa mabeki wa Chuo Kikuu akiondoa mpira langoni mwake walipokuwa wakiumana na Golden Bush na kukubali kipigo cha mabao 3-2.


IBF yampongeza Francis Cheka

Bondia Francis Cheka (kushoto) alipokuwa akitunushiana misuli na Chimwemwe kabla ya pambano lao ma juzi mjini Arusha, ambapo Cheka aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya mpinzani wake huyo kutoka Malawi.
SHIRIKISHO la Ngumi la Kimataifa (IBF) limempongeza bingwa mpya wa uzito wa Super Middle wa Bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki yaa Kati, Francis Cheka kufuatia juzi kumtwanga kwa pointi Mmalawi Chiotcha Chimwemwe.
Katika barua yake iliyotumwa kwa Cheka Desemba 28, Mwenyekiti wa Kamati ya Ubingwa wa IBF/USBA, Lindsey Tucker alisema wamefurahishwa na Cheka kutwaa ubingwa na kumtakia kila la heri katika kulishikilia taji hilo.
"Tunachukua fursa hii kukutakia maisha na mafanikio mazuri kama bingwa wa IBF na kumhimiza kuishi kama bingwa". Sehemu ya barua hiyo inasomeka hivyo.
Aidha Tucker amemwagia sifa mpinzani wa Cheka kwa kuonyesha ushupavu na ushindani katika pambano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ambapo alishindwa kwa pointi na mpinzani wake katika pambano hilo lililokuwa kali..
Katika barua hiyo imemkumbusha Cheka kutetea taji lake hilo ndani ya kipindi cha miezi sita.

Aziz Gilla atoa ya moyoni, adai hana kinyongo na Coastal Union

Aziz Gilla (kulia) alipokuwa Simba

ALIYEKUWA mshambuliaji wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Salim Gilla, ameibuka na kusema hana kinyongo cha kitendo cha kutemwa na klabu hiyo.
Hata hivyo mshambulaji huyo wa zamani wa Simba, aliyeng'ara katika fainali za Kombe la Taifa ya 2009 akiteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mashindano alidai taarifa ya kutemwa kwake na Coastal zilimshtua kupita maelezo.
Akizungumza na MICHARAZO juzi kwa njia ya simu, Gilla aliyeoongoza orodha ya wafungaji ndani ya Coastal kwa msimu uliopita, alisema kama mchezaji anayaheshimu maamuzi yaliyofikiwa na benchi la ufundi la timu hiyo ya kuamua kumtema.
Alisema huenda makocha wa timu hiyo waliomuona sio mchezaji wa mipango yao na kuamua kumtema, hivyo hawezi kupingana na uamuzi hayo zaidi ya kuitakiwa kila la heri timu hiyo katika duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Kwa kweli sina kinyongo na maamuzi yaliyofikiwa juu ya kutemwa kwangu kwani ni uamuzi wa kocha, ila nikiri nilishtushwa mno kusikia jina langu ni mioingoni mwa waliotemwa Coastal Union," alisema Gilla.
Mshambuliaji huyo, alisema ni vigumu kuweza kuiwekea kinyongo Coastal kwa vile ni timu ya mkoa wake na ni klabu anayoipenda kwa dhati moyoni.
"Coastal ni timu ya nyumbani, kufanya kwake vema ni sifa kwa mkoa mzima wa Tanga, hivyo siwezi kuichukua zaidi ya kuitakia kila la heri iendeleze moto wa duru la kwanza ili hatimaye itwae ubingwa msimu huu," alisema Gilla.
Coastal Union ilitangaza kuwatema Gilla na wachezaji wenzake kadhaa katika usajili wa dirisha dogo kama njia ya kukiimarisha kikosi chao.
Wengine waliotemwa na mabingwa hao wa zamani wa soka nchini, ni makipa  Juma Mpongo na Jackson Chove, Juma Jabu, Said Sued, Mohamed Issa na Jamal Bachemanga, huku Phillip Maisela, Razak Khalfan, Gerald Lukindo ‘Sipi’ na Shafii Karumani wakitajwa kupelekwa kwa mkopo kwa timu nyingine.

FAINALI ZA KAWAMBWA CUP KUFANYIKA LEO B'MOYO

Rais wa TFF, Leodger Tenga mmoja wa viiongozi wanaotarajiwa kuhudhuria fainali za Kombe la Kawambwa zinazofanyika leo mjini Bagamoyo, Pwani.

FAINALI za soka za kuwania ya Kombe la Kawambwa, inatarajiwa kufanyika leo mjini Bagamoyo kwa kuzikutanisha timu za Beach Boys na Mataya.
Pambano hilo la fainali za michuano hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa litafanyika kwenye uwanja wa Mwanakalenge, mjini humo.
Timu hizo zitakazoumana fainali zimepata nafasi hiyo baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali, ambapo Beach Boys yenyewe iliizabua Matimbwa mabao 2-0 na Mataya kuigagadua Chaulu kwa mabao 3-1.
Msemaji wa michuano hiyo, Masu Bwire alisema fainali hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga na Waziri Dk Shukuru Kawambwa.
Mgeni rasmi wa fainali hizo kwa mujibu wa msemaji huyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Bwire, aliongeza viongozi wengine watakaohudhuria fainali hizo ni Meneja wa kampuni ya Konyagi wadhamini wakuu wa michuano hiyo, David Mgwasa na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA).
Aliongeza maandalizi ya fainali hizo yamekamilika zikiwamo zawadi za washindi na wale watakaotwaa tuzo mbalimbali za michuano hiyo iliyoanza rasmi Septemba 25 kwa kushirikisha jumla ya timu 84 zilizopo jimboni humo.
Alisema mbali na washindi wa kwanza hadi watatu kuzawadiwa seti za jezi, mipira, vizuia ugoko na fedha taslim, pia Kipa Bora, Mchezaji Bora, na Mwamuzi Bora wa michuano hiyo kila mmoja atazwadiwa Sh. 50,000.
Bwire alisema bingwa wa michuano hiyo atanyakua Sh 400,000, Kombe, jezi seti mbili, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja, huku wa pili atazawadiwa Sh 200,000, seti mbili za jezi, mipira miwili na vizuia ugoko seti moja.
Mshindi wa tatu wa michuano hiyo atajinyakulia seti moja ya jezi, mpira mmoja, seti moja ya vizuia ugoko na fedha taslim Sh 100,000.

Mwalala aamua kutundika daluga, kisa maumivu wa nyonga

Ben Mwalala alipokuwa Yanga

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa timu za Yanga na Coastal Union, Ben Mwalala, ameamua kutundika daluga na kujikita kwenye ukocha kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya nyonga.
Akizungumza na MICHARAZO leo jijini Dar es Salaam, Mwalala aliyewahi kung'ara na timu za Mumias ya Kenya,  Sc Villa ya Uganda na APR Rwanda, alisema maumivu hayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu na ndiyo yaliyomuondoa Coastal Union msimu huu.
Mwalala aliyeichezea Yanga kwa nyakati tofauti kati ya kwa 2006-2009, alisema kwa vile ana mapenzi makubwa na soka ameamua kuendeleza mchezo huo kwa kujikita kwenye ukocha akiwa tayari ameshachukua mafunzo ya awali na ngazi ya kati mpaka sasa.
"Kaka nyonga imenifanya nistaafu soka ningali kijana, hata hivyo bado sijatoka katika katika mchezo huo kwani nimeamua kusomea ukocha ili kuendeleza jahazi na hivi karibuni nimetoka kumaliza kozi za ngazi ya kati iliyoendeshwa na TFF," alisema.
Mwalala aliongeza, mipango yake ni kusomea kozi ya ngazi ya juu ya ukocha wa soka kisha kuja kuwa mwalimu wa timu yoyote itakayokuwa inamhitaji.
Mkenya huyo, ambaye 'amelowea' nchini, alisema anaamini bado ana mchango mkubwa katika soka ndani na nje ya nchi ndio maana imekuwa vigumu kwake kuacha moja kwa moja mchezo huo.
Mwalala anakumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kusaidia kufuta uteja wa miaka nane iliyokuwa nayo klabu hiyo mbele ya watani wao wa jadi, Simba kwa bao pekee alililofunga katika mechi ya kwanza ya msimu wa 2008 iliyoichezwa Oktoba 26.
Pia alikuwa mmoja wa walioifungia  Yanga mabao mawili yalioipa sare ya 2-2 katika mechi ya marudiano na watani zao hao iliyochezwa uwanja wa Taifa, Aprili 19, 2009.

Thursday, December 20, 2012

TANZANIA YAPANDA VIWANGO VYA FIFA

KIkosi cha timu ya soka ya Tanzania iliyopanda kiwango cha ubora duniani kwa mujibu wa FIFA

TANZANIA imepanda kwa nafasi nne katika viwango vya ubora wa soka duniani vilivyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo sasa inakamata nafasi ya 130 duniani kutoka ya 134 iliyokuwa ikiishikilia mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, Tanzania imepanda baada ya ushiriki wake katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) iliyomalizika hivi karibuni jijini Kampala, Uganda.
Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ambayo ndiyo inayoangaliwa na FIFA, iliishia katika hatua ya nusu fainali na matokeo yaliyoangaliwa katika kuipangia nafasi yake kwenye viwango ni ya mechi ya nusu fainali waliyolala 3-0 dhidi ya Uganda, robo fainali waliyoshinda 2-0 dhidi ya Rwanda na pia za hatua ya makundi walizoshinda 7-0 dhidi ya Somalia, 1-0 dhidi ya Sudan na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Burundi.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania inakamata nafasi ya 6 kati ya nchi 11. Mabingwa wa Kombe la Chalenji, Uganda wanaongoza kwenye ukanda huu huku wakishika nafasi ya 84 duniani, wakifuatiwa na Sudan (101), Ethiopia(110), Burundi iliyopanda kwa nafasi 24 na kushika nafasi ya 104 na Tanzania (130).
Kenya na Rwanda ziko pamoja katika nafasi ya 134 na kufuatiwa na Somalia (195), Eritrea (196), Sudani Kusini (199) na Djibout inakamata nafasi ya mwisho kwenye ukanda wa CECAFA baada ya kushika nafasi ya 202 duniani.
Barani Afrika, Ivory Coast ya kina Didier Drogba inaendelea kukamata nafasi ya kwanza huku ikiwa ya 14 katika viwango vya dunia na kufuatiwa na Algeria inayokamata nafasi ya 19, Mali (25), Ghana (30), Zambia (34), Misri (41), Gabon (42), Jamhuri ya Afrika ya Kati (52), Libya (54) na Guinea inayoshika nafasi ya 60.
Hipania ambao ni mabingwa wa Kombe la Dunia na Ulaya wanaendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya kwanza katika viwango vya ubora duniani, wakifuatiwa na nchi za Hispania, Ujerumani, Argentina, Italia, Colombia, England, Ureno, Uholanzi, Urusi na Croatia.

YANGA, PRIME TIME WAINGIA MKATABA



Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Clement Sanga (kushoto) na Mkurugenzi wa kampuni ya Prime Time Promotions Josheph Kusaga (kulia) wakisaini mkataba mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga jana
Klabu ya Young Africans leo imeingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions ya jijini Dar es saaalm kwa ajili ya kuandaa shuguli za mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika Januari 19, 2013 ambapo kampuni ya Prime Time imetoa mil 105,000,000 kwa ajili ya kuratibu shughuli hiyo.
Akiongea na waandishi wa habari, makamu mwenyekiti wa klabu ya Yanga Clement Sanga amesema wamefikia hatua hiyo kuipa nafasi kampuni ya Prime Time kuweza kuuendesha mkutano huo kisasa zaidi, ambapo unategemewa kufanyika na kuonyesha moja kw amoja  (live) kupitia kituo cha Luninga ya Clouds.
Prime Time pia imepewa fursa ya kusaka masoko na wadhamini wa klabu ya Yanga ili kuhakikisha klabu inajijenga vizuri kiuchumi kwa kubuni miradi mbali mbali, ambapo kwa kuanzia itaanda mchezo mmoja wa kirafiki na timu kubwa barani Afrika mwanzoni mwa mwezi Januari 2013.
Naye Mkurugenzi wa Prime Time Promotions Joseph Kusaga amesema amefurahishwa kwa kampun yake kupewa nafasi hiyo na kusema wanaahidi watafanya kazi nzuri kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha Kusaga alisema milango iko wazi kwa timu yoyote kuomba kushirikiana nao, kwani hawana itikadi ya timu yoyote bali lengo lao ni kufanya timu zote ziwe katika nafasi nzuri kiuchumi na kujitangaza kimichezo na kimasoko.
CHANZO:BIN ZUBEIRY

ZUKU TZ NA MAXCOM WAJA NA TEKNOLOJIA MPYA YA MALIPO 

 Meneja  Mkazi wa Zuku Tanzania, Fadhili Mwasyeba akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa kutia saini makubaliano ya ushirikiano baina yao na kampuni ya Maxcom, kupitia huduma ya maxmalipo. Kulia ni Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Maxcom, Ahmed Lussasi.
Mwendeshaji mkuu wa Kampuni ya Maxcom, Ahmed Lussasi akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Mwendeshaji Mkuu wa Maxcom, Ahmed Lussasi akizungumza, hukui maafisa wenzake kutoka Zuku Tanzania wakimsikiliza.
Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya MaxCom, Ahmed Lussasi, (kulia) akionesha mashine ya Maxmalipo  wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa kutia saini makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya Zuku Pay Tv, ambapo wateja wa Zuku watalipia ada zao za mwezi kupitia huduma ya Maxmalipo. Kushoto ni Meneja  Mkazi  Zuku Tanzania, Fadhili Mwasyeba.


KAMPUNI ya Wananchi Satellite Ltd inayomiliki televisheni ya kulipia ya Zuku kikishirikiana na kampuni ya Max Com zimeingia mkataba wa kuanza kutoa huduma rahisi ya malipo kwa wateja wa televisheni hiyo kwa nchi nzima kutumia huduma ya Maxmalipo.
Uzinduzi wa huduma hizo ulifanyika jana jijini Dar es Salaam baada ya viongozi wa pande hizo mbili kusaini mkataba huo mbele ya waandishi wa habari katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond, uliopo  Ubungo.
Meneja wa Wananchi Satellite kwa hapa nchini, Fadhili Mwasyeba alisema wameamua kurahisisha huduma ili kuwapa fursa wateja wao kufanya malipo kwa njia nyepesi na ya haraka tofauti na siku za nyuma kwa kutumia Maximalipo.
"Tuna furaha juu ya ushirikiano huo mpya na utakaowajali wateja wetu wa Zuku. Ahadi yetu ni kutoa ufumbuzi rahisi kwa wateja wetu wafanyabiashara na wauzaji na ufumbuzi huui utatuwezesha kufika mbali zaidi ya matarajio ya vwateja wetu." alisema.
Aidha Mwasyeba aliongeza kuwa wakati wakiwarahisishia unafuu wa kulipa malipo ya kila mwezi kwa wateja wao, pia kampuni yao inaendelea na promosheni yao ya kuwazawadia wateja wao iitwayo Zuku Tunakuthamini-Pata Tv Bure'.
Alisema kinachotakiwa kwa wateja kuwaunganisha wateja watano kujiunga na Zuku na kulipia malipo na kisha kujishindia runinga kati ya inchi 22 na wale watakaofikisha idadi ya wateja 10 watanyakua rungina ya inchi 42 na walioungwanishwa nao wakiambulia 'offer' nyingine zinazotolewa na kampuni yao kupitia promosheni hiyo.
Naye Msimamizi Mkuu wa kampiuni Maxcom, Ahmed Lussasi, alisema kuanza kutoa huduma hiyo kwa wateja wa zuku ni fursa ya kuwapa unafuu wateja wa televisheni hiyo popote walipo nchini kutokana na kampuni yao kuwa na vituo vya malipo ya Max malipo zaidi ya 3500 nchi nzima.
"Tunajitahidi kufanya kazi kwa ufanisi kwa malipo ya ushirikiano wa kipekee na zuku ili kuwafikia wateja kwa ukaribu zaidi," alisema na kuongeza;
Tuna furaha kufanya kazi na Zuku na tunaamini huu ni mwanzo tu wa ushirikiano wa kibiashara," alisema.
Televisheni ya Zuku inatoa uchaguziu mpana wa stesheni za burudani ikiwa ni pamoja na habari, michezo na sinema, majarida na muziki ikiwa imejumuisha chaneli za kimataifa kama BBC, MTV Base. Sentanta Sports, MGM Movies na nyinginezo ka gharama nafuu kwa ubora na kiwango cha hali ya juu.
 

Wednesday, December 19, 2012

Pacha wa Dotnata aja na mpya

Dometria Alphonce 'DD' katika pozi


MUIGIZAJI wa filamu ambaye ni pacha wa nyota wa fani hiyo na muziki, Husna Posh 'Dotnata', Dometria Alphonce 'DD', amepakua filamu mpya iitwayo 'Kua Uyaone' ambayo inasimulia mkasa wa kweli uliowahi kumpata katika maisha yake ya ndoa.
DD, aliiambia MICHARAZO juzi kuwa filamu hiyo imeshakamilika na wakati wowote itaachiwa hadharani, ikiwa imemshirikisha yeye mwenyewe na wasanii wengine waliopo katika kikundi chake cha sanaa cha DD Films kilichopo Ukonga.
Msanii huyo ambaye pia anajihusisha na nyimbo za Injili akishirikiana na pacha wake wakiandaa albamu kwa sasa, alisema hiyo itakuwa filamu yake ya kwanza kuitunga na kuiandaa mwenyewe baada ya kushirikishwa kazi kadhaa siku za nyuma.
'Nimekamilisha filamu yangu mpya iliyojikita kwenye simulizi la kweli ambao limewahi kunitokea katika maisha yangu ya ndoa, nimecheza na wasanii mbalimbali baadhi wakiwa ni askari waliopo katika kikundi changu cha sanaa cha DD Films," alisema.
Alisema filamu hiyo ni maalum kwa wanawake wote waliowahi kukutwa na misukosuko katika maisha ya ndoa zao, kwani mbali na mikasa ya kusisimua, lakini pia inatoa suluhu ya nini kifanyike mtu anapokumbwa na misukosuko kama hiyo.
Msanii huyo ambaye kama pacha wake naye ni mjasiriamali, alisema filamu hiyo ni yenye kuwatia nguvu na ujasiri wanawake wote wanaoteseka katika ndoa zao.
Aliongeza kuwa, wakati filamu hiyo ikiwa katika harakati ya kutolewa hadharani pia tayari anaendelea kuandaa kazi nyingine ambayo hakupenda kuitaja, ingawa alidai imeshaanza kufanyiwa 'shutingi'.

Mwisho

After Death sasa Kanumba Day

Jacklyne Wolper na 'watoto wa Kanumba'
Leah Richard 'Lamata'



FILAMU mpya ya kumuenzi aliyekuwa nyota wa zamani wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba iitwayo 'After Death', inatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki dunia Aprili 7.
Mmoja wa waratibu wa filamu hiyo, Leah Richard 'Lamata' alisema wameamua kuupeleka uzinduzi huo Aprili 7 mwakani, ili kuleta maana halisi ya kumuenzi nyota huyo aliyefariki ghafla nyumbani baada ya kutokea mzozo na mpenziwe.
Lamata, ambaye ndiye muongozaji wa filamu hiyo iliyotungwa na Jacklyne Wolper, alisema awali walipanga wafanye uzinduzi huo Februari, lakini wakaona isingeleta maana ilihali Kanumba alifariki mwezi Aprili na hivyo wamepeleka hadi tarehe hiyo.
"Uzinduzi wa filamu maalum ya kumuenzi Kanumba, iitwayo 'After Death' ambayo tulipanga kuizindua Februari sasa itazinduliwa Aprili 7, ambayo itakuwa siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki," alisema Lamata.
Lamata mmoja wa waongozaji mahiri wa filamu nchini, alisema anaamini siku hiyo itawapa fursa nzuri mashabiki wa filamu hasa waliomzimia Kanumba kumuenzi na kushuhudia baadhi ya kazi za mkali huyo.
Alisema After Death, iliyoigizwa na karibu wasanii wote waliowahi kufanya kazi na Kanumba, itawarejeshea kumbukumbu mashabiki wa filamu kutokana na msanii Philemon Lutwaza 'Uncle D' kucheza nafasi ya nyota huyo aliyefanana naye.
Wengine walioshiriki filamu hiyo ni Mayasa Mrisho, Jacklyne Wolper, Patcho Mwamba, Ben Blanco, Irene Paul, Ruth Suka 'Mainda' na watoto walioibuliwa na marehemu Kanumba kupitia 'This is It' na 'Uncle JJ' Patrick na Jennifa.

Mabingwa wa Afrika, Zambia kutua ncnhini leo




Kikosi cha timu ya taifa ya Zambia
MABINGWA wa kandanda barani Afrika, Zambia ‘Chipolopolo’ wakiwa na msafara wa watu 32 wanatarajiwa kuwasili nchini leo tayari kwa pambano lao la kujipima nguvu dhidi ya Tanzania, Taifa Stars.
Timu hiyo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 kamili jioni kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Lusaka.
Mbali ya wachezaji 24, msafara wa Zambia ambayo inakuja nchini kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars utakuwa na maofisa wengine wanane wakiwemo wa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Herve Renard aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini Gabon.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Christopher Katongo, Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na Francis Kasonde.
Given Singuluma, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga, Rainford Kalaba, Rodrick Kabwe, Salulani Phiri, Shadrack Malambo na Stoppila Sunzu.
Mechi dhidi ya Taifa Stars itafanyika Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Dar es Salaam tangu Desemba 12 mwaka huu chini ya Kocha Kim Poulsen kujiandaa kwa mechi hiyo.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Uhuru, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, kituo cha mafuta cha Ubungo OilCom na Dar Live Mbagala.
Pia tiketi zitauzwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) kwenye tamasha la Kilimanjaro Premium Lager kuhamasisha washabiki wa Taifa Stars litakalofanyika kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe.

Kikosi cha Zambia kilipokuwa kikishiriki michuano ya AFCON 2012

Maugo, Mbwana wawapania waganda


Kocha wa ngumi Pascal Mhagama kushoto anaemfua bondia Mbwana Matumla kwa ajili ya mpambano wake na David Chalanga wa kenya mpambano utakaochezwa Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mbwana Matumla kushoto akionesha ufundi wa kutupa masumbwi mbele ya kocha wake Pascal Mhagama kwa ajili ya mpambano wake na David Chalanga wa kenya mpambano utakaochezwa Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mada MAUGO AKILUKA KAMBA KWA AJILI YA MAANDALIZI YA MPAMBANO WAKE NAbondia Yiga Juma wa Uganda mpambano utakaofanyika Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Kocha wa Mchezo wa Masumbwi Said Chaku kushoto akimwelekeza bondia Mada Maugo jinsi ya kutupa Ngumi wakati wa mazoezi yake ya mwisho kwa ajili ya kumkabili bondia Yiga Juma wa Uganda mpambano utakaofanyika Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com
Bondia Mada Maugo kushoto akionesha umaili wa kutupa makonde na kocha wake Said Chaku wakati wa mazoezi yake ya mwisho kabla ya kupambana na bondia Yiga Juma wa Uganda Desemba 25 katika ukumbi wa Dar Live jijini Dar es salaam Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Kamote kurudiana na Mmalawi Des 29

Kamote akiwa na mataji anayoyashikilia kwa sasa

BONDIA mtanzania ambaye ni bingwa wa Dunia anayetambuliwa na World Boxing Forum, Allan Kamote anatarajiwa kwenda nchini Malawi ili kuzichapa na mwenyeji wake, Osgood Kayuni katika pambano litakalofanyika wiki ijayo.
Kamote aliyetwaa taji hilo la WBF Septemba 28 mwaka huu kwa kumpiga kwa TKO, Mmalawi Wellington Balakasi, atazichapa na Kayuni katika pambano la uzani wa Light raundi 10 litakalofanyika mjini Blantyre siku ya Desemba 29.
Hilo litakuwa pambano la marudiano baina ya mabondia hao kwani Februari mwaka huu walizichapa nchini huo na Kamote kupigwa kwa pointi, kitu "Natarajia kuondoka nchini siku ya Alhamisi kwenda Malawi kupigana na bondia aitwae Osgood Kayuni, ambayo nilipigana naye Februari mwaka huu na kunishinda kwa pointi, sidhani kama nitarudia tena makosa," alisema.
Kamote anayetokea mkoa wa Tanga, alisema anaendelea vema kujiandaa na pambano hilo na ana imani kubwa kurudia kile alichokifanya kwa Balakasi aliyempiga kwa TKO ya raundi ya nne na kutwaa ubingwa huo wa WBF.

Mwisho