MABINGWA wa zamani wa soka nchini, Coastal Union jna ilipanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichakaza JKT Ruvu kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaamm huku mshambuliaji wake nyota Nsa Job alikimbizwa hospitalini kwa kuvunjika mguu.
Magoli mawili kutoka kwa Daniel Lihanga na moja la penalti la Said Swedi, yaliifanya Coastal kufikisha pointi 19, moja juu ya Azam iliyolala 3-1 mikononi mwa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi. Azam wana mechi moja mkononi, hata hivyo.
Coastal, mabingwa wa mwaka 1988, waliorejea kwenye ligi kuu msimu uliopita, sasa wako ponti tatu nyuma ya watetezi Simba wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 22 baada ya mechi 10.
Yanga, ambayo juzi ilishinda 1-0 ugenini dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ni ya pili ikiwa na pointi 20.
Katika mchezo huo, nyota Nsa Job, alikimbizwa hospitalini baada ya kugongana na kipa wa JKT Ruvu na kuelezwa kuwa alikuwa amevunjika mguu wake wa kushoto.
Kitu cha kushangaza katika uwanja huo hakukuwa na gari la wagonjwa hali iliyowafanya mashabiki waliofurika uwanjani hapo kushangazwa na hali hiyo na kuitupia lawama TFF kwa kushindwa kuchukua tahadhari.
Mchezaji huyo alikimbizwa hospitali ya Muhimbili na taarifa zilizotufikia inasema anaendelea vema baada ya kuaptiwa huduma ya kutosha.
Mjini Mwanza, wenyeji Toto African walisawazisha katika dakika za lala salama la kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa Jumatano ambapo mabingwa Simba watakuwa wageni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, Yanga watawakabili JKT Mgambo kwenye Uwanja wa Taifa, Toto Africans watawaalika Kagera Sugar (CCM Kirumba), JKT Ruvu dhidi ya African Lyon (Azam Complex), JKT Oljoro watakipiga dhidi ya Mtibwa Sugar (Sheikh Amri Abeid, Arusha) na Ruvu Shootings watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment