Mwenyekiti mpya wa CHANETA, Anna Kibira |
KAMATI ya utendaji ya chama cha netiboli nchini (CHANETA) inatarajia kukutana Mei 31 kwa ajili ya kujadili uteuzi wa katibu mkuu wa muda atakayekaimu nafasi hiyo kwa muda wa miezi sita.
Kwa mujibu wa katiba mpya ya CHANETA ambayo ilitumika katika uchaguzi mkuu, nafasi ya katibu mkuu ni ya kuajiriwa na si kuchaguliwa na wajumbe kama ilivyokuwa awali.
Mwenyekiti mpya wa CHANETA, Anna Kibira alisema kwavile chama hicho hakina fedha wameamua kukukutana kujadili suala la uteuzi wa katibu wa muda ili kuziba nafasi hiyo.
"Hatuna chanzo chochote cha kutuingizia fedha hivyo ni vigumu kuajiri katibu mkuu kwa sasa, ila tutakapojiweka sawa tutamuajiri," alisema Kibira.
Alisema katiba yao inaruhusu kuteua katibu wa muda kwa ajili ya kufanya kazi ndani ya chama kwa muda uliotajwa.
Kibira alisema katika kikao hicho pia watajadili mambo mbalimbali yanayohusu chama ikiwamo kalenda ya mwaka ambayo itaonyesha ratiba zote za michuano yote pamoja na ushiriki wa timu ya taifa ya netiboli (Taifa Queens) katika mashindano ya netiboli ya kimataifa.
Wakati huo huo, Kibira alisema suala la upatikanaji wa ofisi kwa ajili ya chama hicho ambacho hadi sasa hakina ofisi, wameomba Baraza la Michezo la Taifa (BMT), liwasaidie ofisi ya muda huku wakiendelea kufanya mchakato wa kutafuta ofisi yao binafsi.
No comments:
Post a Comment