Rais wa TFF, Leodger Tenga |
Mkutano wa dharura wa Kamati ya Utendaji ya TFF umeitishwa ili kutekeleza maagizo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambalo wiki iliyopita liliagiza mchakato wa uchaguzi huo uanze upya baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro zilizotokana na kutokuwapo kwa kamati za kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa katika kikao cha leo cha kamati ya utendaji wataamua tarehe ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Dharura wa TFF ambao utakuwa na jukumu la kupitisha marekebisho ya katiba (kuunda Kamati ya Maadili ya TFF).
Wambura alisema kuwa kikao cha leo pia kitapanga utaratibu mzima wa namna mchakato wa uchaguzi utakavyokuwa pamoja na kuamua tarehe rasmi ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya wagombea kuliomba shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka duniani kuingilia kati mchakato wa uchaguzi huo.
Wagombea wawili, Jamal Malinzi anayewania nafasi ya urais wa TFF na Michael Wambura anayeutaka umakamu wa rais ndiwo walioiomba FIFA iingilie kati mchakato wa uchaguzi huo wakidai kutotendewa haki na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF iliyowaengua katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hawakukidhi matakwa ya kanuni za uchaguzi na katiba ya TFF.
Kikao cha leo hakitaishia kutaja tarehe ya mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya marekebisho ya katiba pekee, bali kitazungumza na kupanga utaratibu mzima utakaotumika katika uchaguzi huo, habari za ndani zilisema.
TFF imeiomba FIFA iwapatie fedha kwa ajili ya mkutano mkuu wa dharura wa marekebisho ya katiba ya TFF.
Uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na mwenyekiti Idd Mtiginjola kuwaengua baadhi ya wagombea nafasi za uongozi wa TFF na bodi ya PTL mwanzoni mwa mwaka huu uliibua gumzo kubwa nchini, hali iliyosababisha serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuingilia kati suala hilo huku ikiikataa katiba mpya ya shirikisho hilo iliyofanyia marekebisho kwa njia ya waraka Desemba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment