Nyota wa Azam watakaokosekana katika mechi hiyo ni pamoja na mshambuliaji hatari, John Bocco na beki Hajji Nuhu, ambao ni majeruhi. Wengine ni chipukizi Ismail Lugambo na Farid Musa.
Ofisa Habari wa Azam, Jaffari Iddi alisema mjini Dar es Salaam kuwa, Bocco bado majeruhi wakati Nuhu aliumia goti juzi baada ya kuanguka ghafla wakati wa mazoezi yaliyofanyika Chamazi.
Jaffari alisema Lugambo alivunjika mguu mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Azam na Ashanti wakati Farid amekuwa akisumbuliwa na majeraha mara kwa mara na itabidi afanyiwe vipimo vikubwa.
"Farid itabidi afanyiwe vipimo vya MRY kwenye mgongo ili tujue sababu ya kuumia mara kwa mara na Bocco bado goti lake halijawa sawa. Alipewa mapumziko ya wiki mbili na tayari ameshamaliza wiki moja, hivyo hatacheza mchezo huo," alisema Jaffari.
Pamoja na kuwakosa nyota hao, Jaffari alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Ferroviario na kusisitiza kuwa, wamepania kuweka rekodi ya kufika mbali zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana.
Aliongeza kuwa, wamefurahi kupata ruhusa kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya kucheza mechi hiyo kwenye uwanja wa Chamazi kwa vile wachezaji wao wameuzoea na watautumia vizuri kupata ushindi.
Msimu uliopita, Azam iliiwakikisha Tanzania katika mashindano hayo baada ya kumaliza ligi kuu ikiwa mshindi wa pili, lakini ilitolewa raundi ya tatu. Iwapo Azam itaitoa Ferroviario, itamenyana na mshindi kati ya St. Michel ya Shelisheli na ASSM Elgeco Plus ya Madagacar
No comments:
Post a Comment