STRIKA
USILIKOSE
Friday, February 7, 2014
Rais TFF aeleza mikakati siku 100 ofisini
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na changamoto zilizopo.
Alisema muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa kazi kuwa ni;
Ujenzi wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu kupanda daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu na makocha, utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa waamuzi.
Ametoa mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment