STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 8, 2014

IDFA yaitakia kila la heri Yanga kesho Misri

Yanga yenye kibarua kizito kesho mjini Alexandria
UONGOZI wa Chama cha Sokla Wilaya ya Ilala (IDFA) umeitakia kila la heri na kuwaomba watanzania kuiombea dua njema wawakilishi pekee wa michuano ya kimataifa, Yanga katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Yanga wataumana na wenyeji wao katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Al Ahly ndiyo watetezi wake, ili kuamua hatma ya  kuvuka hatua ya 32 Bora kutinga 16 Bora ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya klabu, mechi ikichezwa mji wa Alexandria badala ya Cairo.
Kwa kutambua Yanga ina kibarua kizito mbele ya Ahly hiyo kesho, uongozi wa IDFA ambao ni walezi wa klabu za Ilala ikiwamo Simba na Yanga, wamewaomba watanzania kuiombea dua njema timu hiyo na wao wenyewe (IDFA)  wakisema wanaitakia kila la heri kuweza kuwang'oa Wamisri.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Daud Kanuti aliiambia MICHARAZO kuwa, IDFA ipo katika maombi kuiombea Yanga ifanye vyema na kuendelea kupeperusha bendera ya taifa na kuwaomba wadau wengine wa soka bila kujali itikadi zao kuwaombea dua njema wawakilishi hao wavuke hatua hiyo.
Kanuti alisema kufanya vyema kwa Yanga katika mechi hiyo na michuano hiyo ya Mabingwa, ni sifa kwa Tanzania na kuongeza, anaamini wachezaji wa Yanga wakicheza 'jihad' na tahadhari kubwa dhidi ya wapinzani wao wanaweza kurejea kilichofanywa na Simba.
Kanuti alisema anaamini wachezaji  wameandaliwa kisaikolojia ili kuhimili vitimbi wanavyoweza kukutana navyo Misri kama ilivyo kawaida ya mechi za timu za kiarabu wanapokuwa uwanja wa nyumbani.
"IDFA tunaitakia kila la heri na kuiombea dua njema ili ifanye vyema kwenye mechi yake ya Jumapili, chama tumefurahishwa na ilichokifanya katika mchezo wa kwanza na tunaamini watarejea tena ugenini," alisema.
"Wana nafasi ya kurejea ilichofanywa na watani zao walipoing'oa Zamalek katika ardhi yao mwaka 2003, ila ni muhimu wachezaji wakaandaliwa kupambana na kuweka akili zao katika pambano hilo ili kuivusha Yanga katika hatua hiyo," aliongeza Kanuni.
Kanuti alisema IDFA inatambua mchezo huo wa kesho utakuwa mgumu kwa vile Al Ahly itakuwa nyumbani na rekodi zinaonyesha timu za kiarabu huwa wagumu kufungwa kwao, lakini Yanga ikipambana itawaondosha watetezi hao kama ilivyofanya Simba kwa Zamalek mwaka 2003.
Katika mwaka huo Simba ilishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Zamalek pia ya Misri waliokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa mwaka huo kisha kwenda kukubali kipigo kama hicho ugenini mjini Cairo na kupigiana penati na Simba kuibuka kidedea kuingia hatua ya makundi.
Iwapo Yanga itafanikiwa kuing'oa Ahly huenda ikakutana kwenye raundi inayofuata kati ya timu ya Berekum Chelsea ya Ghana au Ahly Benghazi ya Libya ambazo zilitoka sare ya 1-1 katika mechi yao ya awali na zinatarajiwa kurudiana leo.

No comments:

Post a Comment