STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 8, 2014

Mbeya City yaishusha Yanga, Ruvu yazinduka


Mbeya City iliyotakata nyumbani
Ruvu Shooting ilizinduka
WAKATI watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wakiwa ugenini kujiandaa na mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, nyumbani wameenguliwa kutoka nafasi ya pili ya Ligi Kuu baada ya Mbeya City kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Rhino Rangers.
Mbeya City ikiwa uwanja wa nyumbani wa Sokoine, jijini Mbeya ilipata ushindi huo na kufikisha jumla ya pointi 39 na kuwa nyuma ya pointi moja dhidi ya Azam wanaoongoza msimamo ikiwa na pointi 40 licha ya kutofautiana michezo iliyocheza.
Mabao ya washindi hao waliwekwa kimiani na Saada Kipanga aliyefunga mabao mawili akiiangamiza timu yake ya zamani aliyoipandisha daraja ambayo inaendelea kukaa mkiani kwa msimamo wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni kabla msimu haujamalizika.
Kabla ya Kipanga kufunga mabao hayo, beki wa Mbeya City Yohana Morris alijifunga katika dakika ya pili ya mchezo huo katika harakati za kuokoa shambulizi kali la Rhino Rangers.
Kipanga alisawazisha dakika ya 8 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 24 na baadaye Deusi kaseke kufunga bao la tatu dakika ya 35.
Kipindi cha pili hakukuwa na jipya zaidi ya matukio ya kibabe yanayodaiwa kufanywa na wachezaji wa Rhino na kocha wao msaidizi, Tumaini Shija kupewa kadi nyekundu kwa kumtolea matusi mwamuzi Godfrey Tumaini.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo 'wazee wa wiki' Ruvu Shooting ikiwa uwanja wa nyumbani Mabatini-Mlandizi, ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya maafande wenzao wa Oljoro JKT na kuwafanya wakwee hadi nafasi ya saba ya msimamo ikiwa na pointi 28.
Bao lililoipa ushindi Ruvu ambayo katika mechi zake mbili zilizopita ilizipoteza kwa Simba na Yanga na kufungwa mabao 10-2, liliwekwa kimiani na Ayoub Kitala katika dakika ya 65.
Nao mabingwa wa zamani wa soka nchini Coastal Union ya Tanga ilishindwa kutamba baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana na Ashanti Utd kwenye uwanja wa Mkwakwani.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi kati ya Prisons-Mbeya itakayoikaribisha Simba kwenye uwanja wa Sokoine na jijini Dar kwenye uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu iliyokea Kagera ilipoenda kukumbana na kipigo kwa Kagera Sugar itaumana na Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment