STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 31, 2014

Simba, Yanga katika mtihani mgumu kesho ugenini

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgMErmaFBzyADXkrz5jimZGD59Rm1nrIi0sRY-xVZ45F1q0-vhzjQLKXe76tJrIwp873fDO1tasiR2EI2nDFdaUionEjaI7xp-UPLbEKMQcVnuvNmAdmKDq-ANMsSU3bMXsc7xRzkbxomQ/s1600/DSC_0007.JPG
Jamani msiniangushe kwa Mtibwa si mmesikia wanene walivyosema? Kocha Patrick Phiri akiteta na wachezaji wake katika moja ya mazoezi ya timu hiyo
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh_wsXksNlhu6sWaVTeRTC_OzK51cPXSB8Peeswe9zSaxYwrrk_-RnovonjYn4Y0d-iJX8cD6X0iEoGJDINtBTAVtW-IIpeBx1ePGLvBe07YW8PUx8bcf__5kB8zEXsebp4WK8c57Xm0CSw/s1600/DSC_6109.JPG
Vita ya Kagera na Yanga kama hii itakuwa kesho Kaitaba
http://www.hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2014/09/azam-web_0.jpg
Azam wameifuata Ndanda wakiugulia kipigoi cha JKT Ruvu. Watapona Nangwanda Sijaona?
KOCHA Patrick Phiri wa Simba kesho anatarajiwa kuanza kibarua chake cha mechi mbili alizopewa kushinda kabla ya kurejeshwa kwao watakapovaana na vinara, Mtibwa Sugar.
Pambano hilo litakalochezwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro ni miongoni mwa mechi sita zitakazochezwa siku ya kesho kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba kupitia uongozi wake ulitangaza kumpa kocha wao mechi mbili dhidi ya Mtibwa na ile itakayofuata wikiendi ijayo dhidi ya Ruvu Shooting kama kipimo cha mwisho cha kumvumilia kutokana na matokeo mabaya inayopata timu yao msimu huu.
Katika mechi tano za awali Simba imeambulia sare huku relodi ikionyesha haijaonja ushindi wa aina yoyote katika jumla ya mechi 11 za Ligi tangu walipoiotea Ruvu Shooting kwa kuilaza mabao 3-2.
Baadhoi ya wadau wa soka wamekuwa wakiushutumu uongozi wa Simba kwa maamuzi hayo ya kumbana Phiri wakati ikijua hakuhusika na usajili wa wachezaji waliopo kikosi kwa sasa Msimbazi.
Hata hivyo Mtibwa kupitia Msemaji wake, Thobias KIfaru amesema kuwa Simba wasitarajie mteremko kwao kwani wamejipanga kuwalipua ili kurahisisha kazi ya kumtimua kocha wao.
Ukiacha mechi hiyo, kesho pia kutakuwa na mechi ya kukata na shoka kati ya Yanga itakayokuwa wageni wa Kagera Sugar uwanja wa Kaitaba, huku watetezi Azam wakiwafuata Ndanda Fc iliyomtimua kocha wao, Dennis Kitambi.
Mechi nyingine za kesho ni  pamoja na maafande wa JKT Ruvu watakaowakaribisha maafande wa Polisi Moro ambao wanauguza kipigo cha 1-0 walichopewa na Ruvu Shooting wikiendi iliyopita.
Pia kesdho kutakuwa na pambano kati ya Coastal Union watakaokuwa wenyeji wa Ruvu Shooting na Stand United kuikaribisha PRisons-Mbeya na siku ya Jujmapili kutakuwa na pambano moja tu kati ya Mgambo JKT itakayoialika Mbeya City uwanja wa Mkwakwani.
Yanga ambayo inatokea Shinyanga ilipoilipua Stand united kwa mabao 3-0 tayari ipo mjini Kagera tayari kwa pambano hilo na msemaji wao, Baraka Kizuguto ameweka bayana kwamba wamezifuata pointi tatu Kaitaba.
Katika mechi yao ya msimu uliopita kwenye uwanja huo Yanga iliwatambia wenyeji wao kwa bao 2-1, jambo ambalo Kizuguto anaamini kitaendelezwa tena kesho.
Mpaka sasa Ligi hiyo inaoongozwa na Mtibwa yenye pointi 13 ikifuatiwa na watetezi Azam wenye pointi 10 sawa na Yanga ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa kisha Coastal Union, JKT Ruvu na Ruvu Shootying, Simba a.k.a Wazee wa Sare wenyewe wanashika nafasi ya 10 wakiwa  na pointi 5.

Nguvu ya Umma yamng'oa Rais Compaore

http://api.ning.com/files/TgHj0KqUN*sX9e*LQOoFNFdBmjR8AKGdAHVfrhLq-iDc3HuWmmMQ4Q1Jdxmu6-BA0j*RTstgln8BgRdlbBGnikzEAvgB0z8g/traore.jpg
Kiongozi wa Mpito wa Burkina Faso
http://www.dw.de/image/0,,18025612_303,00.jpg
Rais aliyeondoka madarakani kwa nguvu ya umma
NGUVU ya umma nchini Burkina Faso zimemng'oa Rais Blaise Compaore. 
Taarifa zinasema Rais huyo amejiuzulu katika kiti hicho licha ya msimamo wake wa awali kwamba asingejiuzulu kama shinikizo la wapinzani. Maandamano ya siku kadhaa ya kupinga mpango wa rais huyo kujiongezea muhula wa madarakani yamesababisha vifo vya watu kadhaa na inaelezwa kuwa Rais Compaore ametoweka na haijulikani alipo.
Kwa sasa nafasi yake inashikiliwa na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Honore Traore ili kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Hatua bya Rais huyo anayedaiwa kuiongoza Burkina Faso kwa Mkono wa Chuma imekuja baaada ya vurugu zilizosababisha uchomaji moto wa Bunge la nchi hiyo na ofisi za chama tawala.

'Lionel Messi ni zaidi ya Cristiano Ronaldo'

http://gms.cachefly.net/images/9332f7310262fe4012a93d5aa2ec54f2/650.jpgKOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Fabio Capello amedai kuwa nyota wa Barcelona Lionel Messi ana kipaji zaidi ya mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo. 
Messi, 27 anatarajiwa kuwa mfungaji mwenye mabao mengi La Liga kama akifunga mabao mawili katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Celta Vigo hapo kesho. 
Ronaldo mwenye umri wa miaka 29 anashikilia nafasi ya 10 katika orodha hiyo. Capello amesema Ronaldo ni mchezaji mwenye nguvu mbinu nzuri lakini huwezi kulinganisha ujuzi wa kiufundi halisi alionao Messi. 
Messi ameshafunga mabao 250 katika mechi 284 alizoichezea Barcelona akiwa amebakisha bao moja kufikia rekodi ya nyota wa zamani wa Atletico Madrid Telmo Zarra aliyoweka kati ya mwaka 1940 na 1950.

Steven Gerrard kuhama Liverpool iwapo...

http://img.thesun.co.uk/aidemitlum/archive/01567/gerrards_1567523a.jpg
Steven Gerrard
NAHODHA wa klabu ya Liverpool, Steven Gerrard amebainisha kuwa atajiunga na klabu nyingine kama timu hiyo ikishindwa kumpatia mkataba mpya. 
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye alijiunga katika shule ya soka ya Liverpool akiwa na umri wa miaka tisa, ameondoa uwezekano wa kustaafu soka wkati mkataba wake utakapomalizika Mei mwaka huu. 
Kiungo huyo amesema hana mpango wa kutundika daruga majira ya kiangazi kwani amepanga kuendelea kucheza soka zaidi. 
Gerrard aliendelea kudai kuwa kwasasa anasubiria kuona kama itakuwa ni Liverpool au mahali pengine, huo utakuwa uamuzi wa klabu hiyo. 
Nahodha huyo wa zamani wa Uingereza ambaye alitangaza kustaafu soka la kimataifa Julai mwaka huu ameichezea Liverpool karibu mechi 700, huku akicheza na washambuliaji mahiri wa zamani Robbie Fowler na Michael Owen.

Dk Ndumbaro amtangazia 'vita' Malinzi

http://api.ning.com/files/E2q56SVxnZdQOwcR6HaKivVPSGgbEBhknIlVqnDS5NGE1d3uRzai0weL*GGoN62tttqwLdV3ITGWsWmHb7LWq2escwr5Sbk8/3.jpg
DK Damas Ndumbaro
MWANASHERIA Dk. Damas Ndumbaro, amefichua kuwa amekata rufaa kupinga adhabu ya miaka 7 aliyopewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku akisisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi zake za kuwawakilisha wadau wa soka watakaohitaji huduma yake ya uwakili.
Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Ndumbaro alisema kuwa TFF na Kamati zake hazina mamlaka ya kumfungia kufanya kazi za uwakili, isipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na serikali.
Ndumbaro alisema kuwa anashangaa kuona amehukumiwa na Kamati ya Nidhamu kwa kosa la maadili na kuongeza kwamba kamati hiyo haikupaswa kusikiliza tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
Alisema kuwa adhabu hiyo aliyopewa ni dalili za wazi za 'chuki' dhidi yake kwa sababu yeye alichokizungumza ilikuwa ni maamuzi ya klabu 12 za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambazo zilikubaliana na kumteua yeye kupitia Kampuni yake ya Uwakili ya Maleta & Ndumbaro ya jijini.
"Sikuzungumza kwa niaba yangu, nilikuwa na ridhaa ya klabu 12, isipokuwa Stand United na Coastal Union, Kamati hii inatumiwa na Jamal Malinzi, ndio kamati iliyoipa ushindi Stand United kupanda Ligi Kuu," alisema Ndumbaro.
Wakili huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba alisema kuwa alianza kuonekana ni adui mara baada ya kukataa kushiriki katika ufujaji wa fedha ambapo kwa vipindi vitatu tofauti alikataa kusaini hundi za fedha ambazo TFF iliomba kutoka kwenye Bodi ya Ligi Kuu (TPL).
Alisema kwamba kwa sasa shirikisho hilo linakabiliwa na ukata baada ya kutumia kiasi cha Dola za Marekani 696,823 bila ya kupata kibali cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao wamezitoa kwa ajili ya udhamini wake wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
Mbali na matumizi hayo, pia Jamal Malinzi anadaiwa kujilipa binafsi Dola za Marekani 159,140 ndio maana sasa wanaamua kufidia fedha hizo katika gharama nyingine ikiwamo makato ya Sh.1,000 kwa kila tiketi," alisema Ndumbaro.
Aliongeza kuwa anashangaa kuona TFF inaendelea kukata Sh. 1,000 katika kila tiketi za mashabiki wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara na kutaja kiasi kilichokatwa hadi kufikia jana ni Sh. milioni 193.2 zilizotokana na mashabiki 193,257 walioingia viwanjani kushuhudia michezo ya ligi iliyoanza Septemba 20 mwaka huu.
Alisema pia anashangaa kuona rufaa yake aliyokata tangu Oktoba 21 mwaka huu haijapangiwa siku ya kusikilizwa lakini kikao cha Kamati ya Nidhamu kilichokutana kumjadili kilichukua siku mbili.
Aliongeza kuwa leo Oktoba 31 mwaka huu siku ya 10 na hakuna dalili za kusikilizwa, tutaendelea kuhesabu,  mambo mengi yako katika rufaa.
Alisema kwamba yeye hajawahi kutoa siri za shirikisho na kueleza kuwa kanuni za ligi na mikataba inayoingiwa si siri.
Taarifa rasmi ya Dk Ndamburo iko hivi:
31 Oktoba 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAMPUNI ya Mawakili ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ambayo inawakilisha vilabu 13 vya LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA, inapenda kutoa tamko kwa umma kama ifuatavyo:
1. Kampuni ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, iliteuliwa na vilabu 13 vya LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA, kwa maandishi, ili kuwawakilisha na kuwatetea katika kudai haki zao ambazo tayari SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF) liliamua kukata fedha za udhamini na viingilio vya mechi pasipo kuwashirikisha. Dk. Damas Daniel Ndumbaro, wakili mwandamizi, ndiye aliyekabidhiwa file hilo kwa mujibu wa utaratibu wa ofisi yetu.
2. Kwamba, tarehe MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, kupitia wakili wake mwandamizi, Dk. Damas Daniel Ndumbaro, iliandika barua ya madai (Demand Notice) TFF na kuongea na waandishi wa habari.
3. Kwamba tarehe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Juma Nkamia (MB) aliitisha mkutano kati ya TFF (ambayo iliwakilishwa na Wilfred Kidau-Mjumbe Kamati ya Utendaji, na Selestine Mwesiga, Katibu Mkuu), Bodi ya Ligi, Vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania na Dk. Damas Daniel Ndumbaro (kama wakili wa vilabu). Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mh. Juma Nkamia alitoa fursa kwa TFF, Bodi ya Ligi, na Wakili wa vilabu kutoa maelezo yao na hatimaye  Mh. Juma Nkamia alitoa maelekezo kama ifuatavyo:
i.  Jamal Malinzi sio Rais wa Nchi, na aliwaagiza wawakilishi wa TFF wafikishe ujumbe huo kwa Bw. Jamal Malinzi.
ii.  Makato ya Tshs. 1000/= kwa kila tiketi ni wizi wa mchana.
iii. TFF isitishe makato ya 5% na Tshs. 1000 kwa kila tiketi mpaka watakapoongea na kukubaliana na vilabu
4. Baadaya hapo, MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ilikutana na vilabu ambayo vilikuwepo siku hiyo na kukubaliana kuwa sasa tusibiri majadiliano na TFF na kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ikiongozwa na Dk. Ndumbaro iandae mapendekezo ili yajadiliwe na mkutano mkuu wa vilabu.
5. Kwamba tarehe 11 Oktoba 2014 TFF ilifanya mkutano wa Kamati ya Utendaji na kutoa tamko kuwa kumekuwa na taarifa za upotoshaji kuhusu kanuni za ligi kuu na kwamba Sekretariati ya TFF imefungua mashtaka dhidi ya Dk. Ndumbaro ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Ligi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba.
6. Kwamba Kamati ya Utendaji ya TFF iliendelea kusema kuwa Kutokana na madai ya klabu kuhusu vipengele kadhaa vya Kanuni za Ligi Kuu 2014/15, Kamati ya Utendaji imepanga kukutana na viongozi wa klabu za Ligi Kuu siku ya Jumamosi, Oktoba 18 mwaka huu ili kuwasikiliza na kushauriana kuhusu changamoto za kikanuni na uendeshaji wa mashindano kwa ujumla na kwamba.
7. TFF imefanya kosa kumshitaki Dk. Ndumbaro kwa kofia ya Mjumbe wa Bodi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Simba kwasababu barua toka MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, barua za vilabu 13 na taarifa kwa vyombo vya habari ilikuwa bayana kuwa Dk. Ndumbaro anawakilisha vilabu vya ligi kuu kama wakili toka kampuni ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES na wala sio mwakilishi wa Bodi au Mwenyekiti wa uchaguzi wa Simba kwasababu hakukuwa na uchaguzi wa Simba.
8. Kwamba TFF inakiri kuwa klabu za Ligi kuu zinapaswa kukutana na TFF kujadili kasoro za Kanuni za Ligi kuu. Hapa TFF inakiri kuwa haikukutana na vilabu katika mchakato wa kutunga kanuni hizi na kwamba kanuni hizo zinakasoro. Ifahamike kwamba hayo ndio madai ambayo vilabu kupitia MALETA & NDUMBARO ADVOCATES iliyapeleka TFF kwa maandishi.
9. Tarehe 7 Oktoba 2014 TFF iliepeleka Mshtaka katika Kamati ya Nidhamu dhidi ya Dk. Ndumbaro. Kamati ya Nidhamu ilipanga kusikiliza Mashtaka hayo tare 09 / 10 / 2014 saa 08: oo mchana, yaani siku mbili tu baadaya ya kuwasilishwa katika kamati ya nidhamu. Mashitaka hayo yalijaa ubabaishaji na chuki binafsi dhidi ya wakili wa vilabu 13 vya Ligi Kuu.
10. Kwamba TFF ililazimisha kusikiliza mashtaka hayo kwa haraka na dharura ya ajabu pasipo kuwepo Dk. Ndumbaro ambaye alitoa taarifa ya maandishi kuwa atakuwa safarini Nchini Marekani kikazi, kwa barua ya tarehe  8th October 2014.
11. Kwamba Kamati ya Nidhamu ya TFF ilitoa maamuzi ya kumfungia Dk. Ndumbaro asijihusishe na Soka kwa kipindi cha miaka saba pasipo kutoa sababu za msingi za kufanya hivyo wala kutoa nakala ya hukumu hiyo.
12. Kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES kwa niaba ya vilabu vya Ligi kuu inapinga adhabu hiyo ya uonevu kwa misingi ifuatayo:
i.  Kamati ya nidhamu ya TFF haina mamlaka ya kisheria ya kushughulikia suala hili. (ARTICLE 2, 3,76 and 77 of TFF Disciplinary  Code)
ii. Kamati ya nidhamu ya TFF ilikosea kuamua suala hili bila kutoa haki ya msingi ya kuisikiliza MALETA & NDUMBARO ADVOCATES na Dk. Damas Daniel Ndumbaro
iii. Hakuna Chombo chochote cha TFF chenye mamlaka ya kumzuia au kumfungia Wakili wa kujitegemea kuwawakilisha wateja wake.
13. MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inaandaa kesi ya madai dhidi ya TFF kwa kuizuia isifanye biashara yake halali.
14. MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inapenda kuwajulisha wadau wote kuwa kupinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF sio kosa. Ikumbukwe kuwa JAMAL MALINZI aliwahi kupinga maamuzi ya FIFA, CAF na TFF kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, kwa njia ya Circular Resolution, ili kuunda Kamati za Rufaa ya Uchaguzi, Kamati ya Maadili na Club Lincensing. Lakini leo Jamal Malinzi hataki kupingwa huyu ni dikteta.
15. Kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inaandaa mashtaka dhidi ya Uongozi wa TFF, katika mambo yafuatayo:
i.  Ubadhirifu wa US$ 200,000 fedha za TBL udhamini wa Taifa Stars
ii. Kupinga Maamuzi ya FIFA kurejea Karume ( Haya yalikuwa mapendekezo haikuwa amri)
iii.Kufanya matumizi na manunuzi bila kibali cha kamati ya fedha ambayo ndiyo kamati ya manunuzi ya TFF kwa mujibu wa kanuni za manunuzi za TFF, manunuzi yaliyofanyika yanahusiana na Vifaa vya michezo wakati wa maboresho ya Taifa stars, Tiketi za ndege za Taifa Stars, timu ya wanawake na za vijana katika michezo yake na hotel za kambi ya timu ya Taifa ambapo hakukuwa na tenda zilizotangazwa wala ushindanishwaji wa aina yoyote jambo linaloashiria matumizi mabaya ya madaraka na fedha na kwa kuwa Rais ndiye msimamizi wa shughuli za sekretariet kikatiba jambo hili linakuwa pamoja na mengine ni suala la kimaadili kwa sheria za mpira.
16.  Kwamba  MALETA& NDUMBARO ADVOCATES inaandaa mashtaka dhidi ya Jamal Malinzi kwa Kupinga Maamuzi ya FIFA, CAF na TFF ili kufanya marekebisho ya Katiba mwaka 2013.
17. Tarehe  21 Oktoba 2014, Dk. Damas Daniel Ndumbaro alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya TFF lakini mpaka sasa Kamati ya Rufaa ya Nidhamu TFF haijasema lina inakaa. Tunatarajia kuwa haraka na dharura iliyotumika katika kuamua shauri katika kamati ya nidhamu itatumika pia kuamua shauri katika rufaa. Leo ni siku ya 10 toka rufaa ikatwe lakini bado kimya wakati ilichukua siku 2 tu kusikiliza kesi ya msingi.
KWAHIYO Dk. Damas Daniel Ndumbaro wa MALETA & NDUMBARO ADVOCATES kwa naiba ya wateja wetu tunasema kuwa:
a. Tutaendelea na kuwawakilisha wateja wetu kwa uadilifu wa hali ya juu.
b. Kwamba madai yote tuliyoyasema katika barua ya awali dhidi ya TFF ikiwemo madai yanayohusiana na Mkutano Mkuu yapo pale pale.
c.  Tumekata Rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya nidhamu ya TFF kuanzia tarehe 21 Okotba 2014
d. Tunaandaa mashtaka dhidi ya Uongozi wa TFF kwa ubadhirifu wa fedha za umma
e. Tunaandaa mashtaka dhidi ya TFF kwa kosa la kupinga agizo la FIFA kurejea Karume
f.  Tunaandaa Mashtaka dhidi ya Jamal Malinzi kwa kosa la kupinga Maamuzi ya TFF, CAF na FIFA katika mabadiliko ya Katiba ya TFF mwaka
2013.
Wako
Dk. Damas Daniel Ndumbaro (PhD)
For: Maleta & Ndumbaro Advocates
www.maletandumbaroadvocates.com
 

Nakala: i. Vilabu 13 vya Ligi Kuu
             ii. Mh. Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
                                      .............
                                  31 Oct 2014

Polisi yakana kunaswa kwa wauaji wa Meyiwa

http://citizen.co.za/wp-content/uploads/sites/18/2013/10/TL_1081310-602x400.jpgJESHI la Polisi nchini Afrika Kusini wamekanusha taarifa kuwa watuhumiwa wa mauaji ya nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, Senzo Meyiwa wamekamatwa katika daraja la Beit lililopo katika mkapa na Zimbabwe. 
Msemaji wa jeshi hilo Neville Malila amesema tetesi hizo kuwa kuna mtu amekamatwa sio za kweli ila uchunguzi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea. 
Awali kulizuka taarifa kuwa mtuhumiwa mmojawapo wa katika mauaji hayo alikamatwa katika daraja hilo lililopo mpakani na Zimbabwe na kuwa alipelekwa Vosloorus mahali ambako alitenda kosa hilo. 
Meyiwa aliuawa siku ya Jumapili kwa kupigwa risasi wakati akiwa katika harakati za kumuokoa mpenzi wake Kelly Khumalo nyumbani kwake wakati majambazi walipovamia na kutaka kuwapora vitu vyao vya thamani.
Kipa na nahodha huyo wa timu ya Orlando Pirates na Bafana Bafana anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumapili.

Sunday Kayuni kuwanoa Makocha 35 wa CAF

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgOJYbBm9mZVhg2ZTJjKq2Q3eAH1n18JM5O-VsglyJ39ous_ViZ7YapGzBkgXSgrI48uNvTR50pMQGK-amClKipv3k7kjxNfbqNQ-12n5HB-4tKvx1owRsfE2ekXuwzuKJipnlsHXQ8QyRt/s1600/kayuni.JPGMAKOCHA 35 wameteuliwa kushiriki kozi ya ukocha ya Leseni C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika mjini Morogoro kuanzia Novemba 5 hadi 19 mwaka huu.
Kozi hiyo itaendeshwa na Mkufunzi wa CAF, Sunday Kayuni na itafanyikia Mchikichini College ambapo washiriki wote wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya ukocha vya ngazi ya Kati (Intermediate) pamoja na vyeti vya kitaaluma vya elimu ya sekondari (academic).
Washiriki wa kozi hiyo ni Abdulmaliki Nemes (Airport FC), Ahmed Haule (Kilimanjaro Talented Youth Sports Centre), Ally Jangalu (Moro Kids), Amri Saidi (Mwadui FC) na Athuman Kambi (Morogoro).

Wengine ni Charles Mwakambaya (Burkina Faso FC), Damian Mussa (Alliance One) na Daudi Sichinga (Kasulu United), Denis Maneva (Shule ya Msingi Logo), Edgar Juvenary (JUT- Mlale) na Hamisi Mangolosho (Shule ya Msingi Mtimbwilimbwili).
Pia wamo Henry Ngondo (Chalinze Academy), Issa Hamisi (Polisi Kilimanjaro), Jumanne Chale (Dar es Salaam), Kizito Mbano (Masasi Alliance), Martin Saanya (Magereza Morogoro) na Masoud Gumbwa (Sokoine University Academy).
Wengine ni Mbwana Makata (Oljoro JKT), Mrage Kabange (Kagera Sugar), Muhibu Muhibu (Stand United FC), Nsubuga Solomon (Kishoto FC), Nyamtimba Muga (Kizuka Secondary), Oscar Mirambo (Makongo), Rashid Abdallah (Tech Fort Academy), Renatus Shija (Rhino Rangers), Safari Nyerere (Elimu Sports Academy) na Said Lyakuka (Kizuka Stars).
Simeon Mwesa (Mtibwa Sugar U20), Simon Shija (Tabora), Suleiman Mtungwe (Ruvu Shooting), Swalehe Allawi Abdul (Alliance Academy), Yasin Bashiri (Kick Off Sports Academy) na Zuberi Katwila (Mtibwa Sugar).
Wakati huo huo, kutakuwa na kozi ya wiki mbili ya ukocha ya ngazi ya Kati (Intermediate) itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 29 mwaka huu.
Makocha wote wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi katika Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA).

HII NDIYO NEMBO YA WORLD CUP 2018

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Sepp Blatter ameiweka hadharani Nembo mahsusi kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 ambazo zitachezwa Nchini Russia.
Blatter, akianua rasmi Nembo hiyo kwenye Kipindi maalum cha TV ya Russia huku akisaidiwa na Wanaanga wa Kirusi wanaosafiri kwenda Anga ya juu na mbali kabisa, alisema Nembo hiyo inaonyesha moyo na ari ya Russia.
Baada ya kutamka hivyo, Nembo hiyo ilianikwa hadharani hewani kwenye Matangazo hayo ya TV na Wanaanga hao wa Kirusi ambao walikuwa juu kwenye Anga ya mbali kabisa toka Duniani wakiwa kwenye Chombo chao maalum kiitwacho ‘International Space Station’ ambacho kinazunguka huko juu Angani.
Nembo hiyo inaonyesha Kombe la Dunia likiwa na Rangi Nyekundu na Bluu, Rangi za Bendera ya Russia, likizungukwa na utepe wa Dhahabu.
Russia hawajawahi kuwa Wenyeji wa Kombe la Dunia na pia hawajahi kulitwaa Kombe hili katika Historia yao.
Fainal hizo za huko Nchini Russia Mwaka 2018 zinafuatia zile za kule Brazil zilizochezwa Juni na Julai Mwaka huu na Germany kuibuka Mabingwa wa Dunia.
Fainali nyingine za Kombe la Dunia zitakuwa Mwaka 2022 huko Nchini Qatar.

Simanzi! Ben Kiko afariki, Rais JK amlilia


Katibu wa Rais maswala ya Habari, Issa Michuzi kulia akiwa na mtangazaji wa siku nyingi, Beni Kiko wakifurahia jambo wakati wa uhai wake katika tuzo za mwandishi bora 

Ben Kiko enzi za uhai wake
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenela Mukangara kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mtangazaji na Mwandishi Mkongwe na Mahiri hapa nchini wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa ni TBC Taifa, Ben Hamis Kikoromo maarufu kama Ben Kiko.
Ben Kiko amefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 31 Oktoba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akiendelea na matibabu ya figo baada ya kuhamishiwa hapo akitokea Hospitali ya Jeshi ya Milambo Mkoani Tabora.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mwanahabari na Mtangazaji huyu Mahiri ambaye ametoa mchango mkubwa wa kihabari kwa Taifa letu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba wa Ben Hamis Kikoromo.
“Namkumbuka Marehemu Ben Kiko, enzi za uhai wake, kama Mtangazaji aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji wake kutokana na namna yake ya kipekee ya kuripoti matukio hususan katika kipindi kilichojizolea umaarufu mkubwa wakati huo cha MAJIRA kilichokuwa kikirushwa hewani na  Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)”.
 Wakati wa vita dhidi ya Nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1978, Ben Hamis Kikoromo alifanya kazi kubwa kwa Taifa kwani aliweza kuripoti matukio mbalimbali kutoka katika uwanja wenyewe wa vita, na hivyo kuliwezesha Taifa na wananchi kwa ujumla kuhabarika vilivyo na matukio yaliyokuwa yakiendelea.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, pokea salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi na Watangazaji Mahiri katika Tasnia ya Habari hapa nchini. 
Vilevile kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo kwa kupoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia.  Nawaomba Wanafamilia wote, ndugu na Jamaa wa Marehemu wawe wavumilivu na wenye subira wanapoomboleza kifo cha mpendwa wao huku wakitambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.
  Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika muda wote wa maombolezo, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo, Amina.
Aidha Rais Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Wanahabari kote nchini ambao kwa hakika msiba wa Ben Kiko utakuwa umewagusa kwa karibu. 
Hata hivyo amesema kuondoka kwa Ben Kiko kusiwe chanzo cha wao kukata tamaa, bali kifo chake hakina budi kuwa chachu katika kujituma zaidi, na wawe tayari kuiga yote mazuri aliyoyafanya Marehemu enzi za uhai wake hapa duniani hususan katika Taaluma ya Uandishi wa Habari.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
31 Oktoba, 2014.

Newz Alert! Ajali yaua Wami lahusisha basi la Simba Mtoto, Lori

Ajali Bus la Simba Mtoto Lagongana Uso kwa Uso na Lori, Tunaomba Radhi kwa Picha hizi
TAARIFA zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa, ajali mbaya iliyohusisha basi la Simba Mtoto na Lori imetokea eneo la Wami na kusababisha maafa.
Taarifa hizo zinasema magari hayo yaligongana uso kwa uso na bado haijafahamika idadi ya waliodhurika ingawa habari za awali zinasema kuwa dereva wa Lori hilo amepoteza uhai papo hapo.
Habari zaidi zinasema kuwa abiria wa Simba Mtoto wamejeruhiwa, ila MICHARAZO inafuatilia taarifa kamili kisha itawafahamisha.
Picha kwa hisani ya Frank Msaki

Javier Mascherano amzidi kete Lionel Messi Barca

http://img.bleacherreport.net/img/images/photos/003/130/926/hi-res-2f26492ba99daf46e3be4f6b4d9e6aec_crop_north.jpg?w=630&h=420&q=75NYOTA wa Argentina, Javier Mascherano ametajwa kuwa mchezaji bora wa Barcelona kwa msimu wa 2013-14.
Lionel Messi alishinda tuzo hiyo kwa miaka mitatu katika kipindi cha miaka minne iliyopita ambayo inakwenda kwa jina la 'Memorial Aldo Rovira' ambapo sasa amezidiwa na muajentina mwenzake  ambaye ameimarisha ubora wa safu ya ulinzi ya 'Blaugrana' katika msimu uliopita licha ya kushindwa kutwaa taji lolote msimu huo.
"Nawashukuru wote ambao wamenipigia kura na kupelekea kupewa tuzo hii," amenukuliwa Mascherano na mtandao wa klabu yake .
"Tutaendelea kufanya mambo kwa kujitoa tukijaribu kuendelea kuwa watiifu kama ambavyo klabu yetu inatutaka."
Tuzo hiyo imepewa jina hilo kufuatia Aldo Rovira, ambaye alikuwa ni mwanachama maarufu wa klabu hiyo ambaye alifariki kwa ajali ya gari mwaka 2009. Ili kumpata mshindi wa tuzo hiyo, watu mashuhuri kutoka Barcelona na vyombo vya habari kutoka Katalunya wanapiga kura.
Mascherano mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani alijiunga Camp Nou akitokea katika klabu ya Liverpool mwak
a 2010.

JUMA KASEJA AVUNJA MKATABA YANGA, KISA...!

http://www.24tanzania.com/wp-content/uploads/2013/07/464dJuma-Kaseja.jpg

KIPA Juma Kaseja ametoa masharti mawili mazito Yanga na kama hayatatekelezwa yuko tayari mkataba wake na klabu hiyo uvunjwe rasmi, imeelezwa.
Hata hivyo, moja ya sharti ambalo ni vigumu kutekelezeka ni pamoja na kutaka kupewa nafasi za kudaka katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambayo hajawahi kusimama langoni msimu huu tangu pazia lilipofunguliwa Septemba 20.
Kupitia meneja wake, Abdulfatah Saleh, Kaseja ameipa masharti Klabu ya Yanga kama inataka kubaki naye immalizie fedha za usajili wake za Sh. milioni 20 na pia kuanza kumpa nafasi ya kudaka.
Kaseja, kipa huyo namba moja wa zamani wa Tanzania, hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya kocha Mbrazil Marcio Maximo.
Katika kipindi cha kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, Kaseja alikuwa anadaka kwa zamu na kipa chaguo la kwanza Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Abdulfatah alisema jana kuwa katika mkataba wao walioingia na Yanga, walikubaliana kukamilishia malipo ya mwisho ya dau la usajili ya (Sh. milioni 20) ifikapo Januari 15, mwaka huu, lakini klabu hiyo hadi sasa alidai haijafanya hivyo.
Alisema wakati wanavumilia hilo, bado mteja wake hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza jambo ambalo ni hatari kwa kipaji cha kipa huyo wa zamani wa Simba.
Abdulfatah alisema wanayaingiza masharti hayo yote kwa maandishi na kuyapeleka kwa uongozi wa Yanga uyatekeleze, vinginevyo hatua za kuuvunja mkataba zitafuata. Meneja huyo, hakutaka kuweka wazi lini watakabidhi barua hiyo kwa uongozi wa Yanga, hata hivyo.
Kaseja ameidakia Yanga mechi 15 tangu asajiliwe mwishoni mwa mwaka jana, akiwa kipa huru baada ya kuachwa na Simba kwa madai ya kushuka kiwango. Kati ya mechi hizo, tano ni za Ligi Kuu na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 
Katika mechi hizo Kaseja amefungwa mabao 10, yakiwamo matatu Yanga ikilala 3-1 mbele ya mahasimu, Simba katika mechi ya 'ndondo ya 'Nani Mtani Jembe' iliyomfukuzisha kocha Mholanzi Ernie Brandts.
Pamoja na kuwa kipa chaguo la kwanza Simba kipindi hicho, Kaseja hakuwahi kumvutia Maximo alipokuwa akiifundisha timu ya Taifa (Taifa Stars) na wakati fulani alidiriki kuwaita Ali Mustafa 'Barthez' na Dida, akimuacha Kaseja.
Wakati Kaseja akitaka kuvunja mkataba wake na Yanga, tayari kumeshaanza kuenea taarifa kuwa timu yake ya zamani ya Simba inataka kumrejesha wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu.
Alipotafutwa na kuzungumzia suala hilo jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema: "Swali lako la kwanza siwezi kukujibu maana mchezaji Juma Kaseja hana meneja anayetambulika na taasisi yoyote, iwe Yanga, TFF au hata Fifa."
Njovu alienda mbali zaidi akinukuu baadhi ya vipengele vya Fifa kwa kusema: "Mawakala wa wachezaji hawatambuliwi na Fifa tangu 2001. Mawakala wa wachezaji wanasajiliwa moja kwa moja na kila chama cha soka. Hivyo, hakuna kitu kama hicho kuwa na wakala wa Fifa wa mchezaji."
Aidha, Njovu alisema: "Jukumu la kupanga timu ni la kocha, wala si mtu yeyote."
NIPASHE

Wakazi wa Dar watajwa kama tatizo la migogoro ya ardhi Bagamoyo

DC Kipozi akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mtendaji wa Bwiligu-Chalinze kabla ya kuzungumza na ugeni wa Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge
DC wa Bagamoyo, Ahmed Kipozi (kati) akiwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Rutabazibwa na Diwani wa Kata ya Bwlingu, Hemed Karama Nassa wakati wa kukabidhi ardhi kwa wanachama wa chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge shughuli iliyofanyika jana Kibiki-Chalinze
DC Kipozi akitoa nasaha zake
DC Kipozi akiwa na viongozi wengine wakati wa makabidhiano ya ardhi kwa wanachama wa MHCS

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi amekiri migogoro mingi ya ardhi iliyopo wilayani mwake inachangiwa na wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikimbilia kununua maeneo katika wilaya hiyo wakati mwingine bila kufuata taratibu.
DC Kipozi aliyasema hayo wakati akibadilishana mawazo na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa na viongozi wa Chama Cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge walipokutana kwenye ofisi ya Mtendaji mjini Chalinze, Pwani.
Kipozi alisema ofisi yake imekuwa haishi kupokea malalamiko kila uchao kuhusiana na migogoro ya ardhi na kudai katika utafiti wake amebaini chanzo kikuu ni wakazi wa Dar es Salaam wanaokimbilia kununua maeneo ya ardhi katika wilaya hiyo bila utaratibu.
Alisema kwa juhudi kubwa akishirikiana na viongozi wenzake wilayani humo wamekuwa wakitatua matatizo hayo, huku akiwaonya wale wanaoenda kununua ardhi wilayani Bagamoyo kufuata taratibu ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Pia aligusia kuwa ofisi yake imeweza kubaini baadhi ya migogoro inachangiwa na watendaji wasio waaminifu wa Idara ya Ardhi wakiwamo wanaotoka wizarani ambao licha ya kubaini eneo husika kuwa tayari lina mtu wamekuwa wakiwapa wanaoenda kuyanunua na kusababisha migogoro isiyoisha.
DC Kipozi alisema kwa kipindi kifupi tangu aanze kuiongoza wilaya hiyo ofisi yake imejitahidi kutatua migogoro hiyo ukiwamo ule wa wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu kwa wananchi wote na kwa kiasi fulani kuifanya wilaya yake kuepuka machafuko kama ambavyo imekuwa ikitokea kila uchao katika maeneo mengine.
"Tunashukuru tumeweza kushughulikia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu ya kutosha, hivyo hata nyinyi mliokuja hapa muwe makini kuepuka kuigia mgogoro wa ardhi usiokuwa wa maana, na ofisi ipo tayari kufanya kazi nanyi bega kwa bega katika kufanikisha yaliyowaleta wilayani hapa," alisema DC Kipozi.

Watetezi City kuwakosa Silva, Toure dhidi ya Man United

http://merdekabola.com/wp-content/uploads/2014/05/toure-dan-silva.jpg
MABINGWA wa England, Manchester City wamekumbwa na hofu ya kuwakosa nyota wake muhimu wawili kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumapili dhidi ya mahasimu wao Manchester United baada ya juzi David Silva na Yaya Toure kuumia wakati wakichezea kichapo katika mchezo wa Kombe la Ligi (Capital One Cup) dhidi ya Newcastle.
Silva alikumbwa na majeraha ya goti wakati  Toure akisumbuliwa na nyonga wakati huo mabingwa hao watetezi wa Capital One Cup wakichezea kichapo cha mabao 2-0 tena nyumbani.
Silva alitonesha goti lake katika dakika ya nne wakati akwania mpira dhidi ya Ryan Taylor, hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Samir Nasri, ambaye alionekana uwanjani kwa mara ya kwanza tangu Septemba baada ya kupona majeraha yake ya nyonga.
Kocha Manuel Pellegrini katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi alisema: "David ana matatizo katika goti lake. Siju ni kwa ukubwa kiasi gani. Tutaona kesho (jana) na daktari."
Toure aliendelea kucheza baada ya kuanguka chini kutokana na kuchezewa rafu na Mehdi Abeid lakini baadaye alitolewa na Pellegrini aliongeza: "Yaya ana matatizo ya nyonga."
Pellegrini aliutetea uamuzi wake wa kumchagua Silva, kwa kusema alipanga kumrejesha Samir Nasri katika nafasi ya Mhispania huyo, ambaye amerejea baada ya kuwa nje kwa mwezi mmoja kutokana na kufanyiwa upasuaji wa nyonga.
Alielezea: "Hapakuwa na sababu, hawezi kucheza. Tulicheza Jumamosi, tuna siku nne za kujiweka vizuri, David alijiandaa kucheza. Labda asingemaliza kucheza mechi yote. Wazo lilikuwa kumbadilisha dhidi ya Samir Nasri."
Silva, msimu huu amekuwa katika kiwango kizuri na aliifungia City bao wakati ikipokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya West Ham Jumamosi.
City tayari imefahamika haitakuwa na huduma ya Frank Lampard Jumamosi dhidi ya kikosi hicho cha Louis van Gaal.
Lakini habari njema kwa Van Gaal ni kurejea kwa Wayne Rooney hivyo kukiongezea nguvu kikosi cha Manchester United Jumamosi.
Jumatatu, Rooney alitia shaka ya kukosa mechi hiyo baada ya kuumia mazoezini, hata hivyo imefahamika kwamba nahodha huyo wa United Jumatano alifanya mazoezi 'fulu muziki' na atakuwa fiti kucheza mechi hiyo ilitakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Etihad.
Rooney hajaichezea timu yake tangu alipopewa kadi nyekundu mwezi uliopita katika mechi dhidi ya West Ham, hata hivyo Van Gaal bado hajamhakikishia nahodha huyo uhakika wa kuanza.
Robin van Persie anabaki kuwa mmoja wa wachezaji asiye na uhakika kutokana na kiwango chake cha kushuka na kupanda licha ya kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Old Trafford Jumamosi iliyopita.
Katika hatua nyingine, kipa wa zamani wa United, Peter Schmeichel kwa sasa anaamini Manchester City ni ‘klabu kubwa’ kuliko wapinzani wao, lakini kwa upande wa kiwango.

Viongozi 'mchwa' Vyama vya Ushirika waonywa

Mrajisi w Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa akizungumza

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi akizungumza na wanachama wa MHCS
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa akizungumza mbele ya wanachama wa MHCS
VIONGOZI wa vyama vya Ushirika nchini wamechimbwa mkwara na kutahadharishwa juu ya tabia zao za wizi na ubadhilifu wa fedha za vyama vyao kwa kuelezwa kuwa watakapobainika kuhusika na vitendo hivyo watafungwa na kulipia fidia kwa hasara zote walizosababisha.
Mkwara huo umetolewa na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabanzibwa wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama Cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge (MHCS Ltd) katika sherehe za uzinduzi wa ofisi ya chama hicho kijiji cha Kibiki-Chalinze zilizofanyika juzi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambayo alikuwa mgeni rasmi.
Dk Rutabazibwa alisema kutokana na mabadiliko ya Sheria namba 6 ya Vyama vya Ushirika, wanaobainika kufanya wizi na ubadhilifu wa mali za vyama hivyo hawafukuzwi kazi tu au kuhamishwa na kuachwa walivyo badala yake wanafikishwa mahakamani na adhabu ya chini ni miaka miwili pamoja na kulipa fidia ya hasara wanazosababisha.
Mrajisi huyo alisema siku za nyuma kabla ya mabadiliko hayo ya mwaka jana, viongozi na watendaji wa vyama hivyo walikuwa wakifanya wizi wa kufuru na ubadhilifu kwa sababu hakukuwa na sheria kali ya kuwabana.
Dk Rutabazibwa aliusifu uongozi wa MHCS kwa kubuni mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wanachama wake na kuwataka wauendeleze na kufikia lengo la kupanua wigo wa chama hicho nchi nzima kama ilivyokuwa lengo la waasisi wa chama hicho akiwamo Hayati Baba wa Taifa, Mwl Nyerere.
"Nimesikia mkisema kuwa mmepanga kuanzisha mradi kama huo katika mikoa saba tofauti, mimi nawataka mjitanue nchi nzima kama ilivyokuwa lengo la Mwalimu Nyerere alipoasisi Mwenge wa Uhuru ili umulike nchi nzima," alisema.
Aliongeza kitu cha muhimu MHCS ijenge kweli nyumba za bei nafuu ili wanachama na wakazi wa Chalinze waweze kuzimudu na katu asifuate mfano wa asasi nyingine zinazotangaza kujenga nyuma za bei nafuu lakini iliyo ya chini kabisa ikiwa inauzwa Sh Mil 40-50.
"Mkifuata mkumbo huo wa kuuza nyuma kwa bei ambazo hazilengi watu wa chini hamtakuwa mmefikia lengo la kuwasaidia wanachama wenu na watu wengine, hivyo nauomba uongozi wa Ushirika wa Mwenge kujenga nyumba za bei ya chini kweli," alisema.
Kabla ya Mgeni rasmi huyo kuyasema hayo uongozi wa MHCS kupitia risala yao iliyosomwa na Mjumbe wa Bodi hiyo, Hellen Khamsini ulisema eneo jipya lililopatikana Kibiki-Chalinze lenye ukubwa wa Ekari 227 litajengwa nyumba za kisasa na bora zaidi na zile za Mwenge ili kuwarahisishia wanachama wao kuishi katika maeneo bora.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi aliwakaribisha wawekezaji hao wapya katika wilaya yake, lakini akiwataka kutowatenga wenyeji katika mradi huo wa nyumba ili kusaidia kujenga umoja na mshikamano.
DC Kipozi alisema amefurahia MHCS wamejitokeza kuanzisha mradi huo wakati mradi mkubwa wa mji wa Bagamoyo unaofahamika kama Satelite City ukiwa njiani ambao utabadilisha mandhari ya mji huo na kuinua maisha bora ya wakazi wake na wananchi wengine.
Katika sherehe hizo, Dk Rutabazibwa alifungua rasmi ofisi ya MHCS, na kugawa vyeti vya hisa kwa baadhi ya wanachama pamoja na kugawa viwanja kwa wanachama wa ushirika huo ulioasisiwa mwaka 1971 ukiwa na wanachama 25 na sasa ukiwa na wanachama 385.

Mchezaji Celtic afungiwa mechi 7 kwa ubaguzi wa rangi

WINGA mahiri wa klabu ya Celtic, Aleksandar Tonev amefungiwa mechi saba kwa kosa la kumfanyia vitendo vya ubaguzi wa rangi beki wa Aberdeen Shay Logan.
Tonev, 24 alilimwa adhabu hiyo kufuatia tukio hilo na Logan ambaye ni raia wa Uingereza katika mechi ya Ligi Kuu nchini Scotland Septemba mwaka huu. 
Winga huyo wa kimataifa wa Bulgaria yuko kwa mkopo Celtic akitokea klabu ya Aston Villa. 
Celtic katika taarifa yake wamesema watakata rufani kupinga adhabu hiyo wakidai kuwa mchezo huyo siyo mbaguzi. 
Tukio hilo limetokea katika kipindi cha cha mchezo ambao Celtic waliifunga Aberdeen mabao 2-1 Septemba 13.

Alex Song achekelea Ligi ya England

http://estaticos.marca.com/imagenes/2012/08/19/en/football/barcelona/1345394833_extras_mosaico_noticia_1_g_0.jpg
KIUNGO Alex Song, 27 anapanga kubaki kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kuanza vyema muda wake wa kucheza kwa mkopo wa muda mfupi katika klabu ya West Ham ambayo ameisaidia kukwea hadi nafasi ya nne katika msimamo baada ya kuwazamisha mabingwa Man City Jumamosi iliyopita.
"Nadhani hatma yangu iko hapa (England)," aliiambia Sky Sports. "Familia yangu, kila mmoja ana furaha hapa. Nina furaha sana kurejea England.
"Daima nimekuwa nikisema kama nitaondoka Barcelona , nitakuja England na hatma yangu iko hapa hata hivyo.
"Nataka kufurahia kucheza soka kwa sasa na tutaona nini kitatokea mwisho wa msimu."  

MHCS Ltd kuwajengea wanachama wake nyumba za kisasa Kibiki

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi ( pili kulia mbele) akiwa na baadhi ya viongozi wa Chalinze mara baada ya sherehe za MHCS Ltd
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Audax Rutabazibwa akipata maelezo toka kwa Marieta Urassa baada ya kumkabidhi kiwanja eneo la Kibiki
Mzee eneo letu ni kuanzia hapa mpaka kule...
Mmoja wanachama wa MHCS Ltd Seleka Sanga (wa pili kulia) akikabidhiwa eneo lake Kibiki
Marieta Urassa akipongezwa na Mrajisi wa vyama mara baada ya kukabidhiwa eneo lake jana
Wachekeshaji Eric Ivyo ivyo na Mkono wa Mkonole nao walikuwa mashuhuda wa shughuli za wanachama wa MHCS walipokabidhiwa viwanja vyao
Viongozi wa MHCS Ltd wakiwa katika picha ya pamoja na wageni wa shughuli zao, DC Kipozi, Mrajisi Dk Rutabazibwa na Diwani wa Bwilingu, Hemed Karama Nassa (mbele).
Sehemu ya wanachama wa MHCS Ltd wakiwa kwenye sherehe hizo kabla ya kukabidhiwa viwanja vyao





Mjumbe wa Bodi ya Uongozi wa MHCS, Hellen Khamsini akisoma risala ya chama chao mbele ya meza kuu
CHAMA cha Ushirika wa Ujenzi wa Nyumba Mwenge (MHCS Ltd) kinatarajiwa kuwajengea nyumba za kisasa na bora za bei nafuu wanachama wake baada ya kufanikiwa kupata ardi yenye ukubwa wa ekari 227 katika eneo la Kibiki-Chalinze wilayani Bagamoyo.
Mradi huo ambao umeanza kwa MHCS kugawa viwanja kwa wanachama  40 jana kijijini hapo, unatarajiwa kuanza mapema mwakani ambapo utawawezesha wanachama wao kumudu kulipia kidogo kidogo gharama za nyumba hizo.
Uongozi wa MHCS kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi wa sherehe za uzinduzi wa ofisi ya chama hicho eneo la Kibiki-Chalinze pamoja na ugawaji wa viwanja na vyeti vya hisa kwa wanachama wao, umesema tumaini lao ni kuhakikisha kila mwanachama wao anakuwa na makazi bora na ya kisasa kama njia ya kutekeleza malengo ya waasisi wa chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1971.
Risala hiyo iliyosomwa na Mjumbe wa Bodi ya Uongozi wa MHCS Ltd, Hellen Khamsini, ilisomwa mbele ya Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa na kudai kuwa awamu ya kwanza ya kupata ardhi ulihusisha ekari 45 ambalo limetoa jumla ya viwanjan93 vikiwamo viwanja vya makazi na huduma za jamii kama misikiti, makanisa na viwanja vya kuwekeza.
"Katika awamu ya pili tulipata eneo la ukubwa wa ekari 177 lililotoa viwanja 374 kati ya hivyo viwanja 278 vimegawiwa kwa wanachama na vilivyobaki ambavyo ni 96 vinabaki kuwa mali ya chama ambavyo vinahusisha makazi, huduma ya kijamii kama masuala ya dini, michezo na eneo la uwekezaji ambapo tuna nia ya kujenga hoteli kubwa ya kisasa ya hadhi ya Nyota Tano."
Uongozi wa chama hicho umesema kuwa matarajio yao mara baada ya kuanza kujenga mradi huo wa nyumba za kisasa kwa wanachama wao katika eneo hilo la Kibiki, wamepanga kupata maeneo zaidi ya ardhi katika mikoa saba ya Arusha, Diodoma, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro na Lindi kabla ya kuyaangalia maeneo mengine lengo likiwa kupanua wigo mpana wa chama chao na kusaidia kusambaza maendeleo ya makazi kwa watanzania wote bila kujali jinsia, dini, rangi au kabila.
Hata hivyo chama hicho kilisema kuwa kimekuwa kikikumbana na changamoto mbalimbali na kuuomba uongozi wa wilaya ya Bagamoyo na serikali kwa ujumla kuwasaidia kuwatatuloia baadhi ya kero kama miundo mbinu ya barabara, huduma za maji, umeme na mfumo wa maji taka katika maeneo wanayoyamiliki kwa sasa ili kuwapa unafuu wanachama wao.
Aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, Dk Rutabazibwa alisema ofisi yake ipo bega kwa bega na MHCS na kuahidi kufuatilia kuona mradi wanaotarajiwa kuufanya unafanikisha na kuwasaidia wanachama wao kupata nyumba wanazomudu kulizipa.
Naye Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema ofisi yake imeupokea mradi huo wa nyumba za kisasa na bora za bei nafuu wilayani mwake, na kuahidi kuwa bega kwa bega na uongozi wa chama hicho huku akiwasisitizia kutowatenga wakazi wenyeji katika mradi huo ili kujijengea mazingira mazuri ya kufanikisha sambamba na kujenga umoja na mshikamano baina yao.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho, Hellen Khamsini, Zahir Mshana na Dionis Moshi walisema wamenufaika mno na chama chao katika kupata makazi ambayo hawakutarajia na kufurahia kuanzishwa kwa mradi mpya eneo la Kibiki wakiamini litazidi kupanua wigo wa kuishi kisasa kwa sababu eneo lao la sasa la Mwenge ni dogo na nyumba zake kwa sasa zinaonekana kama gofu kwa kuchakaa.
"Kwa kweli nashukuru tangu niwe mwanachama nikijiunga mwaka 1972 nimenufaika kwa mengi na kwa mara ya kwanza nimeweza kupata mahali pa kuishi na sasa kumiliki kiwanja eneo la Kibiki, matarajio yangu kuzidi kuendelea kunufaika hata kwa vizazi vyangu vijavyo," alisema Mushi.
Mshana alisema anaamini mradi mpya utamfaa zaidi kwa sababu familia yake imepanuka akiwa na wajukuu na eneo analoishi kwa sasa Mwenge jiji ni dogo hivyo anaushuruku uongozi kwa juhudi wanazofanya, licha ya kukiri mwanzoni chama chao kilionekana kikienda sivyo kutokana na ubadhilifu uliofanywa na viongozi waliopita ambao walitimuliwa na kuweka wapya wanaowaletea maendeleo sasa.
Chama hicho kilichoasisi wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashid Kawawa na waliokuwa mawaziri wa awamu ya kwanza, Dereck Brayson na John Mhaville kikiwa na wanachama 25, lakini mpaka sasa ina jumla ya wanachama 385.

Thursday, October 30, 2014

LIGI DARAJA LA PILI KUANZA NOV 22.

MICHUANO ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar es Salaam jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange ilipitia maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo mwongozo wake (roadmap).
Kwa mujibu wa mwongozo huo, usajili wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11 mwaka huu kwa ajili ya kupitisha usajili.
Pia Kamati ya Mashindano imepitisha viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Uwanja wa Town Small Boys haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu Tunduru ni mgumu kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa kuwa ligi hiyo itachezwa hadi kipindi cha Masika.
Kwa upande wa uwanja wa Mpanda United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa na nyasi na uzio wa kudumu kutenganisha wachezaji na washabiki.
Kutokana na uamuzi huo, Mpanda United sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga wakati Town Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

29 waitwa Stars Maboresho II

http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2014/05/Staz.jpg
Baadhi ya wachezaji wa Maboresho awamu ya kwanza katika kikosi cha Stars kilichopigwa 3-0 na Burundi
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linatarajia kuendelea na awamu ya pili ya maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars) inayojumuisha vijana wenye umri chini ya miaka miaka 23.
Katika awamu hii, Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ameteua majina ya wachezaji 29 ambao watakuwa wakiingia kambini mara moja kwa mwezi siku ya Jumapili baada ya kuwakilisha timu zao kwenye mechi za ligi.
Kikosi hicho cha maboresho kitakuwa kikifanya programu maalumu za mazoezi mpaka siku ya Jumatano na kucheza mechi za kirafiki na timu za ndani au nje ya nchi.
Lengo hasa la programu hiyo ni kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji ambao walipatikana katika awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho mwanzoni mwa mwaka huu Tukuyu mkoani Mbeya, lakini wamekuwa hawatumiki. Pia kuwandaa vijana ili kujenga timu ya ushindani na imara ya Taifa ya muda mrefu.
TFF ina imani kubwa kuwa programu hii itakuwa na manufaa kwa soka ya Tanzania. Timu hiyo itaingia kambini kwa mara ya kwanza Desemba 9 mwaka huu katika hoteli itakayotangazwa baadaye.
Wachezaji walioteuliwa ni Aishi Manula (Azam), Benedict Tinoco (Kagera Sugar), Aboubakar Ally (Coastal Union), Miraji Adam (Simba), Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Gadiel Mbaga (Azam), Emmanuel Semwanda (African Lyon) na Joram Mgeveke (Simba).
Edward Charles (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kassim Simbaulanga (African Lyon), Pato Ngonyani (Yanga), Adam Salamba (Kahama), Abdi Banda (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hashim Magoma (Stand United), Makarani Ally (Mtibwa Sugar), Said Juma (Yanga) na Said Hamis (Simba).
Aboubakary Ally Mohamed (Zanzibar), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Malombe (Geita Gold), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda SC), Kelvin Friday (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Alfred Masumbakenda (Kahama) na Simon Msuva (Yanga).

TFF yatoa dili kwa wabunifu jezi za Stars



http://tff.or.tz/wp-content/uploads/2014/05/Boniface-Wambura.jpg
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. 
Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa. Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja). Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713 210242 au 0714 634838.

MSIBA! MZEE MANENTO WA BONGO MOVIE AFARIKI!


TASNIA ya sanaa imeendelea kukumbwa na majonzi baada ya msanii mwingine wa Bongo Movie, David Manento 'Mzee Manento' kufariki.
Mzee Manento aliyekuwa swahiba mkubwa wa marehEMU Steven Kanumba alifariki usiku wa jana baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kisukari pamoja na Presha akiwa na miaka 73.
Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania, TAFF, Simon Mwakifwamba amethibitisha kufariki kwa Mzee Manento na kusema kuwa msiba wake upo nyumbani kwake Kigogo/Mburahati jijini Dar es Salaam
Mzee Manento atakumbukwa hasa kwa filamu alizocheza kiumakini na marehemu Kanumba. 
Baadhi ya filamu zilizomjengea jina kubwa ni pamoja na Fake Pastor, Dar to Lagos na Hero of the Church.
Marehemu Manento anayetokea mkoa wa Kilimanjaro ameacha watoto 9 na inaelezwa tangu alipofiwa na mkewe miaka michache iliyopita alikuwa mpweke kiasi cha kushindwa hata kula vizuri.
Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Amina.