STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 31, 2014

Wakazi wa Dar watajwa kama tatizo la migogoro ya ardhi Bagamoyo

DC Kipozi akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mtendaji wa Bwiligu-Chalinze kabla ya kuzungumza na ugeni wa Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge
DC wa Bagamoyo, Ahmed Kipozi (kati) akiwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Rutabazibwa na Diwani wa Kata ya Bwlingu, Hemed Karama Nassa wakati wa kukabidhi ardhi kwa wanachama wa chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge shughuli iliyofanyika jana Kibiki-Chalinze
DC Kipozi akitoa nasaha zake
DC Kipozi akiwa na viongozi wengine wakati wa makabidhiano ya ardhi kwa wanachama wa MHCS

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi amekiri migogoro mingi ya ardhi iliyopo wilayani mwake inachangiwa na wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikimbilia kununua maeneo katika wilaya hiyo wakati mwingine bila kufuata taratibu.
DC Kipozi aliyasema hayo wakati akibadilishana mawazo na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa na viongozi wa Chama Cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge walipokutana kwenye ofisi ya Mtendaji mjini Chalinze, Pwani.
Kipozi alisema ofisi yake imekuwa haishi kupokea malalamiko kila uchao kuhusiana na migogoro ya ardhi na kudai katika utafiti wake amebaini chanzo kikuu ni wakazi wa Dar es Salaam wanaokimbilia kununua maeneo ya ardhi katika wilaya hiyo bila utaratibu.
Alisema kwa juhudi kubwa akishirikiana na viongozi wenzake wilayani humo wamekuwa wakitatua matatizo hayo, huku akiwaonya wale wanaoenda kununua ardhi wilayani Bagamoyo kufuata taratibu ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Pia aligusia kuwa ofisi yake imeweza kubaini baadhi ya migogoro inachangiwa na watendaji wasio waaminifu wa Idara ya Ardhi wakiwamo wanaotoka wizarani ambao licha ya kubaini eneo husika kuwa tayari lina mtu wamekuwa wakiwapa wanaoenda kuyanunua na kusababisha migogoro isiyoisha.
DC Kipozi alisema kwa kipindi kifupi tangu aanze kuiongoza wilaya hiyo ofisi yake imejitahidi kutatua migogoro hiyo ukiwamo ule wa wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu kwa wananchi wote na kwa kiasi fulani kuifanya wilaya yake kuepuka machafuko kama ambavyo imekuwa ikitokea kila uchao katika maeneo mengine.
"Tunashukuru tumeweza kushughulikia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu ya kutosha, hivyo hata nyinyi mliokuja hapa muwe makini kuepuka kuigia mgogoro wa ardhi usiokuwa wa maana, na ofisi ipo tayari kufanya kazi nanyi bega kwa bega katika kufanikisha yaliyowaleta wilayani hapa," alisema DC Kipozi.

No comments:

Post a Comment