STRIKA
USILIKOSE
Friday, October 31, 2014
Watetezi City kuwakosa Silva, Toure dhidi ya Man United
MABINGWA wa England, Manchester City wamekumbwa na hofu ya kuwakosa nyota wake muhimu wawili kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumapili dhidi ya mahasimu wao Manchester United baada ya juzi David Silva na Yaya Toure kuumia wakati wakichezea kichapo katika mchezo wa Kombe la Ligi (Capital One Cup) dhidi ya Newcastle.
Silva alikumbwa na majeraha ya goti wakati Toure akisumbuliwa na nyonga wakati huo mabingwa hao watetezi wa Capital One Cup wakichezea kichapo cha mabao 2-0 tena nyumbani.
Silva alitonesha goti lake katika dakika ya nne wakati akwania mpira dhidi ya Ryan Taylor, hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Samir Nasri, ambaye alionekana uwanjani kwa mara ya kwanza tangu Septemba baada ya kupona majeraha yake ya nyonga.
Kocha Manuel Pellegrini katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi alisema: "David ana matatizo katika goti lake. Siju ni kwa ukubwa kiasi gani. Tutaona kesho (jana) na daktari."
Toure aliendelea kucheza baada ya kuanguka chini kutokana na kuchezewa rafu na Mehdi Abeid lakini baadaye alitolewa na Pellegrini aliongeza: "Yaya ana matatizo ya nyonga."
Pellegrini aliutetea uamuzi wake wa kumchagua Silva, kwa kusema alipanga kumrejesha Samir Nasri katika nafasi ya Mhispania huyo, ambaye amerejea baada ya kuwa nje kwa mwezi mmoja kutokana na kufanyiwa upasuaji wa nyonga.
Alielezea: "Hapakuwa na sababu, hawezi kucheza. Tulicheza Jumamosi, tuna siku nne za kujiweka vizuri, David alijiandaa kucheza. Labda asingemaliza kucheza mechi yote. Wazo lilikuwa kumbadilisha dhidi ya Samir Nasri."
Silva, msimu huu amekuwa katika kiwango kizuri na aliifungia City bao wakati ikipokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya West Ham Jumamosi.
City tayari imefahamika haitakuwa na huduma ya Frank Lampard Jumamosi dhidi ya kikosi hicho cha Louis van Gaal.
Lakini habari njema kwa Van Gaal ni kurejea kwa Wayne Rooney hivyo kukiongezea nguvu kikosi cha Manchester United Jumamosi.
Jumatatu, Rooney alitia shaka ya kukosa mechi hiyo baada ya kuumia mazoezini, hata hivyo imefahamika kwamba nahodha huyo wa United Jumatano alifanya mazoezi 'fulu muziki' na atakuwa fiti kucheza mechi hiyo ilitakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Etihad.
Rooney hajaichezea timu yake tangu alipopewa kadi nyekundu mwezi uliopita katika mechi dhidi ya West Ham, hata hivyo Van Gaal bado hajamhakikishia nahodha huyo uhakika wa kuanza.
Robin van Persie anabaki kuwa mmoja wa wachezaji asiye na uhakika kutokana na kiwango chake cha kushuka na kupanda licha ya kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Old Trafford Jumamosi iliyopita.
Katika hatua nyingine, kipa wa zamani wa United, Peter Schmeichel kwa sasa anaamini Manchester City ni ‘klabu kubwa’ kuliko wapinzani wao, lakini kwa upande wa kiwango.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment