STRIKA
USILIKOSE
Sunday, October 14, 2012
Simba hawashikiki Bara licha ya kunasa kwa Coastal Union
Mabingwa wa ligi kuu ya Bara Simba jana walipunguzwa kasi na Coastal Union hapa Tanga, lakini angalau wakamudu kuendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo mpaka robo ya msimu, kufuatia sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Kwa sare hiyo dhidi ya Coastal iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kwa zaidi ya dakika 20, Simba imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Bara baada ya kufikisha pointi 17 kutokana na michezo saba. Wenyeji wamefikisha pointi 10.
Azam imejichimbia katika nafasi ya pili, pointi moja nyuma ya Simba baada ya jana kuifunga Polisi Morogoro bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, huku ikiwa na mechi moja mkononi.
Simba ambayo ilishinda michezo minne mfululizo kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Yanga na kurejea kushinda katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Oljoro, ingeweza kuwa imepoteza mechi yake ya kwanza jana kama Coastal iliyoonyesha soka maridadi ingekuwa makini.
Hemedi Morocco, kocha wa Coastal Union, alisema anashukuru kupata pointi moja licha ya timu yake kushindwa kutumia vizuri nafasi nyingi za kufunga ilizotengeneza.
Kocha wa Simba Milovan Cirkovic aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo kuwa Coastal ilicheza vizuri, lakini pia hakufurahishwa na uchezaji wa mshambuliaji wake wa kulipwa kutoka Ghana Daniel Akuffor.
Chipukizi Haruna Chanongo alikaribia kuipatia Simba bao la kuongoza katika dakika ya 12 baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.
Kama Chanongo angefunga, Nsa Job angeweza kuwa ameisawazishia Coastal Union katika dakika ya 39 wakati shuti lake lililopotoka nje akiwa katika nafasi nzuri, kutokana na krosi ya Selemani Kassim ambaye alikuwa amemtoka beki Pascal Ochieng.
Siku ya mshambuliaji wa kati Job ilimalizika vibaya dakika 20 hivi kabla ya filimbi ya mwisho hata hivyo, baada ya kutolewa uwanjani na muamuzi Haji Mbelwa kutokana na kosa la pili la kadi ya njano dhidi ya mabeki wawili wa kati wa Simba.
Katika kosa la kwanza, Job ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, alimchezea vibaya Shomari Kapombe kabla ya kumfanyia madhambi Ochieng katika kipindi cha pili.
Timu zilikuwa:
COASTAL: Jackson Chove, Said Sued, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal Machelenga, Jerry Santo, Mohammed Athumani, Selemani Kassim, Green Atupele, Nsa Job, Razak Khalfani (Lameck Dayton dk.45).
SIMBA: Juma Kaseja, Said Nasoro, Amiri Maftah, Pascal Ochieng, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi (Uhuru Selemani dk.58), Felix Sunzu, Daniel Akuffor (Salum Kinje dk.72), Haruna Chonongo.
Kutoka Morogoro Idda Mushi anaripoti kwamba bao la Azam lilifungwa na Kipre Tchetche katika dakika ya 54 hivyo kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kukaa kileleni kama itashinda mechi yake ya mkononi.
Kocha wa Azam Boris Bunjak alielezea kutoridhishwa na ukubwa wa ushindi huo kutokana na Polisi kuwa timu ya mkiani.
John Simkoko, mwalimu wa Polisi alisema makosa madogo madogo ya mchezaji mmoja mmoja na si timu, ndiyo yaliyowagharimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment