STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, October 14, 2012

Wakazi Kitunda wahakikishiwa makazi ya kudumu mradi wa viwanda



Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilala, Paul Mbembela akifafanua jambo katika mkutano wake na wakazi wa Kitunda waliojenga makazi yao ndani ya mradi wa viwanda uliotengwa na serikali miaka kadhaa iliyopita

Prisca Bassu mmoja wa wakazi wa Kitunda akiuliza swali katika mkutano huo

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni B, Novatus Nyiratu akifafanua jambo katika mkutano huo wa jana

Mkazi mwingine wa eneo la Kitunda akiuliza swali

Sehemu ya umma uliohudhuria mkutano huo wa jana kujua mustakabali wa waliojenga ndani ya mradi wa viwanda

Nataka kujua tusiokuwa na leseni za makazi inajuwaje hatma yetu? Ndivyo mmoja wa wakazi hao alihoji katika mkutano huo

Ibrahim Ismail naye alisimama na kuuliza swali

Hata kinamama nasi tumo kwa maswali

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kitunda Kati, Seleman Abdallah Mtama akieleza jambo kabla ya kuufunga mkutano huo







UONGOZI wa Manispaa ya Ilala, umewatoa hofu na kuwahakikishia wakazi wa eneo la Kitunda, waliojenga na kuweka makazi ndani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi wa viwanda kwamba kamwe hawataondolewa.
Pia uongozi huo umewahakikishia wakazi hao kuwa maeneo yao yatapimwa upya na kumilikishwa ardhi ili yawe makazi yao ya kudumu mara taratibu za kubadilisha matumizi ya eneo hilo zilizoanza zitakapokamilika.
Akizungumza na wakazi hao katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na uongozi wa serikali za mitaa ya Kipunguni B na Kitunda Kati, uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kipunguni, Afisa Mipango Miji Manispaa ya Ilala, Paul Mbembela alisema wakazi hao hawapaswi kuwa na hofu.
Mbembela alisema licha ya kwamba wakazi wa eneo hilo wapo ndani ya ardhi iliyotengwa kwa miaka mingi na serikali kwa ajili ya mradi wa viwanda, bado hawana hofu kwa vile unafanyika mchakato wa kubadilishwa matumizi yake.
Alisema katika mabadiliko hayo ya matumizi, wakazi waliojenga na kumiliki viwanja katika eneo hilo watafanyiwa utaratibu wa kupimwa maeneo yao na kisha kumilikishwa upya kihalali na mradi huo wa viwanda utahamishiwa maeneo mengine ya viwanja vya serikali vilivyopimwa tayari.
Afisa huyo aliyataja baadhi ya maeneo ambayo mradi huo unaweza kuhamia ni pamoja na Buyuni, Chanika na kwingineko katika manispaa ya Ilala ambayo tayari yameshapimwa na kutengwa.
Aliwasisitiza wakazi hao waliowatuma viongozi wa serikali zao za mitaa katika ofisi za manispaa kuhakikisha wanaipa ushirikiano kamati hiyo katika zoezi la kuwatambua wamiliki halali wa sasa waliopo katika eneo hilo ili kurahisisha mchakato wa kuyapima na kuwamilikisha upya.
Kabla ya ufafanuzi huo wananchi wa maeneo hayo kupitia serikali zao za mitaa walikuwa na hofu kubwa ya kubomolewa na kupoteza mali zao katika eneo hilo baada ya kubainika eneo hilo lilitengwa kwa mradi wa viwanda.
Baadhi ya wananchi katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Kitunda Kati, Seleman Mtama na ile ya Kipunguni B, Novatus Nyiratu walitaka kujua hatma yao iwapo watatimuliwa katika eneo  hilo.
Miongoni mwa wakazi hao, Ibrahim Ismail, Prisca Bassu walitaka kufahamu iwapo wananchi ambao hawana hati au leseni ya makazi katika eneo hilo hatma yao itakuwaje na kuelezwa watasaidiwa  kumilikishwa bila ya tatizo mradi wahakikiwe na kamati yao.

No comments:

Post a Comment