STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 31, 2013

BREAKING NEWS: DIZUMBA WA MAJIMAJI AFARIKI

HABARI zilizotufikia muda huu zinasema kuwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Majimaji Songea inayojiandaa na duru la pili la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ahmed Dizumba amefariki dunia.
Taarifa zilizopatikana asubuhi hii ambazo MICHARAZO inaendelea kuzifuatilia kwa ukaribu zinasema Dizumba amefariki usiku wa kuamkia leo na anatarajiwa kuzikwa leo mjini Songea.
Kwa yeyote mwenye taarifa zaidi anaweza kutupenyezea, juu ya msiba huu ulioikumba Majimaji ikiwa katika harakati za kuanza duru la pili la ligi daraja la kwanza kuwania kurejea ligi kuu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na TFF, Majimaji imepangwa kuanza utepe wa duru hilo kwenye uwanja wake wa Majimaji Songea kuvaana na Kurugenzi mechi ya kundi A.

Mtibwa Sugar ipo tayari kuivaa Yanga, Mgosi majaribuni...!

Kocha wa Mtibwa Mecky Mexime

TIMU ya soka ya Mtibwa Sugar imesema imejiandaa vya kutosha kuweza kuwakabili vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakaovaana nao keshokutwa jijini Dar es Salaam.
Mtibwa inatarajiwa kuvaana na Yanga katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo duru la pili ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 walichopewa nyumbani kwao na Polisi Morogoro.
Katika pambano lao la awali Mtibwa iliisasambua Yanga mjini Morogoro kwa mabao 3-0, hali inayofanya pambano hilo la marudiano kuwa la aina yake, ndio maana benchi la ufundi la timu hiyo limedai kuwa limepania kurekebisha makosa mbele ya wapinzani wao wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime, amesema kuwa kikosi chao kipo katika hali nzuri kuweza kuikabili Yanga na kuendeleza ubabe wao, licha ya kukiri wanatarajia upinzani mkali.
Mexime, alisema hana shaka na pambano hilo kwa namna alivyoweza kurekebisha makosa yaliyowagharimu katika pambano lao lililopita walilopoteza nyumbani.
"Tumejiandaa na tupo tayari kuivaa Yanga na hatuna hofu yoyote, vijana wangu wapo kamili kuweza kurekebisha makosa yaliyotuponza kwa Polisi Moro," alisema Mexime.
Mexime, alisema ushindi pekee ndiyo kitu kinachohitajika kwa Mtibwa ili kuweza kujipanga kwa ajili ya kumaliza nafasi za juu mwishoni mwa msimu.
Mbali na mechi hiyo ya Yanga na Mtibwa, siku hiyo ya jumamosi kutakuwa na mechi nyingine kadhaa kabla ya Jumapili Mabingwa watetezi, Simba kuvaana na JKT Ruvu ambayo .inatarajiwa kumtumia nyota wqa zamani za Msimbani Mussa Hassani Mgosi kuweza kuwasimamisha Simba walioilaza Africans Lyon katika mechi yao iliyopita.

Manchester United yazidi kujichimbia kileleni Ligi ya England

Rooney akipachika mpira wavuni


MABAO mawili yaliyopachikwa wavuni na mshambuliaji Wayne Rooney imeiwezesha Manchester United kuendelea kujikita kileleni mwea msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kuilaza Southampton kwa mabao 2-1 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Mashetani hao Wekundu waliokuwa uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafoord, walijikuta wakishtukizwa kwa kufungwa bao la mapema na wageni wao lililofungwa na Jay  Rodriguez dakika ya tatu tu ya mchezo huo, hata hivyo dakika tano baadae Rooney aliwatuliza mashabiki wa timu yake kwa kusawazisha bao.
Rooney aliendelea kung'ara kwa kuongeza bao la pili dakika ya 27 akimalizia kazi nzuri ya Patric Evra na kufanya hadi mapumziko timu hizo ziwe zimefungana mabao 2-1 yaliyomudu hadi zilipomalizika dakika 90 za pambano hilo.
Kwa ushindi huo Manchester imeongeza pengo la pointi saba kati yao na wapinzani wao, Manchester City ambayo juzi ililazimishwa sare na kusalia na pointi zao 52 huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 24 kila mmoja.
Katika mapambano mengine yaliyochezwa usiku wa jana, Liverpool iliwabana wenyeji wao Arsenal na kufungana nao mabao 2-2, huku Norwich City ilijikuta ikibanwa mbavu nyumbani kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Nayo Reading iliing'ang'ania waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea kwa kufungana nao magoli 2-2 na Fulham iliicharaza West Ham United mabao 3-1 na Everton iliendeleza maajabu wake msimu huu kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 mbele ya West Bromwich.
Ligi hiyo inatarajiwa kuingia mzunguko wa 25  mwishoni mwa wiki kwa mechi katika viwanja mbalimbali nchini humo.
Rooney akishangilia moja ya mabao yake ya jana



Balotelli ilibidi tu aondoke - Mancini


Kocha Mancini akiwa na Balotelli wakipeana majukumu wakati walipokuwa pamoja Manchester City

KOCHA wa Manchester City, Roberto Mancini amesema kuondoka kwa Mario Balotelli kwenda AC Milan kunaifanya timu yake ipungukiwe wachezaji.
Sare yao ya 0-0 dhidi ya QPR usiku wa kuamkia jana iliwaacha mabingwa wakiwa hatarini kupitwa zaidi na vinara Manchester United, ambao usiku wa kuamkia leo walitarajiwa kucheza dhidi ya Southampton.
"Ni ngumu kwa sababu nimempoteza mchezaji mmoja muhimu na ambaye angekuwa muhimu katika mechi 14 zijazo," alisema Mancini.
"Lakini ilikuwa ni muhimu kwa Mario kurejea Italia, kurejea kwenye familia yake na kuchezea Milan."
Mancini anaamini kwamba Balotelli amefanya kazi "nzuri sana" katika miaka yake miwili na nusu akiwa na Man City, ingawa amekubali kwamba msimu huu ulikuwa mgumu zaidi kwa mshambuliaji huyo.
Mancini pia haraka alikanusha mtazamo kwamba kuondoka kwa Balotelli kumetokana na ugumu wa kumdhibiti mshambuliaji huyo mtata.
"Hapana, hapana, hapana, siyo kwangu," alisema. "Kwangu mimi, Mario alikuwa kama mwanangu mwingine.
"Mario yuko hivyo lakini anaweza kukufadhaisha wakati mwingine.
"Klabu imeniambia kwamba imepokea ofa kutoka Milan. Nilizungumza na Mario na nadhani alitaka uhamisho huu.
"Nadhani kwake kucheza miaka mitatu England na kisha kurejea Italia itakuwa ni jambo zuri kwake."
Balotelli alitambulishwa rasmi jana na klabu yake mpya ya AC Milan akikabidhiwa jezi yenye namba kama alivyokuwa akiitumia alipokuwa City, 45.

AZAM, JKT OLJORO ZAZIDI KUPAA LIGI KUU BARA

 
TIMU za soka za Azam na JKT Oljoro zimezidi kupeta katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuendeleza wimbi la ushindi katika mechi zao zilizochezwa katika miji tofauti ya Dar na Arusha.
Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao ya Azam katika mchezo huo yametiwa kimiani na Kipre Michael Balou wa Ivory Coast, dakika ya tisa, Mganda, Brian Umony dakika ya 20 na Mkenya Humphrey Mieno dakika ya 46.
Bao la kufutia machozi la Toto lilitumbukizwa kimiani katika dakika ya 77 na Selemani Kibuta, ambalo hata hivyo halikuwaongezea lolote na kuifanya timu hiyo kupioteza mechi ya pili mfululizo kwa idadi ya mabao hayo 3-1.
Toto ililazwa idadi hiyo na Oljoro JKT katika mechi iliyochezwa mjini Arusha Jumamosi iliyopita, ambapo jana timu hiyo ya maafande wa JKT waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuilaza Kagera Sugar kwa mabao 2-0.

TAIFA STARS KUIVAA CAMEROON WIKI IJAYO


Na Boniface Wambura
TANZANIA (Taifa Stars) itacheza na Cameroon katika moja ya mechi za kirafiki za Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date zitakazofanyika duniani kote Februari 6 mwaka huu.
Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni. Kikosi cha Cameroon kinachoundwa na wachezaji wengi wa kulipwa wanaocheza katika nchi mbalimbali duniani kitaanza kuwasili nchini Februari 3 mwaka huu.
Nchi kadhaa ziliomba kucheza na Taifa Stars katika tarehe hiyo ya FIFA, lakini Kocha wa Stars, Kim Poulsen ameamua kucheza mechi hiyo dhidi ya Cameroon ambayo nahodha wake ni mchezaji nyota wa kimataifa, Samuel Etoo Fils.
Congo Brazzaville, Equatorial Guinea, Rwanda na Swaziland nazo zilikuwa zimeomba kucheza dhidi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager. Ukiondoa Swaziland iliyotaka mechi hiyo ichezwe Dar es Salaam, nyingine zilitaka kucheza nyumbani kwao.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia maandalizi ya mechi hiyo ikiwemo kutaja kikosi ambacho atakitumia. Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Madrid yaidindia Barca Kombe la Mfalme

Cesc Febregas akishangilia bao katika pambano la jana la El Clasico
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Hispania, Real Madrid usiku wa kuamkia leo iliikomalia vinara wa ligi hiyo, Barcelona kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika pambano la nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Mfalme katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, mjini Madrid.
Ikicheza bila baadhi ya nyota wake kutokana na kutumikia adhabu na kuwa majeruhi, Real Madrid iliibana Barca na kwenda nao mapumziko wakiwa nguvu sawa bila kufungana.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Barcelona kuwashtua wenyeji wao kwa kujipatia bao la kuongoza lililofungwa dakika ya 50 na kiungo Cesc Fabregas akimalizia kazi nzuri ya Lionel Messi.
Timu hizo zilizoenda kushambuliana na kufanya kosa kosa kadhaa na kwenye dakika ya 81, wenyeji walifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Raphael Varane aliyemaliza kazi murua ilioyofanywa na Mjerumani Mesut Ozil.
Wapinzani hao wa jadi wa nchini Hispania wanatarajiwa kurudiana mwishoni mwa mwezi Februari, ambapo ndiyo itaamua hatma ya timu ipi itinge fainali za michuano hiyo kuungana na mshindi kati ya Sevilla na Atletico Madrid ambazo nufa fainali yao ya kwanza inatarajiwa kuchezwa kesho mjini Madrid kabla ya kwenda kurudiana nyumbani kwa Sevilla.
Katika pambano hilo la El Clasico lililoshuhudia Barcelona ikiwatumia wachezaji wake waliokuwa nje kwa muda mrefu kwa majereha, wachezaji sita, watatu kila upande wakionyeshwa kadi za njano kwa makosa mbalimbali.

Wednesday, January 30, 2013

WAPAMBE MARUFUKU KUSIKILIZA MAPINGAMIZI UCHAGUZI WA TFF


Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema waliowekewa pingamizi na wa walioweka pingamizi hawaruhusiwi kufika katika kikao cha leo wakiwa na vikundi vya ushangiliaji au wapambe.
Kikao cha kupitia pingamizi kitafanyika saa 4 asubuhi na wapambe au washabiki wa waombaji uongozi pamoja na waweka pingamizi hawakiwi kuwepo kwenye eneo la kikao hicho.
Wote walioweka pingamizi na waliowekewa pingamizi barua zao za mwito wa kuhudhuria kikao cha  Kamati ya Uchaguzi ya TFF zimeshatumwa kwenye anwani za barua-pepe zilizo kwenye taarifa za pingamizi au kwenye fomu za maombi ya uongozi.
Jana waombaji uongozi watatumiwa barua za mwito kwa barua-pepe wa kuhudhuria usaili utakaofanyika tarehe 01-02 Februari 2013. Tarehe 01 Februari 2013 watasailiwa waombaji uongozi wa TPL Board na waombaji ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 1 hadi Kanda ya 8. Waombaji uongozi kupitia Kanda ya 9 hadi ya 13 na waombaji uongozi wa Makamu wa Rais na Rais wa TFF watasailiwa tarehe 02 Februari 2013 kuanzia saa 4 asubuhi.
Vyombo vingi vya habari vimeonyesha nia ya kuwepo mdahalo wa wagombea uongozi katika TPL Board na TFF. Kanuni za Uchaguzi za TFF hazizuii jambo hilo kufanyika, bali tu lizingatie Kanuni za Uchaguzi za TFF. Mojawapo ya mambo ya kuzingatiwa ni kwamba mdahalo huo ufanyike wakati wa kipindi cha Kampeni na usiwe na taswira ya kuwapendelea au kuwabagua baadhi ya wagombea. Kanuni hazimlazimishi mgombea kushiriki mdahalo.
Pia ni vema mdahalo ukaandaliwa na kuratibiwa  na Taasisi inayounganisha vyombo vya habari au waandishi wa habari kama TASWA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF lazima ijulishwe kwa maandishi nia hiyo ya kufanyika mdahalo na utaratibu utakaotumika mapema kabla ya kufanyika mdahalo huo ili kujiridhisha kuwa utaratibu utakaotumika kuandaa na kuendesha mdahalo haukiuki kanuni za Uchaguzi za TFF.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF inavishukuru vyombo vya habari kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi hadi sasa na kuwaomba waendelee kufanya hivyo hadi mwisho wa mchakato wa uchaguzi.

MTANZANIA KUWANIA TAJI LA JUMUIYA YA MADOLA


BONDIA Mtanzania Fadhili Majia sasa atamvaa Mghana Isaac Quaye tarehe 8 March kutafuta nafasi ya kugombea mkanda wa ubingwa wa Jumuiya ya madola (CBC) ambayo unashikiliwa na bondia Kevin Satchell  wa Uingereza.

Mpambano wa Majia na Quaye umemsogezwa mbele kwa kuwa mashindano ya ubingwa wa Afrika yanayoendelea nchini Afrika ya Kusini yanarushwa na televisheni ya Super Sports ambayo ndio wafadhili wakubwa wa mpambano wao.

Wakati huo huo bondia Richard Commey wa Ghana atamvaa Mghana mwenzake Bilal Muhammed kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati uzito wa lightweight siku hiyo hiyo March 30. Aidha bondia Frederick Lawson wa Ghana atazichapa na bondia Isaac Sowah wa Ghana kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati  katika uzito wa Welterweight. Mapambano hayo yatasimamiwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi

Mtanzania mwingine atakaye peperusha bendera ya taifa siku hiyo ni pamoja na Allan Kamote atakayezichapa na bingwa wa zamani wa IBF wa mabara na ambaye ndiye bingwa wa sasa wa WBA wa mabara Emmanuel Tagoe katika pambano lisilo la ubingwa.

Naye bondia wa Kenya Michael Odhiambo atachuana vikali na Mghana George Ashire katika mpambano usio wa ubingwa uzito wa lightweight.

Mapambano hayo yote yatakuwa ni ya utangulizi katika mpambano wa ubingwa wa dunia kati ya bondia maarufu wa Ghana anayeishi nchini Marekani Joseph Agbeko na Luis Mendelez kutoka nchini Columbia.


IBF/Afrika inawaomba watanzania kwa ujumla wao wawaombee mabondia wake ili waweze kupeperusha vyema bendera ya taifa.

 

BONIFACE WAMBURA WA TFF APETA IBF/USBA

Boniface Wambura

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TANZANIA inaelekea kuwa chungu cha kutoa wataalamu wa kusimamia ngumi katika bara la Afrika baada ya Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Afrika  kuorodhesha maofisa wa ulingo watakaopata nafasi za kusimamia mapambano kadhaa ya ubingwa katika bara la Afrika.

Katika orodha iliyotolewa na IBF Africa wako watanzania sita ambao IBF imewataja kuwa watakuwa wanapata nafasi za kusimamia mapambano ndani na nje ya bara la Afrika.

Mwaka huu 2013, IBF Africa na IBF Asia zitaanza mapambano ya kuwakutanisha mabingwa wa mabara yote mawili hivyo maofisa watakaosimamia mapambano haya katika bara la Afrika na bara la Asia watatoka katika mabara haya mawili.

Orodha kamili ya maofisa hao inaongozwa na Rais wa IBF Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi..

(Afrika ya Kusini)  Alfred Buqwana, Wally Snowball, Simon Xamlashe na Jaap Van Niewenhuizen

(Ghana) Rodger Barnor, Fred Ghartey, Confidence Hiagbe na May Mensah Akakpo

(Uganda) Simon Katogole na Ismail Sekisambu.
(Zambia) William Sekeleke and John Shipanuka
(Tanzania) Onesmo Ngowi, Nemes Kavishe, Boniface Wambura, John Chagu, Mark Hatia na mwamuzi anayechipukia kutoka jiji la Tanga Gallous Ligongo,

Kufuatana na orodha iliyotolewa na IBF Afrika, Tanzania inaonekana kuwa na uwezekano wa kutoa maofisa wengi wa ulingo kuliko nchi nyingine za Kiafrika hivyo kuipa nafasi nzuri ya kujitangaza.

Imetolewa na:


IBF AFRICA/USBA

Msondo Ngoma bado yamlilia Mapanga

Mapanga enzi za uhai wake

UONGOZI wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' umeeleza utaendelea kumlilia mpiga besi wao, Ismail Mapanga aliyefariki na kuzikiwa wiki iliyopita kwa madai ya amewaachia pengo.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema marehemu Mapanga alikuwa mmoja wa wanamuziki tegemeo wa Msondo katika safu ya wacharaza magitaa.
Super D, alisema japo msiba ni kitu cha kawaida katika maisha ya wanadamu, lakini kwao Msondo kifo cha Mapanga kinawauma kutokana na mchango mkubwa ambao mwanamuziki huyo alikuwa akiutoa kwa bendi yao.
"Tutamlilia na kumkumbuka Mapanga, alikuwa mpiganaji ndani ya bendi kwa mchango wake, ametuachia pengo kubwa sio siri. Ni msiba mkubwa kwetu," alisema Super D.
Aidha, bendi yao inawashukuru wale wote kwa namna moja au nyingine walishiriki tangu mwanzo hadi mwisho katika msiba huo akidai Msondo haina cha kuwalipa zaidi ya kuwashukuru na kuwaombea kwa Mungu kwa walichokifanya.
"Tunawaombea kwa Mungu awalipe kwa walichokifanya na tunaiomba familia na ndugu jamaa wa marehemu wawe na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi," alisema.
Mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na bendi na makundi mbalimbali ya sanaa likiwemo kundi la Muungano, alifariki Januari 23 kutokana na kuugua akiwa ziarani na Msondo mjini Tabora na kuzikwa siku iliyofuata jijini Dar es Salaam.

EXTRA BONGO, CHID BENZ KUPAGAWISHA MTONI

Waimbaji wa Extra Bongo, Ally Choki na Khadija Kimobitel wakiwajibika jukwaani


BENDI ya Extra Bongo 'Wazee wa Kizigo' inatarajia kufanya onyesho la pamoja na wasanii wa muziki wa kizazi kipya kama njia mojawapo ya kudumisha ushirikiano.
Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki alisema onyesho hilo litakalofanyika kesho eneo la Mtoni Kwa Azaz Ally jijini Dar es Salaam, litawashirikisha baadhi ya wasanii kama; Chid Benz, Amin Tundaman na Saynag.
"taratibu huu tuliuanza tangu mwaka jana na tumekuwa tukishirikisha wasanii mbalimbali kwenye maonyesho yetu kama njia mojawapo ya kuimarisha ushirikiano kati ya wanamuziki wa dansi na kizazi kipya," alisema Choki.
Choki alisema baada ya onyesho hilo, Extra Bongo itaendelea na shindano la kila Jumamosi la kucheza mtindo wa 'Kizigo' ambalo linashirikisha mashabiki wa bendi hiyo lililopewa jina la 'Wiki Nne za Zawadi'.
"Sasa tunaingia Jumamosi ya tatu tangu tuanze mashindano haya ambapo mashabiki wamekuwa wakijishindia fedha taslim kuanzia Sh. 150,000 kwa mshindi wa kwanza na Sh. 100,000 kwa mshindi wa pili," alisema.
Alifafanua kuwa shindano limebuniwa kama njia ya kuwashukuru mashabiki wao ambao wamekuwa wakiiunga mkono bendi hiyo tangu ifufuliwe upya miaka mtatu iliyopita ambapo pia mshindi wa tatu hupewa Sh.50,000.
Bendi hiyo kwa sasa inatamba na albamu ya pili ya 'Mtenda Akitendewa' yenye nyimbo za 'Bakutuka', 'Neema', 'Mashuu', 'Fisadi wa Mapenzi' na 'Watu na Falsafa'.


Zola D aitoa Swahili Hip Hop kwa mashabiki

Zola D katika pozi



NYOTA wa muziki wa Hip hop nchini, David Mlope 'Zola D', amewafyatulia mashabiki wake albamu yenye nyimbo 21 kama njia ya kuwashukuru kwa namna walivyomuunga mkono tangu ajitose kwenye fani hiyo miaka karibu 20 iliyopita.
Alisema albamu hiyo inayotarajiwa kutoka hivi karibuni imekusanya nyimbo mchanganyiko za zamani na mpya kama njia ya kuwapa burudani mashabiki wake hao sambamba na shukrani zake kwao kwa kumsapoti.
Msanii huyo alisema kwa namna mashabiki wake walivyomuunga mkono tangu alipoibuka mwaka 1995 mpaka sasa hana cha kuwapa zaidi wa kuwatolea albamu hiyo itakayofahamika kama 'Swahili Hip Hop'.
Zola D alisema tayari ameshaanza kuitambulisha albamu hiyo kwa nyimbo zake mpya zinazoendelea kutamba kwenye vituo vya redio na runinga kama 'Coast to Coast' na 'Knockout' aliyouimba akishirikiana na P Funk 'Majani'.
"Sijaona cha kuwapa ahsante mashabiki wangu zaidi ya kuwatolea albamu itakayokuwa na nyimbo mchanganyiko zikiwemo za awali na mpya, ambapo atakayeipata albamu hiyo atasuuzika roho," alisema Zola D.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazokuwa katika albamu hiyo ni ya Swahili Hip Hop' ni pamoja na 'Rap Gangster', 'Jana sio Leo', 'Moto wa Tipper', 'Sipati  Mchongo', 'What Going On', 'Hustler King', 'Unde', 'Msela Sana' na 'Rudi'.

KIVUMBI CHA LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA JUMAMOSI

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo itatoa timu tatu zitakazocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2013/2014) unaanza Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) katika viwanja tisa tofauti.
Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mechi za Kundi B, Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Moro United dhidi ya Villa Squad (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Jumapili (Februari 3 mwaka huu) ni Tessema na Green Warriors (Mabatini, Pwani), Ashanti United na Polisi Dar (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam).
Kundi C Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Kikosi cha Azam

AZAM UWANJANI LEO KUIFUKUZIA YANGA KILELENI LIGI KUU BARA

MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 15 leo kwa mechi mbili ambapo Azam iliyo katika nafasi ya pili nyuma ya Yanga itakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam huku Azam ikisaka ushindi ili kuikaribia Yanga inayoongoza wakati Toto Africans inayonolewa na John Tegete ikitaka kurekebisha makosa ya kupoteza mechi yake iliyopita dhidi ya Oljoro JKT.
Katika mechi hiyo ya Arusha iliyochezwa Jumamosi iliyopita, Toto ililala mabao 3-1 idadi ambayo Azam ilipata kwa kuigaragaza Kagera Sugar inayonolewa na Abdallah KIbadeni.
Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT dhidi ya wageni Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo wa Musoma.
Ushindi kwa Oljoro JKT yenye pointi 17 utaihakikishia kubaki katika nafasi yake ya nane wakati Kagera Sugar inayofundishwa na kocha mkongwe Abdallah Kibaden utaifanya ipige hatua moja mbele katika msimamo wa ligi.
Ligi itaendelea tena Jumamosi ya wiki hii kwa kuchezwa mechi tatu ambapo vinara Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 3-1 mbele ya Prisons ya Mbeya.
Mtibwa katika mechi yao ya kwanza ya duru la pili  ilianza kwa kulazwa nyumbani na Polisi Morogoro, lakini wanajivunia ushindi wa mabao 3-0 iliyoinyuka Yanga katika mchezo wao wa duru la kwanza uliosababisha aliyekuwa kocha wa Yanga, Tom Saintfiet kutimuliwa kazi.

KABANGE TWITE AKWAMA KUICHEZEA YANGA, KISA....!

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao dhidi ya Black Leopards ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

MCHEZAJI Alain Kabange Twite hataweza kuichezea Yanga msimu huu (2012/2013) baada ya klabu hiyo kuingiza nyaraka zenye upungufu wakati ikimuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System- TMS).
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), baadhi ya nyaraka zenye upungufu katika maombi hayo ni mkataba kati ya Twite na Yanga, lakini vile vile makubaliano ya mkopo (Loan Agreement) kati ya Yanga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo ndiyo inayommiliki mchezaji huyo.
Ili mchezaji aweze kupata ITC kwa njia ya TMS, kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF kuna nyaraka kadhaa muhimu zinatakiwa kukamilika katika maombi hayo ili hati hiyo iweze kupatikana.

HATIMAYE MSANII LULU AACHIWA KULA RAHA USWAHILINI

Lulu akifurahi baada ya kuachiwa kwa dhamana jana
Lulu akijibu maswali ya waandishi baada ya kuachiwa kwa dhamana

Lulu akilia baada ya kuachiwa kwa dhamana  huku akisaidiwa na muigizaji mwenzake, Dokta Cheni, ambaye alikuwa mstari wa mbele kuwezesha kutoka kwake kwa kipindi chote cha miezi tisa aliyokaa rumande binti huyo

Lulu akijibu maswali ya waandishi baada ya kuachiwa kwa dhamana jana

Lulu akimkumbatia mama yake mzazi Lucrecia Kalugila

Lulu akimkumbatia mama yake mzazi Lucrecia Kalugila

Mungu mkubwa... mama wa Lulu akifurahi baada ya mwanae kuachiwa kwa dhamana jana

Lulu akianza safari ya kwenda uswahilini jana






Sitaki kupigwa picha bana!






Lulu akisaidiwa na Dk Cheni kuanza safari yake ya uswahili, kulia mmoja wa wanahabari


MSANII Elizabert Michael 'Lulu' alionekana akicheka kwa furaha ya kuachiwa huru kwa dhamana kwa dakika chache jana alasiri akiwa na mama yake Lucrecia Kalugila, lakini muda mrefu baadaye wakajikuta wakibubujikwa na machozi bila kikomo ikiwa ni matokeo ya kuzidiwa na hisia za furaha hiyo. pia wakionekana kutoamini juu ya kile kilichotokea.
Msanii huyo nyota wa filamu nchini, ameachiwa kwa dhamana hatimaye baada ya kutimiza masharti aliyiopewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika kesi inayomkabili ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake nyota, marehemu Steven Kanumba.
Awali, mama huyo wa Lulu, ndugu, jamaa, marafiki na wasanii mbalimbali wa filamu nchini walionekana mahakamani tangu saa 2:30 asubuhi juzi, lengo likiwa ni kujua hatma ya mpendwa wao ambaye amekuwa akisota mahabusu tangu Aprili mwaka jana.
Baadaye, mama huyo alionekana kujawa na hisia kali kiasi cha kumwaga machozi yatokanayo na furaha aliyokuwa nayo baada ya mahakama kumuachia binti yake kwa dhamana na wote wawili kuonekana wakikumbatiana; kama watu wasioamini juu ya kile kilichotokea.

ILIVYOKUWA
Lulu mwenye miaka 18, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya bila kukusudia ya msanii mwenzake, Kanumba (28), aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti aliyopewa.
Msanii huyo alifikishwa saa 7:50 mchana akitokea mahabusu ya gereza la Segerea, akiwa katika ‘deffender’ jeupe la Magereza lenye namba za usajili STK 2823.
Mawakili wa pande zote walihakiki nyaraka za dhamana. Ilipofika saa 9:10 alasiri, Lulu alipandishwa kizimbani akiwa na wadhamini wake.
Mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Francis Kabwe, Lulu aliwawakilisha na wadhamini wawili, James Mboneka kutoka Wizara ya Afya na Florian Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi.
Saa 9:20, Lulu alikamilisha taratibu za mahakama na kuachiwa huru hatimaye ambapo mama yake (Lucrecia), ndugu, jamaa na marafiki zake walijikuta wakiangua kilio cha furaha.
Akizungumza baada ya kuwa huru kwa dhamana, Lulu alisema anamshukuru Mungu pamoja na watu wote walio pamoja naye katika kipindi chote kigumu.
"Sina la kusema... nawashukuru wote waliokuwa pamoja na mimi tangu nilipopata kesi hii. Ila bado nawaomba waendelee kuniombea kwa sababu nimepata dhamana tu, bado nina safari ndefu. Kesi  bado mbichi, niombeeni jamani," alisema Lulu huku akilia kabla ya kuondoka kwenye viunga vya mahakama hiyo akiwa ndani ya
gari lenye namba za usajili T 480 CFX, Toyota Land Cruser (V8) la rangi ya kijivu.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisema dhamana ni mchakato wa kisheria unaotakiwa kufuatwa katika mahakama na kwamba mteja wao amefanikiwa kupata dhamana na sasa wanasubiri wito wa mahakama wakati itakapopanga tarehe kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri wa kesi ya msingi.
Mapema Juzi, Jaji Zainabu Mruke alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo baada ya wakili wa utetezi Peter Kibatala kuwasilisha maombi ya dhamana kwa hati ya dharula chini ya kifungu cha 148 kidogo cha (1) na cha (2) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).
Jaji Mruke alisema kosa linalomkabili  mshakiwa lina dhamana kisheria na kwamba mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kufuata masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali watakaosaini  hati ya dhamana ya Sh. milioni 20 kila mmoja.
Alitakiwa pia awasilishe hati zake za kusafiria, kuripoti kila tarehe Mosi ya mwezi kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na asitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha msajili huyo.
Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa  Aprili 7, 2012, katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba bila kukusudia.

ZAMBIA WAVULIWA TAJI AFRIKA, NIGERIA HAOO ROBO FAINALI

Victor Moses wa Nigeria akikimbilia mpira wakati wa mechi yao dhidi ya Ethiopia leo, Nigeria walishinda 2-0 magoli yote yakifungwa na Moses kwa penalti.

Tumewavua ubingwa... Wachezaji wa Burkina Faso wakishangilia baada ya sare yao ya 0-0 dhidi ya Zambia iliyowavua ubingwa wa Afrika watetezi hao jana.

MABINGWA watetezi wa AFCON, Zambia 'Chipolopolo', wamevuliwa ubingwa kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya Burkina Faso, huku Nigeria wakivuka hadi robo fainali kwa magoli mawili ya penalti dakika za lala-salama na kuishinda Ethiopia waliomaliza 10 uwanjani.
Nigeria ambao walimaliza wakiwa wa pili nyuma ya Burkina Faso, watawakabili Ivory Coast katika mechi ya robo fainali inayotarajiwa kutazamwa kama fainali.
Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi alisema baada ya mechi hiyo kwamba ushindi wa jana aliusubiri kwa siku nyingi sana na anaamini utawapa faraja Wanigeria kote duniani.
"Kila mechi ina mbinu zake. Tutaingia kuwakabili Ivory Coast kwa mbinu tofauti na tulizotumia kuwakabili Ethiopia au hata tulizotumia katika mechi mbili zilizotangulia," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Nigeria wakati akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua wanajiandaaje kwa mechi ya ya robo fainali na mbinu gani watakazotumia. "Kuhusu mbinu tutakazotumia siwezi 'kushea' na wewe. Hizo nitashea na wachezaji wangu."
Zambia ambayo ilimuacha nje nahodha wao mhamasishaji, Chris Katongo, aliyewapa ubingwa wao wa kwanza wa Afrika mwaka jana, ilicheza kwa kiwango cha chini huku ikikosa makali katika umaliziaji huku straika wao Collins Mbesuma "akimpasia" kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama, kwa kishuti "mtoto" katika nafasi ya wazi zaidi waliyopata Chipolopolo.
Kocha Mfaransa, Herve Renard, aliyewapa ubingwa mwaka jana, alimuacha nje Katongo kutokana na madai ya kucheza chini ya kiwango katika mechi zao mbili za awali, maamuzi ambayo atayajutia.
Burkina Faso iliyocheza kwa kujilinda zaidi ikihitaji sare tu ili kusonga mbele, ilipata pigo la mapema baada ya kinara wa mabao wa fainali hizi, Alain Traore, kuumia katika dakika ya 10 na kutolewa kwa machela. Traore amefunga magoli matatu yakiwamo mawili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi yao ya pili.
Zambia pia walipata pigo dakika chache baadaye baada ya nyota wao Davis Nkausu kuumia 'enka' kufuatia kukanyagwa vibaya na nahodha wa Burkina Faso, katika tukio ambalo lilistahili kadi nyekundu lakini halikutoka hata onyo. Nafasi ya Nkausu ilichukuliwa na Joseph Musonda.
Burkina Faso wamemaliza vinara wa kundi hilo kwa kuwa na pointi tano, sawa na Nigeria walio katika nafasi ya pili kutokana na kuzidiwa magoli.
Hii ni mara ya kwanza kwa Burkina Faso kutinga raundi ya pili tangu walipoandaa michuano hiyo mwaka 1998.
Zambia "imefia" katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu baada ya sare tatu. Mabingwa hao walikuwa na maandalizi mabovu kwa kuchapwa mechi tatu, ikiwamo dhidi Tanzania kupitia goli pekee la Mrisho Ngassa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na sare moja katika mechi zao nne za kujipima kabla ya michuano hiyo.
Mabingwa kutolewa katika hatua ya awali, ni mara ya kwanza tangu mwaka 1992 wakati Algeria walipotolewa katika hatua ya makundi.
Winga wa Chelsea, Victor Moses, ndiye aliyekuwa shujaa wa Nigeria baada ya kufunga penalti mbili za dakika za lala salama na kuipeleka timu yake hatua ya robo fainali ambayo kama matokeo yangebaki ya 0-0 ingeaga mashindano.
Moses aliangushwa mara mbili ndani ya boksi na akafunga penalti zote mbili, ya pili langoni akiwa amesimama kiungo, Addis Hintsa, aliyelazimika kuvaa jezi ya kipa baada ya mlinda mlango wa Ethiopia, Sisay Bancha, kutolewa kwa kadi ya pili ya njano huku wakiwa tayari wameshamaliza orodha yao ya wachezaji wa kuwabadilisha uwanjani. 

BALOTELLI AKUBALI MIAKA MINNE NA NUSU AC MILAN

Balotelli

KLABU ya AC Milan wameafiki dili la kumsajili mshambuliaji Manchester City, Mario Balotelli kwa mkataba wa miaka minne na nusu, mkurugenzi wa klabu hiyo ya Italia, Umberto Gandini, amethibitisha.
Mfumania nyavu huyo wa zamani wa Inter Milan, Balotelli (22) atafanyiwa vipimo vya afya mjini Milan leo (Jumatano) kabla ya kusaini mkataba wake.
Ada ya awali ya uhamisho inaaminika kuwa ni paundi milioni 19 ambayo inasemekana imeshalipwa na huenda ikaongezeka kufikia paundi milioni 22.
Mchezaji huyo mwenye vituko ndani na nje ya dimba, ataondoka Manchester City huku akiwa ameweka gumzo baada ya mwishoni mwa mwaka jana kukwidana na kocha wake, Roberto Mancini wakati wa mazoezi, mbali na matukio mengine ya utata aliyowahi kuyafanya klabu hapo.
Mchezaji huyo

Thursday, January 24, 2013

Simba kuonyesha makali ya Oman leo Taifa

Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kushuka dimbani leo


MABINGWA wa soka nchini, Simba iliyorejea jana kutoka Oman ilipokuwa kwenye kambi ya mazoezi, inatarajiwa kushuka dimbani leo kuonyesha mambo ya umangani itakapovaana na Black Leopards ya Afrika Kusini katika pambano la kirafiki la kimataifa.
Pambao hilo litakalopigwa majira ya jioni kwenye dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam itakuwa pambano la mwisho kwa Simba kabla ya kuanza kwa duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Jumamosi.
Simba inatarajiwa kuanza duru hilo kwa kuvaana na African Lyon kwenye uwanja wa Taifa.
Black Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ipo nchini kwa ziara ya kujipima nguvu wakisubiri kuendelea na ligi yao iliyosimama kwa sasa kupisha michuano ya AFCON-2013 inayofanyika nchini mwao.
Timu hiyo jana iliendelea kuwa mnyonge kwa Yanga kwa kulazwa mabao 2-1 ikiwa ni siku chache tangu ichezee kichapo cha kukandikwa mabao 3-2.
Simba iliyoenda moja kwa moja kambini mara baada ya kuwasili jana mchana, imetamba kuwapa raha mashabiki wake ambao walimaliza duru la kwanza la ligi kuu kwa masononeko.
Mabingwa hao hiyo itakuwa mechi yao ya nne ya kujipima nguvu baada ya awali kucheza mechi tatu ughaibuni nchini Oman ikishinda mechi moja na kupoteza mbili.

Mashabiki wa soka wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo la leo ili kutaka kushuhudia makali ya timu yao, baada ya watani zao Yanga waliokuwa Uturuki, walivyokonga nyoyo za mashabiki wao kwa kuisasambua Blac Leopards mara mbili.

Wanachama Yanga waanza kugeukana, kisa...!

Ramadhani Kampira, mmoja wa wanachama wa Yanga



BAADHI ya wanachama wa Yanga wameibuka na kuelezea hofu waliyonayo juu ya kupitishwa kwa vipengele vya katiba inayowapa madaraka makubwa Mwenyekiti na Makamu wake klabu hapo.
Wanachama hao walisema kupitishwa kwa vipengele vinavyowapa viongozi hao uwezo wa kumfuta uanachama mwanachama yeyote wa Yanga ni sawa na kuruhusu udikteta pamoja na kuivuruga Yanga.
Mmoja wa wanachama hao, Ramadhani Kampira, alisema japo wanachama wenzake waliafiki vipengele hivyo katika mkutano mkuu ulioitishwa mwishoni mwa wiki, lakini ukweli hakubaliani navyo.
Kampira aliyewahi kuichezea timu hiyo na kung'ara na TAMCO Kibaha na Sifa United, alisema kuruhusu hali hiyo inaweza kutumiwa vibaya na viongozi katika suala la chuki binafsi.
"Mtu anaweza kuamka usingizi au kutoka nyumbani akiwa kagombana na mkewe kisha kuamua kumfukuzisha mtu uanachama kwa chuki na kusiwepo wa kuwahukumu kwa vile lipo kwenye katiba," alisema Kampira.
Naye Mwinjuma Muumini, ambaaye ni mmoja wa waimbaji nyota wa muziki wa dansi, alisema hakubaliani na maamuzi hayo japo alikiri hajui kitu gani kilichowakumba wanachama wenzake na kuafiki jambo hilo.
Muumini, anayefahamika kama 'Kocha wa Dunia' au 'Mzee wa Chelsea' alisema kuwa maamuzi hayo ni kurejesha ukoloni na kuruhusu udikteta katika Yanga kwani haikubaliki hata kwa sheria ya nchi.
"Sijajua ajenda za mkutano huo zilikuwa zipi, lakini kilichofanywa na wanachama wenzetu ni msiba ambao utakuja kuigharimu na kuivuruga Yanga mbele ya safari, huo ni udikteta,:" alisema.
Juu ya suala la kutimuliwa kwa wanachama wenzao waliokuwa waajiriwa wa klabu hiyo, Louis Sendeu na Celestine Mwesigwa, Kampira yeye alisema taratibu na sheria za kazi zizingatiwe na zisiingizwe katika masuala ya michezo.
"Wale walikuwa waajiriwa na kama walitimuliwa kazi bila kuzingatiwa taratibu au kulipwa haki zao stahiki, walikuwa na haki ya kutafuta jasho lao mahali pengine, hivyo suala hilo lisitumiwe kuwaonea watu waliotendwa sivyo ndivyo,": alisema Kampira.
Wanachama wa Yanga waliafiki kwa kauli moja kuwatimua uanachama akina Sendeu kwa madai ya kosa la kukimbilia mahakamani ya usuluhishi kudai haki zao za malimbikizo na misharaha.
Pia mkutano huo uliafiki kubadilishwa kwa vipengele vya katiba yao kwa kuwaruhusu viongozi hao wa juu kuwatimua wanachama mara watakapobainika kufanya makosa bila kusubiri maamuzi ya wengi.

Irene Paul amuibua Kalunde

Msanii Irene Paul


BAADA ya kutumikishwa katika kazi za wasanii wengine, mwanadada mkali wa Bongo Movie, Irene Paul 'Brown Eyes', amefyatua filamu yake binafsi ya kwanza kupitia kampuni binafsi aliyoianzisha hivi karibuni.
Msanii huyo, aliiambia MICHARAZO mapema leo kuwa, filamu hiyo mpya inafahamikwa kwa jina la 'Kalunde' na ipo njiani kuachiwa mtaani ikiwa imewashirikisha wasanii kadhaa nyota nchini.
Irene aliwataja wasanii hao walioshiriki filamu hiyo inayozungumzia masuala ya ndoa za utotoni na changamoto zake, ni pamoja na Grace Mapunda 'Mama Kawele', Hemed Suleiman 'PHD', Ahmed Olotu 'Mzee Chillo', yeye na Richard Mshanga 'Masinde'.
"Kwa mara ya kwanza nimeibuka na filamu yangu binafsi iitwayo 'Kalunde' ambayo mbali na kuigiza mie mwenyewe pia imewashirikisha wasanii kadhaa mahiri nchini kama akina Mzee Masinde, Mzee Chillo, Mama Kawele, Hemed na wengineo," alisema Irene.
Irene alisema kwa sasa anamalizia mambo fulani kabla ya kuitoa hadharani kuwapa mashabiki wake burudani ambayo wamekuwa wakimshuhudia katika kazi za watu wengine.
Muigizaji huyo aliyewajio kuwa mtangazaji na pia mwanamitindo, alisema filamu hiyo imezalishwa na kampuni yake binafsi iitwayo Krema Production na kazi hiyo ni mwanzo wa kudhihirisha kwamba yeye hajabahatisha kuingia katika fani hiyo.

Kabla ya kuipakua kazi hiyo binafsi, mwanadada huyo alishacheza filamu kama Shujaa, I Hate My Birthday, Unpredictable, The Shell, Handsome wa Kijiji, Triple L, Fikra Zangu na nyingine zinazozidi 15 tangu atumbukie kwenye fani hiyo mwaka juzi.

Zola D ana Swahili Hip Hop


Zola D katika pozi
MSANII nyota wa muziki wa hip hop nchini, David Mlope 'Zola D' anajiandaa kupakua albamu yake ya kwanza tangu atuimbukie kwenye fani hiyo itakayokuwa na nyimbo 21.
Akizungumza na MICHARAZO, Zola D, alisema albamu hiyo itafahamikwa kwa jina la 'Swahili Hip Hop' ambayo imekusanya nyimbo zake zote alizozifyatua tangu aingie kwenye fani hjiyo mwaka 1995.
Zola D alisema, baadhi ya nyimbo zitakazokuwa katika albamu hiyo ni pamoja na kibao kilichompa ujiko miaka kadhaa iliyopita cha 'Moto wa Tipper', 'Jana Sio Leo', 'Sipati Mchongo', 'What Going On', 'Hustler King', 'Unde', 'Msela Sana', Rap Gangster' na 'Rudi'.
Nyingine ni nyimbo zake mbili za hivi karibuni ambazo zinaendelea kutamba katika vituo vya redio na runinga za 'Coast to Coast' na 'Knockout' alioimba na P Funk.
"Nimeshakamilisha kila kitu kabla ya kuitoa hadharani albamu yangu itakayokuwa ya kwanza tangu nitumbukie katika fani hii miaka karibu 20 iliyopita, itakuwa na nyimbo za zamani na mpya ambazo baadhi zinaendelea kutamba nchini na nje ya nchi," alisema.
Msanii huyo ambaye pia ni bondia wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu akiwa pia amesilimu kutoka dini ya Ukristo akifahamika kwa jina la Daud, alisema mashabiki wake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiuulizia juu ya albamu hiyo waondoe shaka.

MBUNIFU ALLY REMTULLAH KUIPEPERUSHA BENDERA MAREKANI


Meneja Masoko wa Kampuni ya Tanzania Hair Industry ltd James Walwa – Jimmy akimkabidhi mbunifu wa mavazi nchini Ally Rehmtullah tiketi kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha Afrika Mashariki katika mkutano wa ‘The Economics of the Africa Fashion Industry’ utakaofanyika nchini Marekani mwezi wa Februari. Tanzania Hair Industry ltd ambao ndio watengenezaji wa nywele maarufu aina ya Darling ndio wadhamini wa safari ya mbunifu huyu kwenye mkutano huo wa kihistoria utakaofanyika katika Kikuu cha Havard nchini Marekani.
 
Mbunifu mahiri wa mavazi nchini Tanzania Ally Remtullah amechaguliwa kuiwakilisha Africa Mashariki katika ‘East Africa Fashion Industry’ kuongea katika mkusanyiko wa Afrika Business Conference utakaofanyika Harvard Business School nchini Marekani.
 
Akizungumza na Lenzi ya Michezo  jijini Dar es Salaam jana, Mbunifu huyo Remtullah amesema shughuli hiyo itakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Marekani cha Harvard ambacho ni kikubwa kuliko vyote duniani itafanyika Februari tarehe 15 mwaka 2013.
 
Akifafanua amesema kuwa kila mwaka Chuoni hapo kunafanyika mikutano ya ‘Africa Business Conference’ ikiwa na kauli mbiu tofauti na sasa mwaka huu yeye amechaguliwa kuwa mmoja wa wazungumzaji kuhusiana na ‘The Economic of Africa Fashion’.
 
Ally Remtullah amesema kwa ujumla anaiwakilisha Afrika Mashariki katika kategori hiyo ambapo anatarajiwa kuzungumzia changamoto zinazoikabili na fursa zinazopatikana katika tasnia ya fasheni Afrika Mashariki, ikiwemo tatizo la umeme na gharama za manunuzi ya vitambaa vya Pamba ambayo kimsingi huzalisha katika ukanda huu.
 
Amesema anafurahi kuchaguliwa na wandaaji hao kuziwakilisha nchi za Afrika Mashariki na sasa si kwenda tena kuonyesha mavazi, bali ni kuzungumza mbele ya wadau wakubwa wa kidunia kuhusu nafasi ya masuala ya ubunifu na uchumi.
Wazungumzaji wengine katika mkutano huo ni pamoja na mbunifu maarufu wa Afrika Magharibi Ituen Basi kutoka Nigeria.
 
Katika maandalizi hayo Ally amesema pamoja na kusoma vitu vingi kuhusiana na uchumi katika tasnia ya fasheni na gharama za uzalishaji za viwanda vya nguo, pia amekutana na wafanyabiashara wakubwa wa viwanda vya kutengeneza nguo hasa za kiafrika akiwemo Mfanyabiashara Mkubwa nchini Mh. Mohammed Dewji ambaye kwa namna moja ama nyingine amempa ushirikiano wa kutosha.
 
Safari hiyo ya mbunifu wa mavazi nchini Ally Remtullah katika mkutano mkubwa wa kihistoria wa Boston nchini Marekani, imedhaminiwa na kampuni ya Tanzania Hair Industry Ltd, ambao ni wazalishaji wa nywele maafuru aina ya Darling.

YANGA YAILIZA TENA BLACK LEOPARDS CCM KIRUMBA-MWANZA



Wachezaji wa timu Yanga wakifurahia goli la pili lililofungwa na Jerry Tegete kipindi cha pili mnamo dakika ya 54 kwa njia ya penati.


Golikipa wa timu ya Black Leopards,Posnett Omony akisota kuokoa mpira uliotinga wavuni kutoka kwa mchezaji wa timu ya Yanga Jerry Tegete kwa njia ya penati mnamo dakika ya 54.Timu ya Yanga imeibuka kifua mbele mpaka dakika 90 kwa kuinyuka goli 2-1 timu ya Black Leopards kwenye mchezo wao wa marudiano wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa CCM-Kirumba jijini Mwanza.Picha na JICHIE BLOG-jijini Mwanza.


Mchezaji wa timu ya Yanga David Luhende akitaka kumchomoka mchezaji wa timu ya Black Leopards, Moses Kwena, kwenye mchezo wao wa marudio uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jioni ya leo.


Pichani ni Golikipa wa Black Leopards Posnett Omony akijitahidi kuokoa mpira uliopigwa kwa kichwa na mchezaji wa Yanga, Said Bahanuzi na hatimaye kutinga kimiani mnamo dakika ya saba.


Mchezaji Hamis Kiza wa Yanga akifanya jitihada za kumtoka beki wa timu ya Black Leopards,Victor Kamhuka.


Mchezaji wa wa timu ya Yanga David Luhende akitaka kumtoka mchezaji wa timu ya Black Leopards, Moses Kwena, kwenye mchezo wao wa marudio uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.






Baadhi ya mashabiki wa Mpira wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya kununua tiketi na kujionea kandanda safi kabisa kati ya timu ya Yanga na Black Leopards ya Afrika kusini.


Kikosi cha Yanga kikiwa katika picha ya pamoja.


Sehemu ya umati wa watu waliokuwa wakishuhudia mchezo huo,ambapo timu ya Yanga imetoka kifua mbele goli 2-1 dhidi ya timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini, mchezo huo umechezwa leo kwenye uwanja wa CCM-Kirumba jijini Mwanza.


Mtanange ukikaribia kuanza.


Kikosi cha timu ya Black Leopards.


Benchi la ufundi la timu ya Yanga


Ilikuwa ni patashika nguo  kuchanika, mchezaji wa timu ya Yanga, Jerry Tegete akiwatoka baadhi ya mabeki wa timu ya Black Leopards, Jerry alifanikiwa kufunga goli la pili mnamo dakika ya 54 kipindi cha pili.





Nginja nginja tuu


Makocha wakipongezana mara baada ya mpira kuisha.


Sehemu ya Umati wa mashabiki wa timu ya Yanga.


Mashabiki wakiwa kwenye mstari kwa ajili ya kuingia uwanjani.