STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, May 6, 2013

Azam warejea, Hall ajifariji

Azam Fc

WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Azam kilichokuwa kinashiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho kikirejea leo mchana kutoka Morocco, kocha wa timu hiyo, Stewart Hall amesema kwamba wachezaji wake walipambana kusaka ushindi wa ugenini lakini bahati haikuwa yao.
Azam iliyotoka suluhu katika mechi ya ya kwanza hapa nyumbani, juzi ilifungwa magoli 2-1 na AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo na kutolewa.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Morocco jana mchana, Hall alisema kwamba wanaheshimu matokeo hayo na wanaamini kwamba mwakani wakipata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa watafanya vizuri zaidi ya msimu huu.
Hall alisema kwamba mchezo ulikuwa mgumu katika vipindi vyote na timu zote zilitengeneza nafasi lakini washambuliaji hawakuwa makini na kushindwa kutumia nafasi hizo.
"Tulipambana na tulijitahidi kuwakabili lakini matokeo hayakuwa mazuri katika upande wetu, ila wachezaji na mimi mwenyewe kuna mambo tumejifunza yatakayotusaidia kwa ligi ya nyumbani na mashindano mengine ya kimataifa tutakayoshiriki," alisema Muingereza huyo.
Afisa Habari wa timu hiyo, Jaffer Idd, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kitatua nchini saa 9:00 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates ambapo jana usiku walilala Dubai.
Alisema wachezaji na viongozi wote waliokuwa kwenye safari hiyo wako salama na wanarejea nchini na nguvu mpya kuhakikisha wanashinda mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilizobaki.
Azam iliyoshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ilifika raundi ya pili baada ya kuzitoa Al Nasri ya Sudan Kusini na baadaye Barrack Young Controllers ya Liberia.
Chanzo: NIPASHE

No comments:

Post a Comment