Cheka na Mashali walipopambana wiki iliyopita ukumbi wa PTA |
BONDIA Thomas Mashali amekiri kwamba mpinzani wake Francis Cheka alimzidi ujanja na kumnyuka katika pambano lao la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika, lakini akiapa ni lazima arudiane naye ili kulipiza kisasi.
Hata hivyo Cheka amejibu rai ya Mashali kwa kusema kuwa hawezi kurudiana na bondia huyo kwa madai imekuwa desturi kwa kila bondia anayepingwa naye kutaka kurudiana na kuendelea kuwanyuka, hivyo kiu yake ni kucheza na mabondia wa nje ya nchi.
Mashali alichezea kichapo na kusalimu amri katika raundi ya 10 kwa kupigwa KO katika pambano ambalo, Cheka alikuwa akitetea taji lake la IBF kwa mara ya tatu.
Bondia huyo aliyekuwa na rekodi ya kutopigika nchini, alisema anakubali Cheka alizimdi ujanja na kumtwanga, lakini haina maana yeye ni mbaya kwani ni kati ya mabondia wachache walioweza kukaribia kumaliza raundi zote kabla ya kuteleza raundi hiyo ya kumi.
"Nakubali kanizidi ujanja, Cheka ana nguvu mno na ndipo nilipokosea sikufikiria hilo, lakini kwa vile nimeshagundua makosa ninajipanga ili nirudiane naye tena mkoani Morogoro ili nilipize kisasi," alisema Mashali.
Cheka alipoulizwa juu ya tambo za Mashali, alisema hata kama atatokea promota wa kuandaa pambano hilo la pili hatakuwa radhi kupigana na Mashali kwa kuamini atampiga tu kama ilivyuotokea kwa mabondia wengine aliowadunda na kuomba kurudiana nao.
"Naona ni kupoteza muda, alitamba kabla ya kupigana nami kwamba yeye ndiye jibu la kuzuia vipigo kwa mabondia nchini mbele yangu, sasa nimempiga unadhani hata nikirudiana naye atafanya nini, itakuwa ni sawa na wenzake waliomtangulia, nataka kucheza mechi za kimataifa zaidi serikali inasaidie, nyumbani nimeshamaliza kazi," alisema Cheka.
No comments:
Post a Comment