Na Boniface Wambura
TIMU ya taifa ya soka, Taifa
Stars imepangwa kundi A la michuano ya Kombe la COSAFA ambapo itacheza
mechi yake ya kwanza Julai 6 mwaka huu jijini Lusaka, Zambia dhidi ya
Shelisheli.
Upangaji
ratiba (draw) wa mashindano hayo ulifanyika juzi (Mei 3 mwaka huu)
jijini Lusaka ambapo timu nyingine zilizo na Taifa Stars katika kundi
hilo ni Namibia na Mauritius. Kundi la Taifa Stars litachezea mechi zake
jijini Lusaka.
Mechi
ya pili ya Taifa Stars katika hatua ya makundi itakuwa Julai 8 mwaka
huu dhidi ya Mauritius. Mechi ya mwisho katika hatua hiyo itakuwa Julai
10 mwaka huu dhidi ya Namibia.
Kundi
B lina timu za Kenya (Harambee Stars), Botswana (Zebras), Lesotho na
Swaziland. Hatua itakayofuata baada ya hapo ni ya mtoano (knockout) na
kila kundi litatoa timu moja tu.
Iwapo
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itafuzu kwa
hatua itakayofuata itacheza Julai 13 mwaka huu na Afrika Kusini (Bafana
Bafana) ambayo pamoja na timu nyingine tano zimekwenda moja kwa moja
katika hatua ya mtoano.
Nyingine
zilizokwenda moja kwa moja hatua ya mtoano ni wenyeji Zambia, Angola,
Zimbabwe, Msumbiji na Malawi ambazo kwenye viwango vya ubora vya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ziko juu ya zile
zilizoanzia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA itafanyika Julai 20 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment