Warembo wa Miss Utalii Tanzania wakiwa katika pozi |
JUMLA ya warembo 28 wanatarajiwa kuchuana kwenye shindano la kuwania taji la urembo la taifa la utalii, 'Miss Utalii Tanzania', litakalofanyika Jumapili ijayo (Mei 12) mkoani Tanga.
Warembo tayari wameshatua mkoani Tanga kujiandaa na fainali hizo ambazo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kagasheki.
Akizungumza kwa simu kutoka Tanga, Rais wa Miss Utalii Tanzania, Gideon Chipungahelo alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na kwamba warembo watakaochuana wanaendelea vyema na maandalizi.
Chipungahelo maarufu kama 'Chipps' alisema walishatuma barua ya mualiko katika ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwa ajili ya kumuomba waziri awe mgeni rasmi na wakati wanasubiri majibu, ni matarajio yao kwamba atawakubalia ombi lao.
"Tunatarajia Waziri Dk Kagasheki ndiye atakayekuwa mgeni rasmi wa fainali zetu kwani tumeshatuma ombi na barua ya mualiko katika ofisi yake na kwa sasa tunasubiri majibu," alisema.
Chipps alipoulizwa sababu ya kupungua kwa idadi ya washiriki wa shindano hilo kutoka 40 hadi 28, alisema imetokana na baadhi ya warembo kukatishwa tamaa na danadana za kufanyika kwa fainali hizo kulikosababishwa na ahadi zilizoyeyuka za wadhamini wao.
"Idadi imepungua kwa vile wengine walikata tamaa walipoona fainali zikibadilika tarehe kila mara baada ya wadhamini na wafadhili tuliokuwa tukiwategemea kutuacha solemba kabla ya kupigwa tafu na kulihamishia Tanga badala ya kufanyika jijini Dar es Salaam," alisema.
No comments:
Post a Comment