John Bocco 'Adabayor' anayawania tuzo ya Mwanasoka Bora |
Emmanuel Okwi anayewania tuzo ya mwanasoka bora kutoka nje ya nchi |
WASHAMBULIAJI Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na John Bocco wa Azam ni miongoni mwa nyota sita walioteuliwa kuwania "Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka 2012" inayoandaliwa ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) itakayotolewa mwezi ujao, imefahamika.
Taarifa iliyotolewa jana na mwenyekiti wa kamati ya TASWA kusimamia tuzo za wanamichezo bora wa Tanzania mwaka 2012, Haji Manara, iliwataja nyota wengine waliong'ara katika kipengele cha kuwania tuzo ya mwanasoka bora kuwa ni mshambuliaji Mcha Khamis wa Azam, beki Kelvin Yondani (Yanga) na beki kisiki wa Simba, Shomari Kapombe ambaye atakuwa akiiwania tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa majina ya nyota hao wa soka wanaume yamependekezwa na kamati ya tuzo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutowapatia majina hayo. Nyota wa michezo mingine waliopendekezwa kuwania tuzo (isipokuwa mpira wa kikapu), wote wamependekezwa na vyama vyao na hafla ya kutangaza washindi na kuwapa zawadi itafanyika mwanzoni mwa Juni.
Kwa soka la wanawake, walioteuliwa kuwania tuzo ni Fatuma Mustafa, Asha Rashid,
Mwanahamisi Omar, Sophia Mwasikili na Ester Chabruma 'Lunyamila'.
Nyota wanaowania tuzo katika kipengele cha wachezaji wa nje wanaocheza Tanzania ni Emmanuel Okwi aliyekuwa Simba (sasa Etoile du Sahel ya Tunisia), Kipre Tchetche(Azam),
Haruna Niyonzima (Yanga), Hamis Kiiza (Yanga) na mcheza netiboli Mary Waya wa klabu ya Filbert Bayi.
Wachezaji wanaowania "Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka 2012" ni
Salum Abubakar 'Sure Boy' (Azam), Frank Domayo (Yanga), Edward Cristopher (Simba), mcheza tenis Emmanuel Malya wa klabu ya Gymkhana ya Arusha na mcheza kriketi Tambwe Juma.
Majina ya Samatta na Ulimwengu yamejitokeza pia katika kipengele cha wanaowania tuzo ya mchezaji bora Mtanzania anayecheza nje ya nchi. Wengine wanaowania tuzo hiyo ni kipa Ivo Mapunda-wa klabu ya soka ya Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, nyota wa mpira wa kikapu Hasheem Thabeet anayecheza Oklahoma City Thunder inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (NBA), mchezaji wa mpira wa kikapu Soud Abdulrazak (Uganda) na Mohamed Abdallah ‘Dulah’ ambaye pia anacheza mpira wa kikapu nchini Uganda.
Wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mpira wa magongo (wanaume) ni Sylvester Kigodi, Casto Mayuma, Gurtej Bilu Singh, Vendri Bhamra na Elias Samala wakati nyota wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa gofu ya kulipwa ni Hassan Kadio, Yassin Salehe, Fadhili Nkya, Salim Mwanyenza na Rajabu Iddy.
Walioteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa ridhaa wa gofu (wanawake) ni Madina Iddi, Angel Eaton, Hawa Wanyanche na Ayne Magombe. Nyota wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa gofu ya ridhaa wanaume ni Jimmy Mollel, Frank Roman, Nuru Mollel,
Martin MacDonald na John Said.
Katika ngumi za ridhaa (wanaume), walioteuliwa kuwania tuzo ni Ismail Isack Galiatano, Said Hofu, Selemani Kidunda, Victor Njaiti na Mohamed Chibumbui wakati ngumi za ridhaa wanawake ni Sara Andrew, Irene Kimaro, Easter Kimbe, Mather George na Mariam Nyerere.
Nyota wanaowania tuzo ya mwanamichezo bora wa ngumi za kulipwa ni Francis Miyeyusho, Ramadhan Shauri, Thomas Mashali, Said Mbelwa na Francis Cheka.
Katika mchezo wa judo (wanaume), wanaowania tuzo ni Ahmed Magogo, Andrew Thomas Mlugu, Geofrey Edward Mtawa, Gervas Leonard Chilipweli, Abuu Selemani Mcheteko na Aboubakar Nzige. Judo wanawake Tanzania Bara ni Matrida Temba, Amina Mohamed wakati judo wanaume Zanzibar ni Mohamed Khamis Juma, Masoud Amour Kombo, Mbarouk Suleiman Suleiman. Judo wanawake Zanzibar ni Grace Alphonce na Laylat Mohamed.
Wanaowania tuzo ya mcheza tenis bora (wanawake) ni Rehema Athumani, Vailety Petar, Mkunde iddi, Edna John na Zuhura Baraka huku tenis wanaume wakiwa ni Omary Abdallah, Yassin Shaaban, Hassan Kassim, Kiango Kipingu na Lebric Jacobu.
Ushindani mkali unatarajiwa kuonekana katika kumpata mshindi wa tuzo ya mwanariadha bora wa kike ambayo watakaochuana ni Zakia Mrisho, Mary Naali, Jacklin Sakilu, Sarah Ramadhani, Sara Maja na Anjelin Tsere. Wanariadha wa kiume wanaowania tuzo ni Dickson Marwa, Faustine Mussa, Augstino Sule, Bazil John na Samson Ramadhan.
Michezo mingine ambayo tuzo zake zitawaniwa ni mpira wa mikono, kriketi, mpira wa kikapu na netiboli ambayo itawaniwa na Lilian Sylidion wa Filbert Bayi, Mwanaidi Hassan (JKT), Irene Elias Kanile (Filbert Bayi), Jacqueline Sikozi (Filbert Bayi) na Faraja Malaki wa Jeshi Stars.
"Tuzo ya heshima itatangazwa ukumbini... mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka 2012 atapatikana miongoni mwa washindi wa kila mchezo," imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Manara, ikifafanua zaidi kuwa sherehe zitafanyika mwanzoni mwa Juni.
Kapombe wa Simba ndiye aliyeibuka mshindi wa "Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA Mwaka 2011". Wengine waliowahi kuibuka washindi wa jumla wa tuzo hiyo ni Mwanaidi Hassan (2009 na 2010), Mary Naali (2008), Martin Sulle (2007) na Samson Ramadhan (2006).
No comments:
Post a Comment