Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema tukio hilo la mauaji ya kutisha lilitokea jana majira ya saa kumi na moja jioni nyumbani kwa marehemu.
Alisema siku moja kabla ya mauaji hayo alifika mtu mmoja nyumbani kwa marehemu na kuomba kibarua cha kutengeneza zizi la ng’ombe na ndipo alipokubaliwa na kuanza kazi ambayo hakuimaliza siku hiyo.
Kidavashari alieleza siku iliyofuata kibarua huyo alifika nyumbani kwa marehemu akiwa na kijana mwingine mbaye alionekana kumsaidia kazi hiyo hata marehemu alielewa hivyo.
Alisema ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni marehemu akiwa amelala kwenye jamvi pembeni ya nyumba yake mke wake mdogo aitwaye Tatu Shiranga alimuaga marehemu kuwa anakwenda mtoni kuteka maji na alimuacha marehemu akiwa na vibarua hao pamoja na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka saba.
Baada ya mke wake kuondoka vibarua hao walimfuata mahali alipokuwa amelala marehemu na kuanza kumkatakata kwa shoka kichwani, shingoni na kwenye bega, hali ambayo ilisababisha mwanae huyo mdogo akimbie mbio na kujificha kichakani huku akiwa akishuhudia wanavyomshambulia baba yake na alishindwa kuomba msaada kwa majirani kutokana na wao kuishi mbali na majirani.
Alisema mke wa marehemu alilazimika kwenda kuangalia pale ambapo alikuwa amemuacha mumewe amelala na ndipo alipomkuta akiwa amegalagala chini huku mwili wake ukiwa na majeraha makubwa na damu zikiwa zimetapakaa huku akiwa amefariki dunia.
Alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi baada ya kumhoji mke mdogo wa marehemu na ndugu zake kifo hicho kimesababishwa na sababu mbambali zilizotokana na tabia ya ukorofi na ubabe wa marehemu kwa majirani na ndugu zake.
Marehemu wakati akiishi katika Kijiji cha Mtowisa Mkoa wa Rukwa hapo mwaka 2012 aliwahi kuvamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa mapanga na kuponea chupuchupu na nyumba yake kuchomwa moto na ndipo baada ya hapo marehemu aliamua huhamia katika kijiji hicho mkoani Katavi.
Kamanda Kidavashari alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na jitihada za kuwasaka watu waliohusika katika mauaji ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria zinaendelea.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment