Suarez akishangilia moja ya mabao yake na wachezaji wenzake wa Liverpool jioni hii. |
LIVERPOOL imeendelea kuonyesha nia yake ya kuwania ubingwa wa Ligi ya England baada ya kupata ushindi mnono nyumbani kwa kuilaza Fulham mabao 4-0, huku Southampton wakipata ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Hull City, wakati vijana wa darajani Chelsea wakichomoa kipigo nyumbani dhidi ya West Brom.
Mabao mawili ya 'mtukutu', Luis Suarez na jingine la kujifunga la wageni na lile la Matrin Skrtel yalitosha kuipa ushindi huo mnono kwenye uwanja wao wa Anfield na kufikisha pointi 23.
Chelsea nao wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Stanford Bridge iliponea chupuchupu kwa kuchomoa bao la pili dakika za nyongeza na kutoa sare ya 2-2 na wageni wao West Bromwich.
Chelsea walianza kutangulia kupata bao kupitia kwa Samuel Et'oo aliyeendelea kufunga mabao ya 'miujiza' katika kipindi cha kwanza kabla ya wageni kurejesha mabao hayo na kuelekea kama wangeibuka na ushindi kabla ya wenyeji kuchomoa kwa mkwaju wa penati Eden Hazard, ambayo hata hivyo ilionekana kama siyo penati kutokana na Ramires kujiangusha miguuni mwa beki wa West Brom dakika za nyongeza.
Nayo Southampton waliendelea kuonyesha maajabu katika ligi hiyo kwa kuinyuka Hull City mabao 4-1, wakati Aston Villa wakiifumua Cardiff City kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na katika kipindi cha pili la Leandro Bacuna na Libor Kozak.
Everton ikiwa ugenini ilishindwa kufurukuta baada ya kulazimishwa suluhu na wenyeji wao Crystal Palace.
Ligi hiyo inaendelea hivi kwa pambano moja kati ya Norwich City na West Ham United na kipute kingine kitaendelea kesho kwa michezo kadhaa huku pambano linalosubiriwa kwa hamu likiwa kati yua Arsenal dhidi ya manchester United na Tottenham itakayoumana na Newcastle United.
No comments:
Post a Comment