STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 27, 2013

Majina ya mikopo ya wanavyuo 2013-2014 yatoka Bil 306 zatengwa

NOTICE TO SUCCESSFUL LOAN APPLICANTS FOR 2013/2014 ACADEMIC YEAR

The Higher Education Students’ Loans Board is hereby announcing names of successful first time loan applicants for 2013/2014 Academic Year who applied and were eligible for student loans.

The list includes the Institution to which the student is admitted to and the amounts of loans allocated to a particular student in all or part of the loanable items as per Guidelines and Criteria for Issuance of Loans and Grants for 2013/2014 Academic Year.

Loan applicants can access their loan status by keying in their Form Four Index Numbers to view the results. Loan applicants are reminded that the loan money will be sent to their respective institutions where they will be required to sign to acknowledge receipt of the loans, after registration processes.


Issued by:
The Executive Director
Higher Education Students’ Loans Board
P. O. Box 76068
Ebu Chungulia hapa http://olas.heslb.go.tz/  

Source:JF

Miss Tanzania 2012 afanya kweli Miss World, kivipi?

Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred
  MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la dunia (Miss World), Brigitte Alfred, amefanya kweli baada ya kufanikiwa kutwaa nafasi ya tatu katika shindano dogo la Beauty with a Purpose.
Mrembo huyo, anatarajiwa kupanda jukwaani leo huko Bali, Indonesia kuwania taji la Miss World.
Taji la Beauty with a Purpose limetwaliwa na Ishani Shrestha wa Nepal na kilichomfanya Brigitte ashike nafasi hiyo ni kutokana na video aliyoiwasilisha kuhusu kazi alizofanya kwa jamii hapa nchini.
Video aliyoiwasilisha Brigitte ilionyesha kazi ya jamii aliyoifanya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi.
Nafasi ya pili ilichukuliwa Erin Holland wa Australia, huku lile la ‘Top Model’ likitwaliwa na Megan Young wa Ufilipino, Jacqueline Steenbeek wa Uholanzi akatwaa la michezo, Sancler Frantz wa Brazil akachukua la ‘Beach Fashion’, Vania Larissa wa Indonesia alitwaa la Miss World Talent na Navneet Dhillon wa India akatwaa la Multimedia.
Washindi watano katika mashindano hayo madogo wana uhakika wa kuingia hatua inayofuata, huku Brigitte kwa nafasi hiyo ikiwa imemsaidia kwa kiwango kikubwa kujiamini kwa kusonga mbele.
Brigitte anashiriki fainali leo, huku akiwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anafuata nyayo za Nancy Sumari aliyefanikiwa kutwaa taji la Afrika katika mashindano ya Miss World ya mwaka 2005.
Akizungumza kutoka Indonesia, Brigitte alisema, wengi walifurahi kazi yake aliyopeleka ambayo ilionyesha pia kwa kiasi kikubwa jinsi watu wenye ulemavu wa ngozi wanavyohitaji msaada, hasa kutokana na kuwindwa na baadhi ya watu.
“Waliipenda kazi yangu, lakini kwa shindano la kesho (leo) nina uhakika mkubwa wa kufanya vizuri, kwani vigezo vyote ninavyo na nimejiandaa kwa muda mrefu mno.
“Niseme wazi nimejiandaa kwa muda mrefu mno na nashukuru wote walionisaidia kwa njia moja au nyingine na hii inanipa moyo wa kufanya vizuri zaidi,” alisema.
Wakati akimuaga Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alimtaka ahakikishe anaipeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kufanya vyema katika mashindano hayo.
“Fahamu fika kwamba unakwenda Indonesia kama Miss Tanzania na si Brigitte, hivyo unatuwakilisha Watanzania wote, sisi tuko nyuma yako unachotakiwa ni kujiamini tu na utafanikiwa.”
Mrembo huyo alifanikiwa kulitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania mwishoni mwa mwaka jana, akitokea kitongoji cha Sinza na Kanda ya Kinondoni.
Taji la Miss World linashikiliwa na mrembo Wenxia Yu kutoka China, ambaye tayari alikuwa Indonesia kwa ajili ya kulivua taji hilo.
Redd’s Miss Tanzania kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)

Mrisho Ngassa amaliza ubishi, Ruvu Shooting waapa

Mrisho Ngassa
KIUNGO Mrisho Ngassa ameamua kukata mzizi wa fitina baada ya kulipa jkiasi cha Sh. Mil. 45 kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwa ni sehemu ya malipo ya deni alilotakiwa kulipa ili aweze kuitumikia klabu yake ya Yanga

Mkali huyo amelipa deni hilo kama sehemu ya adhabu aliyokuwa amepewa na TFF kwa kosa la kusaini mkataba wa kuichezea Simba kisha kuitosa na kukimbilia Yanga, adhabu nyingine kusimamishwa kucheza mechi sita ambazo alishazimaliza.

Nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars baada ya leo kulipa deni hilo sasa Ngassa anaruhisiwa kuanza kuichezea timu yake.

Ngassa anatarajiwa kuanza kuonekana kesho uwanja wa Taifa katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, ambao wameapa kesho kuendeleza machungu kwa wanajangwani.

Pambano hilo litachezwa kesho ikiwa ni kati ya mechi nne zitakazochezwa katika mfululizo wa Ligi kuu Tanzania Bara.

Tetesi: Kigogo wa CCM aliyenaswa na 'unga' China ahofiwa kunyongwa

Mfano wa Dawa za Kulevya
ZIPO tetesi zinazodai kwamba kigogo mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya kupitia Jumuiya ya wanawake, anayedaiwa kukamatwa nchini China akiwa na kinachodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya hivi karibuni, anahofiwa kunyongwa.
Hofu hiyo imekuja kutokana na kilichoelezwa kuwa sheria ya nchi hiyo kuhusu dawa za kulevya ni kali na kwamba juhudi zinafanywa kufuatilia tetesi hizo kama zina ukweli na tutaweka hadharani mpaka jina la mhusika.
 
 Kalulunga media

Thursday, September 26, 2013

Maafa mengine Kenya, Polisi wawili wauwawa

Moshi ukifuka kutoka jengo la Westgate.
POLISI wawili wameuawa wakati watatu wakijeruhiwa mapema leo baada ya kuvamiwa na kundi linalodaiwa kuwa la  Al-Shabab.
Tukio hili limetokea wakati Wakenya wakiwa katika maombolezo ya siku tatu kuwakumbuka watu zaidi ya 60 waliopoteza maisha na 175 kujeruhiwa katika shambulio la Jumamosi iliyopita kwenye jengo la biashara la Westgate.
Shambulio hilo limetokea mapema leo katika kituo cha ulinzi kilichopo karibu na mpaka wa Somalia, mjini Mandera.
Kamanda wa Polisi, Charlton Mureithi ameeleza kuwa mbali na polisi wawili kuuawa na watatu kujeruhiwa kundi hilo limechoma magari 11.
Tukio hili limetokea saa chache baada ya kundi la Al-Shabab kutoa taarifa kuwa mashambulio yataendelea mpaka Kenya watakapoondoa wanajeshi wake nchini Somalia.
Kiongozi wa kundi hilo, Ahmed Godane Shaykh Mukhtar Abu Zubayr, alitoa onyo kwa Wakenya kuwa hakuna njia yoyote wangeweza "kuhimili vita ya kulipa kisasi ndani ya nchi yao wenyewe" katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao jana Jumatano.
"Chagua kuondoa majeshi yenu yote,.." Godane alisema. "Vinginevyo jiandae kwa wingi wa damu itakayomwagika nchini kwenu, anguko la kiuchumi na makazi."

TANZIA! Mwanahabari Venance George afariki dunia


TASNIA ya Habari imepata pigo baada ya Mwandishi wa Habari wa magazaeti ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited mkoa wa Morogoro, Venance George (Pichani anayeangalia kamera) kufariki dunia leo mchana katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa toka Morogoro marehemu aliyewahi kuyaandikia pia magazeti ya Uhuru na Mzalendo alifariki na mipango ya mazishi inaendelewa kufanywa na familia yake ikishirikiana na MCL.
MICHARAZO inatoa pole kwa familia, ndugu na jamaa pamoja na wanahabari wote hususani kampuni ya MCL kwa msiba huo na inawatakia subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa kuwakumbusha 'mwenzetu katangulia nasi tu nyuma yake'
'BWANA AMETOA NAYE NDITYE ALIYETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE'

Credit:Juma Mtanda

Kamati TFF yawakomalia Shafii Dauda na wenzake

Shafii Dauda mmoja ya waliotoswa jumla ya TFF
KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza hukumu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake kwa kumsafisha mlalamikiwa mmoja, kutowaadhibu zaidi washtakiwa sita na kuahirisha kusikiliza shauri moja baada ya mlalamikiwa kutokuwepo.
Riziki Juma Majala, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ndiye pekee aliyesafishwa na Kamati ya Maadili dhidi ya mashtaka ya kutoa kauli zilizosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya TFF.
Vilevile Kamati imesita kuwachukulia hatua Shafii Dauda, Nazarius Kilungeja, Wilfred Kidao, Omar Isaak Abdulkadir na Kamwanga Tambwe kutokana na kuridhika kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi, hivyo hawawezi kuadhibiwa mara mbili.
Pia imesema haiwezi kumuadhibu Richard Julius Rukambura, aliyeshtakiwa kwa kukiuka Katiba ya TFF kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, baada ya kubaini kuwa si mwanafamilia wa TFF kutokana na kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Hoja hiyo pia ilitumika kutomchukulia hatua Dauda na mwamuzi wa zamani Omar Abdulkadir kwa hoja kuwa walipoteza sifa za kuwa wanafamilia wa TFF baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi.
Shauri la Omary Mussa Mkwaruro la tuhuma za kutumia cheti cha elimu kisichotambuliwa na mamlaka husika, limeahirishwa kutokana na Mlalamikiwa kutowasilisha utetezi wake, hivyo Kamati imeagiza Sekretarieti kuwasiliana naye ili awasilishe maelezo yake.
Watu hao walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF na baada ya usaili walibainika kuwa na matatizo ya kimaadili, hivyo ili iamue juu ya hadhi yao katika familia ya mpira wa miguu kwa kuwachukulia hatua au kuwaweka huru.
Katika hukumu iliyotolewa leo (Septemba 26 mwaka huu), Kamati ya Maadili imeeleza kuwa Majala hakiuka Kanuni za Maadili kwa kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na TFF vinaonyesha kuwa klabu ya Kiluvya United imesajiliwa na Serikali na vyama wanachama wa TFF.
Kuhusu Rukambura, ambaye alilalamikiwa kwa kuipeleka TFF kwenye mahakama ya kiraia, hivyo kukiuka Kanuni ya 73 (3) (b) ya Kanuni za Maadili, Kamati imesema ushahidi uliowasilishwa na TFF hauonyeshi kama mgombea ni mwanafamilia wa TFF; alishaondolewa katika uchaguzi na hivyo si kati ya wagombea na hivyo mikono ya Kamati kufungwa kwa mujibu wa kanuni ya pili ya Kanuni za Maadili.
Kamati pia imeeleza kuwa Kanuni ya 73 (3) ambayo ingepaswa kutumika kumchukulia hatua, chimbuko lake ni Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF ambayo inawalenga wanachama tu na hivyo kuamua kuwa malalamiko hayo hayana mashiko na kwani Rukambura alishapoteza sifa za kuwa mwanafamilia na hivyo kushindwa kumchukulia hatua.
Kidao alishtakiwa kwa kosa la kumiliki nyaraka za Kamati ya Utendaji kinyume na taratibu na pia kuwasilisha malalamiko yake Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) bila ya kufuata taratibu, lakini Kamati imesema kwa vile mlalamikiwa ameenguliwa kwenye uchaguzi, anatumikia adhabu ya kinidhamu na hivyo haiwezi kumuadhibu mara mbili.
Kuhusu Shafii Dauda, Kamati imesema malalamiko dhidi yake hayana mashiko kwa kuwa si mwanafamilia wa TFF na kwamba lalamiko dhidi yake linatupiliwa mbali kwa kuwa tayari ameshaondolewa kwenye uchaguzi kutokana na kosa la kinidhamu.
Kamati iliona hakukuwa na haja ya kushughulikia mashauri dhidi ya Nazarius Kilungeja, ambaye alishtakiwa kwa kukaidi maagizo ya vyombo halali vya TFF, na Kamwanga Tambwe kwa kuwa tayari wawili hao wanatumikia adhabu ya kufungiwa na Kamati ya Nidhamu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Simba yamruka Okwi yatoa ufafanuzi ujio wake Dar

Emmanuel Okwi enzi akiichezea Simba
KLABU ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwa umma kuhusu masuala yanayoihusu kwa sasa.

Kuhusu Emmanuel Okwi

KATIKA siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimeripoti kuhusu uwepo nchini wa aliyekuwa mchezaji wa zamani wa klabu, Emmanuel Arnold Okwi kutoka nchini Uganda.

Taarifa hizo zimeeleza mambo mbalimbali ikiwamo taarifa kuwa Simba Sports Club ina mawasiliano na mchezaji huyo na alikuja kwa mwaliko wa viongozi wa klabu. Baadhi ya vyombo vimekwenda mbali zaidi na kudai kuwa uongozi wa Simba unamshawishi mchezaji huyo avunje mkataba wake na klabu anayoichezea sasa ya Etoile du Sahel  (ESS) ya Tunisia.

Klabu inapenda kuuarifu umma kwamba Simba au kiongozi wake yeyote (Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Sekretarieti haijahusika kwa namna yoyote ile na ujio wa mchezaji huyo hapa nchini. Hakukuwepo na mwaliko rasmi au usio rasmi kwa viongozi wa Simba.

Taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na uongozi wa Simba ni za upotoshaji na zina lengo la kuharibu heshima na hadhi ambayo uongozi huu umeijenga kitaifa na kimataifa kwenye tasnia ya soka.

Hata hivyo, kisheria, Simba haiwezi kumzuia mchezaji huyo kusafiri kwenda nchi yoyote anayotaka kama amefuata sheria zote za uhamiaji. Mchezaji huyo ana mkataba na timu nyingine na Simba haihusiki na safari zake, matembezi yake au mipango yake ya kimaisha.

Uongozi wa Simba unafahamu kwamba Okwi ni mchezaji halali wa ESS maana wenyewe ndiyo uliomuuza kwa klabu hiyo. Kwa mujibu wa sheria za FIFA, klabu yeyote, ikiwamo Simba SC, haziruhusiwi kufanya mawasiliano na mchezaji huyo au yeyote yule halali wa klabu nyingine bila ruhusa ya klabu yake kama mkataba wa mchezaji husika umebakiza kipindi kinachozidi miezi sita. Hii maana yake ni kwamba uongozi hauwezi kumshawishi mchezaji huyo kujiunga na klabu.

Ikumbukwe kwamba hadi sasa, klabu ya Simba, inaidai klabu ya Etoile du Sahel kiasi cha dola za Marekani 300,000 (laki tatu) ambazo zinapaswa kuwa zimelipwa kabla ya tarehe 30 mwezi huu wa tisa mwaka 2013. Kinyume cha hapo matokeo mengine yataamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya FIFA ambapo makubaliano husika yalisajiliwa.

Uongozi wa Simba ungeomba vyombo vya habari na watu binafsi waache kutoa taarifa zozote za kuhusisha ujio wa Okwi na klabu au kwamba kuna mipango ya kumshawishi avunje mkataba wake kwani taarifa hizo hazina ukweli wowote.

Imetolewa na

Ezekiel Kamwaga,
Ofisa Habari,
Simba Sports Club

'Ulimbukeni unawasumbua wana hip hop'


Ile Ile
MSANII anayezidi kuja juu nchini katika muziki wa Hip Hop, Maishani Ndee 'Ile Ile' amedai ulimbukeni na kutaka kuiga kila kitu toka Marekani ndiko kunakowasumbua baadhi ya wasanii wa miondoko hiyo na kudiriki kujihusisha na matukio ya kibabe.
Ile Ile alisema siyo kweli kama mtu kuwa msanii wa hip hop ni lazima awe mtemi, mfanya fujo na anayejihusisha na matumizi ya pombe au dawa za kulevya isipokuwa wanaofanya hivyo wanasumbuliwa na kasumba ya kuiga mambo tu.
"Binafsi sikubaliani na mambo yanayofanywa na baadhi ya wasanii wa miondoko ya Hip Hop ya kufanya fujo, kujitia wababe na matukio mengine ya ovyo, naamini wanaofanya hivyo wanasumbuliwa na ulimbukeni wa kuiga kila jambo bila kujali kama ni zuri au la ama linaloendana na utamaduni wa Kitanzania," alisema.
Ile Ile anayetamba na nyimbo kama 'Ile Ile', 'Bora Liende' na 'Wazazi' aliouachia hivi karibuni, alisema mila na tamaduni za hip hop ni amani na upendo na kukomboa wengine sna kuhoji ni vipi sasa wanahip hop kupenda kuwanyanyasa wengine.
Alisema ni lazima wasanii wa miondoko hiyo wajaribu kuepuka mambo hayo ambayo alidai yanachangia kuufanya muziki huo kuchukuliwa kama wa wahuni ilihali karibu dunia nzima inakombolewa na harakati za wanahip hop.
Msanii huyo alisema pia japo kila mtu ana uhuru wake wa kutumia kitu chochote, bado wasanii wanapaswa kuepuka matumizi ya ulevi na dawa za kulevya kwani ndizo zinazochangia wengi wao kuwa wakorofi na kuharibu sifa za hip hop.

Ajali tena! moja afa kwa kugandamizwa na gari wanne hoi


Mwili wa kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Rashidi Seleman mkazi wa Isevya manispaa ya Tabora ambaye amepoteza maisha baada ya Lori walilokuwa wamepanda kuanguka eneo la Inala barabara ya kwenda Kigwa.
Polisi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye amekimbia huku watu wengine wanne wakiwa wamejeruhiwa vibaya ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kitete.


Tatizo la ukosefu la ukosefu wa vifaa vya kuokolea vilisababisha maiti ya mtu huyo kukaa muda mrefu akiwa amebanwa na Lori hilo ambalo ni mali ya kampuni ya mkandarasi JOSSAM




Awali jitihada za Polisi na wananchi ziligonga mwamba na kubaki wakiiangalia maiti hiyo pasipo msaada wowote ajali ambayo imetokea majira ya saa kumi jioni hapo jana.


Askari wa usalama barabarani wakiongozwa na kamanda wa Polisi kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Tabora Bw.Swaleh Digega hatimaye wakafanikiwa kuutoa mwili wa marehemu huyo na kuupeleka hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya kuuhifadhi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Sumatra wanakusudia kumfikisha mahakamani mmiliki wa Lori hilo kwa kitendo cha kusafirisha mizigo na wanadamu katika gari hilo lenye nambari za usajili T 702 ACR ambalo ni ISUZU TX
 
MDODOSAJI

Mtibwa Sugar wapo tayari kwa vita sasa

Mecky Mexime
KOCHA Mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema makosa yaliyoiponza timu yake kushindwa kupata ushindi katika mechi zao tatu mfululizo wameyafanyia kazi tayari kwa vita vya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Aidha kocha huyo alisema pamoja na Ashanti United kuonekana kama timu dhaifu katika ligi hiyo watashuka dimbani katika mechi baina yao siku ya Jumapili kwa tahadhari kubwa na bila kuidharau ilimradi kuhakikisha wanapata ushindi.
Akizungumza na MICHARAZO, Mexime, nahodha wa zamani wa timu hiyo ya Mtibwa na Taifa Stars, alisema benchi lao la ufundi tayari limeshagundua wapio walipokuwa wamekosea katika mechi zao zilizopita na kujipanga upya kuianza ligi.
Mexime, alisema kipigo cha mabao 2-0 toka kwa Simba na sare mbili dhidi ya timu za Mbeya City na Prisons za Mbeya vimewafanya wajipange upya kwa kurekebisha makosa yao na sasa wapo tayari kwa vita katika ligi hiyo.
"Tumejipanga upya kwa kuangalia wapi tulipokuwa tunakosea na kurekebisha na sasa tupo tayari kwa vita, hatutakubali kuona tukipoteza tena pointi japo hatuwezi kuidharau Ashanti United tutakaovaana nao Jumapili hii jijini Dar," alisema.
Kocha huyo alisema wataenda uwanja wa Chamazi kwa tahadhari kubwa dhidi ya Ashanti Utd bila kuidharau kwani wanaamini ni timu ngumu na inayoweza kufanya lolote iwapo watawapuuza katika pambano hilo.
Kuhusu kikosi chake, Mexime alisema kinaendelea vyema na hakuna mchezaji yeyote majeruhi kitu kinachompa faraja kwamba watapata pointi tatu muhimu kwa ajili ya kuwatoa nafasi ya tisa waliopo na kurejea nafasi za juu walizokuwa awali.
Mtibwa Sugar katika mechi zake tano ilizocheza mpaka sasa imeshinda mechi moja tu na kupoteza moja huku tatu ikipata sare na kukusanya pointi 6 sawa na Yanga walioopo juu yao wanaotofautiana nao kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba 'kamili gado' kuiua JKT Ruvu


KLABU ya soka ya Simba imetamba kuwa wapo kamili gado kwa ajili ya 'kuiua' JKT Ruvu watakaokutana nao kwenye pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara siku ya Jumapili, licha ya kukiri wanatarajia kupata upinzani mkali kwa wapinzani wao hao.
Simba wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 11 na JKT Ruvu waliopo nafasi ya pili wakiwa na poini zao 9 watavaana kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya sita.
Benchi la ufundi la Simba limekiri kutambua ugumu wa pambano hilo dhidi ya JKT Ruvu, lakini limetamba kuwa hawana hofu yoyote kwa vile kikosi chao kipo fiti ikiwamo kuendelea vyema kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio', aliiambia MICHARAZO kwa njia ya simu jana akiwa kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Bamba Beach, Kigamboni kuwa, kikosi chao kipo tayari kwa vita ya Jumapili ili kuimarisha uongozi wao.
Julio alisema wanajua wanakutana na timu ngumu, lakini wanajipanga ili kuweza kuvuna pointi zote tatu na kuendelea kujikita kileleni baada ya mechi yao iliyopita kupata sare ya mabao 2-2 mbele ya 'wageni' Mbeya City ya Mbeya.
Kocha huyo mwenye maneno mengi alisema kwa kuwa lengo la Simba msimu huu ni kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuupoteza msimu uliopita kwa watani zao Yanga, hawatafanya makosa kwa JKT au klabu yoyote watakayokutana nao.
"Kambi yetu inaendelea vyema ikiwamo wachezaji waliokuwa majeruhi wakiendelea vyema na imani yetu tutapata ushindi kwa JKT Ruvu ili kuendelea kukaa kileleni, japo tunajua litakuwa pambano gumu mno," alisema Julio.
Julio aliongeza pamoja na kukiamini kikosi chao, hawaidharau timu yoyote katika ligi hiyo na badala yake watakuwa wakishuka dimbani kama wanacheza fainali muhimu kuvuna pointi zitakazowasaidia mbele ya safari.

KARAMA NYILAWILA KUZIPIGA OCTOBA 20




Karama Nyilawila
BONDIAw a ngumi za kulipwa nchini, Karama Nyilawila aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa WBF uzito wa middle anatarajiwa kupanda ulingoni mwezi ujao kuzipiga na Sado Philemon.
Nyilawila aliyempiga Kreshnik Qato wa Czech wakati akitwaa taji lake la WBF ambalo alilitema baada ya kushindwa kwenda kulitetea ili apate nafasi ya kuzipiga kirafiki na Francis Cheka mjini Morogoro na kudundwa, atazipiga na Philemon kwenye ukumbi wa CCM Mwinjuma siku ya Oktoba 20, pambano lililoandaliwa na kampuni ya Bigright Promotion.
Mratibu wa pambano hilo, Ibrahim kamwe alisema kuwa maandalizi mpaka sasa yanaenda vizuri.
Hata hivyo Kamwe alisema mabondia wanaendelea kujifua kimkandamkanda kutokana na kukosekana kwa wadhamini na hasa mabondia watakaosindikiza pambano hilo.
Kamwe alisema Nyilawila na mwenzake wameshasaini makubaliano ya kupanda ulingoni siku hiyo ambapo watasindikizwa na michezo kadhaa itakayohusisha mabondia chipukizi.

AIRTEL YAPIGA JEKI MBIO ZA ROCK CITY MARATHON

13
 Meneja Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Katikati ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.

Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando akionesha fomu za kujisajili kushiriki mbio hizo.  Kulia ni Meneja Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.

Na Mwandishi Wetu


KAMPUNI ya Airtel ya Tanzania kupitia huduma yake ya Airtel Money kwa mara ya tano mfululizo imetangaza kudhamini mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zilizopangwa kufanyika mkoani Mwanza tarehe 27, Oktoba 2013 ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya mchezo wa riadha nchini.

Airtel imekuwa mdhamini mkuu kwa upande wa mawasiliano katika mbiyo hizo, wakishirikiana na wadhaminiwa wengine kama NSSF, Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications pamoja na Umoja Switch, ili kutoa fursa ya kuinua mchezo wa riadha inchini.

Akizungumza wakati wa tukio fupi lililofanyika katika makao makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando alisema kampuni yake imejidhatiti kusaidia  shughuli mbali mbali za maendeleo ya jamii na mbio za Rock City Marathon pia ni fursa pekee ya kukuza vipaji katika michezo huo kwa ujumla.

“Kampuni ya Airtel Tanzania kwa mwaka wa tano mfululizo, leo hii tunatangaza udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu ikiwa ni sehemu ya jitihada zetu za kusaidia maendeleo ya michezo nchi nzima.

“Tunaamini kuwa mchango wetu utasaidia katika kuvumbua vipaji vipya vitakavyoshiriki si tu kwa mashindano ya kitaifa lakini pia na ya kimataifa,” alisema. 

Mmbando aliongeza kuwa washiriki kwa mwaka huu wataweza kusajili moja kwa moja kupitia huduma ya kampuni yake ya Airtel Money kwa kutuma malipo yao kwa neno MARATHON na kuhifadhi ujumbe kwa ajili ya kuuonyesha wakati wa kuchukua fomu katika vituo mbali mbali.

Kwa upande wake mratibu wa mbio za Rock City Marathon 2013, Bw. Mathew Kasonta wakati wa tukio alisema kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa kubwa na bora zaidi kwa kuleta pamoja washiriki kutoka ndani ya nje ya nchi.

 “Kwa mwaka huu tumeungana na kampuni ya Airtel lakini kupitia Airtel Money ili kutanua wigo wa ushiriki zaidi. Katika miaka iliyopita, watu wengi wamekuwa wakikosa nafasi ya kushiriki au wakilazimika kusafiri umbali mkubwa kwenda kwenye vituo vichache tulivyoviandaa ili waweze kununua fomu za usajili, kwa kupitia Airtel Money zoezi hili litakuwa limerahisishwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Kasonta.

Kasonta aliongeza, “ukishamaliza zoezi hilo, utapokea ujumbe utakaouonyesha pale utakapokwenda kuchukua fomu za usajili katika ofisi za makao makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya, Arusha na Mwanza.”

Alisema kuwa washiriki wenye vigezo pia wataweza kusajili kwa kupata fomu zipatikanazo katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, na katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu, upande wa kulia katika jengo la ATC, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.

Kasonta alibainisha kuwa fomu za usajili zitapatikana katika viwango vya bei vifuatavyo; shilingi 5,000 kwa mbio za km 21 (kwa watu wote), shilingi 3,000 kwa mbio za km 5 (mbio kwa makampuni na taasisi).

Alisema kuwa fomu kwa mbio za kilometa 3 (kwa wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye ulemavu wa ngozi) na mbio za kilometa 2 kwa watoto (wenye umri wa miaka 7 mpaka 10) zitapatikana bure.

Cheka mdogo, Shauri kumaliza ubishi Oktoba 27

Mabondia Ramadhani Shauri na Cosmas Cheka  wakitunishiana misuri wakati wa utambulisho wa mpambano wao wa ubingwa wa UBO Dar es  salaam utakaofanyika tarehe 27 mwezi wa kumi 
Promota wa Mpambano wa Ubingwa wa UBO Kaike Siraju katikati akiwanyoosha mikono juu mabondia Ramadhani Shauri kushoto na Cosmasi Cheka watakaopigana tarehe 27 Mwezi wa kumi  jijini Dar es Salaam
MPAMBANO mwingine wa masumbwi unatarajia kufanyika Oktoba 27 katika ukumbi wa Friends Coner  Manzese Dar es salaam litakalo wakutanisha mabondia Ramadhani Shauri na Cosmas Cheka mpambano huo ulidhaminiwa na Hotel ya Tanamera ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani
Akizungumza mratibu wa mpambano huo Kaike Siraju amesema amepata sapoti katika hotel hiyo ili aweze kuendeleza vipaji vya vijana unakumbuka mimi ndie ninae andaaga mapambano makubwa nchini kama utakumbuka ila nilisimama kidogo kwa ajili ya kutafakali na kulekebisha mambo yangu binafsi lakini kwa sasa nimekuja kuinua mchezo huu kwa vijana chipkizi kwanza ndio msingi wa ngumi duniani kote
 Aliongeza kwa kutaja mapambano ya utangulizi kuwa ni Mohamed Matumla anamenyana na Sadiki Momba huku Amosi Mwamakula akizichapa na Hamisi Ajali na Juma Fundi atazipiga na Shabani Kilumbelumbe
Siku hiyo kutakuwa pia na huzwaji wa DVD kali za ngumi wakiwemo mabondia wakali wanaotamba Duniani na hapa nchini kama. Manny Pacquaio, Saul 'canelo' alverez, Floyd Mayweather, Mike Tyson, Muhammed Ali, Ferex Trinidad, Miguel Cotto na wengine wengi
DVD hizo za ngumi kali zitakuwa zikiuzwa na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D'
Pamoja na kutambua sheria na taratibu za mchezo huo siku hiyo pia kuta kuwa na vifaa vya mchezo huo wa masumbwi vitakavyotolewa  zawadi kwa mabondia na Kocha Super D  ambaye ameahidi kutoa vikinga meno, bandeji, bukta, na dvd za mafunzo kwa mabondia na vifaa mbalimbali kwa mabondia watakao onesha uwezo wa ali ya juu wa kutupiana masumbwi

TPBF yalia ngumi kudhalilishwa


Na Suleiman Msuya
SHIRIKISHO la Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBF) limesema linasikitishwa na watu ambao wanadhalilisha mchezo wa ngumi hapa nchini kwa maslahi yao binafsi.
Kauli hiyo ya masikitiko imetolewa na Rais wa TPBF Chatta Michael wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Rais huyo alisema baada ya pambano la bondia Francis Cheka kupigana mwezi mmoja uliopita yameibuka makundi ya watu ambao wanaonekana kuwa na mikakati yao binafsi jambo ambalo halipaswi kunyamaziwa kwani linaweza kuleta picha mbaya kwa nchi.
Alisema kitendo cha Cheka kuibuka bingwa katika mpambano huo wa dunia ingetakiwa iwe ni sehemu ya nchi kuungana ili kuhakikisha kuwa fursa hiyo haiondoki kirahisi na iwe ni moja kufungua njia ya ujio wa mabondi wengine.
Michael alisema baada ya mpambano huo hadi sasa wamejitokeza mabondia kutoka nchi za Mexico na Australia kuhitaji kupambana na Cheka kutokana na kuridhishwa na kiwango chake.
“Napenda kutumia fursa hii kuzungumza na jamii ya kitanzania ambayo inafuatilia mchezo huu wa ngumi kuwa ni vema kuachana na maneno ya baadhi ya watu ambao wapo kwa nia ya kupotosha hali ambayo inaweza kuathiri dhima nzima za wadau wenye nia ya kukuza mchezo huo,” alisema.
Rais huyo alisema mikakati ambayo ipo ni kuhakikisha kupitia shirikisho la Ngumi la Dunia (WBF) Tanzania inapata mapambano mengi makubwa ya kimataifa ili kuweza kukuza vipaji vya vijana ambao wapo tayari.
Alisema TPBF imejipanga vilivyo ili kuweza kushirikiana na WBF ili kuhakikisha kuwa mchezo wa ngumi Tanzania unapiga hatua kwani ni moja ya mchezo ambao unatoa fursa za mafanikio kwa haraka.

Azam Tv yamkosha Julio

KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ameipongeza kampuni ya Azam TV  kwa kitendo chao cha kuongeza udhamini katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kitu alichodai kimesaidia kuongeza ushindani katika ligi tofauti na zamani.
Julio alisema udhamini huo wa Azam TV ambao umezihusisha timu zote umesaidia kuondoa ligi ya timu chache na ndiyo maana mpaka sasa kumekuwa na matokeo ya kushangaza hata kwa timu ambazo zilikuwa zikionekana kama nyonge.
Akizungumza na MICHARAZO, Julio alisema udhamini mpya wa Azam umezifanya kila timu kuwa na maandalizi mazuri na ari ya kutaka kufanya vyema katika ligi kitu ambacho kimesababisha baadhii ya timu zilizozoea 'kupeta' kuwa na wakati mgumu.
"Kama mdau wa soka naipongeza kampuni ya Azam Media kwa uamuzi wake wa kuongeza udhamini katika ligi, imeifanya ligi kuwa tamu na yenye ushindani wa kweli kitu ambacho kitasaidia kupanda kwa soka la Tanzania," alisema.
"Ule utamaduni wa timu ndogo kuwa wanyonge mbele ya timu kubwa ni kama sasa unaondoka na hiki ni kitu kizuri kwa mustakabali wa soka letu, hivyo nawapongeza na kutaka wengine wajitokeze kusaidia kuinua soka la Tanzania," aliongeza Julio.
Alisema anaamini ushindani uliopo katika ligi msimu huu utasaidia kutoa mabingwa na wawakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa wanaostahili na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika anga hizo badalaya kuwa wasindikizaji tu,
"Ligi inapokuwa ngumu na yenye ushindani inasaidia kutoa mabingwa wa kweli na wanaostahili ambao wataiwakilisha vyema kimataifa, hivyo narejea kuipongeza Azam Media walichokifanya na kuomba wasapotiwe na kila mtu," alisema Julio.
Kampuni hiyo ya Azam Media imeingia mkataba wa kuidhamini Ligi Kuu Tanzania Bara wenye thamani ya Sh. Bilioni 6 ambapo kila klabu ya ligi itakuwa ikivuna Sh Milioni 100, hiyo ni mbali na udhamini wa wadhamini wakuu wa ligi hiyo Vodacom

Vodacom yazipiga tafu Shule 12 vifaa vya michezo






KAMPUNI ya VODACOM Tanzania imetoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 11kwa shule 12 za Sekondari katika mkoa wa Dar es Salaam ikiwa na lengo la kukuza mchezo wa soka kuanzia ngazi za chini.
Msaada huo umekabidhiwa na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa VODACOM Tanzania Kelvin Twissa kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mkandara leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waanahabari Twissa alisema msaada huo ni mwendelezo wa kampuni yao katika kuhakikisha kuwa michezo inakuwa nchini kuanzia ngazi ya chini ambapo wanatarajia kuendelea na mikoa mingine.
Twissa alisema VODACOM pamoja na ukweli kuwa imekuwa ikisaidia sekta mbalimbali ila michezo ni sehemu kubwa ya ufadhili wao wakiamini kuwa ni sehemu ambayo inahusisha jamii kubwa.
“Mh. Waziri napenda kukuambia baada ya majadiliano yetu ya muda tumeweza kutoa msaada huu kwa kuanza ambapo zipo jezi pea 12 na mipira 40 jambo ambalo litaweza kuleta tija kwa sasa,” alisema.
Kwa upande Waziri Mkandara alisema wizara yake imefarijika sana kwa kupata msaada huo kwani ni moja ya malengo yao ya kukuza michezo kwa kushirikiana na wadau wengine.
Alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa michezo inachezwa kila wakati katika maeneo yote ya nchi hasa kwa kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari ili kuwa na mwelekeo mzuri wa kimichezo.
Dk. Mkandara alisema mashindano hayo ya majaribio yatahusisha Wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam kwa kila Wilaya kutoa shule nne za sekondari ambao michezo miwili ya mpira wa pete na mpira wa miguu.
Waziri alisema michezo ni ajira, afya na pia inajenga akili hivyo ni vyema kwa kuanzia ngazi ya chini ili iweze kuwaathiri vijana wakiwa wadogo.
Aidha waziri alitoa rai kwa wadau mbalimbali na taasisi kujitokeza kusaidia michezo mbalimbali kwani hiyo ndiyo njia sahihi ya kufikia malengo ya kukuza michezo hapa nchini.

Cash Money watoa msaada TMK Hosp, Gurumo naye...



Wana kikundi cha Cash Money wakiwa tayali kwa kutoa msaada katika hospitali ya Temeke
Mlezi wa Kikundi cha Cash Money ,Ratifa Masasi kulia akimkabibi muhuguzi wa wodi ya watoto bi, Nuswe Ambokile zawai mbalimbali walizoleta kwa ajili ya watoto waliolaza katika hospital ya Temeke
Baadhi ya wana kikundi cha Cash Money wakiwa katika picha ya pamoja na wahuguzi wa word ya watoto Hospitali ya temeke baada ya kukabidhi msaada


Na Mwandishi Wetu
MSANII nguli wa muziki wa dansi aliyestaafu, Muhidini Gurumo, atapanda
jukwaani leo kutumbuiza na mkewe, sambamba na kupewa zawadi za
heshima.

Gurumo atatoa  burudani hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwaaga mashabiki,
ambapo shughuli hiyo itaambatana na uzinduzi wa kundi la Cash Money,
la Tandika mjini Dar es Salaam.

"Tumeandaa zawadi kwa mzee Gurumo kutokana na heshima kubwa aliyonayo
katika tasnia ya muziki na kujenga maadili kwa taifa kutokana na
nyimbo zake.

Hivyo zawadi zetu zitaenda sambamba na uzinduzi, ambapo tumepanga
hivyo, ili lee mwenye chochote ampe mzee wetu,"Aliongeza Latifa Masasi
mlezi wa kundi hilo.

Uzinduzi huo unafanyika kwenye ukumbi wa Equator Grill, Mtoni kwa Aziz
Ali, Dar es Salaam na utapambwa na bendi mbalimbali za taarabu
zikiwemo Coast na G Five.

Kundi la Cash Money ambalo lilianzishwa mwaka 2011, pia limetoa vitu
mbalimbali kwa wodi ya watoto, na vituo vya watoto yatima jana, ikiwa
ni sehemu ya uzinduzi huo
Mlezi wa kikundi cha Cash Money akimfaliji mama Samir Nassoro, Naomi Ramadhani walipokutana wakati kundi hilo likitoa msaada kwa wagojwa katika hod ya watoto
Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Cash Money wakimfariji Bi Naomi Ramadhani
Msanii wa bendi ya Msondo ngoma Saddy Ally katikati akisalimiana na wanakikundi cha cash money walipokutana katika hospitali ya Temeke wakitokea kutoa msaada
Wana kikundi wa chass money kushoto Amina Uredi 'Mmanyema ' na Zulfa Kasongo
Mlezi wa kikundi cha cash money bi, Ratifa Masasa akimfariji mtoto Salimu Ally wakati walipokwenda kutoa msaada katika hospitali ya temeke dar es salaam mwingine ni mama mtoto Tabu Salumu mkadhi wa Tandika

Uwanja wa Taifa sasa hata kwa Kitchen Party, serikali yafunguka


Na Suleiman Msuya
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imetoa wito kwa Wananchi ambao wanapendelea kuingia uwanja wa Taifa kushughudia michezo na shughuli zingine za kijamii wawe watunzaji wa rasilimali zilizopo katika uwanja huo.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara hiyo Godblease Malisa wakati akizungumza na mwandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vema kila mpenda michezo kuwa sehemu ya kulinda na kutunza uwanja huo kutokana na ukweli kuwa gharama kubwa zilitumika hadi kupatikana kwake.
Malisa alisema serikali inajitahidi kutunza na kuboresha huduma uwanja hapo ili kuhakikisha kuwa unakuwa wa salama na bora kwa muda wote ili vizazi vijavyo viweze kufaidika.
“Napenda kuwaomba wanamichezo na wasio wanamichezo kuutunza uwanja wetu wa Taifa ili uweze kudumu kwa muda mrefu pia ni vema tutambue kuwa uwanja huo ni wa gharama kubwa,” alisema.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanja vya michezo vinakuwa bora na vinatumika wakati ote hali ambayo itakuwa ni sehemu ya kukuza michezo hapa nchini.
Msemaji huyo alisema uwanja mkubwa wa Taifa unahitahiji gharama kubwa za kuutunza hivyo ni vema kwa wadau ambao wanauomba kuutumia katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Aidha Malisa aliwataka wananchi kutumia uwanja huo kwa shughuli mbalimbali kama za mikutano na sherehe za harusi kwani una kumbi za kutosha na nzuri kwani ni vigumu kwa uwanja huo kujiendasha kwa mapato ya mechi zinazochezwa.
Malisa alisema pamoja na uwanja wa Taifa pia Serikali inaendelea na maboresho ya uwanja wa Uhuru, ujenzi wa uwanja wa ndani, mabwawa ya kuogolea yenye viwango vya olimpiki na hosteli.