STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 18, 2010

Baba Diana a.k.a Lukasa kuzikwa kesho mjini Tanga

MWANAMUZIKI Mkongwe wa muziki wa dansi, Abuu Semhando 'Baba Diana', 57, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajili ya barabarani anatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda wilayani Muheza, Tanga kuzikwa.
Kwa mujibu Meneja Masoko wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' aliyokuwa akiifanyia kazi marehemu huyo,Martin Sospeter ni kwamba Semhando aliyefahamika pia kama Lukasa enzi akiwa Super Matimila, atazikwa kesho nyumbani kwao Tanga, ingawa msiba upo Mwananyamala Kisiwani alipokuwa akiishi enzi za uhai wake.
Sospeter, alisema mwili wa marehemu kwa sasa upo Muhimbili na wanafanya mipango ya kuusafirisha kwenda kuzikwa kwao Tanga kesho alasiri.
"Marehemu anatarajiwa kusafirishwa kwao Tanga kwa ajili ya mazishi, ingawa kwa sasa msiba upo nyumbani kwake, Mwananyamala Kisiwani na mwili wake umeshapelekwa hospitali ya Muhimbili," alisema Sospter.
Meneja huyo alisema kuwa marehemu aliyezaliwa Oktoba 24, 1953 na kuanza muziki mwaka 1974 katika bendi ya Sola Tv kabla ya kupita bendi mbalimbali Twanga Pepeta aliyoiongoza kama Katibu wake, amewaachia pengo kubwa lisilozibika aslan.
"Ni pigo kwetu na tumeshtushwa na kuhuzunishwa na kifo chake cha ghafla," alisema Sospeter.
Kifo cha mkongwe huyo aliuyewahi kuzipigia bendi za Super matimila, Orchestra Toma Toma, Tango Musica, Diamond Sound 'Wana Kibinda Nkoy', Beta Musica kabla ya kuasisi Twanga Pepeta, kimekuja masaa machache tangu fani ya muziki kumpoteza Ramadhan MToro Ongalla aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Dk Remmy alifariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis, huku Semhando na wanamuziki wenzake wakishiriki mwanzo mwisho katika msiba huo.

Mwisho

Buriani Baba Diana utakumbukwa daima





KIFO kimeumbwa kwa usiri mkubwa hata hujaji wake, pia huwa ni siri mno, kiasi ni vigumu kwa kiumbe chochote duniani kubaini lini atakumbana nacho.
Lau kisingekuwa na usiri katika suala la kifo, kwamtu kufahamu kitakufikia lini, wapi na kwa njia gani, sidhani kama kuna ambaye angekuwa akitoka nje siku ya ahadi yake kwa kuhofia kukutana nacho.
Ila kwa kuwa Mungu ana hekima na maana kubwa ya kukifanya kuendelea kuwa ni siri yake pekee yake duniani na ahera, kifo kinaendelea kuogopwa.
Ndio maana hata mwanamuziki gwiji wa muziki wa dansi, marehemu Marijani Rajabu 'Jabari la Muziki' enzi za uhai wake alitunga wimbo ulioelezea hamu yake ya kutaka kuwepo rufaa ya kifo ili mradi kuwarudisha wapendwa wetu wanaondoka ghafla bila kutarajiwa.
Abuu Semhando maarufu kama 'Baba Diana' au 'Lukasa' ambaye kwa siku zote nne za msiba wa mwanamuziki mwenzake, Ramadhani Ongolla 'Dk Remmy' alishiriki mwanzo mwisho hadi alipopumzishwa makaburini Sinza, Dar es Salaam, naye amefariki dunia.
Semhando, aliyekuwa mpiga dramu na Katibu wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' alifariki usiku wa kuamkia jana, ikiwa ni masaa machache tangu amzike mwenzake baada ya kupatwa na ajali mbaya ya barabarani.
Marehemu huyo alikumbwa na mauti hayo maeneo ya Mbezi Beach, akitokea kazini kwake baada ya kugongwa na gari akiwa anaendesha pikipiki na kujeruhiwa vibaya kichwani kabla ya kufa papo hapo.
Mwili wa mkongwe huyo aliyefanyia kazi bendi mbalimbali hapa nchini tangu miaka ya 1970 na aliyekuwa mpiganiaji wa haki za wanamuziki wenzake kama baadhi ya waliowahi kufanya nae kazi wanavyomueleza, uliohifadhiwa katika hospitali ya Muhimbili, utasafirishwa leo kwenda kuzikwa Muheza jiji Tanga.
Baadhi ya wanamuziki wa dansi nchini wamedai kushtushwa na kifo hicho cha ghafla cha Semhando, wakirejea kwamba walikuwa naye katika safari ya kumsindikiza Remmy aliyefariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis, masaa machache kabla naye hajapatwa na mauti hayo.
Tshimanga Kalala Assosa, mtunzi na muimbaji aliyezipigia bendi mbalimbali kama Lipualipua, Le Kamalee, Fuka Fuka na Orchestra Marquis, alisema kama sio kuogopa kufuru, angeweza kusema Mungu ni kama amewaonea wanamuziki wa Tanzania wiki hii kwa vifo hivyo mfululizo.
"Naogopa kumkufuru Mungu, lakini misiba hii na hasa huu wa Semhando niliofahamishwa usiku wa manane kwa kupigiwa simu umeniuma kupindukia, ila sina jinsi kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa," alisema Assosa.
Assosa, alisema kuondoka kwa wakongwe hao ni kama uzindushi kwa waliosalia juu ya umuhimu wa kushikamana na kumcha Mungu, pamoja na kufanya maandalizi ya kusaka warithi wa nafasi zao katika muziki kwa sababu bila ya hivyo fani yao itatereka.
Ally Choki 'Mzee wa Farasi', aliyewahi kufanya kazi na Semhando wakati akiwa mwanamuziki na kiongozi wa Twanga Pepeta, alisema kifo cha Semhando ni pigo kwa familia ya marehemu, wadau wa muziki na hususani bendi yake ya Africana Stars kwa kuwa alikuwa nguzo.
"Sio siri ni msiba mkubwa na pengo kubwa katika muziki wa dansi na hasa Twanga Pepeta kwa vile nafahamu jinsi gani marehemu alivyokuwa 'roho' ya bendi hiyo, licha ya kwamba wapo waliokuwa wakimuona kama 'mnoko' fulani, namlilia milele Semhando," alisema Choki.
Choki alisema uzoefu wake katika fani ya muziki, ilimfanya marehemu kuwa mhimili wa bendi hiyo na muziki wa dansi kwa ujumla, akipigania masilahi ya wanamuziki wenzake na kusema hajui nani wa kuliziba pengo lake.
"Muhimu ni kumuombea kwa Mungu na pia kuiombea familia yake iwe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema Choki.
Meneja wa Masoko wa bendi hiyo, Martin Sospeter, alisema kifo cha kiongozi mwenzao na mwanamuziki wao, ni pigo kubwa kutokana na kutokea kwake ghafla, lakini wanamuachia Mungu kwa kuwa alimpenda zaidi kuliko walivyompenda na kumthamini wao.
"Ni pigo kwetu na fani nzima ya muziki, tunajipanga kufanya maandalizi ya kumplekea mwenzetu katika makazi yake ya milele, ambapo atazikwa kesho (leo) nyumbani kwao mjini Tanga," alisema.
Marehemu Semhando ambaye majina yake kamili ni Abubakar Semhando, alizaliwa Oktoba 24, mwaka 1953 huko Muheza Tanga na kupata elimu ya msingi huko huko kwao, kabla ya kutumbukiza kwenye muziki miaka ya mwanzoni ya 1970.
Bendi yake ya kwanza kuifanyia kazi ni Sola TV ya jijini Dar mnamo mwaka 1974 kabla ya kutua Tanga International na kukaa nao hadi miaka ya 1980 alipohamia Super Matimila iliyokuwa chini ya Dk Remmy.
Aliihama Matimila na kutua Tomatoma Jazz akiwa na marehemu Adam Bakar 'Sauti ya Zege', kabla ya kuhamia Orchestra Safari Sound 'OSS' na kukaa nao hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 alipohamia Tango Musica, kisha kujiunga Vijana Jazz.
Baadae alitua Diamond Sound 'Wana Kibinda Nkoy' mwaka 1996 na kutunga kibao cha Neema kilichoipaisha bendi hiyo, miaka miwili baadae alihamia Beta Musica na kukaa nao kwa muda mfupi kabla ya kuhamia African Stars akiwa mmoja wa waasisi wake.
Amekuwa na bendi hiyo ya Twanga Pepeta tangu wakati huo hadi mauti yalipomkuta juzi akiwa ameshiriki kupiga dramu karibu nyimbo zote za albamu 10 za bendi hiyo kuanzia ile ya Kisa cha Mpenda hadi Mwana Dar es Salaam iliyozinduliwa mwaka huu.

Mwisho

BREAKING NEWS-ABUU SEMHANDO 'BABA DIANA' IS NO MORE





MWANAMUZIKI Mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Abuu Semhando 'Baba Diana' amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari baada ya kugongwa akiwa kwenye pikipiki eneo la Africana, Mbezi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mapema zinasema kifo hicho kilitokea majira ya saa 9 usiku baada ya kugongwa na gari aina ya Benz lililomjeruhi vibaya sehemu ya kichwani.
Abuu aliyetamba miaka ya 1970 akiwa na bendi ya Vijana Jazz, amepatwa na mauti hayo ikiwa ni siku moja tu tangu ashiriki kumziba mkongwe mwenzake, Ramadhani Mtoro Ongalla 'Dk Remmy' aliyefariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis.
Kwa hakika ni pigo kwa wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wa muziki wa dansi kwa ujumla, ingawa Kazi ya Mola Haina Makosa kwa sababu alishatuambia mapema kwamba KILA NAFSI ITAONJA MAUTI, wametangulia sisi tu nyuma yao tuwadhaike na vifo vyao kwa vile hatujui saa au siku ambayo Malaikat Maut, Izraili atatupitia kuchukua AMANA.
INNALILLAH WAINNA ILAHI RAJIUN!

Thursday, December 16, 2010

Amer Lugunga Mwenyekiti Mpya Halmashauri ya Kilosa

DIWANI wa Kata ya Kimamba, wilayani Kilosa, Amer Lugunga, amefanikiwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kuwaangusha wagombea wenzake wenzake wawili.
Wagombea walioangushwa na Lugunga, ni pamoja na Leonard Mapunda na mtu mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mbiza.
Katika mchuano huo uliofanyika kwenye ofisi za CCM wilaya ya Kilosa, Lugunga aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 40 kati ya 60 zilizopigwa kwenye kinyang'anyiro hicho kilichokuwa na ushindani mkali.
Mbiza alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 17 na Mapunda aliambulia tatu tu.
Akizungumza na MICHARAZO mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Lugunga alisema atafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kuhakikisha Kilosa inaondokana na aibu iliyoighubika kwa sasa.
"Nawashukuru walionichagua, na ahadi yangu ni kwamba nitafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, ili kuirejeshea heshima wilaya yetu iliyopewa hati chafu hivi karibuni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo," alisema Lugunga.
Alipoulizwa juu ya 'zengwe' alilokuwa akiwekewa na baadhi ya wapinzani wake, Lugunga, alisema mambo yote yameisha na hana kinyongo na mtu.

Mwisho

Extra Bongo yawanyatia akina Chokoraa





BAADA ya bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kuwatimua kundini, wanamuziki wao nyota wawili, Khalid Chokoraa na Kalala Junior, uongozi wa bendi ya Extra Bongo, umeanza mipango ya kuwachukua wanamuziki hao kuimarisha kikosi chao.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki, aliiambia MICHARAZO kuwa, tayari wameshaanza mazungumzo ya awali na wanamuziki hao ambao pia wanaunda kundi la Mapacha Watatu wakishirikiana na Jose Mara wa FM Academia.
Choki alisema walikuwa na mipango ya kuwachukua waimbaji hao kitambo kirefu,ila walikuwa wakisita kuhofia kutifuana na uongozi wa Twanga Pepeta, lakini kutimuliwea kwao kwa utovu wa nidhamu ni kama kumewarahisishia kazi.
"Kutimuliwa kwao Twanga Pepeta kumeturahisishia kazi ya kuwapata waimbaji hawa wenye vipaji vya aina yake na tumeshaanza mazungumzo ya awali, nadhani ndani ya wiki hii mambo yatakuwa shwari na wataanza kazi Extra Bongo," alisema Choki.
Choki aliongeza katika kuonyesha kuwa wapo karibu na wanamuziki hao na kuwakubali kwa kazi zao kupitia kundi lao la Mapacha watatu wanatarajia kufanya nazo onyesho la pamoja wakati wa Mkesha wa Mwaka Mpya na siku ya Mwaka Mpya wenyewe jijini Dar es Salaam.
Alisema onyesho la kwanza baina yao na Mapacha Watatu linalotamba na albamu ya 'Jasho la Mtu' litafanyika mkesha wa Mwaka Mpya, Vatican Hotel, Sinza na kisha siku ya Mwaka Mpya watakuwa wote pale TCC Chang'ombe.
"huwezi jua kwenye maonyesho hayo mawili yanaweza kutumiwa kama utambulisho wao ndani ya Extra Bongo," Choki alitania.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, lengo la bendi yao ni kutaka kuona wanatamba kwenye muziki wa dansi nchini baada ya kurejea kwa mara ya pili baada ya kufariki enzi ikitumia miondoko ya 3x3.
Choki aliongeza wakati wakiwa, katika harakati hizo za kuwanyakua akina Chokoraa, aliyekuwa mmoja wa waasisi wa Extra Bongo ya awali, pia bendi yao inajiandaa kufanya uzinduzi wa albamu ya 'Mjini Mipango'.
Alisema uzinduzi uliofanyika Mei 25 mwaka huu ulikuwa ni wa bendi yao iliyofufuliwa upya na sio wa albamu kama baadhi ya watu walivyokuwa wanadhani na hivyo wanajipanga kuifanyia uzinduzi wake.
Choki alisema watazindua albamu hiyo yenye nyimbo sita ambazo baadhi zinaendelea kutamba kwenye vituo vya redio na runinga, huku wakiendelea kuandaa ya pili ambayo tayari baadhi ya nyimbo zake zimeshakamilika.

Dk Remmy kuzikwa leo





SAFARI ya mwisho ya hapa duniani kwa mwanamuziki nguli wa muziki wa dansi na ule wa Injili, Ramadhan Mtoro Ongalla 'Dk Remmy' aliyefariki mapema wiki hii, inatarajiwa kuhitimishwa rasmi leo atakapozikwa kwenye makaburi ya Sinza, jirani na nyumbani kwake.
Remmy, aliyezaliwa nchini Zaire (sasa DR Congo) miaka 63 iliyopita alifariki Jumatatu baada ya kuugua kwa muda mrefu atazikwa jioni ya leo kwenye makaburi hayo baada ya kuagwa kwa tamasha la muziki wa Injili kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, jijini.
Mjomba wa marehemu, Mzee Makassy, alisema mwili wa marehemu utazikwa kwenye makuburi hayo jirani kabisa na mahali alipokuwa akiishi, Sinza kwa Remmy.
Marehemu Remmy aliingia nchini mwaka 1977 na kujiunga na bendi ya mjomba wake, Makassy Band na kutamba na kibao cha Siku ya Kufa kabla ya baadae kuhamis Super Matimila ambayo ilimpa umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake wa kutunga, kuimba na kupiga gita la solo ambapo alishiriki matamasha makubwa barani Ulaya mara kwa mara.
Hata hivyo miaka michache iliyopita alipata kiharusi na kupooza, ambapo aliamua kuokoka na kuanza kutumikia muziki wa Injili hadi mauti yalipompata akiwa ameacha mke na watoto kadhaa akiwemo mshambuliaji wa timu ya Azam, Kalimangonga 'Kally' Ongalla.
Bwana Alitoa Naye Ametwaa Jina Lake Lihimidiwe. Micharazo tunamtakia safari njema aendako nasi tu nyuma yake kwa kuwa kila nafsi ni lazima ionje mauti.

Monday, December 13, 2010

Cheka, Maugo kumaliza Ubishi Dar






MABONDIA Francis Cheka 'SMG' na Mada Maugo 'King Maugo Jn' wanatarajia kumaliza ubishi baina yao watakapopigana kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam badala ya uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Mratibu wa pambano hilo, Kaike Siraju, aliiambia MICHARAZO mapema leo kuwa, pambano la wababe hao wawili litafanyika Dar na sio Morogoro kama alivyokuwa akitaka iwe na kuingia kwenye mzozo na Mada Maugo.
Maugo, anayeshikilia taji la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, alitishia kutopigana na Cheka kama pambano hilo lingehamishiwa Morogoro.
Siraju, alisema wameangalia mambo mengi kabla ya kusitisha uamuzi wa kulibakisha pambano hilo Dar na kueleza kuwa maandalizi kwa ujumla yanaendelea vema ikiwemo mabondia wote kuendelea kujifua.
"Maandalizi ya pambano la Cheka na Maugo, yanaendelea vema na litafanyika Dar kama ilivyokuwa awali, baada ya jaribio la kulihamishia Moro kushindikana," alisema Siraju.
Siraju alisema pambano hilo la uzani wa Middle la raundi nane lisilo la kuwania Mkanda litakalofanyika Januari Mosi, mwakani, likisindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Mratibu huyo aliitaja michezo ya utangulizi siku hiyo ni pamoja na pambano kati ya Mshihiri Kidira atakayezidunda na Deo Njiku, Jafari Majid dhidi ya Juma Afande na Hussein Mbonde atakayezichapa na Cosmas Cheka.
Michezo mingine ni ile ya Simba wa Tunduru ataonyeshana kazi na Albert Mbena, Arafati ‘Ngumi Jiwe’ atapambana na Juma Kihio wakati Sadik Momba atafunga kazi na Smoo Njiku.
Michezo yote hiyo inasimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO na ni maalum kwa kukata mzizi wa fitina baina ya mabondia hao wanaotambiana kila mmoja akitamba ni bora kuliko mwenzie.

Mwisho

BREAKING NEWS-DK REMMY IS NO MORE


MWANAMUZIKI maarufu nchini aliyewahi kutamba na bendi za Makasy na Super Matimila kabla ya kuhamia kwenye muziki wa Injili, Ramadhani Mtoro Ongalla 'Dk Remmy' amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa tatizo la Ini, bado tunafuatilia kujua taratibu za mazishi yake.
Dk Remmy atakumbukwa kwa vibao vyake matata kama Nataka Mtoto, Siku ya Kufa, Muziki Sio Uhuni, Mambo kwa Soksi, Mrema, Mariam, Mwanza na kadhalika....!
Mungu Ilaze Roho ya Marehemu Mahali Pema. Amin

Friday, December 10, 2010

Sam wa Ukweli kuwasindikiza Mapacha Watatu J'3



MSANII anayekuja juu kwenye muziki wa kizazi kipya, Salum Mohammed 'Sam wa Ukweli', anayetamba na kibao cha 'Sina Raha' anatarajia kulisindikiza kundi la muziki wa danis la 'Mapacha Watatu' katika onyesho la 'Usiku wa Sauti ya Kizazi Kipya cha Dansi' linalofanyika keshokutwa.
Onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Stereo Bar, Kinondoni jijini Dar es Salaam na Sam wa Ukweli, atakuwepo kulipamba onyesho hilo kwa vibao vyake murua kikiwemo cha 'Sina Raha' kinachotamba kwa sasa nchini.
Akizungumza na MICHARAZO, mratibu wa onyesho hilo, Sauda Mwilima, alisema onyesho hilo ni maalum kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa dansi kupitia kundi hilo la Mapacha Watatu linaloundwa na waimbaji nyota watatu toka bendi za Africana Stars na Fm Academia.
Waimbaji hao wanaouunda kundi hilo linalotamba na albamu yao ya 'Jasho la Mtu' ni Khalid Chokoraa na Kalala Junior wa Twanga Pepeta pamoja na Jose Mara toka FM Academia.
"Katika kuwapa raha mashabiki wa muziki wanaojiandaa kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha 2011, nimeandaa Usiku wa Sauti ya Kizazi Kipya cha Dansi utakaofanyika Jumatatu ya Desemba 13, ambapo utapambwa na burudani toka kundi la Mapacha Watatu watakaosindikizwa na nyota wa muziki wa kizazi kipya, Sam wa Ukweli," alisema.
Sauda, alisema maandalizi ya onyesho lao yamekamilika kwa asilimia zote na kuwataka mashabiki kukaa mkao wa kula kupata burudani kabambe toka kwa wakali hao.

Munishi aja kuchangia yatima Bongo



MUIMBAJI nyota na mkongwe wa muziki wa Injili, Faustin Munishi anayeishi Kenya, anatarajia kutua nchini wiki ijayo kwa ajili ya kuja kutumbuiza kwenye tamasha maalum la muziki wa Injili la kuchangisha fedha kwa ajili ya yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Tamasha hiloi litakalofanyika kwenye viwanja vya Posta, Kijitonyama siku ya Desemba 26, limeandaliwa na asasi ya Keep a Child Alive, ambapo wasanii mbalimbali wa muziki wa injili wa ndani ya nje ya nchi wamealikwa kuja kulipamba.
Mratibu wa tamasha hilo, Godfrey Katunzi, aliiambia MICHARAZO kuwa, kati ya wasanii wa muziki wa Injili watakaotumbuiza siku hiyo ya 'Boxing Day' ni muimbaji mkongwe, Mtanzania Faustin Munishi, ambaye kwa miaka mingi anafanya shughuli zake nchini Kenya.
Katunzi, alisema mbali na Munishi anayetamba na vibao kama Chini ya Mwamba, Paulo na Sila, Amua Mwenyewe, Nimuogope Nani na nyingine, wengine watakaotumbuiza siku siku hiyo ni Dk Aaron, Jane Misso, Beatrice Muone na kwaya mbalimbali za jijini Dar es Salaam.
Mratibu huyo ambaye ni Katibu wa asasi hiyo ya Keep a Child Alive, alizitaja baadhi ya kwaya hizo ni ile ya New Life Church wanaotamba na albamu yao ya 'Sipati Picha', Tabata Menonite maarufu kama Wakunyatanyata na nyinginezo.
Katunzi alisema, lengo la tamasha hilo la injili ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia yatima na watoto hao wa mitaani walipiwe ada na kununuliwa vifaa na sare za shule pamoja na kutatua matatizo mbalimbali waliyonayo.
Aliwaomba watu binafsi na makampuni yenye uwezo kujitokeza kuwapiga tafu katika tamasha hilo, ili kutimiza malengo la kuwaonyesha upendo watoto hao, akidai jukumu la kusaidia na kulea yatima ni la watu wote bila kujali, dini, rangi, kabila au jinsia.

Levent kurekodi tatu mpya

BAADA ya ukimya mrefu tangu ilipofyatua albamu yao ya pili ya Mama Kabibi, bendi ya muziki wa dansi ya Levent Musica ya mjini Morogoro wiki ijayo itaingia studio kurekodi nyimbo tatu kwa ajili ya maandalizi ya albamu yao ijayo mpya.
Kiongozi wa bendi hiyo, Seleman Ramadhani 'Suzuki Sauti ya Malaika', aliiambia MICHARAZO jana kuwa nyimbo zitakazorekodiwa ni 'Pongezi Baba Madinda' na 'Mapenzi Maradhi' alizotunga yeye (Suzuki) na 'Mapenzi Sio Pesa' wa Steve Dokta.
Suzuki, alisema nyimbo hizo ni katyi ya nyimbo sita mpya za bendi hiyo zilizopangwa kurekodiwa kwa ajili ya albamu yao mpya na ya tatu ambayo wamepanga kuitoa mapema mwakani.
"Tupo katika maandalizi ya kwenda kurekodi nyimbo mpya tatu, tukiwa tunajiandaa kupakua albamu yetu ya tatu, kwa kweli kwa sasa Levent tupo kamili na tumepania," alisema Suzuki.
Mtunzi na muimbaji huyo, aliyerejea katika bendi hiyo baada ya kuikimbia kwa muda na kujiunga na Extra Bongo, alisema nyimbo nyingine tatu zimeshaanza kufanyiwa mazoezi na mara baada ya kumaliza kurekodi hizo za awali watarejea tena studio kukamilisha nyimbo hizo.
Kuhusu kikosi chao, Suzuki alisemakipo kamili, kila idara kuanzia safu ya unenguaji, wapiga ala na waimbaji ambao mbali na yeye yupo pia Steve Dokta na Salum Mzalamo 'Baba Mapacha'.
Bendi hiyo ya Levent ilianzishwa mwaka 2004 na imewahi kufyatua albamu mbili tu hadi sasa ambazo ni Rafiki ya 2006 na ile ya Mama Kabibi ya mwaka 2008 wakati bendi ikiwa chini ya Richard Malifa, alioyewahi kung';ara na bendi mbalimbali hapa nchini.

Msondo yamuombea Gurumo



WAKATI hali yake ikizidi kuwa tete, uongozi wa bendi ya Msondo Ngoma umemuombea dua njema na kuwataka Watanzania kuzidi kumuombea kiongozi wao na muimbaji mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Maalim Muhidin Gurumo aliyelazwa hospitalini kwa matatizo ya mapafu.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D', alisema wanamuziki na uongozi mzima wa Msondo umekuwa ukiendesha dua maalum kila siku kumtakia kila la heri na afueni, Gurumo ili aweze kurejea tena jukwaani.
Super D, alisema Msondo bado inamhitaji mno Gurumo kutokana na umahiri wake katika muziki na uongozi kwa ujumla na kuwaomba mashabiki wao na wadau wa muziki wa ujumla kuzidi kumuombea mwanamuziki huyo mkongwe awe kupona haraka.
"Kwa kweli tunamuombea sana mwenzetu aweze kupona na tunawasihi watanzania bila kujali dini, rangi au kabila na ushabiki wa muziki, wamuombee kamanda Gurumo, Mwenyezi Mungu amfanyie tahafif apone haraka," alisema Super D.
Super D, alisema pamoja na kumuombea kiongozi wao huyo, bendi yao bado inaendelea na maonyesho yao kama kawaida pamoja na kufanya maandalizi ya kufyatua albamu yao mpya.
Alisema kwa leo Jumamosi bendi yao itakuwa kwenye bonanza lao kwenye viwanja vya Sigara, TCC- Changombe na kesho Jumapili watawachezesha wapenzi wa muziki miondoko yao ya Msondo kwenye onyesho litakalofanyika Max Bar, Bungoni Ilala jijini Dar es Salaam.
"Hatuwezi kuacha maonyesho, tunaendelea na shoo huku tukizidi kumuombea mwenzetu, leo (jana) Ijumaa tutakuwa Postal Club, Jumamosi tunaendelea na bonanza letu pale TCC-Chang'ombe na tutamalizia wikiendi yetu kwenye ukumbi wa Maxi Bar, Ilala," alisema.
Msondo inayotamba na albamu ya HUna Shukrani iliyotoka mwaka jana, ipo katika maandalizi ya kutoa albamu mpya ambapo hadi sasa tayari imeshaachia nyimbo tatu ambazo ni Dawa ya Deni, Lipi Jema na Mjomba.

Ally Choki awafunda wanamuziki wenzake



NYOTA wa muziki wa dansi nchini, Ally Choki amewafunda wanamuziki wenzake akiwataka wajenge tabia ya kuwa na shukrani wakikumbuka mazuri wanayofanyiwa na bendi wanazozihama badala ya kuziponda na kutaja mabaya tu.
Choki alisema tabia ya wanamuziki wanaohama bendi kuponda na kukashfu kule watokapo sio tu zinavunja umoja, ila inajenga uhasama miongoni mwa wasanii na wamiliki na mwisho wa siku ni kudidimiza muziki ambao umekuwa ukisaidia vijana wengi kupata ajira zao.
Akizungumza na MICHARAZO, Choki, alisema yeye binafsi pamoja na kutamba kimuziki nchini, katu hawezi kusahau fadhila na mazuri aliyofanyiwa na Asha Baraka, kitu alichotaka hata wasanii wengine wawe na moyo wa namna hiyo wa kukumbuka fadhila.
Choki alisema amelazimika kusema hayo kutokana na baadhi ya wasanii walioihama bendi yake kusambaza maneno ya kashfa juu yake na bendi yake, wakati kabla ya kuhama walikuwa wakifanyiwa fadhila zilizowafanya wamuone kama 'Mungu-Mtu'.
"Siwalazimishi, lakini nawaasa wanamuziki wenzake na wasanii kwa ujumla kuwa na shukrani kwa mazuri wanayofanyiwa na makundi yao, kuhama hakukatazwi, lakini sio kwa kukashfu au kuponda tu, kwani ndiko kunakodumaza muziki," alisema Choki.
Aliongeza kama sio kuwa na moyo wa kutaka muziki wa dansi usonge mbele na kusaidia vijana wengine wenye vipaji kupata riziki kupitia ajira ya sanaa hiyo, asingeanzisha na kuendesha bendi ya Extra Bongo na badala yake angekuwa mwanamuziki wa kujitegemea ili ale kuku kwa raha.
"Kwa jina na umaarufu nilionao ndani na nje ya nchi naweza kuendesha shughuli zangu za muziki kama solo artist, lakini naguswa na kupenda kusaidia wengine kutokana, ili kulifanya jina langu liendelee kutajwa katika mchango wa muziki huu," alisema.
Choki, alisema hata leo Mbaraka Mwinshehe na Marijab Rajab pamoja na kufa wanatajwa kwa sababu waliwasaidia wengi kupitia bendi zao hali ambayo anatamani naye iwe hivyo milele.

Dance Music Competition laiva

USAILI wa wasanii chipukizi wa muziki wa dansi watakaoshiriki shindano la kusaka nyota wapya wa muziki huo nchini, kupitia shindano la 'Dance Music Competation' unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 20-21 kwenye ukumbi wa Afri Center, Ilala jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa shindano hilo, Seleman Mathew alisema maandalizi ya mchakato huo umeshaanza kwa kuanza kutoa fomu za ushiriki kwa wanaopenda kushiriki mchuano huo kuzichangamkia kabla ya usaili huo utakaoendeshwa na majaji wanne.
Mathew aliwataja majaji hao kuwa ni wanamuziki wakongwe wa muziki huo nchini, Ally Choki wa Extra Bongo, Tshamanga Kalala Assosa wa Bana Marquiz, Nyota Waziri wa Kilimanjaro Band 'Wana Njenje' na Abdul Salvador 'Father Kidevu' wa Hisia Kali Band.
'Mchujo wa kusaka vijana kwa ajili ya shindano letu na nyota wapya wa muziki wa dansi utaanza rasmi Desemba 20-21 kwenye ukumbi wa Afri Center Ilala kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni, na watakaopenya wataingia kwenye kinyang'anyiro hicho," alisema Mathew.
Alisema kinyang'anyiro cha shindano hilo kitaanza Januari 16 kwa washiriki kuingia kambini na kupigiwa kura hadi atakapopatikana mshindi katika fainali zitakazofanyika Machi 6 mwakani.
Mathew, beki za zamani wa timu za Simba, Yanga, Plisner na Ndovu-Arusha, alisema lenye lengo la shindano hilo ni kuibua wanamuziki wapya wa dansi na kuendeleza muziki huo nchini kuwabadili vijana wengi kuona hakuna muziki mwingine zaidi ya Bongofleva tu.
Alisema washiriki wanaotaka kushiriki wanapaswa kuwa katika kundi la kuanzia wasanii watano hadi saba wenye uwezo wa kuimba nyimbo za muziki wa dansi na kuongeza kwa wale ambao hawana makundi pia wanaruhusiwa muhimu wawe na uwezo katika muziki huo.
Alisema fomu za ushiriki wa shindano hilo zinapatikana kwenye ukumbi wa Afri Center kwa gharama ya Sh 3,000 na kuwataka wenye vipaji hivyo kuchangamkia nafasi hiyo, huku akiwataka wadhamini kujitokeza kuwapiga tafu kufanikisha shindano hilo la kwanza nchini kwa muziki huo.

Kanumba, apania uzinduzi wa Off Side DR Congo



NYOTA wa filamu nchini, Stephen Kanumba, ametamba kuwa uzinduzi wa kazi mpya aliyotoa pamoja na Vincent Kigosi 'Ray' iitwayo 'Off Side' utakaofanyika wiki ijayo nchini DR Kongo, utakuwa wa aina yake kutokana na jinsi walivyojiandaa kuwapa raha mashabiki wao nchini humo.
Uzinduzi wa filamu hiyo iliyowarejesha tena wawili hao pamoja tangu walipotoa Ophra miaka miwili iliyopita, unatarajiwa kufanyika kati ya Desemba 15-20 katika miji miwili ya nchi hiyo ya Goma na Bukavu.
Akizungumzia uzinduzi huo, Kanumba, alisema wamepania kufanya kweli ili kusuuza nyoyo za mashabiki wao lukuki waliopo katika nchini hiyo na Ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati na pia kutaka kujitengenezea majina yao katika anga la kimataifa.
"Hii ni nafasi ambayo haipaswi kuichezea na ndio maana tunaenda kamili kuwapa raha mashabiki wetu wakati wa uzinduzi huo, ili kujitangaza kimataifa," alisema Kanumba.
Kanumba, atakayeambatana na washiriki vinara wa filamu hiyo, Ray, Irene Owoya, Aunty Ezekiel na mtoto Jennifa aliyecheza filamu za This is It na Uncle JJ, alisema maandalizi yao ya kwenda kufanya uzinduzi huo yamekamilika na kwamba wakati wowote wiki ijayo watatua nchini humo kufanya mambo.
"Tunaendelea vema na maandalizi ya shughuli hiyo na tunawasihi wakazi wa Kongo wakae mkao wa kula kupata klitu roho inapenda kqwani tutafanya onyesho la jukwaani la dakika kama 30 ili kukonga nyoyo zao," alisema.
Katika filamu hiyo ya kimapenzi, Kanumba amecheza kama kijana maskini anayelazimishwa mapenzi na mke wa tajiri kitu ambacho kinamletea kizaazaa cha aina yake.
Kanumba alisema mara baada ya uzinduzi huo wa Kongo wataenda Burundi kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya kuitoa hadharani kupitia kampuni ya Steps Entertainment ambayo ndiyo yenye kibali cha kuisambaza kazi hiyo.

Huba wana Bangkok Deal

BAADA ya kutamba na filamu ya Hazina, kampuni ya Huba, ipo mbioni kufyatua kazi mpya iitwayo Bangkok Deal ambayo imeshirikisha nyota kadhaa wa fani hiyo nchini.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Husseni Ramadhan 'Swagger' aliiambia NIPASHE jana kuwa, wapo hatua ya mwisho ya upigaji wa picha za filamu hiyo ambayo ameshirikishwa mkali Charles Magali.
Swagger alisema ndani ya filamu hiyo mbali na Mzee Magali, pia kuna wachina walioshirikishwa katika kuipa ladha kulingana na simulizi ya kazi hiyo aliyodai italeta mapinduzi ya fani hiyo nchini.
"Walioishuhudia Hazina na kazi nyingine tulizofyatua kupitia kampuni hii ni chamtoto tu, Bangkok Deal ni kazi isiyo na maelezo, tuombe tumalize na kuiingiza sokoni mashabiki ndio watakaijaji," alisema.
Swagger, alisema pamoja na kuendelea kurekodi filamu hiyo, pia kampuni hiyo tayari imeshaanza maandalizi ya kazi nyingine itayofahamika kwa jina la Hofu Tupu, aliyopanga kuitoa mapema mwakani.
Swagger aliyekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya kupitia makundi ya 2 Wise Boy na The Crime Busters, alisema ndani ya filamu hizo wasanii wakali na wanaotamba katika fani hiyo wameshirikishwa.

Monday, December 6, 2010

Mapacha Watatu, Sam wa Ukweli kupimana Ubavu Dar

KUNDI la Mapacha Watatu linaloundwa na waimbaji mahiri nchini, Khalid Chokoraa, Jose Mara na Kalala Junior wanatarajia kuonyeshana kazi na msanii anayekuja juu katika miondoko ya muziki wa kizazi kipya Sam wa Ukweli.
Mapacha hao watatu na Sam wa Ukweli watakutanishwa kwenye onyesho la pamoja lifahamikalo kama 'Usiku wa Sauti za Kizazi Kipya cha Dansi' litakalofanyika Desemba 13, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa onyesho hilo, Sauda Mwilima, aliiambia Micharazo kuwa, onyesho hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Stereo Bar, Kinondoni na wasanii hao wataonyesha umahiri wao.
Mwilima alisema onyesho hilo linawagusa Mapacha Watatu, watakaofanya vitu vyao kwa kutoa burudani na watasindikizwa na msanii Salum Mohamed 'Sam wa Ukweli' anayetamba na ngoma yake iitwayo 'Sina Raha'.
"Usiku wa Sauti ya Kizazi Kipya cha Dansi utaporomoshwa na Mapacha Watatu, wakisindikizwa na shoo ya ukweli mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini Sam wa Ukweli, yaani ni usiku usio wa kawaida," alisema Mwilima.
Mwilima ambaye ni mtangazaji wa kituo cha runinga cha Star Tv, alisema maandalizi ya onyesho hilo yanaendelea vema na kuwataka mashabiki wa muziki kukaa mkao wa kula kupata uhondo toka kwa wakali hao.
Kundi hilo la Mapacha Watatu linaundwa na waimbaji hao toka bendi hasimu za African Stars 'Twanga Pepeta' na FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma'.

Mwisho

Mkulo: Nimewasamehe walionichafua, ila sintowasahau

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amesema pamoja na kuwasamehe wale wote waliompakazia mabaya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, bado hawezi kuwasahau hadi anaingia kaburini.
Pia, amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Kilosa kwa ujumla, kuzika tofauti zao zilizosababishwa mchakato wa uchaguzi mkuu, ili kuweza kushikamana kuijenga wilaya na jimbo lao la Kilosa liweze kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Akizungumza kwenye mapokezi na hafla ya kupongezwa kuteuliwa tena kuwa waziri, Waziri Mkulo, alisema kashfa alizokuwa akipewa akidaiwa sio raia wa Tanzania na kejeli zingine ni vitu ambavyo vilimuumiza, ila amewasamehe wote waliomfanyia jambo hilo.
Waziri alisema hata hivyo pamoja na kuwasamehe wahusika, katu hatawasahau kwa vile walimpa wakati mgumu na kumnyima raha, kitu alichodai kitaendelea kubaki kichwani mwake hadi kifo.
Alisema wale walioanzisha na kueneza maneno hayo na waliomtusi, wasimuogope kwa sababu anafahamu siasa ni mchezo usio na simile na wenye kuhitaji uvumilivu mkubwa kitu alichoweza kukimudu na ndio maana amewasamehe kwa yote.
"Walionitusi na kunizushia kwamba mie sio raia na wengine kufikia hata kumhusisha mke wangu, wote nimewasamehe, ila kwa hakika sintowasahau, muhimu nataka kuwaambia wahusika wasiwe na hofu juu yangu yale yamepita kwani najua siasa ndivyo zilivyo," alisema Mkulo.
Alisema kama sio mambo ya siasa, kwa hakika angeweza kuwafungulia mashtaka na kudai fidia kubwa wahusika wote waliomchafua kipindi cha kura za maoni ndani ya CCM na hata kwenye uchaguzi mkuu uliompa ushindi wa kishindo yeye Mkulo na chama chake.
Waziri Mkulo, alisema kwa kuwa uchaguzi umeshapita kwa sasa yeye ni mbunge wa wakazi wote wa Jimbo la Kilosa na hivyo atawatumikia wananchi wote kwa ajili ya kuwaletea maendeleo, akiomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha aliyopanga kwa miaka mitano ijayo.
Wakati wa mchakato wa kura za maoni, Waziri Mkulo alivumishiwa kuwa yeye si raia wa Tanzania na kikundi cha watu waliojiita Wazee wa Kilosa, ambao walikuja kurukwa na uongozi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo waliodai hawakumtuma mhusika aliyeanzisha chokochoko hizo.
Pia baada ya kushinda kiti hicho cha Ubunge kwa mara ya pili, baadhi ya watu walidaiwa kuapa kuwa asingekuwa miongoni mwa wateule wa Baraza Jipya la Mawaziri, kitu kilichoenda kinyume kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumtangaza kuendelea kushikilia wizara hiyo ya Fedha.

CCM Kilosa waambiana kweli, wapashana kuacha majungu




UONGOZI wa Chama cha Mapinduzi, CCM, Wilaya ya Kilosa, umewataka wanachama wake waache majungu na mifarakano na badala yake washikamane kukijenga chama chao pamoja na kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi walioshinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Viongozi wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Christopher Wegga na Katibu wake, Gervas Makoye walitoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati wa mapokezi na sherehe ya kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi zilizofanyika wilayani humo.
Makoye, aliyehutubia katika mkutano wa mapokezi ya Mkulo, yaliyofanyika kwenye uwanja wa CCM wilayani hapo, alisema kwa kuwa uchaguzi mkuu umeshamalizika ni vema wanachama wa chama hicho wakazika tofauti zao na kushirikiana na walioshinda kukijenga chama chao.
Katibu huyo, alisema pamoja na uchaguzi huo kumalizika na chama chao kuzoa ushindi wa kishindo, bado wapo baadhi ya wanachama wanaendeleza majungu na maneno kitu alichodai haisaidii.
Alisema wanaofanya hivyo ni wanachama waliozoea kupiga mizinga (kuomba hela) na kuwataka wenye tabia hiyo kubadilika kwa sababu chama hakitawavumilia.
"Wanachama wa CCM na wana Kilosa kwa ujumla acheni kupiga maneno, acheni majungu tushikamane kukijenga chama, tuwape ushirikiano wa kutosha viongozi walioshinda kwa sababu uchaguzi umeisha na hivyo tunapaswa kuvunja kambi zetu tuwe kitu kimoja," alisema.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Christopher Wegga, akihutubia kwenye hafla ya kupongeza Waziri Mkulo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Babylon, alisema kuendeleza majungu na tofauti baada ya uchaguzi ni kukwaza maendeleo ya wilaya yao na kuwataka wananchi kushirikiana.
Alisema binafsi anampongeza Waziri Mkulo kwa kurejeshwa kwenye cheo chake cha uwaziri na kuwapongeza wazee walioandaa sherehe hiyo.
Sherehe hiyo ya kumpongeza Mkulo, iliandaliwa na Baraza la Wazee wa Kilosa, ambapo Mwenyekiti wake, Raphael Chayeka, alisema wamefurahishwa mno na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumrejesha Mbunge wao kwenye nafasi hiyo kwa imani Kilosa itapata maendeleo zaidi.
"Imani yetu ni kwamba cheo ulichopewa ni fahari kwetu wana Kilosa, wewe ni kama Rais wetu na tunaamini Kilosa itasonga mbele, tunakutakia kila la heri mna mafanikio," alisema Chayeka.
Waziri Mkulo, aliwashukuru wazee hao, wanachama na wananchi wa Kilosa kwa ujumla kwa kuonyesha imani yake kwake na kuwaahidi kuwasaidia kuwaletea maendeleo ili miaka mitano ijayo Jimbo hilo libadilike na litofautiane kuliko miaka mitano iliyopita.
Ila alisema jambo la muhimu ni wananchi bila kujali itikadi za vyama, dini, jinsia, kabila kushirikiana pamoja katika kupigania wilaya yao iondokane na vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo yao.
****



Na Badru Kimwaga, Aliyekuwa Kilosa
WAZIRI wa Fedha na Uchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amesema pamoja na kuwasamehe wale wote waliompakazia mabaya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, bado hawezi kuwasahau hadi anaingia kaburini.
Pia, amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Kilosa kwa ujumla, kuzika tofauti zao zilizosababishwa mchakato wa uchaguzi mkuu, ili kuweza kushikamana kuijenga wilaya na jimbo lao la Kilosa liweze kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Akizungumza kwenye mapokezi na hafla ya kupongezwa kuteuliwa tena kuwa waziri, Waziri Mkulo, alisema kashfa alizokuwa akipewa akidaiwa sio raia wa Tanzania na kejeli zingine ni vitu ambavyo vilimuumiza, ila amewasamehe wote waliomfanyia jambo hilo.
Waziri alisema hata hivyo pamoja na kuwasamehe wahusika, katu hatawasahau kwa vile walimpa wakati mgumu na kumnyima raha, kitu alichodai kitaendelea kubaki kichwani mwake hadi kifo.
Alisema wale walioanzisha na kueneza maneno hayo na waliomtusi, wasimuogope kwa sababu anafahamu siasa ni mchezo usio na simile na wenye kuhitaji uvumilivu mkubwa kitu alichoweza kukimudu na ndio maana amewasamehe kwa yote.
"Walionitusi na kunizushia kwamba mie sio raia na wengine kufikia hata kumhusisha mke wangu, wote nimewasamehe, ila kwa hakika sintowasahau, muhimu nataka kuwaambia wahusika wasiwe na hofu juu yangu yale yamepita kwani najua siasa ndivyo zilivyo," alisema Mkulo.
Alisema kama sio mambo ya siasa, kwa hakika angeweza kuwafungulia mashtaka na kudai fidia kubwa wahusika wote waliomchafua kipindi cha kura za maoni ndani ya CCM na hata kwenye uchaguzi mkuu uliompa ushindi wa kishindo yeye Mkulo na chama chake.
Waziri Mkulo, alisema kwa kuwa uchaguzi umeshapita kwa sasa yeye ni mbunge wa wakazi wote wa Jimbo la Kilosa na hivyo atawatumikia wananchi wote kwa ajili ya kuwaletea maendeleo, akiomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha aliyopanga kwa miaka mitano ijayo.
Wakati wa mchakato wa kura za maoni, Waziri Mkulo alivumishiwa kuwa yeye si raia wa Tanzania na kikundi cha watu waliojiita Wazee wa Kilosa, ambao walikuja kurukwa na uongozi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo waliodai hawakumtuma mhusika aliyeanzisha chokochoko hizo.
Pia baada ya kushinda kiti hicho cha Ubunge kwa mara ya pili, baadhi ya watu walidaiwa kuapa kuwa asingekuwa miongoni mwa wateule wa Baraza Jipya la Mawaziri, kitu kilichoenda kinyume kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumtangaza kuendelea kushikilia wizara hiyo ya Fedha.

Mwisho
Mwisho

BFT yaandaa kozi ya ukocha, Super D apigwa tafu

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania, BFT, limeandaa kozi ya ukocha wa mchezo huo kwa vijana na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, ili kukuza na kuendeleza ngumi nchini.
Afisa Habari wa BFT, Eckland Mwaffisi, aliiambia Micharazo kuwa, kozi hiyo ya siku 10 inatarajiwa kuanza Desemba 14-24 ikifanyika jijini Dar es Salaam.
Mwaffisi alisema kozi hiyo itahusisha vijana wenye kupenda kufundisha mchezo huo, pia wangependa walimu wa shule za Msingi na Sekondari wajitokeze kwa wingi kwa sababu lengo lao ni kutaka kuusambaza mchezo huo shuleni kwa manufaa ya baadae kwa taifa.
"BFT katika mikakati yake ya kukuza na kuendeleza michezo kuanzia mitaani hadi shuleni imeandaa kozi ya siku 10 itakayowahusisha wote wenye 'idea' ya mchezo wa ngumi kwa lengo la kwenda kufundisha wenzao ili kuufanya mchezo huo urejee katika hadhi yake," alisema Mwaffisi.
Alisema tayari baadhi ya wanaopenda kushiriki kozi hiyo wameshaanza kujitokeza na alizidi kutoa wito kwa wenye kuhitaji kujifunza ukocha wa ngumi kujitokeza mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine, Kocha wa Ngumi wa Klabu ya Ashanti, Rajabu Mhamila 'Super D' amepewa msaada wa Sh. Laki 1.5 zitakazomwezesha kushiriki kozi ya siku 10 ya ukocha iliyoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT).
Msaada huo ambao ni wa pili kwa kocha huyo kupewa ulitolewa na mdau wa michezo Zulfiqal Ali kumwezesha Super D kufanikisha malengo yake ya kuendeleza mchezo wa ngumi kwa vijana
Akizungumza Dar es Salaam, wakati akimkabidhi pesa hizo Zulfiqal alisema ameamua kufanya hivyo ili kuungana na wadau wengine wa michezo ikiwemo serikali katika kuendeleza michezo.
Hata hivyo Zulfiqal amewaomba wadau wengine kujitokeza kuungana na jamii kusaidia kukuza michezo ili kuwawezesha vijana wasio na ajira waweze kujiajili.
Naye Super D alisema anashukuru na kuahidi kuzingatia kozi hiyo siku zote ili aweze kupanua ujuzi ambao utawawezesha kuwasaidia mabondia wanaochipukia hapa nchini.
Awali kocha huyo alipewa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi laki tatu na zaidi kwa ajili ya mazoezi ya mabondia wanaohudhuria mafunzo yanayotolewa na kocha huyo

Extra Bongo kupeleka Vuvuzela Kilosa



BENDI ya Extra Bongo, inayotamba na mitindo ya 'Vuvuzela' na 'Kizigo' inatarajiwa kwenda kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na wakazi wa Kilosa watakapoenda kufanya onyesho wilayani humo.
Extra Bongo inayomilikiwa na mtunzi na muimbaji mahiri nchini, Ally Choki, itaenda Kilosa kufanya onyesho siku ya sikukuu hiyo kwenye ukumbi wa Babylon Luxury Pub.
Meneja wa ukumbi huo, Robert Chipindula, aliiambia MICHARAZO, kwa muda mrefu wamekuwa wakiombwa na mashabiki wa muziki kuwapelekea bendi hiyo ya Extra Bongo na ndio maana wameialika kwenda kutumbuiza wakati wa sikukuu hiyo.
Chipindula, alisema tayari wameshamalizana kila kitu na uongozi wa bendi hiyo na kukubali kutua wilayani humo kwa onyesho hilo litakaloenda sambamba na utambulisho wa nyimbo na miondoko mipya ya bendi hiyo.
Extra Bongo iliyokuwa ikifahamika kwa miondoko ya Kujinafasi Next Level kwa sasa inatamba na mitindo yao mipya miwili ya Kizigo na Vuvuzela, ambayo wamekuwa wakiitambulisha kila wanapoenda kufanya maonyesho katika maeneo mbalimbali.
Bendi hiyo inayotamba na albamu yao mpya ya Mjini Mipango, tayari imeshaanza kufyatua vibao vipya kwa ajili ya albamu ya pili, baadhi ya nyimbo hizo ni Nguvu na Akili na Neema ambazo zimekuwa zikiwachengua mashabiki wa muziki wa dansi kila zinapopigwa ukumbini.

Wahanga wa Kilosa waulalamika kutelekezwa







WAHANGA wa Mafuriko ya Kilosa, wanaoishi kwenye Kambi ya Mazulia wilayani humo, wameulalamikia uongozi wa wilaya hiyo kwa kuwatelekeza bila msaada wowote, huku vyakula vyao vya misaada vikiharibika na kutupwa na vingine kuchomwa moto jalalani.
Pia wahanga hao wamedai hadi sasa hawajui hatma yao ndani ya kambi hizo zilizopo Kata ya Magomeni, kutokana na mara kwa mara kupokea vitisho vya kuhamishwa vinavyotolewa na watendaji wa wilaya hiyo wanaodai wanatumwa na Mkuu wao wa wilaya, Halima Dendegu.
Wakizungumza na Micharazo kwenye kambi hizo, iliyopo Kata ya Magomeni, wahanga hao walidai uongozi wa wilaya hiyo umewatelekeza bila kuwapa misaada iliyotolewa na wasamaria wema na badala yake vyakula na misaada hiyo ikiharibika na kutupwa au kuchomwa moto.
Wakazi hao walisema mara ya mwisho kupelekewa misaada ilikuwa ni Mwezi Machi na kwa mujibu wa makubaliano ya awali ni kwamba wangekuwa wakipewa misaada hiyo kila baada ya miezi mitatu vitu ambavyo havikufanyika.
Walisema misaada ya mwezi Juni hawakupewa kwa maelezo ya kwamba walilimiwa mashamba na uongozi wa serikali ya wilaya, ambayo walidai hayakutoa mavuno ya kutosha kwa vile yalilimwa wakati mbaya na cha ajabu tangu hapo hawajapewa tena.
"Hatujapewa misaada tangu Machi na hivi karibuni baadhi ya misaada yetu kama nguo na chakula vilienda kutupwa eneo la Ilonga kutokana na kuharibika na Novemba 18 vyakula vyetu vilichomwa moto kwa maelezo vimeharibika, hii ni haki kweli?" alihoji Peter Thomas, 68.
Thomas, alisema hata pale wanapojaribu kuulizia sababu ya kufanyiwa ukatili huo kana kwamba wamependa kuishi kambini hapo, wamekuwa wakipokea vitisho ikiwemo watu walioenda kwao kama Tume maalum ya kuhakiki kambi hiyo waliowaeleza karibia watahamishwa warejee makwao.
"Yaani kwa kifupi tumekuwa tukiishi kwa mashaka bila kujua hatma yetu ndani ya kambi hii, misaada yetu inayeyuka na kibaya tunatishwa tukiambiwa tulikuwa tukibembelezwa kwa sababu ya uchaguzi tu, na sasa uchaguzi umeisha tutalijua jiji," alisema Thomas.
Naye Verena Philipo Mcharo, alisema hivi karibuni mkuu wao wa wilaya aliwapelekea msaada wa mabati sita, mbao moja, misumari kilo moja na mfuko mmoja wa saruji kwa wale waliobomokewa na nyumba zao ili kwenda kujenga katika viwanja walivyopewa bila kujua vilipo.
"Ebu fikiria vifaa hivyo vitatosha nini kama sio kutaka kuwadhihaki watu, tena sio wote waliopewa hati za viwanja walivyoelezwa wametengewa kwenda kujenga makazi yao mapya na sisi tuliokuwa wapangaji tumeambiwa tujue la kufanya kwani misaada hiyo haituhusu," alisema.
Verana, alisema yeye alipohoji kubaguliwa huko miongoni mwa wahanga wa janga hilo la Mafuriko lililotokea mwishoni mwa mwaka jana, aliambiwa anapaswa kurejea kwao Iringa, bila kujali kama alikuja Kilosa kama raia mwingine kwa ajili ya kutafuta maisha.
Mwenyekiti wa kambi hiyo, Msagati, alisema kwa kifupi ni kwamba wao hawajui hatma yao ndani ya kambi hiyo kutokana na mambo yanavyoendelea, huku akitaka waonyeshwe viwanja walivyopewa hati ya kuvimiliki wajue cha kufanya ili kuondokana na dhiki wazipatazo.
Naye Tabia Athuman Matiangu, 71, alidai Septemba 20, mwaka huu alipigwa kofi na Mkuu wa Wilaya kwa kile kilichoelezwa kuwa na kiherehere cha kuwasemea wenzake wakati wa ukaguzi wa wahanga kambini hapo.
Madai ya ajuza huyo, yalithibitishwa pia na baadhi ya wahanga hao, wakidai lilifanyika kama moja ya vitisho dhidi ya malalamiko yao kwa uongozi huo wa wilaya.
Micharazo iliwasiliana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Dendegu, aliyekuwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam, kwa njia ya simu ambapo alikiri kusikia malalamiko hayo, ila alisema ni 'mtandao' maalum ulioundwa kumchafua kutokana na msimamo wake wa kuwakomalia watendaji wa halmashauri hiyo.
"Madai ya wananchi hao hata mie yamenifikia, lakini mengi ni yenye nia ya kutaka kunichafua na yanafanywa na watu wa halmashauri kutokana na madudu yao yaliyofanya hadi wilaya hii ipewe hati chafu kwa upotevu wa fedha kibao za miradi ya maendeleo," alisema Dendegu.
Alikiri kuchomwa kwa vyakula, bila kufananua kiwango chake na sababu zilizofanya kufanywa kwa kitendo hicho kwa madai yupo nje ya ofisi na hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila kitu na kumuomba mwandishi huyu aonane nae baada ya kurejea ofisini kitu kilichoshindikana.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi zilizopatikana ndani ya wilaya hiyo chakula kilichoharibika na kuchomwa moto vikijumuisha Maharage, Ngano, Mchele na Unga wa Sembe ni karibu tani mbili (kilo 1,700).
Alipoulizwa juu ya dai la kumpiga kofi mmoja wa wahanga hao, Mkuu huyo, alionyesha mshangao na kukanusha, huku akihoji mambo hayo yameibukia wapi kipindi hiki ambacho ofisi yake inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wahanga hao.
Juu ya mgao wa vifaa vya ujenzi kwa wahanga hao, alisema ni kweli alitoa mgao huo kiduchu kutokana na jinsi msaada wenyewe ulivyoletwa kwenye ofisi yake.
"Ni kweli niliwapa vifaa hivyo kama walivyokuambia, ila vinaonmekana vichache kwa sababu ndivyo vilivyolewa na wasamaria wema, hatuna mahali pa kuhifadhia hivyo tumewapa wahifadhi wenyewe wakati tunasubiri vingine," alisema.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema, anaamini wanaeneza taarifa hizo kwa kutumia vyombo vya habari wana nia ya kumchafua mbele ya umma, ila alisisitiza hatishiki kwa vile tangu aanze kuaminiwa na serikali na kuteuliwa hajawahi kuharibu mahali popote.

Mwisho

Sunday, December 5, 2010

TAKUKURU-Kilosa yafichua kucha zake

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Wilaya ya Kilosa, imeanza makali yake kwa kuwafikisha mahakamani baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa na ubadhilifu wa fedha za halmashauri hiyo.
Kaimu Kamanda wa Takukuru wilayani humo, Heri Mwankusye, aliiambia Micharazo mjini humo kuwa, tangu ofisi yao ifanyiwe mabadiliko ya kupelekwa watendaji wapya, wameweza kufungua jumla ya kesi tano ambazo watuhumiwa wake wamefikishwa mahakamani.
Mwankusye alisema kesi hizo ni za kuanzia kipindi cha Januari na Desemba mwaka huu, ambapo moja inawahusisha watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Kilosa, ambayo ilifunguliwa mwezi uliopita ikihusisha utafunwaji wa Sh. Mil. 3.7.
Katika kesi hiyo inamhusisha pia karani wa benki ya NMB wilayani humo pamoja na maafisa wengine wakuu wa halmashauri hiyo (idadi na majina yao tunayo).
Mwankusye alizitaja kesi zingine ni ile inayomhusisha Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbumi, aliyestakiwa kwa kosa la kupokea hongo ya Sh 5,000 ambapo kesi yake ipo hatua ya mwisho kabla ya kutolewa hukumu.
"Kesi hii ipo hatua ya mwisho na hukumu yake itatolewa Desemba 17 mwaka huu, kesi nyingi ni ile inayomhusu Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo yta Msowelo, anayeshtakiwa kwa kupokea rushwa ya Sh 60,000," alisema.
Kamanda huyo alizitaja kesi zingine kuwa ni ile ya Afisa Mifugo wa Kata ya Kisanga aliyeshtakiwa pamoja na askari kwa tuhuma za rushwa ya Ng'ombe nane na fedha taslim, Sh.Mil. 1, huku kesi ya mwisho ikiwa inahusisha askari wawili, nao wakidaiwa kupokea rushwa ya ng'ombe katika kata hiyo hiyo ya Kisanga.
Mwankusye alisema kesi hizo ni mwanzo wa taasisi yao kushughulikia tuhuma zinazowasilishwa kwao kila kukicha juu ya kuwepo kwa ubadhilifu na vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwa watendaji wa halmashauri hiyo ya Kilosa.
"Huu ni mwanzo wa kasi yetu ya kushughulikia vitendo vya rushwa na ubadhilifu, lengo ni kutaka kuthibitishia umma kwamba tupo kazini na hasa baada ya Rais kutupa meno," alisema Mwankusye.
Alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano kuweza kuwashughulikia watendaji hao na kuisaidia serikali katika kupambana na kukomesha vitendo hivyo vinavyochangia kurudisha maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Mwisho

Waziri Mkulo ataka Wezi wasipewe uongozi Kilosa





WAZIRI wa Fedha na Uchumi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amewaomba wananchi wa wilaya ya Kilosa kuwashawishi madiwani wao kutowachagua wenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ambao ni wezi na wasio na uchungu fedha za umma.
Pia, Waziri Mkulo, amesema anajisikia aibu kwa wilaya hiyo ya Kilosa kupata hati chafu kutokana na kukithiri kwa wizi na ubadhilifu mkubwa wa fedha za miradi ya maendeleo zilizopelekwa katika halmashauri hiyo, akitishia kuzuia mabilioni ya fedha yaliyoidhinishwa kwa halmashauri hiyo.
Akiwahutubia wanachama wa CCM na wakazi wa wilaya hiyo katika mapokezi yake na hafla ya kumpongeza kwa kuteuliwa tena kuwa Waziri, Mkulo, alisema ili kuweza kuzuia wizi na ubadhilifu wa fedha za maendeleo za halmashauri yao ni vema wananchi wakawabana madiwani wao na kuwasihi wasiwachague wenyekiti wa kuiongoza halmashauri hiyo ambao ni wezi.
Uchaguzi huo wa Wenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Kilosa, unatarajiwa kufanyika ndani ya mwezi huu, ambapo wagombea wanne wamejitokeza kuomba nafasi za Uenyekiti wakisubiri kupitishwa kuwania wadhifa huo.
Ili kuifanya halmashauri hiyo kupata viongozi waadilifu, waaminifu na wenye uchungu wa kweli wa maendeleo ya wananchi, Waziri Mkulo, alisema ni vema wananchi wakawabana madiwani wao kuchagua wenyeviti safi.
Waziri Mkulo alisema, kwa deni kubwa alilonalo kwa wananchi wa Jimbo lake la kuwaletea maendeleo ni vema nao wamsaidie jambo moja la kuhakikisha halmashauri hiyo haiwaingizi madarakani wenyekiti ambao ni wezi, watakaoenda kutafuna fedha za miradi ya maendeleo.
"Kwanza nawashukuru kwa kuniwezesha kuwa Mbunge na kumfanya Rais Jakaya Kikwete kunirejeshea cheo hiki cha Uwaziri wa Fedha, kwa hakika nina deni kubwa kwenu la kuwapa maendeleo, ila nina ombi moja kwenu," alisema Waziri Mkulo.
"Naomba mshawishi madiwani wenu kunichagulia wenyekiti was halmashauri ya wilaya wasio wezi na wenye uchu wa kutafuna fedha za miradi ya maendeleo, bahati nzuri serikali imetuidhinishia Sh. Bil 6.83 kutoka Sh Mil 82 ilizokuwa ikipewa awali halmashauri yetu, hivyo tunataka watu wasafi ili Kilosa iwe na maendeleo na kutofautika na ile ya mwaka 2005," aliongeza.
Alisema katika watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo wamekuwa kama 'mchwa' kwa jinsi wanavyotafuna fedha za miradi na kufanya wananchi waendelee kutaabika, kitu ambacho kama Waziri wa Fedha na Uchumi anaumia na ndio maana anawaomba wananchi wasimwangushe.
"Kama Waziri wa Fedha na Uchumi, najisikia aibu kuona halmashauri yetu ya Kilosa mimi nikiwa Mbunge wake, tukipewa hati chafu kutokana na utafunaji wa fedha za miradi, kama wezi watachaguliwa kuiongoza halmashauri hii nitazuia fedha zilizoidhinishwa zisije," alisema Mkulo.
Alisema kama kusingekuwa na ulaji wa fedha za miradi, wilaya ya Kilosa ingekuwa mbali kwa maendeleo na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutorudia tena makosa kwa kuwarejesha madarakani madiwani ambao ni sehemu ya 'mchwa' wanatafuna fedha hizo.
Hafla ya kumpongeza Waziri Mkulo iliandaliwa na Baraza la Wazee wa wilaya hiyo chini ya Uenyekiti wa DC wa zamani, Raphael Chayeka na Katibu wake, Gervas Makoye, ambapo wanachama wa CCM na Jumuiya zake walimzawadiwa Mbunge huyo wa Kilosa.

Mwisho

Wednesday, September 29, 2010

Mtakuwa wa kwanza kutupongeza kwa ubingwa-Adebayor

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Azam, John Bocco 'Adebayor' amesema pamoja na kwamba hajaonyesha makeke yake kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado anatumaini ya kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora.
Aidha nyota huyo amekiri kufanya vibaya kwa timu yao katika baadhi ya mechi zake kumewaweka mahali pabaya, lakini anaamini mwisho wa siku wanaoiponda Azam watakuwa wa kwanza kuwapongeza kwa taji la ubingwa.
Akizungumza na Micharazo, Bocco, alisema ingawa amechwa na washambuliaji Jerry Tegete na Mussa Mgosi wenye mabao zaidi yake, bado anaamini ataibuka kinara wa mabao.
Bocco alisema mabao mawili aliyoyapata kupitia mechi mbili ni dalili za wazi kasi yake haijapungua, ila kilichotokea ni hali ya kawaida ya soka lenye ushindani kama ilivyo msimu huu nchini.
"Sina hofu ya kiatu cha dhahabu, kwani najiona nipo vema kutokana na ukweli nimecheza mechi mbili na nina mabao mawili, wakati wenzangu wamecheza mechi kibao wamenipita mabao mawili tu," alisema Bocco.
Kuhusu kuboronga kwa timu yake nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa, alisema ni wameyumba, lakini hiyo haina maana ndoto yao ya kutwaa ubingwa ndio imeyeyuka kwa sababu mechi za ligi hiyo bado zipo nyingi.
"Wanaotucheka sasa ndio watakaokuwa wa kwanza kutupongeza, naamini tutakaa vema na kufanya vizuri katika mechi zetu zijazo kwa vile tuna kikosi kizuri kinachocheza kitimu haswa," alisema Bocco.
Timu hiyo iliyoshika nafasi ya tatu msimu uliopita hivi karibuni iliyumba katika mechi zake tatu baada ya kufungwa na Simba, Kagera Sugara na Toto Afrika kabla ya kuzinduka mwishoni mwa wiki kwa kuilaza African Lyon.
Kikosi cha timu hiyo kimesheheni nyota kama Mrisho Ngassa, Bocco, Kally Ongala, Patrick Mafisango, Peter Ssenyonjo, Jabir Aziz na wengineo.

Mwisho

Mgossi hana hofu ya kiatu cha dhahabu

NYOYA wa Simba na mpachika mabao bora msimu uliopita, Mussa Mgosi amesema kasi ndogo ya ufungaji mabao aliyoanza nayo kwenye Ligi Kuu msimu huu, haina maana kwamba makali yake ya kuzifuma nyavu yamekwisha.
Msimu uliopita, Mgosi alitwaa kiatu cha dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora na kumshinda aliyekuwa akichuana naye kwa karibu Mrisho Ngassa aliyekuwa akiichezea Yanga kabla ya msimu huu kujiunga na Azam FC.
Mgosi aliyeifunga Yanga mara mbili msimu uliopita, amesema hana sababu ya kuwa na hofu katika kupachika mabao kwani ndio kwanza ligi iko hatua ya awali.
Mgosi ameongeza pamoja na Jerry Tegete kurejesha mbio zake za ufungaji kama ilivyokuwa msimu, hana huwezo wa kuifikia kasi yake itakayoibuka tena msimu huu.
"Ligi ndio kwanza imeanza, sioni sababu ya wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa na hofu kiatu cha dhahabu nitakitwaa tena na taji la ubingwa litaenda Msimbazi mwishoni mwa msimu huu," alisema.
Kuhusu pambano lao lijalo dhidi ya Yanga, Mgosi alisema kama ilivyokuwa msimu uliopita pia safari hii kajiandaa kuwazamisha watani zao ili kulinda heshima yao ambayo ilitibuliwa kwenye mechi ya ngao ya hisani ambapo Simba walilazwa mikwaju ya penati 3-1.
"Sitaki kuanza kusema sana, tusubiri Oktoba 16 itafika na utaona kitu gani nitakachoifanyia timu yangu dhidi ya Yanga," alisema.
Wakati ligi ikiingia mapumzikoni kupisha pambano la kuwania kufuzu fainali za Afrika za mwaka 2012, kati ya Tanzania na Morocco, Jerry Tegete ndiye aliyekuwa kiongoza kwa ufungaji magoli akipachika mabao manne dhidi ya matatu ya Mgosi.
Hata hivyo Mgosi alikuwa na nafasi ya kumpita Tegete kwani timu yao ilikuwa ikiumana na Mtibwa Sugar dimba la Jamhuri Morogoro, wakati tukiingia mitamboni.

AIBU! Ulimboka anaswa akihonga Mtibwa



WINGA wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya soka, Ulimboka Mwakingwe, alikamatwa na polisi na kulazwa korokoroni juzi kwa tuhuma za kumhonga fedha kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado ili aachie magoli wakati Mtibwa itakapocheza dhidi ya Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo jioni.
Ulimboka alinaswa na kisha kutupwa mbaroni katika kituo cha polisi Mtibwa, ikiwa ni muda mfupi baada ya kunaswa kwenye eneo la kambi ya Mtibwa iliyopo Manungu, Turiani Morogoro, akidaiwa kumhonga Kado kiasi cha fedha kinachotajwa kuwa ni Sh. 400,000 ili aiachie Simba katika mechi yao.
Habari zilizoifikia Micharazo jana, zilisema kuwa Ulimboka, winga aliyeng’ara Simba kwa misimu kadhaa kabla ya kuomba apumzike msimu huu, alinaswa kirahisi kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni mtego uliowekwa mapema dhidi yake.
Chanzo kingine kilidai kwamba alikamatwa majira ya saa 2:30 usiku na kupata kashkash za kupewa kipigo baada ya kukutwa na Kado kwenye kota za Mtibwa, na kudaiwa vilevile kwamba alikutwa na fedha zote zinazodaiwa kuwa za hongo.
Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alithibitisha juu ya kukamatwa kwa Ulimboka kambini kwa timu ya Mtibwa na kwamba kilichomkamatisha ni hizo tuhuma za kumhonga Kado.
Alisema kuwa polisi walimshikilia katika kituo chao cha Mtibwa hadi jana asubuhi kabla ya kumuachia kwa dhamana.
"Ni kweli… taarifa za kukamatwa kwa mchezaji huyo (Ulimboka) ninazo, ila sina uhakika kama alipigwa. Nilichoambiwa ni kwamba alinaswa na fedha na kufikishwa kituoni na watu wa Mtibwa Sugar ambapo alihojiwa, akafunguliwa kesi na kisha kuachiwa asubuhi hii (jana)," alisema Kamanda Andengenye.
Kamanda huyo alisema kuwa pamoja na kuachiwa kwake (Ulimboka), bado jeshi lao linaendelea na upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Awali, kocha msaidizi wa Mtibwa, kipa wa zamani wa Simba, Patrick Mwangata, alikiri pia kutokea kwa tukio hilo kambini kwao, lakini hakutaka kuzungumza zaidi kwavile yeye si msemaji rasmi na kwamba, suala hilo liko mikononi mwa polisi.
Micharazo haikumpata Ulimboka ili aelezee sakata hilo na sababu za kuhusishwa na Simba wakati akiwa ameshaachana nao na kubaki kuwa mchezaji mstaafu wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Baadhi ya viongozi wa Simba hawakupatikana pia kupitia simu zao za mikononi, ingawa Afisa Habari wa klabu hiyo, Clifford Ndimbo, alipatikana awali na kuomba apigiwe baada ya dakika kumi, jambo ambalo halikufanikiwa kwani alipopigiwa tena baada ya muda huo kwa zaidi ya mara mbili, simu yake haikuwa ikipatikana.
Wakati Simba na Mtibwa zikishuka dimbani leo, Idda Mushi anaripoti kutoka Morogoro kuwa African Lyon walilazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya ligi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kagera walipata goli la utangulizi katika dakika ya 43 kupitia kwa Gaudence Mwaikimba na Lyon wakasawazisha katika dakika ya 54 kwa penati iliyopigwa na Adam Kingwande kufuatia kipa Amani Simba kumdaka miguu Idrisa Rashid na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Huku wakiwa 10 uwanjani, Kagera walipata goli la pili katika dakika ya 66 kupitia kwa Sunday Hinju kabla Kingwande tena kuisawazishia Lyon kwa goli la dakika ya 88.

Thursday, September 23, 2010

Vicky Kamata aimwagia sifa hospitali ya Geita


UONGOZI pamoja na watumishi wa hospitali ya mkoa wa Geita, wamemwagiwa pongezi kutokana na ubora wa huduma zao kwa wagonjwa hospitalini hapo.
Pongezi hizo zimetolewa na mshindi wa kura za maoni za Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Geita, Vicky Kamata, alipozungumza na Micharazo kwa njia ya simu toka mjini humo.
Kamata ambaye alilazwa kwenye hospitali hiyo kumuugua mwanae mwenye umri wa miaka minne, alisema huduma wapewazo wagonjwa kwenye hospitali hiyo ni ya kupongezwa.
Alisema tofauti na siku za nyuma huduma zinazotolewa na madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo ni za kuvutia na kuonyesha kuboreshwa kwa huduma na kuumwagia sifa uongozi na watendaji hao.
Kamata, ambaye pia ni mwanamuziki wa kizazi kipya, alisema hatoi pongezi hizo kwa kuwa alihudumiwa vema kwa wasifu wake, bali ukweli alioushuhudia kwa wagonjwa wengine ndani ya hospitali hiyo ambao baadhi walisifia pia.
"Kwenye ukweli lazima lisemwe, huduma katika hospitali ya Geita ni ya kuridhisha na inayoonyesha mabadiliko makubwa na ninaupongeza uongozi na watumishi kwa ujumla kwa husuma hizo," alisema.
Alisema mwanae aliyelazwa kwa siku nne kutokana na kusumbuliwa na malaria kali tayari ameshatoka na anaendelea vema.
Kuhusu matarajio ya uchaguzi mkuu, Kamata alisema anaamini CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao kutokana na kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005 kwa ufanisi wakiwapelekea maendeleo wananchi.
"Japokuwa wapinzani safari hii wanaonyesha kucharuka, lakini bado ushindi wa CCM ni kwa kishindo na kuwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kuelekeza kura zao kwa wagombea wa CCM kuanzia Urais, Ubunge na Udiwani kwa nchi nzima," alisema Kamata.

Mwisho

Friday, September 17, 2010

Super Nyamwela na safari yake kimuziki







KUJITUMA kwake na kiu kubwa ya mafanikio aliyokuwa nayo wakati akichipukia kwenye sanaa ndio silaha kubwa ya mafanikio ya dansa, Super Nyamwela, mmoja wa madansa wakongwe waliodumu katika fani hiyo kwa muda mrefu nchini.
Nyamwela ambaye majina yake kamili ni Hassani Mussa Mohammed, alisema juhudi za mazoezi na kujituma bila kuchoka ndivyo vilivyomfikisha alipo, akimiliki kundi lake binafsi la sanaa pamoja na kuendesha miradi kadhaa ya maduka mbali magari na nyumba ya kuishi.
Nyamwela aliyerejea nchini hivi karibuni akitokea nchi kadhaa za kiafrika kwa ajili ya 'shoo' za kundi lake binafsi, anasema katu hawezi kuidharau sanaa hiyo kwa kuwa imemfanya awe mtu katika watu tofauti na mtazamo wa watu wengi juu ya muziki na sanaa kwa ujumla.
"Leo hii kama sio sanaa hii ya kunengua, pengine nisingefika huko Namibia, Liberia, Afrika Kusini, Botswana na kwingineko kama ilivyokuwa miezi 11 ya ziara yangu katika nchi hizo acha zile ninazoambatana na bendi yangu ya African Stars 'Twanga Pepeta," alisema.
Dansa huyo aliyeanza fani hiyo tangu akiwa kinda, hajutii kwake kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari kwa kuwa hakuna anachokikosa kwa sasa, ingawa mipango yake ni kujiendeleza pale alipoishia.
Akiwa amejinyakulia mataji mbalimbali ya mashindano ya disko nchini likiwemo lile la Mkoa wa Dar es Salaam, alisema safari yake ilianzia alipomaliza elimu ya msingi alipojitosa jumla kwenye fani hiyo aliyokuwa huku akiendelea na 'kitabu'.
Baadae aliungana na wasanii wenzake kadhaa kuunda kundi la Top Family lililotamba pale 'Kwa Macheni' kabla ya kwenda kuasisi kundi la Billbums ambalo lilisheheni wasanii wakali waliokuja kunyakuliwa na bendi ya African Stars.
Tangu awe Twanga Papeta, Nyamwela hajawahi kuhama hata mara moja licha ya kuwepo kwa majaribio kadhaa ya kutaka kumng'oa ASET bila ya mafanikio.
"Sidhani kama nitaondoka Twanga kirahisi, labda kama nitaenda kwenye bendi yangu binafsi ambayo naipigia mahesabu kuja kuunda siku za usoni wakati mambo yangu yamekaa vema, lakini si kwenda bendi zingine za hapa nchini," alisema.
Mkali huyo ambaye amejitumbukiza katika uimbaji na upigaji tumba na dramu, alisema kwa sasa akili zake zote ni kuhakikisha anaiboresha kampuni yake binafsi ya SN Stars Entertainment, ili iendeshwe kisasa na kujitanua nje ya Dar es Salaam.
Nyamwela aliyemaliza kuikarabati nyumba yake iliyopo Mbezi Beach ambayo iliunguzwa kwa moto na watu aliodai 'maadui' zake, alisema mbali na kuiboresha kampuni yake pia malengo yake ni kugeukia kazi ya kurapu na kufyatua filamu izungumziayo maisha yake.
Alisema filamu hiyo itafahamika kwa jina la My Talent ambayo itaanza kurekodiwa mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani ikienda sambamba na maandalizi ya albamu yake mpya ya tatu ambayo imeshakilishika wimbo mmoja wa Tumechete.
Albamu yake ya kwanza iliyouza sana ilifahamika kwa jina la Master of the Tample na ile ya pili ni Afrika Kilomondo aliyoiingiza sokoni hivi karibuni ikiwa na nyimbo sita alzioshirikiana na waimbaji mbalimbali akiwemo Ally Choki, Richard Maalifa na Juma Nature.
Kuhusu matukio ambayo hataondoka akilini mwake hadi anaingia kaburini, Nyamwela alisema ni kuunguliwa kwa nyumba yake na kumpoteza mzazi mwenzie, marehemu Halima White.
"Aisee hili la kuunguliwa nyumba na lile la kumpoteza mzazi mwenzangu, marehemu Halima White, ni vigumu kuyasahau," alisema.
Aliongeza, amefarijika baada ya kumpata mwandani wake mpya Upendo Merere ambaye anatarajia kuuona nae hivi karibuni mipango yake ikienda vema, ili waweze kuwalea watoto watatu alionao.
Dansa huyo asiyependa majungu na uvivu kazini alisema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatamshukuru Mkurugenzi wa ASET Asha Baraka na uongozi na wasanii wote wa bendi ya Twanga Pepeta kwa kushirikiana naye kwa hali na mali.
"Siwezi kumsahau Da Asha Baraka kwa jinsi nilivyokaa naye tangu alipotuchukua toka Billbums hadi leo hii, pia uongozi mzima wa Twanga Pepeta, wasanii na vyombo vya habari vinavyonipa sapoti katika tangu nikiwa kinda katika sanaa hadi leo hii,"
Aliwaasa wenzake kujituma kama yeye na kutokubali kukata tamaa ili waweze kufanikiwa na kubwa ni kuipenda kazi zao na kujithamini wenyewe wakijilinda na ugonjwa wa Ukimwi.
Mkali huyo aliyezaliwa karibu miaka 30 iliyopita huko Zanzibar, alisema kutojidhamini kwa ujumla ndiko kunakopelekea wasanii wengine kutumbukia kwenye maambukizo ya ugonjwa huo.

Mwisho

Jane Misso kuzindua albamu yake Diamond Jumapili







MSANII nyota wa muziki wa Injili nchini, Jane Misso kesho anatarajia kuzindua albamu yake mpya na ya pili ya 'Uinuliwe' akisindikizwa na wasanii mbalimbali wa miondoko hiyo wa ndani na nje ya nchi.
Uzinduzi wa albamu hiyo utakaoenda sambamba na kuachiwa hadharani video yake, umepangwa kufanyika mchana wa kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Micharazo, Misso, ambaye ni mchungaji na mwalimu aliyewahi kufanya kazi nchini Uganda kabla ya kujikita kwenye miondoko hiyo na kuachia albamu yake ya kwanza ya 'Umoyo', alisema wasanii karibu wote watakaomsindikiza kesho wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Misso aliwataja wasanii waliotua kwa ajili ya kumsindikiza katika uzinduzi wake ni pamoja na Mcongo, David Esengo, Peace Mhulu kutoka Kenya watakoshirikiana na nyota wa Kitanzania wa muziki huo na kwaya mbalimbali kumpambia onyesho lake.
Mwanamama huyo aliwataja wasanii wa Injili wa Tanzania watakaompiga tafu kesho ni Christina Shusho, Upendo Nkone, Martha Mwaipaja, Steve Wambura na Joseph Nyuki.
"Kwaya zitakazonisinidkiza ni pamoja na Joy Bring'res, The Whispers Band, AIC Chang'ombe na kwaya ya Watoto Yatima kutoka Dodoma inayoongozwa na mlemavu wa ngozi, Timotheo Maginga," alisema Misso.
Misso alisema albamu hiyo ina nyimbo sita na baadhi yake zinahamasisha wananchi juu ya ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa Urais, Ubunge na Udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31.
Nyimbo zilizoibeba albamu hiyo ni 'Pokea Sifa', 'Motema', 'Nyosha Mkono Wako', 'Uinuliwe', 'Unaweza Yote' na 'Mimi Najua Neno Moja'.

Friday, September 10, 2010

Chagueni watu kwa sifa zao sio vyama-Sheikh Mapeyo

WAUMINI wa dini ya Kiislam na Watanzania kwa ujumla wameaswa kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu ujao bila kujali aina ya vyama vyao ilimradi ni watu wenye uchungu, uadilifu na dhamira ya kweli ya kuwakomboa.
Aidha waumini na watanzania wamehimiza kuhakikisha wanashiriki kwa wingi siku ya kupiga kura na kujichagulia viongozi wawatakao badala ya kusubiri kuchaguliwa kisha waje kulalama mambo yatakapokuwa yakienda kombo.
Wito huo umetolewa na Imamu wa Msikiti wa Mwenge Islamic Center, Sheikh Shaaban Mapeyo alipokuwa wakiwahutubia waumini baada ya swala ya Eid iliyoswaliwa msikini hapo, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Mapeyo ambaye ni mgombea wa kiti cha Ubunge Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Wananchi, CUF, alisema waumini wa Kiislam na wananchi kwa ujumla wasihadaiwe na propaganda za kuchagua viongozi kwa kuangalia chama bali wasifu wa mgombea kwa nia ya kujiletea maendeleo.
Alisema kuendelea kuchagua wagombea kwa kuzingatia chama ndio ambayo yamefanya Tanzania kuendelea kudumaa kwa muda mrefu kwa kuwa wapo baadhi ya wagombea hawana sifa za uongozi lakini wamechaguliwa kupitia vyama vyao.
"Waislam wakati tukizingatia 'darasa' tulilolipata kipindi cha Ramadhani ni vema tukajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, tusiupuuze na muhimu ni kuhakikisha tunachagua watu wenye sifa na sio kuangalia chama," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka waumini nao na watanzania kwa ujumla kushiriki kwa wingi kwenye uchaguzi huo kwa kujitokeza kupiga kura ili kuhakikisha wanajichagulia viongozi na makini watakaowaletea maendeleo ya maeneo yao.
"Bila kujali jinsia jitokezeni kwa wingi kushiriki kupiga kura Oktoba 31, puuzeni propaganda zinazosambazwa na baadhi ya watu kwamba kushiriki uchaguzi ni haramu, mtajiletea maendeleo vipi kama hampigi kura?" Alihoji.
Sheikh Mapeyo alisema mambo mengi hapa nchini yamekuwa yakienda kombo kwa sababu wananchi wengi wamekuwa sio makini katika kushiriki uchaguzi mkuu ambayo ndio silaha ya kujiletea maendeleo ya kweli.
Uchaguzi Mkuu wa kuchagua madiwani, wabunge na Urais utafanyika Oktoba 31 na kwa sasa wagombea wanaendelea na kampeni zao.

Mwisho

Monday, September 6, 2010

Mpeni kura Mkullo, namuamini mno-Dk KIkwete






RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Dk Jakaya Kikwete, amewaomba wakazi wa Jimbo la Kilosa, kumpa tena ubunge mgombea wa chama hicho na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo kwa madai anamuamini.
Aidha mgombea huyo aliwaomba wapiga kura wa majimbo mengine yaliyopo wilayani Kilosa kuhakikisha wanaipa kura CCM kupitia viti vya ubunge na udiwani ili kumrahisishia kazi ya kuongoza nchi kwa mara ya pili mfululizo.
Akiwahutubia wakazi wa wilaya ya Kilosa kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja uliopo njia panda Ilonga na Kimamba, Rais Kikwete alisema angependa kuona wakazi wa Kilosa wakimpa tena ubunge waziri Mkullo kwa vile ni mmoja wa mawaziri anayewaamini.
"Naombeni mnichagulie tena Mkullo kuwa Mbunge wa Kilosa kwa kuwa kumuamini kwangu ndiko kulikonifanya nimpe dhamana ya kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi," alisema Dk Kikwete.
Dk Kikwete alisema, chini ya Mkullo Kilosa imeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa serikali yake kushawishika kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Pia mgombea huyo wa Urais, aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo kuwachagua pia wagombea wengine wa majimbo ya Gairo na Mikumi pamoja na wale wa udiwani wa kata zilizopo wilayani humo ili kumrahisishia kazi katika kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Naye Mkullo, alipopewa nafasi ya kuwasalimia wapiga kura wake, aliwaomba wampigie kura na kumpa ubunge kwa mara ya pili ili aweze kukamilisha baadhi ya ahadi zake alizowatolea kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2005.
"Sina cha ziada ila kuwaomba mnichague tena kwa awamu ya pili ya kiti cha jimbo la ubunge la Kilosa ili kutekeleza ahadi zangu na kuwaletea maendeleo kwa ujumla kwa sababu nia na sababu ninayo," alisema Mkullo.
Akisoma Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005, Katibu wa CCM wilayani Kilosa, Gervas Makoye, alisema asilimia kubwa zimetekelezwa au kuanza kutekelezwa na hivyo ni fursa ya wakazi wa mji humo kuhakikisha wanaichagua tena CCM Oktoba 31, ili kujiletea maendeleo ya kweli.

Mwisho

Sunday, September 5, 2010

Dk Kikwete akiri watumishi wake wengi ni wezi



MGOMBEA wa Urais wa Chama cha Mapinduzi, CCM, Dk Jakaya Kikwete, amekiri wazi kuwa, watumishi wengi wa Halmashauri ni wezi na ndio wanaokwamisha miradi mingi ya maendeleo.
Aidha mgombea huyo amesema kuwa watanzania wengi wanajitakia kupata maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kuendekeza starehe na 'kiherehere' cha kupapia mapenzi yasiyo salama licha ya hamasa mbalimbali zinazotokea juu ya kujikinga na maradhi hayo.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana katika mkutano wake wa kuomba kura katika uchaguzi mkuu ujao na kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge wa wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Alisema kuwa, pamoja na juhudi za serikali chini ya CCM kutaka kuleta maendeleo kwa wananchi, wapoo baadhi yawatumishi wa Halmashauri ambao ni wezi na wanaoangalia masilahi yao kwa kuzifuja fedha za miradi katika maeneo yao.
"Watumishi wengi wa Halmashauri ni wezi na wanaokwamisha miradi ya maendeleo kwa kuzitumia vibaya fedha wanazopelekewa na serikali kwa ajili ya kuwainua wananchi katika sekta mbalimbali jambo ambalo ni baya," alisema Dk Kikwete.
Katika kukaribia na hilo, mgombea huyo alisema akipata nafasi ya kuchaguliwa tena atahakikisha anapambana nao kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kama ilivyo kauli mbiu yao kwa kuwa kufanya hivyo kutaondoa kikwazo cha kuwapelekea wananchi maendeleo.
Akizungumza suala la maambukizi ya Ukimwi, mgombea huyo wa CCM, alisema anaamini kuwa, ugonjwa huo unakingika na kuepukika iwapo wananchi wataamua kuzingatia mahubiri na makatazo ya viongozi wa kidini juu ya suala la zinaa.
Dk Kikwete alisema maambukizi mengi yaliyopo nchini ni kama wananchi wanajitakia wenyewe kwa kutawaliwa na kuendekeza starehe na kiherehere cha kukimbilia mapenzi yasiyo salama.
"Kama sio kiherehere ni vipi mwanafunzi badala ya kushughulika na masomo shuleni yeye anakimbilia mapenzi?" alihoji Dk Kikwete.
Alitoa ushauri kwa wananchi juu ya kuwa makini na ugonjwa huo kwa kuoa, kujizuia kuwa waaminifu au kutumia kinga.
Kwani kwa kutokufanya hivyo maambukizi yatazidi kuongezeka na taifa kupoteza nguvu kazi ilihali Tanzania Bila Ukimwi Inawezekana!
Alizungumzia dawa za kurefusha maisha ya waathirika, Dk Kikwete serikali yake inatoa dawa hizo bure na kudai kama kuna wanananchi wanaouziwa basi watakuwa wanaibiwa na wanapaswa kutoa taarifa ili wahusika washuighulikiwe.
Juu ya malaria, aliyodai seikali yake inaumia kuona wananchi wanakufa kwa ugonjwa huo kuliko hata Ukimwi na kudai wameweka mikakati ya kupambana nao kwa kuongeza ugawaji wa vyandarua, kupuliza dawa katika kila nyumba nchi nzima na kuhakikisha wanaua mbu wanaoambukiza ugonjwa huo.

Mwisho

Chagueni CCM Tanzania istawi-Dk Kikwete





MGOMBEA wa Urais wa kiteki ya CCM, Dk Jakaya Kikwete, amewataka wananchi kukichagua chama chake kwa mara nyingine ili kuistawisha nchi, kwa maelezo kwamba vyama vya upinzani vilivyopo ni vya msimu na havina uwezo wa kuongoza.
Dk Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano aliyasema hayo leo alipokuwa akiwatuhubia wakazi wa wilaya ya Kilosa katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Wahanga wa Mafuriko lililopo njia panda ya Ilonga na Kimamba, mkoani Morogoro.
Rais Kikwete alisema kuwa, pamoja na kwamba wapinzani wamekuwa wakitoa kejeli dhidi ya utendaji wa CCM, ukweli ni kwamba vyama hivyo havina uwezo wa kuongoza na hivyo ni vema wananchi wakaichagua tena CCM kustawisha maendeleo yaliyopo.
Alisema pamoja na utitiri wa vyama vya upinzani, vingi vyake ni vya msimu tu, ambapo huibuka wakati wa uchaguzi na hasa wanapofanikiwa kuwapata wanaohama toka CCM.
"Wananchi wa Kilosa na Watanzania kwa ujumla nawaombeni muichague CCM kwa mara nyingine kwa kuwa ndio chama pekee bora kinachoweza kustawisha maendeleo ya nchi yaliyopo pamoja na kudumisha amani na utulivu, vyama vingi vya upinzani ni vya msimu tu na hasa vinapofanikiwa kuwanasa wanaohama toka CCM pale wanapogombea na kutochaguliwa," alisema Dk Kikwete.
Dk Kikwete alisema CCM imfanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005 kwa asilimia kubwa katika nyanja na sekta za Afya, Elimu, Maji, Miundo Mbinu, Kilimo na Ufugaji na ikipewa nafasi tena itamalizia sehemu zilizobakia.
Alitoa mfano suala la elimu kwa wilaya ya Kilosa, imefanikiwa kuongeza majengo ya shule kuanzia chekechea hadi sekondari, ambapo alisema kwa mfanoi mwaka 2005 idadi ya wanafunzi katika sekondari ilikuwa ni 6969 ambapo kwa sasa idadi hiyo imefikia 17666 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wanafunzi 10,000.
Pia alisema juhudi hizo za kuboresha sekta hiyo zinaendana na kuongeza idadi ya walimu ambapop alisema mwaka 2005 idadi ya wahitimu wa ualimu nchi nzima ilikuwa ni 600 tu, lakini awamu ya nne imejitahidi na kufanya idadi hiyo kufikia 16,000.
Alisema, anafahamu idadi hiyo bado haikidhi hivyo serikali yake kupitia CCM inafanya mipango ya kuongeza walimu zaidi kupitia vyuo vyake na vile vya watu binafsi ili kufikia lengo sambamba na kuwezesha kupatikana kwa vitabu, maabara na nyumba za walimu.
Kuhusiana na vitabu,Dk Kikwete alisema tayari jitihada zimeshafanywa kwa kuomba msaada toka kwa nchi marafiki ikiwemo Marekani ambayo imejitolea kutoa jumla ya vitabu 800,000 vya masomo mbalimbali ya sekondari na mapema mwakani itapokea vitabu vingine zaidi ya Mil 2.4.
Alisema hayo na mengine ambayo yamekuwa yakifanywa na CCM tangu iwe madarakani hayawezi kufanywa na vyama vya upinzani na kuwataka wapiga kura kutofanya makosa Oktoba 31 watakapochagua viongozi kwa ajili ya miaka mitano ijayo.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo alizungumzia suala la wahanga wa mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo mnamo Desemba mwaka jana, kuwa serikali ipo katika mpango wa kuwajengea nyumba za kudumu wahanga hao wanaishi kambini kwa sasa.
Dk Kikwete alisema kazi ya ujenzi wa nyumba hizo utafanywa na Jeshi la Kujenga Taifa, JKT, kwa lengo la kuwarejesha maisha ya amani na utulivu wakazi hao ambao kwa sasa wanaishi katika nyumba za mabati.
Pia alisema, serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa jipya la Kidete pamoja na kujenga tuta jipya la kudhibiti maji ya Mto Mkondoa ambao aliutaja kuwa ndio tatizo lililosababisha mafuriko hayo yaliyoleta maafa makubwa.
Katika ziara yake ya kampeni wilayani humo, mgombea huyo wa CCM alikuwa akisimamishwa yeye na msafara wake na wananchi mbalimbali wa vijiji kwa ajili ya kumueleza kero zao.
Alipofika kata ya Dumila wananchi wa eneo hilo kupitia Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Dumila, Douglas Mwaigumila, walimueleza mgombea huyo juu ya kero zinazowakabili ambapo walizitaja ni huduma ya maji, afya, umeme na uporwaji wa ardhi yao ipatayo ekta 400 shutuma alizozipeleka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya yao.
Dk Kikwete aliwajibu wananchi hao kuwa serikali yao inayatambua kero hizo na tayari ilishaanza kuzitekeleza kwa awamu, huku akishangaa kusikia tukio la uporwaji huyo wa ardhi na kuahidi kulifuatilia.