STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 11, 2011

Sikinde, Msondo zaanza tambo, zitakutana Februari 18

BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park 'Sikinde' ambazo zinatarajiwa kuonyeshana kazi wiki ijayo, zimetambiana kwa kila moja ikijinasibu kuizima nyingine katika onyesho lao la pamoja litakalofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.r
Msondo na Sikinde zitakutana tena Februari 18 ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili baada ya kuchuana awali Desemba 30 katika onyesho lililofanyika ndani ya ukumbi wa Mzalendo Pub, uliopo Millenium Tower, Makumbusho Dar es Salaam.
Wakati siku zikikaribia kabla ya pambano hilo, viongozi wa bendi hizo wameanza kurushiana vijembe kila upande ukitamba kuwazima wenzake.
Msemaji wa Msondo, Rajabu Mhamila "Super D', alisema wanaamini kama walivyowazima Sikinde katika onyesho lao la Desemba, ndivyo watakavyofanya wiki ijayo kutokana na kikosi chao kinachoundwa na wanamuziki vijana na wachapakazi.
"Tunajua kwa sasa Sikinde watakuwa wanatafuta namna ya kutukabili, lakini kwa kifupi watarajie kufunikwa kama tulivyofanya kwenye onyesho la Mzalendo Pub," alisema Super D.
Hata hivyo, Sikinde ambao walikuwa visiwani Zanzibar kwenye Tamasha la Sauti za Busara wamejinasibu kuwa Msondo hawana ubavu mbele yao na kuwataka mashabiki wa muziki waende Diamond Jubilee kushuhudia ukweli wa wanachokisema.
Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo alisema Sikinde ni zaidi ya Msondo kutokana na kukamilika kila idara kuanzia safu ya uimbaji, wapiga magitaa na wapuliza tarumbeta walichodai watatumia kama silaha ya kuwazima mahasimu wao.
"Sisi ni kama Barcelona, tuna safu kali ya ushambuliaji nikimaanisha waimbaji na viungo mahiri ambao ni wapuliza ala za upepo sikuambii wapiga magita, sijui kama Msondo watafua dafu," alisema Milambo.
Milambo alisema bendi yao inatarajia kurejea leo mchana kuendelea na utambulisho wa vibao vyao vipya vinavyoandaliwa kwa ajili ya albamu yao ijayo.