STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, January 14, 2014

Coastal yaendelea kutoa vipigo Oman



MABINGWA wa zamani wa soka nchini Tanzania, Coastal Union imeendelea kutoa dozi ya vipigo kwa wenyeji wao nchini Oman baada ya jioni ya leo kuilaza kwa mabao 2-0 Oman Club ikiwa ni ushindi wake wa pili mfululizo tangu watue nchini huyo kwa kambi ya mazoezi ya wiki mbili.
Awali Coastal iliinyoa kwa idadi kama hiyo timu ya Al Mussanah mabao yaliyofungwa na Yayo Kato na Kenneth Masumbuko.
Katika mechi ya leo iliyochezwa kwenye uwanja wa Nadi Oman katika wilaya ya Boshra jijini Muscat.
Magoli ya Coastal katika mechi hiyo yaliwekwa kimaini na Mohammed Miraji dakika 35, na Yusuf Chuma dakika 75.
Kikosi hicho kinachonolewa na Mkenya Yusuf Chipo kinatarajiwa kucheza mechi nyingine mbili ikiwa nchini humo chini ya uenyeji wa Fanja Fc tangu Januari 9. mechi hizo zitahusisha timu za Seeb Club na Fanja Club,zilizopo Ligi Kuu ya nchi hiyo. Oman Club yenyewe inashiriki Ligi daraja la Kwanza.

DR Congo yatakata CHAN yailaza Mauritania 1-0

 DR Congo edge Cameroon to reach CHAN 2014 finals
BAO la mkwaju wa penati lililotupiwa kambani kwenye dakika ya 51 na Emomo Ngoyi imeiwezesha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kuanza na ushindi kwenye michuano ya CHAN 2014 inayoendela nchini Afrika Kusini katika pambano lililomalizika hivi punde.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Peter Mokaba, uliopo Polokwane (Pietersburgs) Kongo ikiizamisha Mauritania katika mechi ya kwanza ya kundi D.
Katika pambano hilo timu zote zilionyesha soka la kukamiana na kosakosa za hapa na pale na mpaka mwisho DR Congo walikuwa wababe na kukwea kileleni wakisubiri matokeo ya mechi inayotarajiwa kupigwa muda mfupi ujao kati ya Gabon dhidi ya Burundi kukamilisha mechi za mkondo wa kwanza kwa makundi yote manne yanayoshirikisha jumla ya timu 16.
Kesho mechi za mkondo wa pili utaanza kwa kushuhudia timu za kundi A kutupa karata zao ambapo Nigeria iliyoanza kwa kipigo itapepetana na Msumbiji waliolala kwa mabao 3-1 mbele ya wenyeji Afrika Kusini ambao watakabiliana nna Mali walioitoa nishai Mabingwa wa Afrika (AFCON) Nigeria katika mechi ya fungua dimba siku ya Jumamosi kwa kuilaza mabao 2-1.

Taifa Stars kuwakabili Namibia Kalenda ya FIFA

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia (Brave Warriors) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON) zitakazochezwa mwakani nchini Morocco.

Stars na Brave Warriors zitacheza mechi hiyo Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia. Mechi hiyo ipo katika kalenda ya mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Makubaliano ya kucheza mechi hiyo yamefikiwa kutokana na mazungumzo kati ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA), John Muinjo.

Benchi la Ufundi la Brave Warriors linaongozwa na kocha mzawa Ricardo Mannetti, na mechi hiyo itachezwa ama Uwanja wa Sam Nujoma au Uwanja wa Uhuru jijini Windhoek.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inafundishwa na kocha Kim Poulsen kutoka Denmark na inatarajia kuanza kucheza mechi za mchujo za AFCON Septemba mwaka huu.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Maofisa wa TFF kukagua viwanja 19 vya VPL, FDL

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh5LSEj1U0RgmU2DS-iUGSW-MUCE9nFy_mWlUF8lL2mTNba0QqPQxJBniS-sqbO7kBQ-JCTUtZioSAkByPirmKgZdAYxkiakLojEMLXLHsazl5z5vsLmshyOy1CA3G_R8TlOwCZFba_zLk/s640/IMG-20120915-WA0005.jpg
Uwanja wa Sokoine-Mbeya
Sehemu ya uwanja wa Azam Complex unavyoonekana kwa sasa ukiendelea kuboreshwa

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeteua maofisa wanaoanza leo  kukagua viwanja 19 vitakavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Ukaguzi huo pia unahusisha viwanja ambavyo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilizuia mechi za VPL na FDL kuchezwa mpaka hapo vitakapokuwa vimefanyiwa marekebisho ili kukidhi sifa za kutumiwa kwa mechi hizo.

Viwanja vinavyokaguliwa ni Ali Hassan Mwinyi (Tabora), CCM Kirumba (Mwanza), Jamhuri (Dodoma), Jamhuri (Morogoro), Kaitaba (Bukoba), Kambarage (Shinyanga), Kumbukumbu ya Karume (Musoma) na Kumbukumbu ya Samora (Iringa).

Kumbukumbu ya Sokoine (Mbeya), Lake Tanganyika (Kigoma), Mabatini (Pwani), Majimaji (Songea), Mbinga (Mbinga), Mkwakwani (Tanga), Mwadui (Shinyanga), Wambi (Mufindi, Iringa), Sheikh Kaluta Amri Abeid (Arusha), Umoja (Mtwara) na Vwawa (Mbozi).

Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika na mameneja wa viwanja husika wanatakiwa kuwapa ushirikiano wakaguzi hao kutoka TFF.

Abiria 48 wanusurika kufa ajali ya basi la Shabiby


ABIRIA wapatao 48 waliokuwa wakisafiri na basi la Shabiby kutoka Arusha kuelekea Dodoma wamenusurika kufa, huku 28 wakijeruhiwa baada ya basi lao kupata ajali.
Basi hilo linadaiwa lilipata ajali wakati likitaka kulipita lori la mafuta wakati basi lingine la Princes Munaa nalo likiwa linalipita basi la Shabiby katika mlima Kisaki na kusababisha basi la Shabiby kuanguka.
Wakieleza kondakta wa basi hilo aina ya Yunton lenye usajili wa namba T 930 BUW ambaye amevunjika miguu yote miwili, Thadei Muhando na mkaguzi wa basi la Shabiby, William Ofyenge wamesema wakati basi lao lilikuwa likilipita lori la mafuta ghafla waliona basi lingine  likiwapita na kuwa magari matatu katika njia moja na hatimaye dereva wao alishindwa kulimudu basi lao na kusababisha kupinduka.
Mganga mfawidhi wa  hospitali ya mkoa wa Singida daktari Banuba Deogratius amethibitisha kupokea majeruhi 28 waliopatiwa matibabu na mgonjwa moja ambaye alikuwa kondakta wa basi amevunjika miguu yote miwili na wanampatia matibabu.
Kwa upande wake dereva wa lori la mafuta aina ya Benz lenye usajili wa namba Raa 496N na tela lake lenye usajili wa namba RL 0255  ambalo lilikuwa likitokea nchi ya Rwanda, Hadimana Benjamini amesema alipitwa na mabasi mawili na moja  likamgonga upande wake na hatimaye kuanguka .
Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi aliyefika katika ajali hiyo pamoja na kuwatembelea majeruhi amewataka madereva wote kuzingatia sheria za barabarani  ilikuweza kunusuru uhai wa watu na majeruhi.