STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 22, 2010

Wagombea Kilosa kuanza kampeni Agosti 26

WAGOMBEA wa CCM wanaowania viti vya Ubunge na Udiwani wilaya ya Kilosa wanatarajia kuanza rasmi kampeni zao Agosti 26 mwaka huu, wakati mgombea wao wa Urais, Rais Jakaya Kikwete atakapoenda kuzindua kampeni hizo jimbo la Mikumi.
Katibu wa CCM-Kilosa, Gervase Makoye, alisema wagombea wa CCM wataanza kampeni zao rasmi siku hiyo wakati rais atakapozuru Mikumi kuendelea kujikampenia kuomba kura za wananchi kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
Makoye alisema, wagombea wote watatu wa majimbo matatu yaliyopo wilayani kwao watahudhuria kampeni hiyo kabla ya kila mmoja kutawanyika jimboni mwake kuanza kuomba kura za wananchi wa maeneo yao.
Katibu huyo alisema baada ya Rais kuzindua Mikumi Agosti 26, siku inayofuata atakuwa Kilosa kisha kumalizia Gairo na kuwaacha wagombea wahusika wakiendelea na kampeni zao.
Jimbo hilo la Mikumi linawaniwa na Abdulsalaam Nahad Suleiman 'SAS', ambaye alisema amejipanga kuhakikisha anaibuka kidedea kwenye kinyang'anyiro hicho kinachowaniwa na wagombea wengine wa vyama vya mbalimbali vya upinzani.
Naye mgombea wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkullo alisema yeye ataanza rasmi kampeni zake Agosti 27 baada ya Rais kuzindua kampeni za wilaya hiyo huko Mikumi na hapo ndipo atakapoanika kila kitu juu ya ukweli kuhusu alichowafanyia wakazi wa jimbo hilo na yale ambayo amepania kuyaendelea na kufanya mengine mapya.
Mkullo alisema mbali na hilo, lakini pia atazitumia siku 70 za kampeni hizo kuweka bayana juu ya tuhuma dhidi yake kuwa yeye sio raia wa Tanzania bali ni Mmalawi, madai aliyodai yametolewa na mmoja wa waliokuwa wagombea wenzake asiyekubali matokeo.
"Kampeni zangu nitazianza Agosti 27 na hapo ndipo nitapata fursa nzuri ya kusema kila kitu juu ya mipango yangu ya maendeleo kwa wakazi wa jimbo langu na pia kuweka hadharani madai juu ya tuhuma za utata wa uraia wangu," alisema Mkullo.
Mgombea wa Gairo, Ahmed Shabiby, yeye alisema yupo vema na atajinadi ili kuomba ridhaa ya wakazi wa jimbo hilo kumpa tena nafasi ya kuwatumikia kama walivyompa katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005.

Masilahi ya Ubunge ndio chanzo cha watu kuchafuana-ChayekaMASILAHI makubwa wanayolipwa na kuyapata Wabunge, yanaelezwa ndio chanzo cha mfarakano miongoni mwa wana CCm kiasi cha kufikia kuchafuana wakipakaziana masuala ya utata wa uraia na mambo mengine yakudhalilishana.
Hayo yamesemwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya wa Tarime, Raphael Chayeka, alipozungumza na Micharazo wilayani Kilosa, ambapo alisema masilahi manono wanayolipwa wabunge ndiyo yanayofanya kila mmoja kupigana kufa na kupona kuona anakuwa mbunge.
Chayeka alisema hali hiyo ya tamaa na uchu iliyowanayo watu wengi wanaojitosa kwenye siasa ndio wanaopelekea wanaoangushwa kuwachafua wenzao kwa minajili ya kuona wanapata nafasi ya kuteuliwa, kitu alichodai sio uungwana katika dunia ya wastaarabu.
Alisema donge nono la kwenye masuala ya ubunge na siasa kwa ujumla ndiyo inayofanya kila mtu sasa bila kujali wa kada gani kutaka kuwa mwanasiasa na hasa ubunge na pale wanaposhindwa kwenye kura ndipo wanapoibuka kuwachafua wengine.
"Masilahi manono yaliyopo kwenye Ubunge na Siasa kwa ujumla ndio yanayopelekea watu kuchafuana na kupakaziana mambo mabaya, lakini kama sio hivyo wala yasingetokea hayo yaliyojitokeza miaka ya hivi karibuni," alisema Chayeka.
Naye Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kilosa, Alhaj Shaweji Abdallah naye alisema ifike wakati wanachama wa CCM na wagombea wengine wawe waungwana kwa kubali matokeo badala ya kuwapakazia wenzao masuala ambayo yanayowadhalilisha wengine bila sababu ya msingi.
Wazee hao walitoa kauli hizo wakati wakimtetea mgombea ubunge wa jimbo la Kilosa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo aliyevumishiwa kuwa sio raia wa Tanzania bali ni mtu wa Malawi kitu kilichomshangaza waziri mwenyewe kwa madai anatambue yeye ni raia.

Mwisho