STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 11, 2012

Kivumbi cha awali cha BancABC Super8 kesho

KIVUMBI cha hatua ya makundi ya michuano ya BancABC Super8 inatarajiwa kuhitimishwa kesho kwa viwanja vinne kuwaka moto katika miji tofauti ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa mujibu wa ratiba ya makundi ya michuano hiyo inayoshirikisha timu nane, nne toka kila upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ni kwamba Simba ambao walizinduka toka kwenye kipigo cha mabao 3-1 toka kwa Wakenya City Stars kwenye Simba Day kwa kuinyuka Mtende, itakuwa kwenye dimba la CCm Kirumba, Mwanza kuumana na Zimamoto ya Zanzibar. Mechi nyingine ya kundi hilo itazikutanisha timu za Jamhuri na Mtende zote za visiwani Zanzibae kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Kwa mechi za kundi B ratiba inaoonyesha Mtibwa Sugar iliyoigaragaza Azam nyumbani kwao 'Chamazi' kwa mabao 2-0 itashuka dimba la Amaan Zanzibar kuumana na mabingwa wa Ze nji, Falcon iliyolala kwa Polisi Moro katika mechi yao iliyopita. Nao Polisi Moro iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, itakuwa kwenye uwanja wa Ushirika Moshi kuumana na Azam Fc. Timu nne, mbili toka kila kundi zitakazoshika nafasi mbili za juu zitacheza hatua ya nusu fainali ambazo zitachezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wanamasumbwi chipukizi Bongo kuvuna nini Idd Pili?

MASHABIKI wa ngumi za kulipwa nchini wanatarajia kupata burudani ya aina yake siku ya Idd Pili, wakati mabondia wawili chipukizi Ramadhani Shauri na Nassib Ramadhani watakapoanda ulingoni kuzipiga. Mabondia hao walio chini ya kocha Christopher Mzazi watazipiga na mabondia kutoka Kenya na Uganda katika michez itakayofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kuwania mataji ya IBF. Shauri yeye atapanda ulingoni kuzichapa katika pambano la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika uzani wa vinyoya (Featherweight) la raundi 10 dhidi ya Mganda, Sunday Kizito. Bondia Nassib anayeshikilia taji la chama cha World Boxing Forum (WBF), atatangulia kuzipiga na Twalib Mubiru kutoka Kenya katika pambano la uzani wa Bantam kuwania ubingwa wa IBF-Afrika Mashariki na Kati. Michezo hiyo yote inaratibiwa na promota Lucas Rutainurwa ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Kitwe General Traders na kusimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBC. Kwa mujibu wa Rais wa TPBC ambaye pia ni Rais wa IBF Afrika/USBA, Onesmo Ngowi, pambano la Shauri na Kizito ndilo pigano kuu (main bout) na limepewa jina la 'The Rumble in the City of Heaven's Peace'. Ngowi, amemtaja Shauri kama 'mfalme' mpya aliyeanza kutishia hadhi za mabondia wengine nchini kutokana na kipaji kikubwa alichonacho katika mchezo huo wa ngumi za kulipwa. Rais huyo alisema rekodi aliyonayo na namna ya uchezaji wake akiwa ulingoni imemfanya awe anamfananisa na nyota wa zamani wa ngumi za kulipwa kutoka Marekani Sugar Ray Leonard. Katika umri alionao usiozidi miaka 25, Shauri tayari amekuwa na kivutio cha aina yake kutokana na haiba yake ya uchezaji na rekodi aliyonao tangu aanze kucheza mchezo huo chini ya kocha Mzazi wa gym iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam. Bondia huyo amecheza mapambano 15, akishinda michezo 12, kupoteza miwili na kuambulia sare moja, huku akishikilia nafasi ya pili kati ya 40 katika orodha wa mabondia wa uzito wake akitangliwa na Roger Mtagwa. Kwa upande wa mpinzani wake yeye ana rekodi ya kucheza mapambano 22 akishinda 12, kupoteza tisa na kupata sare moja. Ngowi anaamini pambano hilo litasisimua mashabiki wengi wa ngumi ambao kwa mua mrefu hawajapata kushuhudia mabondia vijana wakiwania mataji ya kimataifa. 'Ni zamu ya kuwapa nafasi mabondia chipukizi kuonyesha vipaji vyao na kuwania mataji ya kimataifa kuitangaza Tanzania," alisema Ngowi. Kuhusu pambano la Nassib Ramadhani, Ngowi alisema nalo linatarajiwa kuwa gumzo kutoka na rekodi alizonazo bondia huyo aliyecheza mapambano 11 na kushinda tisa akipoteza mawili. Nassib pia ndiye anayeongoza orodha wa mabondia 21 wa Tanzania wa uzani wake huku katika orodha ya dunia akishika nafasi ya 88 kati ya mabondia 636. Mpinzani anayecheza nae rekodi yake inaonyesha amecheza michezo 20 akishinda 11 na kupoteza saba huku akitoka sare miwili, hali inayofanya pambano lao litakuwa na msisimko na mvuto wa aina yake. Mbali na michezo hiyo siku hiyo kwa mujibu wa Ngowi kutakuwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi ambayo itatoa burudani kwa mashabiki wa ngumi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani. Ngowi alisema lengo la Kamisheni la Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBC ni kuhakikisha kila miezi miwili kunakuwa na mapambano ya kimataifa kwa mabondia wa Tanzania baada ya kushuhudiwa 'ukame' wa mataji kwa muda mrefu. "Pia lengo letu ni kutoa nafasi kwa mabondia chipukizi kuonyesha vipaji vyao sambamba na kuendeleza mpango maalum ulianzishwa na IBF-Afrika/USBA kutangaza utalii kupitia mchezo huo wa ngumi," alisema. Tayari mabondia hao watakaoonyeshana kazi siku hiyo ya Idd Pili, wamejichimbia kambini wakijiandaa na mapambano hayo, huku mratibu Lucas Rutainurwa, akisisitiza kila kitu kinaendelea vema akiwataka mashabiki wa ngumi kujitokeza siku ya siku. Kama alivyonukuliwa Rais wa TPBO ambaye pia ni msemaji wa TPBC, Yassin 'Ustaadh' Abdallah, huenda hiyo ikawa ni nafasi nzuri kwa mabondia hao chipukizi wa Tanzania kuanza safari ndefu ya kufikia mafanikio yaliyowahi kufikiwa na wakongwe kama Rashid Matumla aliyewahi kunyakua ubingwa wa dunia wa WBU. Tusubiri tuone kipi kitakachovunwa na mabondia hao katika michezo
yao hiyo, ambayo itafanyika wiki chache kabla ya kumshuhudia Mtanzania mwingine, Thomas Mashale hajapanda ulingoni nchini Ujerumani kuwania taji la UBO Vijana uzani wa Kati kwa kupigana na mwenyeji wake Arthur Hermann. Awali pambano hilo linaloratibiwa na Becker BoxPromotion lilipangwa kufanyika wiki iliyopita nchini humo, lakini limeahirishwa hadi Septemba 5 mjini Berlin, Ujerumani.

African Lyon yamnasa kocha mpya toka Argentina

KLABU ya soka ya African Lyon jana imemtambulisha kocha wao mpya kutoka Argentina, Pablo Ignacio Velez, waliyeingia naye mkataba wa mwaka mmoja, huku mwenyewe akiahidi kufanya mabadiliko zaidi ya soka kwenye timu hiyo. Pablo raia wa Argentina aliyasema hayo jana baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo na kusisitiza lengo lake kubwa ni kuhakikisha vijana wanapewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na ndivyo itakavyokuwa Afrika Lyon. “Sikuja Tanzania kutafuta pesa, ndoto yangu kubwa ilikuwa kufundisha soka barani Afrika hivyo wakati ni sasa,” alisisitiza kocha anayezungumza lugha ya ‘kiispanyola’. Pablo alisema “kazi ya aina yoyote lazima ipewe muda na mchezaji lazima atengenezwe hivyo watanzania wawe na subira kwa ajili ya kupata matunda mazuri ya vijana hapo baadae kutoka African Lyon. Kocha huyo aliyewahi kuzichezea timu za taifa za vijana chini ya miaka 17 na 20 za Argentina hakusita kusisitiza suala la nidhamu kwa wachezaji wa timu hiyo ya ndani na nje ya uwanja. “Nidhamu ni muhimu kwa wachezaji wangu cha msingi tushirikiane katika kufanikisha hili kwa vijana kwani mchezaji anatakiwa kati ya miaka 18 na 19 awe ametengeneza jina kupitia soka ,” alisema Pablo. Naye Mmiliki wa African Lyon, Rahmu Kangezi alisema lengo la kumleta kocha huyo ni kuhakikisha timu hiyo inajongea mbele zaidi. Kangezi alisema licha ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja lakini wanaweza kumtumia Pablo kwa kipindi kirefu kulingana na mfumo wa kuhakikisha wanaendeleza vijana katika timu yao. “Pablo ni zaidi ya kocha, ana uwezo pia amecheza mpira pia ni kocha wa kwanza kutoka Argentina kuja Tanzania hivyo tunaimani timu yetu ya African Lyon itafika mbali zaidi kisoka,” alisitiza Kangezi. Pablo mwenye miaka 38 aliyechukua mikoba iliyoachwa na Jumanne Chale amewai kuifundisha klabu ya Atletico Colo Colo De Chile (1998). Klabu nyingine alizowai kufundisha ni Atletico Calchin (2000), Atletico Belgrano De Cordoba (1997), Atletico River Plate (1993-1995). Klabu nyingine ni Banco De Cordoba (1991 na 1997), Deportivo Lasallano (1992) Atletico Argentino Penarol kwa miaka minne na klabu nyingine nyingi za Hispania na Argentina.

Yanga kutafuta kocha mwingine iwapo...!

UONGOZI wa mabingwa wa soka Afrika mashariki na Kati, Yanga, umesema utatafuta kocha mwingine kama mwalimu wao Tom Saintfiet atapata kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya. Hata hivyo, Yanga imesema mpaka sasa haina taarifa rasmi juu ya kocha wake huyo kutakiwa na Shirikisho la soka Kenya kwa ajili ya kuifundisha timu yake ya taifa hivyo inasubiri barua kutoka KFF. Akizungumza na Nipashe jana, Afisa habari wa Yanga, Luis Sendeu, alisema endapo KFF itaonyesha dhamira ya kumtaka Saintfiet hawatomzuia. "Hatutaweza kumzuia," alisema Sendeu. "Tutakaa naye na kujua nini cha kufanya, lakini napenda kuwaambia kuwa sisi kama Yanga hatuna taarifa za kocha wetu kutakiwa Kenya. "Ila kama tutapata taarifa rasmi uongozi utajua nini cha kufanya," alisema Sendeu. Itabidi klabu itafute kocha mwingine endapo itaridhia kusitisha mkataba wa miaka miwili wa mwalimu huyo Mbelgiji aliyeanza kuifundisha mwezi uliopita. Sendeu alisema kuwa kwa sasa kocha huyo anaendelea na programu zake za kuiandaa timu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Bara ambao utaanza mwezi ujao. "Kocha Tom yupo na kikosi akikiandaa kwa ajili ya ligi kuu ya Bara... na yeye ana programu zake ambazo anazifanyia kazi kuhakikisha timu inakuwa katika kiwango cha juu zaidi ya sasa pindi ligi kuu itakapoanza," alisema. Alisema viongozi wa Yanga wanaamini uwezo ambao timu hiyo ilionyesha kwenye mashindano ya Kagame ndiyo ambao utahamishiwa kwenye ligi na kufuta makosa waliyoyafanya msimu uliopita ambapo ilivuliwa ubingwa na mahasimu wao Simba. Yanga ilionyesha soka la hali juu kwenye michuano hiyo licha ya kuanza kwa kipigo, ikishinda michezo yake sita iliyofuatia hadi kutetea Kombe la Kagame. CHANZO:NIPASHE JUMAMOSI

Mkali wa mikono aimwagia sifa Azam Fc

NYOTA wa klabu ya mpira wa mikono ya Ngome, Ally Khamis 'Muba' ameimwagia sifa klabu ya Azam Fc kwa mafanikio makubwa iliyopata kwa kipindi kifupi tangu iingie kwenye Ligi Kuu Tanzania na kudai imeleta mapinduzi yanayopaswa kuwa changamoto kwa Simba na Yanga. Muba, aliyewahi kuwa mlinda mlango enzi akisoma kabla ya kujitosa kwenye mpira wa mikono, alisema kinachofanywa na Azam, kinapaswa kuigwa na klabu nyingine katika kuendeleza mchezo huo sambamba na kurejesha heshima ya timu za Tanzania katika anga la kimataifa. Alisema, anaamini kungekuwa na klabu zenye malengo na mipango inayotekelezeka kama Azam ni wazi soka la Tanzania lingepiga hatua kubwa. "Lazima niseme ukweli mie nakunwa na mafanikio ya Azam, yanatia moyo na kuonyesha wenye timu hiyo walivyo na malengo na nadhani klabu nyingine zinapaswa kujifunza kutoka kwao iwapo zinataka kufika mbali," alisema. Muba, alisema pamoja na kuipongeza klabu hiyo, bado haipaswi kubweteka kwani safari iliyopo mbele yao ni kubwa na inayohitaji moyo wa ustahamilivu hususani katika ushiriki wao wa michuano ya kimataifa ambapo mwakani itaiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Juventus atupwa 'jela', kisa...Rushwa!

ROME, Italia MAHAKAMA ya Michezo ya Italia imemtupa 'jela' kocha wa mabingwa wa nchini humo, Juventus, Antonio Conte kwa muda wa miezi 10 jana kwa kosa la kushindwa kuripoti tukio la upangaji matokeo ya mechi katika kashfa ya kamari ya upangaji matokeo ambayo imetikisa soka ya Italia, shirikisho la soka limesema. Kocha huyo aliyeiongoza Juventus kutwaa ubingwa wa Serie A msimu uliopita, ameadhibiwa kwa mechi mbili za Siena za Mei 2011, wakati akiwa kocha wa timu hiyo ya daraja la kwanza, Serie B. Mahakama hiyo ilimuachia beki wa klabu hiyo Leonardo Bonucci na winga wa kulia Simone Pepe kwa kuwaona hawakuhusika na kashfa hiyo. Waendesha mashitaka walisema kundi la wacheza kamari maharamia wa kimataifa lilikuwa likilipa wachezaji ili wafungishe timu zao katika kashfa ya upangaji matokeo michezoni ambayo inafanana na ile iliyochafua sifa ya soka ya Italia katika miaka ya 1980. Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, mpo!
Chanzo: Reuters

Mabeki wa pembeni waipa presha Simba

BAADHI ya wanachama na mashabiki wa klabu ya soka ya Simba, wameanza kuwa na wasiwasi na uwezo wa timu yao, wakiushauri uongozi kushirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha wanaimarisha safu ya ulinzi hususani mabeki wa pembeni. Wanachama na mashabiki hao wamedai kuingiwa na wasiwasi kutokana na matokeo ya hivi karibuni iliyopata timu yao ikionekana kupwaya karibu kila idara jambo linalowatia shaka kama wataweza kutetea taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara. Mmoja wa wanachama hao, aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema beki za pembeni wa Simba zimepwaya na kukosekana watu wa kuifanya timu yao itishe kama ilivyozoeleka na kudai ukuta huo umeathiriwa kutokana na kuumia mara kwa mara kwa ajina Nassor Cholo na Amir Maftah. "Kwa miaka mingi Simba imekuwa ikisifika kuwa na 'ma-fullback' visiki na viungo imara, lakini kwa mechi kadhaa zilizopita tumebaini safu hizo zimepwaya na ajabu uongozi umeimarisha kiungo na kusahau beki hizo za pembeni," alisema mwanachama huyo. Naye mnazi mkubwa wa klabu hiyo Leila Mwambungu, alisema kuna haja viongozi na benchi la ufundi kuhakikisha wanasaka wachezaji wa pembeni mapema ili kuimarisha kikosi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu Septemba Mosi na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani. "Safu ya ulinzi ya Simba ina tatizo hasa mabeki wa pembeni, hivyo viongozi na benchi la ufundi lifanyie kazi dosari hiyo mapema kabla ya kuanza kwa ligi ili tusije tukaumbuka," alisema Leila. Simba iliyong'olewa kwenye hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Kagame kwa kipigo cha mabao 3-1 toka kwa Azam, ilirejea kupokea kipigo kama hicho Jumatano iliyopita dhidi ya City Stars ya Kenya wakati wa sherehe za Simba Day zilizofanyika jijini Dar. Kabla ya kipigo hicho cha Wakenya, Simba ililazimishwa sare ya baoa 1-1 na Jamhuri ya Kenya katika michuano ya Super 8 baada ya kuongoza bao 1-0 katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jijini Dar.

Sikia hii, eti :Kazimoto ni kama Xavi, Iniesta

MCHEZAJI nyota wa timu ya mpira wa kikapu ya ABC, Gilbert Batunga 'B10' amesema kwa sasa nchini hakuna kiungo mwenye kiwango cha kipekee kama alichonacho Mwinyi Kazimoto wa klabu ya Simba. Batunga, alisema kwa kiwango alichonacho Kazimoto kiuchezaji anaweza kumlinganisha na viungo nyota wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Xavi na Andre Iniesta. Mkali huyo, alisema Kazimoto ana sifa zote za mchezaji wa nafasi yake na kudai iwapo kama atapewa nafasi zaidi huenda akafika mbali kwa sababu kokote anaweza kucheza. "Kwa kweli licha ya Tanzania kuwa na vijana wenye vipaji katika soka, binafsi sijaona kama Mwinyi Kazimoto. Huyu jamaa ana ujua na kuuchezea mpira, nadhani akipewa nafasi huenda akafika mbali na kuitangaza nchi kimataifa," alisema. Alisema, anaamini umahiri wake ndio ulioifanya Simba kuamua kumvua 'gwanda' toka JKT Ruvu ili wapate huduma zake, ingawa alisema hali ya majeruhi imekuwa ikimuangusha mkali huyo. Mwinyi Kazimoto, anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars alitua Simba msimu uliopita akitokea JKT Ruvu, amekuwa akitajwa kama mmoja wa viungo mahiri nchini kwa sasa akiwekwa kundi moja na wakali kama Salum Abubakar 'Sure Boy', Shaaban Nditi na wengineo.

Baada ya Chaguo, Richie ana Tamaa kwa Rado

BAADA ya kukamua vilivyo katika filamu ya 'Chaguo Langu', muigizaji mahiri nchini Single Mtambalike 'Richie', ameibuka katika kazi nyingine ambayo imekuwa ikifanya vema sokoni iitwayo 'Tamaa Yangu' ya msanii, Simon Mwapagata 'Rado'. Akizungumza na MICHARAZO, Rado alisema filamu hiyo miongoni mwa kazi zake tatu ambazo zimeingizwa sokoni hivi karibuni, ambapo mbali na 'Tamaa Yangu', nyingine ni 'Hatia' na 'XXL'. Rado alisema katika filamu ya 'Tamaa Yangu', mbali na Richie, pia ameigiza na wakali kama Deo Shija na mwanadada Regina Mroni, aliyewahi kutamba na filamu ya 'Aisha'. "Nimeachia kazi tatu kwa mpigo, XXL, 'Hatia' na 'Tamaa Yangu' ambayo nimeigiza na mkongwe Single Mtambalike, Deo Shija na Regina Mroni," alisema Rado. Kutoka kwa kazi hiyo ya 'Tamaa Yangu' kunamfanya Richie, aendelea kukimbiza sokoni miongoni mwa wakongwe wa fani hiyo kwani ni wiki kadhaa ameachia kazi yake mpya ya 'Chaguo Langu aliyoigiza na wakali kama Jacklyn Wolper na Adam Kuambiana. Kabla ya 'Chaguo Langu', Richie alitamba kwa muda mrefu na filamu ya 'Diana', aliyoigiza na Halima Yahya 'Davina' na Sabrina Rupia 'Cath'. Mkongwe huyo aliyewahi kutamba akiwa na makundi ya Mambo Hayo na Kamanda Assemble yaliyokuwa wakionyesha michezo yake kwenye vituo vya ITV na CTN, kwa sasa inaelezwa yupo 'location' kwa ajili ya kufyatua kazi nyingine mpya.

TAFF, Bongo Movie, wasambazaji waungana kudhibiti wezi

MAKAMPUNI ya usambazaji wa kazi za wasanii kwa kushirikiana na Shirikisho la Filamu Tanzania, TAFF na Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, wameungana pamoja na kutangaza 'vita' dhidi ya maharamia na wezi wa kazi za wasanii kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo. Wasambazaji hao, Steps Entertainment, PAPAZI, Msama Promotions na wengine wameamua kushirikiana na TRA, Bongo Movie na TAFF kwa nia ya kukomesha vitendo hivyo sawia na kulinda masilahi ya wasanii ambao wamenyonywa kwa muda mrefu. Wakizungumza katika mkutano uliofanyika jana jijini Dar es Salaam
viongozi wa 'umoja' huo walisema umefika wakati wa kukomesha tatizo hilo la muda mrefu ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wadau wa sanaa nchini. Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba, alisema wameona hakuna njia ya kukomesha hilo kama sio kufanya kazi kwa pamoja katika kulishughulikia akidai anashangazwa na kukithiri kwa hali hiyo ilihali kuna sheria juu ya udhibiti wa jambo hilo. Alisema, mbali na muunganiko wao, pia wanaiomba serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wasanii kupambana na maharamia, aliodai wapo kila pembe ya nchi hii wakifanya uhalifu wao kwa kujiamini kana kwamba wapo juu ya sheria. Mwakifwamba aliongeza kwa kusema lau kazi za wasanii zitasimamiwa vizuri, zitaliongezea taifa pato kubwa kw avile soko la sanaa kwa sasa limekuwa na mafanikio makubwa ingawa bado inawanufaisha wachache. Naye Mwenyekiti wa Bongo Movie, Jacob Steven 'JB' alisema sanaa inaweza kuwa na nafasi ya tatu kwa kuchangia pato la taifa ukiacha pato linalotokana na sekta za madini, maliasili na utalii. Kwa upande wa TRA, Meneja Usimamizi, Msafiri Ndimbo alisema Mamlaka hiyo imejipanga kudhibiti wizi wa kazi hizo kuanzia Januari mwakani baada ya serikali kupitia Bunge lake kukubalina kuweka mikakati ya kupamba na suala hilo.