STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, February 19, 2015

Ally Mustafa 'Barthez' ni Nouma sana!

http://1.bp.blogspot.com/-jwqUI0Zc0JI/UBQR56kKWVI/AAAAAAAAK8w/o79LfKoNk5Y/s1600/35.jpg
Barthez mbele kushoto akiwaongoza wachezaji wenzakle wa Yanga
PAMBANO la Yanga dhidi ya Prisons-Mbeya lililochezwa uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kwa vijana wa Jangwani wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 umezidi kumpandisha chati kipa Ally Mustafa 'Barthez' ambaye amedaka mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara bila kuruhusu bao lolote.
Kipa huyo aliyekuwa na wakati mgumu mbele ya kikosi cha Jangwani tangu Yanga ilipolazimishwa sare ya mabao 3-3 na Simba Oktoba mwaka juzi, hajafungwa bao lolote katika muda wa dakika 540 huku kwenye uwanja wa Sokoine akigeuka kuwa shujaa kwa kuokoa michomo mingi ya wachezaji wa Prisons.
Hizo ni mbali na dakika 90 za pambano la kimataifa la Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0 na yeye akiwa kwenye milingoni mitatu ya lango ya vijana wa Jangwani.
Barthez aliyesajiliwa na Yanga akitokea Simba, rekodi zake zinaonyesha kuwa ameshuka dimba katika mechi hizo kama ifuatavyo na kuwafunika makipa wote wa timu nyingine 13 zinazoshiriki ligi hiyo.
Jan 17, 2015Yanga vs Ruvu Shooting (0-0)
Jan 24, 2015Polisi Moro vs Yanga (1-0)
Feb 01, 2015Yanga vs Ndanda (0-0)
Feb 4, 2018Coastal Union vs Yanga (0-1)
Feb 08, 2015Yanga vs Mtibwa Sugar (2-0)
 Feb 14, 2015-Kimataifa
Yanga vs BDF XI (2-0)
Feb 19, 2015
Prisons vs Yanga (0-3)

FAINALI ZA DUNIA 2022 KUFANYIKA DESEMBA?

http://www.shalomlife.com/img/2014/12/27573/qatar_.jpg
MTANDAO mmoja barani Ulaya umetoa taarifa kuwa tayari muafaka umeshafikiwa kwa michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2022 kufanyika katika kipindi cha Novemba na Desemba ili kuwepa joto kali katika kipindi cha kiangazi.
Wakiorodhesha vyanzo mbalimbali mtandao huo umedai kuwa uamuzi umeshafanyika kwani kikosi kazi kilichoteuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kinatarajia kuwasilisha miezi hiyo katika kikao chao kitakachofanyika wiki ijayo jijini Doha kabla ya kamati ya utendaji haijakamilisha mpango huo wakati wa kikao cha mwezi ujao jijini Zurich.
Wiki tatu zilizopita, Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke katika mahojiano yake na radio moja nchini Ufaransa alisema Kombe la Dunia nchini Qatar linatakiwa kuandaliwa wakati wa majira ya baridi lakini kugongana na michuano ya Olimpiki ya kwenye baridi Februari mwaka 2022 pia ni hatihati.
Hata hivyo mpango huo haujafafanua kwa undani zaidi kuwa michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo huchezwa mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia kama nayo itasogezwa mbele kuepuka majira ya kiangazi.
Desemba mwaka jana Chama cha Vilabu barani Ulaya na Muungano wa Ligi za Soka barani humo vilipendekeza michuano hiyo ya Qatar kuchezwa kati ya May na Juni ili kutovuruga ratiba zingine za kawaida za msimu.
Uteuzi wa Qatar kuandaa fainali hizo na zile za mwaka 2018 nchini Russia zimeghubikwa na mizengwe na kuelezwa kujaa vitendo vya rushwa, ingawa FIFA imekuwa ikijitetea.

BAHANUZI, MAHUNDI WANG'ARA VPL

http://2.bp.blogspot.com/-ORUnNfNV-xE/VM0wOPMp6vI/AAAAAAABdBc/1sAbma_8dB4/s1600/BAHANUZI.jpg
Said Bahanuzi
http://2.bp.blogspot.com/-OgW82_5TAnQ/UYKSRp52TMI/AAAAAAAAgQc/E5SL6W0-Kv4/s1600/IMG_1197.jpg
Mahundi (kulia) akichuana na Niyonzima katika moja ya mechi ya Ligi Kuu
KIUNGO wa timu ya Coastal Union ya Tanga, John Mahundi amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba 2014 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mahundi alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi huo na kuchaguliwa na jopo la makocha linalofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora wa kila mwezi.
Aidha mshambuliaji wa timu ya Polisi Morogoro, Said Bahanuzi 'Spider Man' amechaguliwa kuwa mchezaji bora mwezi Januari 2015.
Bahanuzi anayechezea timu ya Polisi Moro kwa mkopo akitokea timu ya Young Africans amekua na mchango mkubwa kwa timu yake tangu kujiunga nayo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom nchini.
Kwa kuibuka wachezaji bora, Mahundi na Bahanuzi watazawadiwa fedha taslimu Sh. Mil. 1/ kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
Jopo maalum la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.

Yanga wafanya mauaji Mbeya, Azam yabanwa

Yanga
Msuva na Coutinho walipokuwa wakijiandaa kuiangamiza Prisons-Mbeya

Azam
Azam walishindwa kushangilia kama hivi leo kwa Ruvu Shooting
KLABU ya Yanga imeendeleza rekodi yake ya kugawa dozi kwa wapinzani wao katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuilaza Prisons-Mbeya kwa mabao 3-0 na kukwea kileleni mwa msimamo wakiiengua Azam.
Azam waliokuwa uwanja wa Mabatini-Mlandizi wameshindwa kutamba kwa kulazimishwa suluhu mbele ya maafande wa Ruvu Shooting na kutoa nafasi kwa Yanga kuwaacha kwa pointi mbili kileleni.
Kwa suluhu iliyopata kwa Ruvu, imeifanya mabingwa watetezi Azam kufikisha pointi 26 na kushuka hadi nafasi ya pili licha ya timu zote mbili kulingana mechi zote zikicheza michezo 14 kila moja.
Yanga ikicheza kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya walipata ushindi huo murua na uliowafanya kufikisha pointi 28 baada ya kupata mabao yake mawili katika kipindi cha kwanza na jingine kipindi cha pili.
Mabao hayo yaliwekwa kimiani na Simon Msuva aliyefunga dakika ya tatu tu ya mchezo kabla ya Coutinho kuongeza la pili.
Msuva alirudi tena kambani kwa kufunga bao la tatu kipindi cha pili na kumfanya afikishe jumla ya mabao sita akibakisha mabao mawili kumkuta Didier Kavumbagu wa Azam mwenye mabao nane.
Yanga wataendelea kusalia jijini humo kwa ajili yua kusubiri pambano lake la Jumapili dhidi ya Mbeya City kabla ya kutimka zao Botswana kuwafuata BDF XI kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo wao wa kwanza uliochezwa mwishoni mwa wiki, Yanga iliitambia BDF kwa kuilaza mabao mawili yote yakiwekwa kimiani na Mrundi, Amissi Tambwe.