STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 12, 2011

Kanumba atambia 'The Shock'MUIGIZAJI Nyota wa Filamu Tanzania, Steven Kanumba, ametamba kuwa kazi yake mpya ya 'The Shock' ambayo ipo kwenye foleni kabla ya kuachiwa mitaani ni 'funika bovu' ya mwaka 2011.
Kanumba, mshindi wa tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume 2010, alisema filamu hiyo iliyoandaliwa na kampuni yake ya Kanumba The Great Films ni moja ya kazi itakayokimbiza kwenye soko la filamu kutokana na namna iliyoandaliwa pamoja na washiriki wake walivyofanya kweli.
Akizungumza na Micharazo, Kanumba, alisema sio kawaida yake kujisifu, ila kazi hiyo ni moja ya kazi nzuri iliyouanza mwaka 2011.
Alisema wakati kazi hiyo ambayo inamuibua muigizaji mpya wa kike nchini Shez Sadry, ikiwa kwenye foleni kabla ya kuingia mitaani, kampuni yake inaendelea na maandalizi ya kazi nyingine.
"Sio siri kama kuna kazi itakayokimbiza mwaka huu, basi ni The Shock, kutokana na jinsi nilivyoiandaa na namna washiriki walivyofanya kazi ya ziada kudhihirisha kuwa fani yetu inazidi kupaa nchini," alisema.
Washiriki wengine waliopo ndani ya filamu hiyo ni mwanamuziki mahiri wa bendi ya FM Academia, Patcho Mwamba na wengine wengi.
Katika hatua nyingine, kampuni ya kusambaza filamu ya Kapico, imeamua kuibeba filamu mpya ya kusisimua ya Bangkok Deal inayohusisha majoka makubwa kama ilivyokuwa 'Anaconda'.
Filamu hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya Huba Production, imewashirikisha wasanii wakali kama Charles Magali, Bambucha na wengine, wakati wowote itakuwa hewani kupitia Kapico moja ya wasambazaji wakubwa wa filamua za Kibongo nchini.
Mwisho

Sikinde wavamia ngome ya Msondo

BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' imevamia ngome ya wapinzani wao, Msondo Ngoma kwa kuanzisha bonanza linalofanyika kila Jumapili kwenye ukumbi wa TCC Club-Chang'ombe.
Msondo kwa muda mrefu imekuwa ikifanya bonanza kila Jumamosi kwenye klabu hiyo, hivyo kutua kwa Sikinde ni kama kuwachokoza ikiwa ni wiki kadhaa tangu pambano lao kuahirishwa.
Katibu wa bendi ya Sikinde, Hamis Milambo, alisema bendi yao imelianza bonanza hilo tangu wiki iliyopita kwa kutumbuiza kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 kabla ya kumalizia burudani zao kwenye ukumbi wa SUWATA.
Milambo, alisema hilo ni bonanza la pili kwa bendi yao, baada ya kufanya pia bonanza jingine linalifahamika kama Konyagi Bonanza kila Jumamosi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo.
"Tangu wiki iliyopita tumekuwa tukifanya bonanza jipya kwenye ukumbi wa TCC Chang'ombe majira ya saa 8-12 kisha kuendelea na ratiba yetu pale SUWATA kuanzia saa 1-5 usiku," alisema.
Aliongeza kwa leo bendi yao itakamua kwenye bonanza lao la Konyagi ikitambulisha nyimbo zao mpya na zile za zamani zilizoifanya bendi hiyo kuwa Mabingwa wa Muziki Tanzania.
Baadhi ya nyimbo mpya za bendi hiyo ni Tunu ya Huba, Wanawake Wakiwezeshwa, Urithi, sambamba na zile za albamu yao ya Supu Imetiwa Nazi.
Mwisho

Filamu ya ngumi hadharani leoFILAMU mpya inayozungumzia maisha ya bondia wa zamani na kocha wa sasa wa klabu ya Ashanti, Rajabu Mhamila 'Super D' iitwayo 'Super D:Boxing Coach', inatarajiwa kutolewa rasmi leo.
Filamu hiyo ambayo inahusisha pia mapambano kadhaa ya mabondia nyota duniani, itatolewa rasmi leo katika sherehe maalum itakayofanyika kwenye klabu ya ngumi ya Ashanti inayoadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza na micharazao, Super D, aliyewahi kuzichezea klabu za Simba, Reli na Amana na kupigana na mabondia kama Mbwana Ally na wengineo, alisema filamu hiyo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha mchezo wa ngumi ambao umeshuka kiwango kwa sasa.
"Pamoja na kusimulia na kuonyesha michezo yangu tangu wakati nikipigana mwaka 1984, pia kuna mapambano ya wakali wa dunia katika mchezo wa ngumi za kulipwa," alisema Super D.
Super D, alisema filamu hiyo itazinduliwa leo na kuachiwa hadharani ili mashabiki wa ngumi na filamu kwa ujumla kuipata na kwenda kuishuhudia uhondo wake.
Aliyataja mapambano yaliyopo ndani ya filamu hiyo kuwa ni, ya Muhammad Ally, Iron Mike Tyson, Manu Pacquiao, Michael Moore, Llyod Mayweather, Oscar de La Hoya na wengineo.
"Kazi yangu itakuwa mitaani kuanzia Machi 12, wakati tukiadhimisha mwaka mmoja tangu Ashanti Boxing ianzishwe mie nikiwa miongoni mwa makocha wake," alisema.
Hiyo itakuwa ni filamu ya pili inayozungumzia mabondia wa zamani na mafunzo ya ngumi, awali bingwa wa dunia, Francis Cheka 'SMG' akifanya hivyo mwaka juzi kwa kutoa filamu kama hiyo ikiwa na jina na Francis Cheka na Historia Yake.

Talent wasubiri kidogo videoniBENDI ya Talent 'Wazee wa Kuchechemea' imekamilisha kurekodi video ya nyimbo za albamu yao mpya ya 'Subiri Kidogo', huku ikiendelea kuandaa albamu ya pili.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Husseni Jumbe, alisema video ya albamu hiyo imekamilika mapema wiki hii na kwa sasa inafanyiwa uhariri kabla ya kusambazwa sokoni na kwenye vituo vya runinga.
Jumbe, alisema video ya albamu hiyo yenye nyimbo sita imetayarishwa na kampuni moja ya jijini na ina mandhari ya kuvutia ikirekodiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
"Tumekamilisha kuiweka kwenye video albamu yetu mpya ya Subiri Kidogo, kwa sasa inahaririwa kabla ya kuanza kusambazwa ili mashabiki wetu wapate uhondo," alisema Jumbe.
Alizitaja nyimbo zilizorekodiwa kwenye video hiyo ni 'Subiri Kidogo', 'Dillema', 'Nyuma ya Pazia', 'Songombingo' na 'Nimeamua Kunyamaza'.
Jumbe alisema video hiyo ikikamilika, tayari bendi yake yenye wanamuziki 10, imeshaanza kuandaa albamu mpya ijayo.
Alisema nyimbo nne kati ya sita za albamu hiyo zimeshakamilika na kuanza kutambulishwa kwenye maonyesho yao ambazo ni pamoja na 'Shoka la Bucha', 'Jipu la Moyo' na 'Kilio cha Swahiba' ambao awali ulipangwa kuwepo kwenye albamu yao ya kwanza.
"Kibao cha Kilio cha Swahiba tuliamua kukiweka kwa ajili ya albamu hii ya pili, ambayo tayari ina nyimbo zingine tatu," alisema Jumbe.
Jumbe, alisema kabla ya Juni, albamu hiyo aliyopanga kuiitwa kwa jina la Shoka la Bucha huenda ikakamilika rasmi.

Riyama Ally: Kisura mkali anayewagusa wengiAKIIGIZA mwenye majonzi utamuonea huruma kwa jinsi atakavyolia kwa kumwaga machozi kama yupo msibani, akicheza kama mwendawazimu utamsikitikia kwa jinsi atakavyokuwa akila jalalani na kufanya vituko vyote wafanyavyo watu wenye kuugua kichaa.
Wengi hudhani yale anayoyafanya kwenye filamu ni mambo ya kweli kutokana na kucheza uhalisia asilimia 100, kitu kinachomfanya Riyama Ally kuwa mvuto wa pekee katika filamu anazoziigiza.
Mwanadada huyo mmoja wa waigizaji wa kike wakali nchini,alianza kufahamika mwishoni mwa miaka ya 1990 alipokuwa na kundi la Taswira na hasa igizo la Jabari lililokuwa likionyeshwa kwenye kituo cha ITV mwaka 2000.Katika igizo hilo lililokuwa gumzo nchini miaka hiyo, Riyama aliigiza kama mtoto aliyegeuzwa kichaa na mama yake mzazi aliyekosea masharti ya dawa za mganga ili kumdhibiti mumewe, ndilo lilothibitisha kuwa kisura huyo ni mkali.
Miaka mitatu baadae, yaani mwaka 2003 Riyama aliachana na Taswira na kutua kundi la Tamba Art, lililowahi kutamba na filamu kama Nsyuka na kuzidi kuonyesha makali yake.
Akiwa na kundi hilo linalomilikiwa na mganga maarufu wa tiba asilia, Dk Maneno Tamba, Riyama, alishiriki filamu mbalimbali zilizozidi kumjengea jina kutokana na staili yake ya uigizaji kama anayefanya kweli.
Baadhi ya filamu alizofyatua akiwa na kundi hilo ni pamoja na 'Miwani ya Maisha', 'Mzee wa Busara', Fungu la Kukosa na nyinginezo kabla ya kupata bahati ya kushiriki kazi nyingine nje ya kundi hilo.
Filamu kama 'My Darling','Simu ya Kifo', 'Darkness Night', 'Mwana Pango', 'Kolelo','Segito', Fake Promise na nyinginezo ni baadhi ya kazi hizo za nje zilizompaisha mrembo huyo mwenye asili ya mkoa wa Tanga.
Akiwa mmoja wa waigizaji wa kike wanaojiheshimu akiwa hana kashfa yoyote kama mastaa wengine wa aina yake, Riyama mbali na uigizaji, pia ni mtunzi wa filamu na mtayarishaji moja ya kazi yake binafsi ikiwa ni Mwasu iliyofanya vema sokoni kwa kitambo kirefu.
Riyama, mshindi wa tuzo ya Uigizaji Bora ya Risasi 2005-2006, kwa sasa yupo mbioni kuibuka na filamu mpya ya Second Wife, aliyoigiza na Vincent Kigosi 'Ray', Aisha Bui, Colleta Raymond na wengine.
Filamu hiyo inatarajiwa kuachiwa hadharani keshokutwa, ambapo kama kawaida yake, Riyama 'chozi' linamtoka kutokana na kutendwa sivyo ndivyo na 'mumewe' ndani ya filamu hiyo.
Riyama anayependa kusafiri, kupika na kulala anapokuwa nje ya fani yake ya uigizaji, ni shabiki mkubwa wa muziki wa taarab, kundi la Mambo Jambo na pia kusoma vitabu mbalimbali.

Mwisho

Benita: Kimwana aliyekacha 'utawa' aigizeTAMTHILIA ya 'Beyond Our Dreams'iliyokuwa ikirushwa kupitia kituo cha runinga cha NTA miaka ya katikati ya 1996 ndiyo iliyomtangaza Benita Nzeribe, mmoja wa waigizaji nyota wa Nigeria.
Mwaka 1998 alijitumbukiza kwenye fani ya uchezaji filamu na kazi mbili za awali za 'Notorious Virgin' na 'Gold Diggers' zilizomtangaza vema kwenye ulingwengu wa fani hiyo.
Filamu hizo ilitoka mwaka 1999-2000 na tangu hapo ameshiriki kazi mbalimbali zilizomjengea jina katika ukanda wa Nollywood na kufahamika kimataifa.
Mzaliwa huyo wa Jimbo la Anambra aliyewahi kunusurika kufa kwenye ajali ya gari, alisema pamoja na kipaji cha sanaa kuwa cha kuzaliwa, lakini kuvutiwa kwake na waigizaji Liz Benson wa Nigeria, Angeline Jolie na Cameroon Diaz wa Marekani ndiko kulikomtumbukiza huko.
Alisema, hata alipojiunga na Chuo Kikuu cha Abia, lengo lake lilikuwa kusomea masomo ya sanaa, lakini chuo hicho hakikuwa na kozi hizo na hivyo kuchukua masomo ya Lugha ya Kiingereza aliyohitimu kabla ya kuanza kuuza sura kwenye runinga.
Aliongeza kuwa bahati nzuri ni kwamba alipoanza kuigiza wazazi wake hawakumuangusha, ingawa baadhi ya wahitimu wenzake walimshangaa kwa kuichagua kazi hiyo ya uigizaji.
Benita, mtoto wa tatu kati ya wanne wa mfanyabiashara maarufu Mr Nzeribe na mama muuguzi mstaafu, tangu alipoanza kushiriki uigizaji wa filamu amecheza zaidi ya kazi 100 kati ya hizo akishirikiana na wakali kama mkongwe Olu Jacobs, Ejike Asiegbu, Ken Okonkwo, Fred Amata, Juliet Ibe na wengineo.
Moja ya filamu anayojivunia ni ile ya Peace of Mind, aliyocheza kama mke anayenyanyaswa na kupigwa na mumewe, kitu alichodai kimewahi kumtokea katika maisha yake ya kimapenzi.
Mwanadada huyo, ambaye pia ni mwanamitindo na mpambaji, majina yake kamili ni Benita Nnenna Adaeze Nzeribe, aliyezaliwa Uzoakwa, Ihiala, Jimbo la Anambra, elimu yake ya msingi na sekondari aliisoma katika miji ya Aba na Umuahia.
Pia alipitia mafunzo ya kiroho akiwa na lengfo la kuja kuwa mtawa, kabla ya kufuta wazo hilo na kati ya vitu anavyokumbuka katika makuzi yake ni tukio la baba yake kumnunulia gari lake la kwanza akiwa na miaka 14 tu.
"Tukio hili la baba kuninunulia gari nikiwa na miaka 14 siwezi kulisahau maishani mwangu kwani lililonyesha alivyonijali na kunithamini," alinukuliwa.
Kuhusu uigizaji wake wa filamu za kimapenzi, alisema ni jambo la kawaida kulingana na nafasia anayopangiwa na muongozaji wake, ila ni mtu anayejiheshimu na kuithamini kazi yake.
Alipoulizwa kama yupo tayari kuchojoa ili aigize utupu, Benita alisema katu hawezi kufanya upuuzi huo hata kwa kisi gani cha fedha hasa kutokana na hadhi ya familia yake nchini kwao.
Baadhi ya kazi alizoshiriki kisura huyo, mbali na zile zilizomtambulisha Nollywood ni Cross My Heart, Cross & Tinapa,Endless Madness,Tears of a Saint, Treasure Hunt,Breath Again,Buried Emotion,Enemies in Love, Games Men Play, Girls Cot,King of the Town na Life Abroad.
Pia ameshiriki Peace Talk, The Final Days, Christian Girls, Fools in Love, Hold Me Down, Paradise to Hell, Secret Affairs, The Scorpion, Under Arrest, Beyond Reason, My Desire,Stand by Me, A Night to Remember, Arrows, Great Change, Lagos Babes, Mission to Africa, Saved by Grace, Street Life, The One I Trust, Agony of a Mother, Fire on the Mountain na kadhalika.