STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, April 7, 2014

Majambazi yateka magari ya makampuni ya magazetiMadereva wa gari la magazeti ya kampuni ya The Guardian Rashid Yusuph Kahese (37) kushoto na mwenzake Ally Malinda (44) ambao wamenusurika katika utekaji huo.

Gari la magazeti la kampuni ya The Guardian ambalo limetua Iringa hivi sasa saa 2.40 Asubuhi hii baada ya kupona kutekwa
MAJAMBAZI ambayo idadi yao haikufaanika mara moja usiku wa leo wamefunga barabara ya Morogoro -Iringa eneo la Doma na kufanya unyama wa kutisha kwa wasafiri wa barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha kufanya mapenzi wanaume kwa wanaume na kuwatesa vibaya madereva kabla ya kuwapora mali zao .
Miongoni mwa walioteswa na pamoja na rasta dereva wa gari la magazeti ya kampuni ya globalpublishers ambae anadaiwa kujeruhiwa mkono wake huku dereva wa gari la magazeti ya kampuni ya Mwananchi akinusurika na gari lake kupinduka wakati akikwepa vizuizi vya magogo vilivyotegwa barabarani.
Wakizungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.com asubuhi ya leo mjini Iringa wahanga wa tukio hilo Ally Malinda (44) mkazi wa Itunda Dar es Salaam na Rashid Yusuph Kahese (37) mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam ambao kwa pamoja wanaendesha gari ya magazeti ya kampuni ya The
Guardian walisema kuwa tukio hilo lilmetokea mida ya saa 8 usiku wa leo hadi saa 11 Alfajiri baada ya watekaji hao kuachia mateka hao .
Malinda alisema kuwa kabla ya kufika eneo ambalo watekaji hao walikuwa wamewateka abiria wengi zaidi walikutana na makundi ya watu waliotekwa na kuporwa ambao walikuwa wakiwasimamisha wasiendelee na safari ila hawakusimama wakijua ni wezi .
" Tulienda mbele kidogo tukakutana na kundi jingine ila bado tulipuuza na kupita baada ya kufika mbele ndipo tuliona magari yakiwa yamegeuka huku na kule huku wengine wakiteswa na ndipo tulipofanikiwa kugeuza gari letu lenye namba za usajili T 812 CNZ na kukimbia .
Hata hivyo alisema polisi Morogoro walipigiwa simu ila hawakuweza kufika hadi majira ya saa 11 Alfajiri watekaji hao walipoamua kuwaachia mateka.
" Kila tukimpigia kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro aliishia kusema kuna askari wametumwa kuja eneo la tukio ila hadi asubuhi hakuna askari aliyefika .....na majeruhi wamepelekwa Hospital ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi"
Mtandao huu wa matukiodaima .com unaendelea kumtafuta kamanda wa polisi wa mkoa wa Morogoro ili kuzungumzia tukio hilo zaidi .
Chanzo: francis godwin blog

Tanzia! Prof Juma Bhalo afariki

ALIYEKUWA gwiji la muziki wa mwambao Afrika Mashariki na Kati Profesa Juma Bhalo, amefariki dunia mwishoni mwa wiki na kuzikwa jana mjini Mombasa.
Mkali huyo wa kuimba, kughani mashairi, alifariki siku ya Jumamosi kwa mujibu kutoka Kenya na kuzikwa jana.
Kwa wanamkumbuka msanii huyo alitamba na nyimbo kadhaa kama Pete, Bunduki Bila Risasi, Alacho Kuku, Ameumbika, Asiyefunzwa na Mamaye, Ganda la Muwa la Jana pamoja na kibao maarufu cha Uliyataka Mwenyewe.
Marehemu alizaliwa mwaka 1942, Malindi na kutamba katika masuala ya muziki miaka ya 1960 akifanya kazi nchini Tanzania na Kenya na alikuja kustaafu miaka michache iliyopita ingawa bado aliendelea kutoa burudani kwa waliomhitaji.
Mungu ilaze roho ya marehemu Juma Bhalo, mahala pema peponi, Ameen

Timu ya Watoto Tanzania mabingwa wa Dunia

TIMU ya soka ya taifa ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania, imetwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuilaza Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil. Mshambuliaji Frank William alifunga mabao matatu katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.
Tanzania ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuitandika Marekani mabao 6-1 ambapo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.
Burundi ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika mechi ya nusu fainali ya pili.
Timu ya Tanzania inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates.

Hatma Chelsea, Dortmund kufanya majabu gani Ulaya kesho?

HATMA ya vijana wa kocha Jose Mourinho, Chelsea ya Uingereza kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itajulikana kesho watakaporudiana na PSG ya Ufaransa kwenye uwanja wa Stanford Bridge jijini London baada ya kufungwa bao 3-1 ugenini Paris, Ufaransa.
Chelsea iliyo katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England, ina nafasi kubwa kupenya hatua hiyo kutokana na bao la ugenini ililopata, ambalo linaifanya kuhitaji bao 2-0 kutangulia hatua hiyo.
Hata hivyo, itakuwa na kibarua kigumu mbele ya matajiri wa Ufaransa ambao wangependa kutinga hatua hiyo baada  ya kipindi kirefu kupita bila kufikia nusu fainali licha ya kutumia fedha nyingi kujenga kikosi imara Ulaya.
Timu nne zitakazofuzu  nusu fainali zinatarajiwa kujulikana wiki hii wakati timu nane za robo fainali zitakapokuwa zikimalizia mechi zao za mkondo wa pili kati ya kesho na keshokutwa.
Ikiwa bila mfumania nyavu wake mahiri, Zlatan Ibrahimovic aliyeumia mechi iliyopita, PSG itawategemea wakali wengine akiwemo Ezequiel Lavezzi, Edinson Cavani ili kuipa wakati mgumu Chelsea na kutokubali kuwa daraja la kuwavusha wapinzani wao kuingia nusu fainali.
Kivumbi kingine cha mechi ya marudiano ya robo fainali kitakuwa nchini Ujerumani wakati Borussia Dortmund ikiwaalika Real Madrid wakiwa na machungu ya kubutuliwa bao 3-0 wiki iliyopita.
Real itahitaji sare ya aina yoyote ili kulipa kisasi kwa wapinzani wao waliowang'oa hatua ya nusu fainali mwaka jana kwa kipigo cha mabao 5-3, ilifungwa ugenini mabao 4-1 na kushinda nyumbani kwao 2-0 na kuiacha Dortmund ikienda kucheza fainali na Bayern.
Pamoja na kufungwa mabao 3-0 ugenini, Dortmund siyo timu ya kubezwa na huenda ikafanya maajabu kwa kuing'oa Real kwani itakuwa na 'muuaji' wake Robert Lewandowski aliyekuwa akitumikia kadi, licha ya kwamba kocha wa Real, Carlo Ancelotte ametamba wana kiu ya kutaka kunyakua ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.
Ancelotte alinukuliwa mbali na taji hilo pia anataka kunyakua mataji mengine mawili nyumbani kwao yaani Ligi Kuu wanaochuana na majirani zao Atletico Madrid na mahasimu wao Barcelona ambao wanakuna nao kwenye fainali ya Kombe la FA, taji jingine wanaloliwinda vijana hao wa Santiago Bernabeu.
Kivumbi cha ligi hiyo ya Ulaya kitaendelea Jumatano wakati, watetezi wa taji hilo, Bayern Munich watakapowakaribisha Mashetani Wekundu kwenye uwanja wao wa Allianz Arena. Mechi ya awali Munich ilifungana bao 1-1 na Manchester United.
Nazo timu zinazochuana kileleni mwa msimamo wa La Liga, Atletico Madrid na Barcelona zenyewe zitakuwa katika kitatange kingine mjini Madrid baada ya wiki iliyopita kushindwa kupata mbabe kati yao kwa sare ya bao 1-1.

Shule, Zahanati kufungiwa umeme wa sola bure

Afisa Uhusiano wa Steps Solar Ltd, Moses Mwanyilu (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza mpango wa kampuni yao kufunga vifaa vya kuzalisha umeme wa jua kwa baadhi ya shule, zahanati na vituo vya Polisi.
SHULE  za Sekondari mbili pamoja na Zahanati nne zilizopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam zinatarajiwa kufungiwa vifaa vya kuzalisha umeme wa jua bure ili kuwarahisishia watumiaji wa taasisi hizo kuwa na uhakika wa kupata nishati ya umeme kwa saa 24 za kila siku.
Ufungwaji huo pia utahusisha vituo vya kulele yatima, ofisi za serikali pamoja na vituyo vya Polisi na utafanywa na kampuni ya kusambaza vifaa vya umeme wa jua, Steps Solar.
Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Moses Mwanyilu aliliambia gazeti hili kuwa, shule zitakazonufaika na mradi huo wanaoufanya Steps na TAREA ni Kidete na Kibugumo, wakati Zahanati ni za Kibugumo, Mji Mwema, Tuangoma na Homboza, huku vituo vya kulelea yatima vitakavyofungiwa vifaa hivyo vya kuzalisha umeme wa jua ni Ungindoni, Mji Mwema , Miti Mirefu na Yatima Charity vyote vilivyopo Kigamboni, wilaya ya Temeke.
Mwanyilu alivitaja pia vituo vya Polisi vya Mjia Mwema na Chanika pamoja na ofisi za serikali za Mji Mwema na Feri navyo pia vitanufaika na mradi huo wenye lengo la kurejesha shukrani zao kwa jamii, sambamba na asasi hizo kuwa na uhakika wa umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za umeme na hata yale yenye umeme kujihakikisha kuipata nishati hiyo kwa saa 24.
"Kwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya watanzania hawapati huduma ya umeme Steps na TAREA tukiwatumia mabalozi wetum Jacob Stephen, Irene Uwoya na Athuman Amri 'King Majuto' tunatarajia kufunga vifaa vya kuzalisha umeme wa jua katika asasa tulizotaja ambazo zitatugharimu kati ya Sh. Mil. 20-30," alisema Mwanyilu.
Aliongeza, kampuni yao ya kuzalisha vifaa vya umeme jua iliasisiwa mwaka jana, na kudai pamoja na kuuza na kusambaza vifaa hivyo alivyoviiuta vya Umeme Nuru, pia wamepania kugawa vifaa na ufungaji bure katika maeneo mbalimbali ya Tanzania hasa yasiyokuwa na uhakika wa umeme, ambayo yataambatana matamasha ya sanaa na elimu pamoja na kugawa zawadi kwa washiriki watakaokuwa wakijibu maswali ya papo kwa papo.
"Lengo ni kutaka kuona mpaka miaka mitano ijayo asilimia kubwa la watanzania wanakuwa wakiwa na uhakiki wa kupata nishati ya umeme na kuwarahisishia shugfhuli zao za kimaendeleo," alisema.

DC Mkuranga akabidhi nyumba kwa wasanii

Moja ya nyumba walizokabidhiwa wasanii juzi na DC wa Mkuranga Mercy Silla
MKUU wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Silla ameahidi kusaidia kijiji cha wasanii cha Mwanzega wilayani hapa kujengewa barabara, kupata umeme na kuchimbiwa kisima cha maji.
Akizungumza katika sherehe za kukabidhi nyumba 26 za awamu ya pili kwa wasanii wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) iliyofanyika kijijini hapo jana, Mkuu wa wilaya alisema Serikali ya wilaya imeona juhudi za dhati za wasanii kuanzisha kijiji cha kisasa kwa ajili makazi na kilimo hivyo Serikali haiwezi kukaa kimya.
Alisema uwekezaji huo ni mkubwa na kuwataka wasanii kumalizia nyumba zao wahamie na kuahidi kuomba mamlaka husika kukisajili kiwe kijiji chenye uongozi uliokamilika.
Mkuu wa wilaya silla, alishauri SHIWATA kuandika barua Halmashauri ya Wilaya Mkuranga kuomba kupimiwa eneo hilo la makazi lenye hekari 300 ili kupata hati itakayowasaidia kukopa mikopo ya kujiendeleza.
Alimuomba Diwani wa Kata ya Mbezi atumie fursa aliyonayo kuomba Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kufungua barabara ya kwenda kijiji cha wasanii Mwanzega ili ifikike kwa urahisi.
Mkuu huyo pia aliwashauri wasanii hao kuomba Mradi wa Umeme Vijijini (REA)kuingiza umeme kijijini hapo ili kuraahisisha maendeleo ya kijiji hicho nakuahidi kutafuta wawekezaji watakaochimba kisima kirefu.
Alishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni vijana na Michezo kushirikiana na wasanii katika mipango yao ya kujenga nyumba za wasanii.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Mkuranga, Thobias Mapalala aliwaahidi wasanii wasitie hofu kuhusu usalama wa mali zao kwa sababu ulinzi unaimarishwa.
Awali Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Cassim Taalib alisema jumla ya nyumba 59 zimekabidhiwa kwa wasanii kati ya 262 wanaochangia ujenzi wa nyumba Mwanzega, Mkuranga.
SHIWATA inamiliki eneo la hekqari 300 kwa ajili ya kujrnga makazi ya waasanii na hekari 500 kwa ajili ya kilimo kwanza wilayani Mkuranga.

'Wasanii kuweni wabunifu mteke soko la kimataifa'

Vitalis Maembe
WASANII nchini wamekumbushwa kuwa wabunifu zaidi na kuvuka mipaka ya nchi ili kuweza kujitangaza katika anga la kimataifa badala ya kuridhika kutamba nyumbani tu.
Wito huo umetolewa na mwanamuziki mahiri, Vitalis Maembe alipokuwa akizungumza na wasanii wa Kaole Sanaa hivi karibuni ambapo alisema umefika wakati wasanii wakaacha kujiangalia wenyewe kwa wenyewe nchini na badala yake kutupa macho nje na kutoa vitu vitakavyowatangaza wenyewe na taifa kwa ujumla.
Staa huyo wa nyimbo za 'Sumu ya Teja' na 'Kariakoo' alisema soko la kimataifa lina manufaa makubwa kwa wasanii kama wakiamua kulichangamkia na kuwasisitiza wajikite kwenye ubunifu na hasa kulenga vionjo vya Kitanzania kurahisisha utambuzi wa kazi hizo.
"Ubunifu na hasa utakaojikita kwenye vionjo vya Kitanzania ili kujitofautisha na kazi za wengine ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa na mimi nipo tayari kuwasaidia yeyote mwenye kuhitaji msaada wangu, ilimradi kusogeza mbele gurudumu la sanaa Tanzania," alisema.
Maembe aliwamwagia sifa kundi la Kaole kwa namna walivyoibua wazo la kurejesha kundi hilo lililoanzisha mwaka 1996 na kutamba na michezo yao mbalimbali kwenye vituo vya ITV na TVT kabla ya kutoweka baada ya nyota wake kujitosa kwenye uigizaji wa filamu.

Dar Modern waachia video yao mpya

Hassan Vocha, mmoja waimbaji wa Dar Modern Tarab
Sikudhani Ally, muimbaji mwingine wa kundi la Dar Modern
KUNDI la muziki wa taarab la Dar Modern 'Wana wa Jiji' wanatarajia kuitoa hadharani video ya albamu yao mpya ya 'Ngoma Imepasuka' huku wakijiandaa kuanza ziara mikoani kwa ajili ya kulitambulisha kundi hilo, sambamba na albamu zao mbili walizozizindua jijini Dar es Salaam Siku ya Wapendanao.
Akizungumza na MICHARAZO, mkurugenzi wa kundi hilo Hassan Bakar alisema kuwa video ya albamu hiyo itaingizwa sokoni kuanzia leo, huku ile nyingine ya 'Ooh My Honey' wakiiweka kiporo kwanza kwa kuhofia kuwakanganya mashabiki wao kama wangetoa video za albamu hizo mbili kwa mpigo.
Bakar alisema tayari baadhi ya video vya albamu hiyo zimeshaanza kurushwa hewani ili kuwaonyesha mashabiki uhondo uliopo katika albamu hiyo yenye nyimbo sita na nyimbo zake kuimbwa na nyota wao, Hassani Vocha, Mwanahawa Ally, Sikudhani Ally na wengine wanaounda kundi hilo lililorejea upya baada ya ukimya mrefu.
"Video ya albamu yetu ya 'Ngoma Imepasuka' itaachiwa Jumatatu, ingawa baadhi ya nyimbo tumeshasambaza na kurushwa na vituo vya runinga na sasa tunajipanga kwa ajili ya kuanza maonyesho ya mikoani kuzitangaza albamu hizo," alisema.
Bakar alisema wakati video yao ya albamu yao ya kwanza ikitoka pia kundi hilo lipo kwenye maandalizi makali kwa ajili ya onyesho maalum la 'Usiku wa Mwambao Asilia' ambalo watajumuika pamoja kutoa burudani na kundi la Naddi Ikhwan Safaa (Malindi).
"Tupo kwenye mandalizi makali ya onyesho hilo la Usiku wa Mwambao Asilia dhidi yetu na Malindi, ambapo mashabiki watapata kushuhudia taarab asilia ilivyo sambamba na kuwashuhudia magwiji wa miondoko hiyo kama Mohammed Elias," alisema Bakar.
Onyesho hilo litafanyika Aprili 19 kwenye ukumbi maarufu uliopo Magomeni, ambapo Dar Modern na Malindi watapiga nyimbo zao za zamani na mpya.

Ridhiwani Kikwete ashinda Chalinze, lakini...?!Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akimnyanyua mkono Ridhiwani Kikwete kuashiria ushindi kwa chama hicho.
Habari zilizotufikia zinasema kwamba, mgombea wa CCM, Ridhiwani Kikwete ameibuka mshindi katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Chalinze.
Matokeo ya ushindi kwenye Kata zote 15, yanamfanya Ridhiwani bila shaka yoyote kuwa Mbunge mpya wa jimbo hilo.
Hadi tunakwenda mitamboni, Ridhiwani alikuwa akiwatimulia vumbi wapinzani wake kwa kujikusanyia zaidi ya kura 23,612 ambazo ni sawa na zaidi ya asilimia 84.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa CCM kuwabwaga wapinzani wao wakuu, Chadema baada ya Geofrey Mgimwa kushinda kiti cha ubunge Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja. Hata hivyo inadaiwa asilimia kubwa ya wapiga kura wameukacha uchaguzi huo kwani waliotarajiwa kupiga kura ni 90,000 kwa maana hiyo ni kama watu 70,000 wamechomoa na hivyo pamoja na Kikwete kushinda, lakini wengi ni kama 'wamemchomolea' kiaina
Kwa taarifa zaidi endelea kuperuzi MICHARAZO. Yafuatayo ni matokeo ya mwisho kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura:-
Talawanda: CCM (1,192), CHADEMA (104), CUF (4).
Msoga: CCM (1,248), CHADEMA (68), CUF (9)
Lugoba: CCM (1,594), CHADEMA (174), CUF (4)
Kiwangwa: CCM (1,180), CHADEMA (80), CUF (14)
Kibindu: CCM (1,131), CHADEMA (300), CUF (3)
Fukayosi: CCM (1,105), CHADEMA (69), CUF (17)
Mandela: CCM (1,394), CHADEMA (112), CUF (8)
Mbwewe: CCM (1,319), CHADEMA (166), CUF (23)
Pera: CCM (1,139), CHADEMA (49), CUF (19)

Monaco bado yakomaa na PSG Ufaransa