STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 22, 2012

Ramadhani Singano: Messi wa Simba anayemzimia Boban

<
KIPAJI kikubwa cha soka alichonacho hasa kumiliki mpira, kupiga chenga, mbio na kufunga, kimemfanya kinda la timu ya Simba, Ramadhani Singano kufananishwa na nyota wa Barcelona, Lionel Messi. Wadau wa soka hasa wa klabu ya Simba humfahamu zaidi kwa jina la Messi kuliko majina yake halisi, wakimlinganisha kiuchezaji na nyota huyo wa Argentina anayetajwa kama mwenye kipaji cha pekee duniani. Licha ya kufurahia jina hilo, Singano anakiri hajafikia hata robo ya umahiri wa Messi anayemhusudu na kumuiga uchezaji wake. Singano, aliyewapoteza wazazi wake akiwa na miaka 11, alisema anamshukuru Mungu kwa kumjalia kipaji hicho, ila anaamini ana kazi kubwa ya kufika alipo 'wajina' wake. Hata hivyo, Messi aliyeanza kucheza kama beki enzi za soka la chandimu, alisema nidhamu, mazoezi, kujituma na kumtumainia Mungu kutamfikisha mbali kisoka. "Naamini nikijituma zaidi, nikazingatia nidhamu na kumtanguliza Allah, katika kila kitu, nitafika mbali kwani najiamini naweza," alisema. Messi, alizichezea timu za Ubatani na Bombom kabla ya kuonwa na Simba B, alisema japo hana muda mrefu katika soka, anashukuru mafanikio aliyopata. "Soka limenisaidia mengi kimaisha na kiuchumi, ila sipendi yaandikwe, lakini kufahamika, kuheshimiwa na kumudu kuwasaidia ndugu na jamaa zangu, ni vitu vya kujivunia," alisema. Pia, alisema kutwaa mataji, medali na tuzo mbalimbali akiwa na Bombom na Simba B, ikiwemo kuwa Mchezaji Bora mara tatu katika michuano ya Rolling Stone, Uhai Cup na Copa Coca Cola 2009 ni mengine yanayomfariji. "Mwaka jana pekee nimetwaa mataji mawili ya Uhai na Kinesi nikiwa Simba B na msimu huu nimesherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara nikiwa na Simba," alisema. Messi, anayemzimia na kuvutiwa na soka la Haruna Moshi 'Boban', alisema hakuna tukio la furaha kwake kama alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mchezaji bora wa michuano ya Uhai-2009. "Furaha niliyokuwa nayo ilinifanya nigawe fedha za zawadi kwa wachezaji wenzangu wa Simba B, nakumbuka nilitoa Sh. 150,000 kati ya 400,000," alisema. Kwa matukio ya huzuni, Messi alisema ni kuwapoteza wazazi akiwa mdogo na kunusurika kufa kwa ajali ya gari alipotoka kumzika baba yake mjini Tanga mwaka 2003. Mchezaji huyo anayependa kula mihogo ya kuchemsha, ugali kwa bamia na kunywa juisi ya Parachichi, alisema hupenda kutumia muda wake mwingi kufanya ibada na kuangalia 'muvi' hasa za filamu za Jean Claud van Damme. Aliwashukuru makocha wake, Ahmed Mohammed Kibonge, Teddy na Bosco waliokivumbua na kukiendeleza kipaji chake kiasi cha leo kuonekana 'lulu'. "Nawashukuru mno hasa Kibonge aliyetambua kipaji changu wakati anasoma Shule ya Sekondari Al Farouk na kunipeleka katika timu yake ya Bombom." Alisema, Simba B ilivutiwa naye baada ya kung'ara katika mechi dhidi ya Bombom na kusajiliwa katika kikosi hicho mwaka 2009 na kuja kupandishwa timu ya wakubwa msimu huu akiwa na wenzake wanne. Messi, anayemudu karibu nafasi zote dimbani, japo hufarahia kucheza kama mshambuliaji, alisema hawezi kuzisahau mechi mbili akiwa na Simba dhidi ya Azam na Kiyovu Sport ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika. "Nazikumbuka kwa vile zilizokuwa mechi kubwa za kwanza kwangu na namna nilivyoonyesha kiwango cha hali ya juu nikisaidia moja ya mabao mawili ya ushindi dhidi ya Azam katika Ligi Kuu," alisema. Mkali huyo anayeota kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuanzisha asasi ya kusaidia yatima na wenye matatizo, alisema soka la Bongo lipo juu, ila baadhi ya wachezaji hawajitambui na kuchangia kulikwamisha. Alisema huenda kukosa misingi bora ya soka ni tatizo kwa wachezaji nchini, ila aliwataka wazinduke na kutambua soka ni ajira yao hivyo walitumikie kwa ufanisi ili wafike mbali kama nyota wa mataifa mengine ni tatizo. Pia, alidai tabia ya wadau kuwaingilia kazi makocha na kuwakatisha tamaa wachezaji ni tatizo jingine, sawa na kukosekana kwa wadhamini katika soka la vijana. Alisema angekutana na Rais, licha ya kumuomba aboreshe miundo mbinu na huduma za jamii, angemsihi pia atumie nafasi yake kushawishi wawekezaji na wafadhili kuangalia soka la vijana na timu nyingine ndogondogo. Ila yeye angelikuwa ni Rais, angeboresha huduma za jamii hasa elimu na kuwekeza katika michezo akidai ni njia nzuri ya kusaidia ajira kwa wengi. Kuhusu Stars, alisema timu hiyo inashindwa kufanya vema kutokana na tabia ya u-Simba na u-Yanga inayoendekezwa na wadau wakiwemo hata wachezaji, pia kuingiliwa kazi kwa makocha wa timu hiyo. "Tunaweza kufuzu fainali za Afrika na Dunia, kama wadau wataacha u-simba na u-yanga unaowaathiri hata wachezaji, pia makocha waachiwe wafanye kazi na timu ziandaliwe vema," alisema. Shabiki huyo wa Manchester United anayechizishwa na nguo za rangi yoyote, alisema anaamini kila mmoja akitimiza wajibu wake katika klabu au timu ya taifa, Tanzania zitaweza kutamba kimataifa. Ramadhani Yahya Singano, alizaliwa Desemba 31, 1992 akiwa ni mtoto wa mwisho wa familia ya watoto sita wa Yahya Singano mwenyeji wa Tanga akitanguliwa na kaka wanne na dada mmoja. Shule ya Msingi alisoma Mgulani kati ya mwaka 2000-2006 kabla ya kusoma kama yatima katika Shule ya Sekondari Al Farouk alipozidi kung'ara katika soka baada ya awali kuanza kucheza akiwa darasa la nne. Chandimu alilichezea timu ya G Spar Kavela, kabla ya kutua Ubatani akicheza nao michuano ya mchangani kisha kusajiliwa Bombom na baade Simba B. Kwa upande wa timu za taifa, alianza kuchezea timu za vijana U17 na U20 tangu 2010 kabla ya wiki iliyopita kuitwa Taifa Staras na kocha Kim Poulsen. --------------------

Doyi Moke: Kipa wa zamani aliyejitosa kwenye biashara ya madini

TANGU alipostaafu baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa, kipa wa zamani wa timu za Majimaji ya Songea, Simba na Yanga, Doyi Moke, amewekeza nguvu zake katika biashara za kununua na kuuza madini katika nchi za Afrika. Nyota huyo aliyeibebesha taji la ubingwa wa Ligi ya Muungano, Majimaji mwaka 1997, alisema amejikita katika shughuli hiyo kwa fedha za soka. Alisema japo soka halikumpa fedha nyingi, lakini kidogo alichopata aliweka akiba inayomfanya leo aishi maisha mazuri akifanya biashara hiyo ya madini akishirikiana na nduguze. Moke, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyeanza kucheza soka tangu Shule ya Msingi na kucheza soka la kulipwa akiwa na miaka 17 tu katika timu ya Muungano ya Bukavu, anauza madini chini ya kampuni yake. Kampuni hiyo inaitwa GFK Limited, yeye akiwa ndiye Mkurugenzi akinunua madini kama almasi na dhahabu toka Kongo na kuuza Tanzania na nchi nyingine za Afrika na kumfanya awe mtu wa kusafiri. Moke alisema kabla ya kufanya biashara hiyo alijikita katika biashara nyingine mara alipotundika daluga mwaka 2003 hata hivyo hazikumlipa kama biashara yake ya sasa. Mkali huyo aliyewahi kuwika pia na timu za Aspwara, Rayon za Rwanda na Afya Sport ya Goma, alisema ni vema wachezaji wa sasa wakawa makini na kile wanazovuna katika soka kwa ajili ya manufaa ya ya baadae. "Tulipokuwa tukicheza fedha hazikuwepo kama leo, hata hivyo baadhi yetu tulikuwa na fikra za mbali ndio maana leo tunaishi vema, kwa wanaocheza sasa ni wajibu wao kukumbuka kesho yao kwa kujiwekea akiba," alisema. ALIPOTOKA Doyi Moke alizaliwa Oktoba 4, 1967 Bukavu nchini Zaire, sasa Kongo akiwa ni mtoto wa sita kati ya 10 wa familia yao. Shule ya Msingi aliisoma College Alfajiri kisha Atenend Banda Sec kabla ya kusomea Diploma ya Lugha ya Kifaransa. Kisoka alianza kucheza tangu kinda akidakia timu za shule na kutwaa nao mataji ya mashindano ya shule nchini mwao, akimtaja kocha Gabie Mugimbi kuwa ndiye aliyekivumbua kipaji chake. Moke alikiri alimvutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Ufaransa Michel Platin na kuitaja klabu yake ya kwanza ya kulipwa kuwa ni Muungano aliotwaa nao taji la Ligi ya Mkoa wa Bukavu mwaka 1987. Baada ya kung'ara na timu hiyo kocha wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu alimuona na kumpeleka Rwanda kuichezea ASPWARA 1989 kabla ya kutua Rayon Sport kwa muda na kurudi Kongo kuichezea Afya ya Goma. Alitua baadae Vital'O ya Burundi na kufanya mambo makubwa akiwapiku makipa wanne aliowakuta kikosi ikiwemo mmoja, Ramadhani Ally aliyemsusia jezi alipopewa nafasi mara ya kwanza kikosini. Alisema anakumbuka kocha alimpa nafasi katika mechi dhidi ya wapinzani wao Port Louis walioifunga mabao 2-0 na kujihakikishia namba akiipa ubingwa na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika 1992. Alisema aliachana na Vital'O mwaka 1995 aliposhuhudia mchezaji mwenzake, Kamala Jeff akipigwa risasi na waasi wa Burundi mpakani mwa nchi hiyo na Kongo na kuamua kuachana na soka ili aende Afrika Kusini kusaka maisha. "Hata hivyo nilipofika Tanzania nikielekea 'Bondeni', nilikutana Mackenzie Ramadhani aliyenishawishi kuendelea na soka na kunikutanisha na kocha Nzoysaba Tauzany, aliyenisajili kuichezea timu yake ya Majimaji," alisema. Alisema hakuamini alipopokelewa kama 'Mfalme' mjini Songea na viongozi wa mkoa akiwemo RC, ambaye kwa sasa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaja dau alilosajiliwa likiwa Sh 700,000. Baada ya kuipa ubingwa wa Muungano kutokana na kumaliza Ligi ya Tanzania Bara wakiwa watatu nyuma ya Yanga na Simba, mwaka 1999 alihama na kutua Simba alioichezea kwa mafanikio kabla ya kusajiliwa Yanga. Alisema aliamua kuachana na Simba baada ya 'kuzikwa' fedha zake za usajili na mmoja wa viongozi (jina kapuni) na kuhamia Yanga mwishoni mwa mwaka 2000 na kuichezea hadi mwaka 2003 alipoenda Rayon Sport na kustaafu huko. Alisema tangu alipostaafu amekuwa mshauri kwa klabu ya Yanga na wachezaji wanaocheza sasa, pia akimpiga tafu shemejie, Henry Kalekwa anayemiliki timu ya Sofapaka ya Kenya. Moke anayependa kula wali kwa kisamvu na kunywa bia ya Safari, alisema kati ya klabu zote alizochezea, Vital'O na Yanga ndizo bomba kwake. Alisema mbali na kuichezea, pia yeye ni mshabiki mkubwa wa Yanga, Arsenal na TP Mazembe, huku akidai anapenda kuogelea na kubadilishana mawazo. HUJUMA Moke aliyemtaja Mbwana Samatta anayecheza TP Mazembe kama 'nembo' ya Tanzania katika soka la kulipwa kwa kipaji kikubwa alichonacho, alisema ndani ya soka amekumbana na mambo mengi. Alitaja mojawapo ni tuhuma alizodai kubambikiwa klabu ya Simba akidaiwa kuihujumu timu hiyo dhidi ya Yanga katika mechi iliyochezwa mwaka 2000 ambapo Yanga walishinda 2-0 kwa mabao ya 'Bwana Harusi' Idd Moshi. "Jambo hilo linaniuma hadi sasa na ndilo lililonifanya niichukie Simba kwa vile uongozi uliamua kunipakazia baada ya kuumbua kwa wanahabari juu ya kunizika fedha zangu za usajili," alisema. Juu ya mechi ngumu, Moke, alisema ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 akiichezea Yanga na Highlander ya Zimbabwe lililochezwa Harare ambapo Yanga ilishakata tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani. "Naikumbuka kwa namna nilivyowaapia wanayanga waliokata tamaa na kutishwa na kauli ya kocha wa Highlander aliyetutaka tusisumbuke kuwafuata kwao kwa maana tulikuwa tunajisumbua tu," alisema. Alisema hata hivyo aliwapa moyo wenzake na kwenda kufanya vitu adiumu uwanjani na kuisaidia Yanga kushinda mabao 2-0 na kusonga mbele. Moke aliyemhofia Mohammed Husseni 'Mmachinga', alisema soka la Bongo, litasonga mbele iwapo nyota wa zamani watapewa nafasi za kuongoza klabu na FA badala ya 'wavamizi' wanaotambia elimu zao kubwa. Alisema wengi wa viongozi waliojipenyeza kwenye soka wanafanya hivyo kwa kusaka masilahi ikiwemo umaarufu wa kugombea nafasi za kisiasa, huku wakiliacha soka likiporomoka. "Ni kweli elimu ni kitu cha muhimu, ila wachezaji wa zamani wana umuhimu katika kuinua soka la Tanzania, watumiwe kama wenzetu wanavyowatumia wachezaji wao," alisema. Moke anayesikitishwa na kifo cha baba yake kilichotokea akiwa na miaka 13 tu, ameoa na ana watoto wawili, pia aliwashukuru mama yake mzazi kwa jinsi alivyomlea na kumuongoza hadi kufika alipo, sambamba na Rashid Haradee na marehemu Tauzany. Aliwaasa wachezaji kujituma na kutambua soka ni ajira lao, sambamba na kuzipigania klabu na timu za taifa pale wanapozichezea ili kuzisaidia na kujitangaza vema kimataifa. --------------------

Stanley Msungu: 'Seneta' anayemzimia Ramsey Nouah

INGAWA filamu ya 'Second Wife', aliyoigiza na 'Ray' ndio inayoonekana kama iliyomtambulisha kwa mashabiki, ukweli ni kwamba msanii Stanley Msungu, alishaanza kuonyesha makeke yake kitambo kirefu katika fani hiyo ya uigizaji. Msanii huyo anayefahamika kisanii kama 'Seneta Msungu', tangu akiwa shuleni alikuwa mahiri katika fani hiyo sambamba na uchezaji wa ngoma na uimbaji na alishauza sura katika michezo kadhaa ya runinga kupitia kituo cvha ITV akiwa na kundi la Amka Sanaa. Miongoni mwa michezo hiyo iliyodhihirisha kipaji cha msanii huyo ambaye pia ni mahiri katika muziki akiwa ameshafyatua nyimbo tatu mpaka sasa ili kutoa albamu kamili ni pamoja na 'Lulu', 'Safina' na 'Dunia'. Mwenyewe alisema michezo hiyo ilimpa uzoefu wa kutosha katika uigizaji na haikuwa ajabu kwake kuamua kujiengua katika kundi hilo na kutumbukia kwenye uigizaji za filamu kazi yake ya awali kabisa ikiwa ni Last Minutes iliyotoka miaka minne iliyopita. "Baada ya kujiona nimeiva na hali ilivyokuwa katika kundi letu, niliamua kujiengua na kujitosa kwenye filamu na kazi ya kwanza kucheza ni Last Minutes kabla ya kufungukiwa neema kwa kucheza filamu zinazokaribia 30 kwa sasa," alisema. Msungu, aliyetumbukia kwenye uigizaji kutokana na kuvutiwa na Ramsey Noauh wa Nigeria, alisema baada ya Last Minutes, alicheza filamu za Peace of Mind, Devorce, Devil's Kingdom, Moses, Ndoa Yangu, I Hate My Birthday, The Shell, Shortcut na sasa akitamba na Rude, moja ya kazi binafsi za mwanadada Jenifer Kyaka 'Odama'. Mkali huyo, aliyewahi kung'ara katika soka akiichezea timu yake ya shule na zile mtaani, alisema kati ya kazi zote alizocheza, filamu za Moses, Devil's Kingdom aliyoigiza na marehemu Steven Kanumba na Ramsey Nouah, Rude na Second Wife ndizo kali kwake. Alisema wakati alipoitwa kwenda kucheza filamu ya Devil's Kingdom alikaribia kuzimia kutokana na kushindwa kuamini kama angeigiza na Ramsey Nouah anayemhusudu mno. "Sio siri Kanumba ni kama alinifanyia 'surprise' kwa kunipa taarifa ya ghafla kwenda kuigiza na hata nilipofika na kuonana uso kwa uso na Ramsey sikuamini. Kwa kweli namzimia mno huyu jamaa na anaweza kazi," alisema. KIFO Msungu, aliyezaliwa mwaka 1979 wilayani Lushoto, mkoani Tanga akiwa mtoto wa kwanza kati ya sita wa familia yao, alisema wakati tukio la kukutana na Ramsey likiwa ni furaha kwake, kwa upande wa huzuni yapo mambo makuu mawili. Moja alisema kifo cha wazazi wake, na kunusurika kwake kuuwawa kwa risasi katika tukio la uhalifu lililowahi kutokea eneo la Kigamboni. Alisimulia, Msungu alisema alishawishiwa na rafiki zake aliokuwa akiwaonea wivu kwa namna walivyokuwa 'mambo safi' na kumueleza kama anaweza aungane nao kusaka fedha bila kujua kama walikuwa wezi. "Siku moja wananiambia niambatane nao kwenda kuvuna fedha na kuibukia TIPPER ambako kabla sijajua kilichoendelea tulijikuta tukivamiwa na kuwekwa chini ya ulinzi na askari wenye silaha. Kwa kweli nilitahayari mno," alisema. Alisema askari aliyemwelekezea silaha, alimwambia akisogea hatua moja tu, angemlipua risasi, lakini kwa ujasiri na kukata kwake tamaa, alimwambia askari yule kama ni risasi basi ampige ya kichwa ili afe mara moja. "Nilimweleza mie sikuwa mhalifu ila niliwafuata wenzangu bila kujua kama ni wezi, hivyo ni bora aniue kwa kunitwanga risasi ya kichwa badala ya kwingine nikihofia kuwapa tabu wadogo zangu niliokuwa nawatunza," alisema. Alisema aliyatamka hayo huku akitembea kuelekea baharini akiamini askari yile angemuua, cha ajabu alikuja kuzinduka keshoye akiwa majini alfajiri bila jeraha lolote ilihali mwanzoni aliamini alikuwa amekufa. Alidai tangu tukio hilo, alishika adabu na kuwaepuka rafiki zake hao na kuamua kuhangaika kwa kutumia vipaji vyake vya uigizaji na muziki. Msungu anayependa kula ugali kwa bamia au wali kwa njegere na kunywa juisi, alisema japo hajanufaika sana na sanaa, lakini anashukuru fani hiyo imemsaidia kwa mengi kimaisha. "Sina cha kujivunia, ila nashukuru sanaa imenisaidia kwa mengi na jinsi fani inavyozidi kukua naamini nitafika mbali kimaisha, na kutimiza ndoto za kuwa mtayarishaji na kumiliki kampuni binafsi ya filamu," alisema. MUZIKI Msungu, anayezishabikia timu za Yanga, Barcelona na Liverpool, akiwazimikia nyota wa timu hizo, Haruna Niyonzima, Lionel Messi na Luis Suarez, alisema baada ya kutamba kwenye filamu sasa amehamishia makali kwenye muziki. Alisema mpaka sasa amepakua nyimbo tatu, ya kwanza ikiendelea kutesa kwenye runinga unaoitwa 'Unanitesa' alioimba na Milan wa Bana Marquiz, 'Nalia' na mapema wiki hii alirekodi kibao kiitwacho 'Mikosi'. "Lengo langu kabla ya mwisho wa mwaka huu niwe nimeshatoa albamu kamili itakayokuwa na nyimbo nane za miondoko mchanganyiko ya Zouk na Kwaito," alisema. Alidokeza atakuwa akisambaza video za nyimbo hizo tu kabla ya kutoa 'audio' baadae ili kuepuka 'kuchakachuliwa' na baadhi ya wajanja wanaiba kazi za wasanii. Msungu anayewakubali waigizaji kama Sajuki, marehemu Kanumba, Ray, Gabo, Odama, Riyama Ally na Jackline Wolper, alisema ili wasanii wa Tanzania wafike mbali ni lazima wapendane, kushirikiana na kuwa wa moja. "Sio siri wasanii wengi nchini hatupendani na tunaendekeza majungu na unafiki vitu ambavyo sio vizuri kwa maendeleo ya sanaa zetu," alisema. Alisema, pia ni vema wasanii hasa watayarishaji na waigizaji wa filamu kuwa wabunifu kwa kutunga visa vinavyorandana na mazingira ya Tanzania. "Tubuni kazi zinazoendana na uhalisi wa maisha wa watanzania, pia serikali itusaidie na kuturuhusu kutumia maeneo yatakayoitangaza nchi," alisema. Alisema wasanii wanapotaka kuigiza katika maeneo yatakayotoa uhalisia wa simulizi la kazi zao, hupata usumbufu na kuchangia kazi nyingi kulipuliwa na kutokuwa na uhalisia wa mambo. Msungu aliyepania kuja kuwasaidia vijana wenye vipaji, alisema kuna haja pia ya serikali kusaidia kukomesha wizi wanaofanyiwa wasanii katika kazi zao, sambamba na kutazama sanaa kama eneo la kupatia pato la taifa. Mkali huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya kahawia (brown), hajaoa ila ana watoto wawili ambao mmoja anasoma mjini Morogoro na mwingine Kigamboni anapoishi yeye. Mwisho

Bango la TFF kuhusu mapinduzi ya wazee wa Yanga

TAARIFA YA TFF KUHUSU MAPINDUZI YALIYOFANYIKA KATIKA KLABU YA YANGA SIKU YA JUMAPILI

Malawi njiani kuja kuivaa Stars

TIMU ya soka ya taifa ya Malawi inatarajia kuwasili nchini keshokutwa Alhamisi kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wenyeji wao Taifa Stars itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah, alisema jana jijini kuwa kikosi hicho cha Malawi kinatarajia kuja na msafara wa watu 27 na maandalizi ya mechi hiyo yako kwenye hatua za mwisho. Osiah alisema kuwa wanaamini mechi hiyo ya Jumamosi itakuwa ni kipimo sahihi kwa wachezaji wa Taifa Stars ambao wanakabiliwa na mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi dhidi ya Ivory Coast huko jijini Abdijan. Aliongeza kuwa wachezaji wa Taifa Stars walioko kambini wanaendelea na mazoezi chini ya kocha wao mpya, Kim Poulsen, na wote wanajua umuhimu wa mchezo huo wa kirafiki. "Tunafahamu Stars inakabiliwa na mechi ya ushindani, Malawi pia ni kipimo kizuri kwao, wenzetu wako juu katika viwango vya FIFA, ni mechi itakayotusaidia," aliongeza Osiah. Hata hivyo, wachezaji watatu kati ya 25 walioutwa Stars kwa sasa wanakosa kushiriki katika programu ya mazoezi inayoendelea ya kocha Kim Piulsen kutokana na kutokuwepo nchini. Wachezaji ambao hawako kambini ni pamoja na Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, ambao watatua nchini Jumatatu Mei 27 wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakoichezea TP Mazembe huku mwingine akiwa ni Haruna Moshi 'Boban' ambaye alikwenda Kinshasa kumzika kiungo wa Simba, marehemu, Patrick Mafisango, aliyezikwa juzi. Katika mechi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo za Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka 2014, Taifa Stars iliyokuwa chini ya kocha aliyemaliza mkataba wake, Jan Poulsen, ilitoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mechi hiyo ya Jumamosi ndio utakuwa mchezo wa kwanza kwa Kim kuiongoza Taifa Stars huku akiwa na matokeo mazuri na timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes. Chanzo:NIPASHE

Sita Simba hatarini kupigwa panga

HATMA ya wachezaji sita wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, iko shakani baada ya mikataba ya kuichezea klabu hiyo kumalizika huku kikao cha Kamati ya Usajili kilichofanyika juzi usiku kikishindwa kufikia maamuzi ya kuwapa mikataba mipya. Nyota hao ambao kanuni zinawaruhusu kufanya mazungumzo na klabu yoyote sasa ni pamoja na Ally Mustapha 'Barthez', Uhuru Suleiman, Juma Jabu, Juma Nyosso, Derick Walulya na Gervais Kago, ambaye ni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati. Uhuru alithibisha kuwa hana mkataba na Simba hivi sasa na yoyote anayemuhitaji milango iko wazi kumfuata. "Ila Simba ni zaidi, wamenisaidia sana (wakati alipovunjika mguu) siwezi kuwasahau," alisema kiungo huyo. Hata hivyo, wachezaji Mganda Walulya na Kago tayari wameshatupiwa virago na msimu ujao hawatavaa jezi tena za klabu hiyo, habari hizo zilisema. "Kago si mbaya ila ameshindwa kuendana na mfumo unaotumika sasa katika timu yetu ila bado timu yake ya taifa (Jamhuri ya Afrika ya Kati) inamuhitaji, Walulya amekuwa mzito na anashindwa kumudu kasi ya washambuliaji anaowakaba," alisema mmoja wa viongozi wa kamati ya usajili. Kiongozi huyo alisema kuwa kamati inaendelea kufanyia kazi ushauri kutoka katika benchi la ufundi la timu hiyo ili kuziba nafasi zenye mapungufu na hatimaye kufanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia mwezi ujao. Aliwataja wachezaji wapya waliosajiliwa kuwa ni mshambuliaji Abdallah Juma kutoka JKT Ruvu, kiungo mmoja wa DC Motema Pembe huku pia Simba ikipanga kwenda Uganda kumfuata Mussa Mude ambaye pia anawaniwa na Azam na Santos ya Afrika Kusini. Kamati ya Usajili ya Simba inaongozwa na mwenyekiti wake, Hanspope Zacharia, ambaye Ijumaa iliyopita alitarajia kumsainisha marehemu Patrick Mafisango, lakini mipango hiyo haikutimia kufuatia ajali iliyotokea asubuhi ya siku hiyo na kuchukua uhai wa kiungo huyo mkabaji aliyekuwa na uraia wa Rwanda. Wachezaji nyota wengine waliobaki akiwemo Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Mwinyi Kazimoto, Shomary Kapombe, Kevin Yondani, Haruna Moshi 'Boban', Salum Machaku, Felix Sunzu, Nassor Masoud 'Chollo', Amir Maftah na yosso kutoka Simba B waliopandishwa wote mikataba yao bado haijaisha. Chanzo;NIPASHE

TFF yawagomea wanachama wa Yanga, yadai haitambuii mapinduzi yao dhidi ya Nchunga

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa msimamo wake ni kuwa halitatambua maamuzi yoyote yanayofanywa na wanachama wake ambayo yako nje ya taratibu na maelekezo yaliyoainishwa katika katiba ya klabu hiyo. Kauli hiyo ya TFF imekuja kufuatia mkutano wa wanachama wa Yanga uliofanyika juzi Jumapili kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo walitangaza kuwa wamemuondoa madarakani Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Lloyd Nchunga, kwa madai kwamba ameshindwa kuwaongoza na anavunja katiba yao. Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa wanachama wote wanatakiwa kuheshimu na kulinda katiba za klabu yao na hawana budi kufuata katiba hizo katika kufanya mabadiliko ya uongozi endapo wana sababu ya kutekeleza maamuzi hayo. Osiah alisema kuwa hakuna mwanachama (klabu au vyama vya michezo) ambaye atafanya mabadiliko bila kufuata katiba na mabadiliko hayo yakatambuliwa. "Wasivuke taratibu kuanzia chini halafu wakafikiri wakija huku kwetu tutawatambua, tunasisitiza kuwa msimamo wetu ni kutotambua uongozi ambao utateuliwa kwa muda, hiyo ni kwa mujibu wa ibara ya 12 (2) ya TFF inavyoeleza," alisema Katibu huyo. Aliwataka wanachama kuwa na subira na kuwaeleza kwamba hakuna katiba inayokataa mabadiliko ya uongozi na wafahamu kwamba hakuna matatizo au migogoro itakayotatuliwa nje ya katiba. Alieleza kuwa tayari shirikisho limeshakutana na viongozi wa Yanga na kuwaeleza kwamba wakutane na upande wa pili ili kumaliza matatizo yao kwa njia ya busara kwa lengo la kuhakikisha wanajipanga kusajili wachezaji wenye uwezo na kufanya maandalizi ya kutetea ubingwa wao wa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 23 hadi Julai 8 mwaka huu. Naye mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga, alikielezea kilichofanywa na wanachama wa Yanga waliokutana Jumapili si jambo sahihi na anaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa ni kama 'sinema'. Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa wanachama wake wanatakiwa kuwa na subira endapo wanaitakia mafanikio klabu hiyo kongwe hapa Afrika Mashariki. Alisema kuwa Julai 15 sio mbali na Kamati yake ya Utendaji ilipanga siku hiyo kwa kuzingatia taratibu zilizoelezwa katika katiba yao kwa uongozi kuitisha Mkutano Mkuu. Aliongeza kuwa mkutano huo aliouitisha ni Mkutano Mkuu wa mwaka na agenda zake zimeelezwa katika Ibara ya 21 ya katiba ya Yanga. Aliwataka wanachama kuendelea na maandalizi ya kujitokeza katika mkutano huo aliouitisha huku akisema kwamba uongozi uko kwenye mchakato wa zoezi la usajili wa wachezaji na kusaka mrithi wa kocha Mserbia Kostadin Papic. Kwa mujibu wa katiba ya Yanga Ibara ya 17, Mkutano Mkuu ni ule tu ulioitishwa kwa kufuata utaratibu na ndio wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Na miongoni mamlaka ya mkutano huo kama yalivyoelezwa katika Ibara ya 19 kipengele cha (13) na (15), ni kubatilisha mamlaka ya mwanachama na pia kumsimamisha au kumfukuza mwanachama.

Mr Nice akamailisha albamu, atamba itamtoa

MSANII anayefurukuta kurejesha makali yake ya zamani, Lucas Mkenda 'Mr Nice' amekamilisha albamu yake mpya itakayofahamika kwa jina la 'Tabia Gani'. Albamu hiyo inatarajiwa kuingizwa sokoni muda wowote kuanzia sasa, itakuwa na nyimbo nane zilizoandaliwa chini ya mtayarishaji nyota, Lamar wa Fishcrab Records. Akizungumza na MICHARAZO, Mr Nice alisema albamu hiyo imekamilika na sasa wanafanya mipango ya kuiigiza sokoni baada ya kutambulishwa na vibao viwili vya 'Tabia Gani' na 'Nionje' alioimba na Muimbaji Bora wa Kiume nchini, Barnaba. Mr Nice alizitaja nyimbo zitakazokuwa katika albamu hiyo kuwa ni 'Tabia Gani' yenyewe, 'Nionje', 'Kupata', 'Maneno Maneno', 'Mfalme', 'Nionaje', 'Amini' na 'Ulisemaje'. "Kaka nimekamilisha ile albamu yangu mpya ya kunirejesha upya katika ulimwengu wa muziki baada ya kimya cha muda mrefu, itakuwa na nyimbo nane na kwa sasa najipanga na wasimamizi wangu ili kuiingiza sokoni," alisema. Mr Nice, alisema kwa namna albamu hiyo ilivyoandaliwa na Lamar, huenda akarejesha heshima na makali yake yaliyomfanya abatizwe jina la 'Mfalme wa TAKEU'. "Ni moja ya kazi yenye kiwango cha hali ya juu, si unajua makali ya Lamar na ukichanganya na vionjo vyangu vya 'TAKEU Reloaded', sina shaka itabamba sokoni," alisema. Mr Nice, aliyevuma miaka saba iliyopita na nyimbo matata kama 'Fagilia', 'Kikulacho', 'Friday Night', 'Bwana Shamba' na nyingine, ameibuka upya baada ya kushindwa kusimama hata alipojitosa kwenye muziki wa Injili alipotoa albamu ya 'Fungu la Kukosa'.

Viuno vya Shilole hadharani

NYOTA wa filamu aliyetumbukia kwenye fani ya muziki, Zuwena Mohammed 'Shilole' amefyatua wimbo mpya uitwao 'Viuno kwa Viuno' ameanza kuusambaza jana Jumatatu. Kisura huyo, alisema kibao hicho ambacho ni cha tatu kwake baada ya awali kuachia 'Lawama' na 'Dume Dada' vinavyokimbiza nchini kwasasa, ameshirikiana kuimba na wakali Kalidjo Kitokololo wa Fm Academia na Rich Mavoko. Shilole, alisema amepanga kuusambaza katika vituo mbalimbali vya redio leo ili uanze kuchezwa hewani, huku akijipanga kuachia nyimbo nyingine kwa ajili ya kuhitimisha albamu aliyopanga iwe na nyimbo sita au nane. "Nimekamilisha kibao kipya kiitwacho 'Viuno kwa Viuno ambao nadhani nitaanza kuusambaza redioni siku ya Jumatatu (jana ili uanze kurushwa hewani," alisema. Shilole, alisema anaamini kama ilivyokuwa kwa nyimbo zake mbili za awali, hata 'singo' hiyo itawabamba mashabiki kutokana na namna ulivyoandaliwa na kazi kubwa iliyofanywa nae na wasanii alioshirikiana nao. "Nataka kuwathibitishia mashabiki wangu, sijavamia fani, bali nauweza muziki kwa vile ni kipaji cha kuzaliwa licha ya kwamba naonekana ni mkali zaidi katika filamu," alisema. Mwanadada huyo, ambaye hujishughulisha na ujasiriamali, alisema mbali na kujipanga kutoa albamu pia anaendelea na maandalizi ya kupakua filamu zake binafsi.

Warembo Redd's Miss Bagamoyo waanza kambi Dar

WAREMBO 10 waliojitokeza kushiriki kinyang'anyiro cha kumsaka kisura wa Bagamoyo 'Redd's Miss Bagamoyo 2012', wameanza rasmi kambi ya mazoezi jijini Dar. Mkurugenzi wa Asilia Decoration inayoratibu shindano hilo, Awetu Salim, alisema warembo hao wameanza kambi katika ukumbi wa Meridian Hotel, iliyopo Kinondoni tayari kujiwinda na mchuano huo utakaofanyika Juni 15, mjini Bagamoyo, Pwani. Awetu, alisema kambi hilo ilianza Jumapili na itaendelea hadi siku ya shindano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Sanaa, TaSUBA- Bagamoyo. Mratibu huyo aliwataja baadhi ya warembo hao watakaokuwa chini ya mkufunzi wao Sadah Salim kuwa ni Julieth Jeremiah, Rose Lucas, Beatrice, Rachel, Celine Wangusu na Maria. Aliongeza, kwa kushukuru kujitokeza zaidi kwa wadhamini akiitaja kampuni ya Kishen Enterprises ilijitokeza hivi karibuni kuwapiga tafu katika shindano lao. Awetu, alisema wadhamini hao wapya wameungana na wale wa awali ambao baadhi ni Twanga Pepeta', Kiu Investment, Asilia Boutique & Hair Dressing, Dr Osborn na Dk Kalenga. Juu ya burudani itakaowasindikiza warembo hao, mratibu huyo aliitaja bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' ndio watakaotumbuiza ukumbini siku ya onyesho lao.

Kumekucha Miss Kurasini 2012

WAREMBO 16 wanatarajiwa kupanda katika jukwaa la ukumbi wa Equator Grill jijini Dar es Salaam Ijumaa ya May 25 katika shindano la kumsaka Miss Kurasini 2012. Mkurugenzi wa ZUM Fashion & entertainment,inayoandaa shindano hilo Zuwena Mustapha alisema jana kwamba maandalizi kwa ajili ya shindano hilo yanaendelea vema na kwamba mwaka huu wataendeleza historia ya kutoa mrembo bomba atakayetikisa hadi ngazi ya Taifa. Alisema mpaka sasa wameshapatikana wadhamini 14 kwa ajili ya kusaidia shindano hilo ambalo linatarajiwa kuwa bomba, huku likiambatana na burudani kabambe.Taji la kitongoji hicho linashikiliwa na Top Model wa Miss Tanzania 2011, Mwajabu Juma (pichani). “Leo napenda kuwaambia kuwa hadi sasa tunajumla ya wadhamini 14 ambao wamejitokeza kudhamini shindano hilo, lakini bado milango ipo wazi kwa yeyote anaependa kutuzamini na kusaidia warembo wetu wa kurasini kupata zawadi nono na shindano kuwea zuri,”alisema Mustapha. Mustapha alisema wadhamini wakuu wa shindano hilo ni Nameems Wear wakisaidiwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Redds, Dodoma wine, Clouds FM, Lady Pepeta, Father Kidevu Blog, Jambo Leo, Aucland Tours & Safaris, Candy Bureau de Change, Flexip, PJ Amusement, Renzo Salon na Madishisha Video Production. Aliwataja warembo waliopo kambini na kunolewa na Mwajabu Juma akisaidiwa na Malkia wa vipaji wa Miss Tanzania 2011, Rose Hurbert ni Mariam Sadic (19), Johari Juma (20),Linda Deus (20),Irene Sostheness 20),Neemadoree Sylvery(29),Edna Magige (22), Lindanancy Joseph(20), Elizabeth Mkende (19), Betty Peter (22), Jennifer Njabili (18), Lilian Joseph (20), Farida Mrope (23),Christina Moses (20), Angle Gasper (19), Flaviana Maeda(22) na Sia Kimambo (19).