STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 12, 2013

Ni vita vya Barca na Bavarian, Chelsea waangukia kwa Basel


MABINGWA wapya wa Ujerumani, Bayern Munich imeangukia mikononi mwa Barcelona katika mechi za hatua na Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku wapinzani wao Borussia Dortmund wakipangiwa Real Madrid.
Aidha Chelsea ya Uingereza timu pekee inayoiwakilisha Uingereza imepangwa kukwaruzana na Basel ya Uswiss katika mechi za Nusu Fainali ya UEFA Ndogo, huku Benfica ya Ureno na Fenarbeche ya Uturuki zikipangwa pamoja.
Kupangwa kwa droo hiyo iliyozitenganisha timu hasimu kutoka nchi moja inamaanisha kwamba fainali za mwaka huu ya Ligi ya Ulaya itazikutanisha timu za taifa moja baada ya kipindi kirefu.
Mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kucheza kati ya Aprili 23 na 24 na zile za marudiano zitachezwa Aprili 30 na Mei Mosi kabla ya fainali kupigwa uwanja wa Wembley Uingereza Mei 25.
Kwa mechi za UEFA Ndogo mkondo wa kwanza utaanza Aprili 25 na za mkondo wa pili Mei 2 kabla ya fainali Mei 15.
Barcelona watakuwa wageni wa wana fainali za mwaka jana katia mkondo wa kwanza kabla ya kurudiana wiki moja baadaye kwenye dimba lake la Camp Nou, kadhalika Wahispania wengine Real Madrid watasafiri pia Ujerumani kuvaana na wenyeji wao Dortmund kabla ya kurejea nyumbani katika mechi ya mkondo wa pili.
Kwenye mechi za UEFA Ndogo Chelsea wataanzia ugenini sawa na itakavyokuwa kwa Benfica na kurudiana na wapinzani wao kwenye viwanja vyao vya nyumbani dhidi ya Basel na Fenerbeche.

Kivumbi cha VPL kuendelea wikiendi, Simba, Yanga, Azam kuvuna nini?
Na Boniface Wambura
Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Aprili 13 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Sokoine utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting.

Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 14 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Simba. Mechi hiyo namba 155 itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Shelisheli kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS FAR ya Morocco itakayofanyika Aprili 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi hao ni Emile Fred atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Steve Maire na Jean Ernesta. Mwamuzi wa mezani (fourth official) atakuwa Jean Claude Labrossa. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.

Wakati huo huo, CAF imemteua Mtanzania Alfred Lwiza kuwa Kamishna wa mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Liga Muculmana ya Msumbiji na Wydad Casablanca ya Morocco.

Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 19,20 au 21 mwaka huu nchini Msumbiji itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe wakiongozwa na Ruzive Ruzive.


UJUMBE WA FIFA KUWASILI APRILI 15
Na Boniface Wambura
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwatangazia wadau wa mpira wa miguu kuwa ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utawasili nchini Jumatatu (Aprili 15 mwaka huu) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo Covarro na utafanya kazi kwa siku tatu kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili 18 mwaka huu.

Ukiwa nchini, ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.

Wajumbe hao wangependa kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF imeiandikia Wizara ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na wakuu wengine wa michezo Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi zao.

Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni:
1.   Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.

2.   Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa upya, kukataliwa.


3.   Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.

4.   Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.

5.   Jamal Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.

6.   Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata rufani FIFA.

Shirikisho linawaomba wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya kutosha na kwamba barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa)

Kigogo Yanga matatani, kisa...!

Makamui Mwenyekiti wa Yanga, Clement  Sanga
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa timu yao inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwamba inahujumiwa na ndiyo maana mechi yao dhidi ya JKT Oljoro imesogezwa mbele na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Awali, mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Oljoro ilipangwa kufanyika juzi (Jumatano ya Aprili 10) lakini sasa itachezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa kauli kama za Sanga zinachangia kujenga chuki  zisizokuwa na sababu kati ya shirikisho hilo na mashabiki wa soka nchini.
Kwa sababu hiyo, Osiah alisema kuwa Sanga atatakiwa athibitishe ni kwa namna gani Yanga inahujumiwa baada ya kuwapo kwa mabadiliko hayo ya ratiba ambayo yalizihusu pia timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, zikiwamo za Simba na Azam ambazo sasa zitacheza Jumapili.
Osiah alisema kuwa anashangaa kusikia madai ya Sanga kuwa klabu hazijashirikishwa katika kufanya marekebisho hayo wakati ukweli ni kwamba klabu hizo ziliwakilishwa na viongozi wao walioko kwenye kamati ya ligi na timu yao ina mjumbe kwenye kamati hiyo.
Katibu huyo wa TFF alisema kuwa viongozi wa klabu walielezwa katika kikao kilichofanyika mapema kabla ya ligi kuanza kwamba kutakuwa na 'Super Week' katika hatua ya mwisho wa ligi ambayo itatekelezwa kupitia nafasi itakayopatikana katika kituo cha televisheni ya kulipia cha Afrika Kusini cha  Super Sport.
"Mnapotafuta wadhamini kuna wakati ni lazima mjitoe mhanga... na kuonekana kwetu kupitia Super Sport kumesaidia kuleta wadhamini wengi ambao tayari wamevutiwa na ligi yetu," alisema Osiah.
Katika mahojiano yake na vyombo vya habari hivi karibuni, Sanga alisema kuwa wao walikuwa tayari wameshaiandaa timu yao na kwa mabadiliko hayo ambayo hawaoni faida yake zaidi ya kuwapunguzia mashabiki viwanjani yamewapa hasara kubwa itokanayo na kuendelea kuiweka timu kambini.
Aliyewahi kuwa Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage waliwahi kuadhibiwa na TFF baada ya kukutwa na hatia ya kutoa kauli ambazo baadaye walishindwa kuzithibitisha.


Chanzo:NIPASHE

Matapeli wamhujumu rais wa IBF nchini

Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi
MATAPELI wa kimataifa wanaoingilia barua pepe na akaunti nyingine za watu mbalimbali wamemvamia rais wa hapa nchini wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF/USBA), Onesmo Ngowi na kutumia jina lake kwa nia ya kuwatapeli fedha watu mbalimbali anaojuana nao.
Jina la Ngowi ambaye pia ni Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, (TPBC), limetumiwa na matapeli hao kutuma ujumbe wa barua pepe kwa watu mbalimbali anaowasiliana nao, wahusika wakijifanya ni Ngowi na kuomba msaada wa fedha.
Katika barua pepe mojawapo iliyotumwa kwa mwandishi, inaeleza Ngowi alikuwa akiomba msaada wa Euro 2,950 (Sh. milioni 6.2) ili kumuwezesha kujinasua na tatizo lililomkumba akiwa nchini Ugiriki; jambo ambalo Ngowi amelilaani na kuwatahadharisha watu anaojuana nao kuwa wawe macho na matapeli hao.
"Matapeli wanatuma akaunti yangu (ya email) na kuomba pesa kwa watu mbalimbali... mimi siko Ugiriki na wala sijamuomba mtu fedha. Tafadhali naomba usijibu meseji hizo," alisema Ngowi kuelezea utapeli huo ambao umeshawakuta pia watu wengi.

TFF ipo tayari kukutana na Nsa Job utetezi wa Rushwa

Nsa Job (kulia)
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema liko tayari wakati wowote kukutana na mchezaji wa Coastal Union ya jijini Tanga, Nsa Job, ambaye alikiri hadharani kuwa aliwahi kupokea rushwa ya Sh.milioni mbili kutoka kwa kiongozi mmoja wa timu vigogo nchini ili asifunge magoli.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema katika barua yao waliyomuandikia mshambuliaji huyo hawakumpa siku maalumu lakini endapo nyota huyo atachelewa kujisalimisha atakumbushwa kabla ya kuchukuliwa hatua kupitia kamati husika.
"Tuliiweka wazi lakini tutamuandikia barua nyingine ya kumkumbusha na itakayofuata itakuwa imetoa muda fulani, ila tunaamini atatoa ushirikiano kama alivyokaririwa na gazeti (la NIPASHE)," alisema Katibu mkuu huyo.
Osiah alisema TFF inaamini mchezaji huyo atatoa ushirikiano kama alivyolieleza gazeti la NIPASHE lilipozungumza naye mapema wiki hii.
Aliongeza kwamba wanaamini akiwa wazi mhusika wa tuhuma hizo atajulikana na hatimaye adhabu itatolewa na kukomesha suala la rushwa katika soka la nchini.
Osiah alisema pia tayari Mkurugenzi wa Vipindi wa kituo cha redio cha Clouds ameahidi kuwapa ushirikiano katika kupata nakala ya kipindi kilichorushwa mahojiano na Nsa ambacho kilifanyika Aprili 3 mwaka huu.
Nsa alizungumza katika mahojiano na kituo cha redio hiyo akisema aliwahi kupokea rushwa lakini aliifungia timu yake goli pekee la ushindi.
Hata hivyo, hadharani, hakuitaja timu aliyokuwa anaichezea wakati huo wala timu aliyoifunga na wala jina la kiongozi aliyemhonga, ambaye alisema alianza kumsumbua kudai fedha zake pale “alipowatungua”.
Nyota huyo ambaye kwa sasa anafanya mazoezi binafsi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti nchini India aliwahi kuchezea timu za Simba, Yanga, Moro United, Azam, Villa Squad na sasa Coastal Union zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Nsa aliiambia NIPASHE kwamba atatoa ushirikiano kwa TFF kama alivyotakiwa na kwa sasa anajiandaa kwenda kukutana nao.
Alisema pia alipokea barua hiyo tangu wiki iliyopita na atafanya kila linalowezekana ili kutekeleza kile atakachoambiwa na wajumbe wa kamati hiyo.


CHANZO:NIPASHE.

Azam yamalizana na wachezaji wake iliyowasimamia kwa rushwa

 
Add captionKLABU ya soka ya Azam ambayo Jumapili inatarajiwa kuvaana na Simba, imemalizana na wachezaji wake wanne iliyokuwa imewasimamisha kwa tuhuma za Rushwa kabla ya kusafishwa na TAKUKURU.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu ya Azam, imesema wachezaji wote wanne waliosimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa dhidi yao wameripoti kambini tayari kuikabili Simba SC siku ya jumapili

Kurejea kwa wachezaji hao kunamaliza mgogoro uliokuwepo na kudumu kwa takribani miezi mitano kufuatia shutuma za rushwa ambazo zilipelekwa takukuru kuchunguzwa ili kujua ukweli na uongozi wa Azam FC unaishukuru takukuru kwa kazi nzuri ambapo imegundulika kuwa wachezaji hao hawakuhusika na hivyo kusafishwa na chombo hicho chenye mamlaka ya kuchunguza tuhuma za rushwa.
Wachezaji hao wote wanatarajiwa kuwemo kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Simba SC ikiwa mwalimu ataona inafaa na wapo katika hali nzuri kuweza kucheza.
Mchezo huo wa jumapili ni muhimu sana kwa Azam FC kwani ikishinda itaizidi Simba SC pointi 14 huku simba ikisaliwa na michezo minne na hivyo kumaanisha kuwa Kagera Sugar atabaki kuwa mpinzani pekee wa Azam FC katika kuwania nafasi ya pili.