STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 25, 2013

Hatimaye Javu atua rasmi Jangwani

Mshambuliaji mpya wa timu ya Yanga Hussein Javu


HATIMAYE klabu ya soka ya Yanga imekamilisha usajili wa mshambuliaji nyota wa timu ya Mtibwa Sugar, Hussein Javu ambapo mchezaji huyo asubuhi ya leo alianza mazoezi Jangwani.
Javu ambaye alikuwa akisisitiza kuwa alikuwa hajasaini kokote licha ya kutangazwa alishasajiliwa na klabu hiyo, zoezi lake la kutua Jangwani lilikamilika leo na kuungana na wenzake katika  mazoezi kwenye uwanja wa shule ya sekondari Loyola Mabibo jijini Dar es salaam.
Hussein Javu amesajili Young Africans kwa mkataba wa miaka miwili ambapo atavaa jezi za watoto wa Jangwani mpaka mwishoni mwa msimu wa 2014/2015.
Usajili wa Javu unafikisha idadi ya washambuliaji sita mpaka sasa wakiwemo Didier Kavumbagu, Jerson Tegete, Said Bahanuzi, Shaban Kondo (mpya - Msumbiji) na Realintus Lusajo (mpya kutoka Machava FC - Moshi).
Kikosi cha Mholanzi Ernie Brandts kinaendelea na mazoezi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom unaotarajiwa kuanza agosti 24 kwa kufungua dimba na timu ya Ashanti United iliyopanda msimu huu.
Agosti 17-2013  Young Africans itacheza mchezo wa Ngao ya Hisani na timu ya Azam FC katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu kwa msimu wa 2013/2014.
Mpaka sasa klabu ya Yanga imekamilisha usajili wa wachezaji saba (7) wapya ambao ni:
1. Deogratius Munishi 'Dida' -  Huru Azam FC (Golikipa)
2.Rajab Zahir -  Huru Mtibwa Sugar  (Mlinzi wa kati)
3.Hamis Thabit - Huru Ureno (Kiungo)
4.Shaban Kondo - Huru Msumbiji (Mshambuliaji)
5.Mrisho Ngassa - Huru Azam FC (Kiungo mshambuliaji)
6.Reanlintus Lusajo - Huru Machava FC (mshambuliaji)
7. Hussein Javu - Mtibwa Sugar (mshambuliaji)
Kikosi kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kila siku saa 2 asubuhi na wachezaji waliopo katika timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) wanatarajiwa kuungana na wenzao katika mazoezi siku ya jumatatu.

Young SC

Hivi ndivyo ilivyokuwa Siku ya Mashujaa Tanzania

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka ngao na sime katika mnara wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa katika kambi ya jeshi ya Kaboya, Bukoba, mkoani Kagera leo Julai 25, 2013


Viongozi wa dini wakisoma dua kwenye maadhimisho hayo. Pembeni ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Mohamed Ali Shein, Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali, Jaji Mkuu Mheshimiwa Chande Othman na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Othman Makungu
Rais Jakaya Kikwete akitembelea makaburi ya mashujaa waliopoteza maisha wakati wa vita na Nduli Iddi Amini wa Uganda

                                  Rais JK akisalimiana na askari wastaafu
Maskini Kibosile wa Home Shopping Centre!


MFANYABIASHARA maarufu na Mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center (HSC), Said Mohamed Saad, ambaye wiki iliyopita alimwagiwa tindikali maeneo ya Msasani City Mall, jijini Dar es Salaam, sasa yuko Afrika Kusini kwa matibabu zaidi .

Wiki iliyopita majira ya saa moja jioni, mfanyabiashara huyo alimwagiwa tindikali na mtu mmoja ambaye hakufahamika na mara baada ya kutenda tukio hilo, mhusika alikimbia huku mlinzi wa eneo hilo akijaribu kumkimbiza pasipo mafanikio baada ya kuteleza na kuanguka.

Hatua hiyo ilitoa mwanya kwa mtuhumiwa kutoroka eneo la tukio kwa kutumia usafiri aina ya pikipiki.

Hapo awali ilidaiwa kuwa Saad alikuwa anaweza kuzungumza japo amefungwa mashine sehemu ya pua kwa ajili ya kumsaidia kupumua.  Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yameonekana kushamiri nchini katika siku za hivi karibuni.

Tukio la kumwagiwa tindikali mmiliki huyo wa Home Shopping Centre, limekuja ikiwa ni takribani wiki mbili tangu Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Said Juma Makamba naye ajeruhiwe vibaya usoni kwa kumwagiwa maji maji yanayosadikiwa kuwa ni tindikali majira ya usiku akiwa nyumbani kwake.SOURCE BOFYA HAPA

Vialli kuwakosa Uganda The Cranes Jumamosi?

Vialli (kati) anayeweza kuikosa Uganda Jumamosi

Na Boniface Wambura
TIMU ya taifa, Taifa Stars imewasili salama hapa Kampala tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.

Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.

Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.

Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.

Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

JUma Fundi, Nasibu Ramadhani hapatoshi Idd Pili

IMG_4971
Mabondia Juma Fundi (kushoto) na Nasibu Ramadhani (kulia) wakinyakuliwa mikono na mratibu wa pambano lao la Idd Pili

BONDIA Nassibu Ramadhani na Juma Fundi ambao ni wapinzani wa jadi wanatarajiwa kuvaana kayika pambano litakalofanyika siku ya Idd Pili, huku wakitambiana.
Mabondia hao watavaana kwenye ukumbi wa Friends Corners katika pambano la kumaliza ubishi baina yao baada ya kutambiana kwa muda mrefu kila mmoja akijinasibu kuwa ni mkali zaidi ya mwenzake.
Pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 linaratibiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST).
Bondia Nasibu Ramadhani amesema hana hofu na mpinzani wake kwa sababu anamuona mwepesi kwa vile alishampinga na kutwaa ubingwa wa Dunia wa WB-Forum.
"Anayeniumiza kichwa katika uzito wa Bantam ni Francis Miyeyusho pekee, wengine nawaona wa kawaida tu," alisema Nasibu.
Bondia huyo alisema Fundi atarajie kipigo kikali toka kwake kwani amejiandaa vyema ili kuendeleza rekodi ya ubabe kwa mpinzani wake huyo.
Hata hivyo Fundi alisema yeye hana maneno mengi anasubiri kwa hamu siku ya pambani lifike ili aweze kuzima kilimilimi cha Nasibu.
"Tunaandikia mate ya nini wakati wino upo, tusubiri Idd Pili kisha tujue nani mbabe kati yangu na Nasibu, nimejiandaa kufanya vyema siku hiyo," alisema.

Falcao akana kuwa 'kijeba'

Falcao (kushoto) alipokuwa Atletico Madrid
PARIS, Ufaransa
MSHAMBULIAJI mpya wa klabu iliyorejea Ligi Kuu nchini Ufaransa ya Monaco, Radamel Falcao amekanusha ripoti zinazodai kwamba alidanganya kuhusu umri wake, huku vyombo mbalimbali vya habari vikidai mfumania nyavu huyo ni 'kijeba' akiwa kazaliwa mwaka 1984 tofauti na unaofahamika wa 1986.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia, ambaye alikamilisha uhamisho wa kutua Monaco katika kipindi hiki cha usajili kwa ada ya uhamisho ya euro milioni 60 mwezi Juni, anatuhumiwa kudanganya tarehe yake ya kuzaliwa kufuatia kutolewa kwa rekodi zake za shule ambazo zinaonyesha kwamba mshambuliaji huyo ana umri wa miaka 29.
Kwa mujibu wa rekodi za usajili za mshambuliaji huyo za Fifa, Falcao alizaliwa Februari 10, 1986 lakini kituo cha televisheni cha Noticias Uno cha Colombia kimedai kuwa nyota huyo alizaliwa miaka miwili kabla.
Hata hivyo, nyota huyo wa zamani wa Atletico Madrid alitumia ukurasa wake wa Twitter kukanusha uvumi huo, ambao aliuelezea kuwa ni "upuuzi mtupu".
Aliandika: "Nimeshangazwa na ripoti hizi mpya zilizozunguka umri wangu, na madai haya ni upuuzi mtupu."
"Napenda kukanusha madai haya na naufunga rasmi mjadala huu."
Falcao alipata uhamisho wake wa pesa nyingi wa kutua Monaco baada ya kufunga magoli 70 katika mechi 90 akiwa na Atletico aliyodumu nayo kwa misimu miwili tu.

Joseph Owino 'aota' mbawa Msimbazi


Joseph Owino alipokuwa akiichezea Simba
JUHUDI za viongozi wa klabu ya Simba kutaka kumrejesha beki wa zamani wa timu hiyo, Joseph Owino kutoka Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), zimegonga mwamba baada ya kukosekana pesa za kumlipa.
Mbali ya kukosekana kwa pesa anazotaka mchezaji huyo, uongozi wa URA  umegoma kumuuza Owino kwa Simba kwa vile amepata ofa nzuri ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Qatar, Vietnam na China.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshafanya mazungumzo na Owino na kukubaliana naye mambo kadhaa, lakini dau analotaka ni kubwa.
Hata hivyo, Hanspope hakuwa tayari kutaja dau hilo, lakini alisisitiza kuwa bado wanaendelea na juhudi za kutafuta pesa ili waweze kukamilisha usajili wa mchezaji huyo.
Owino aliichezea Simba msimu wa 2009/2010 akiwa na Emmanuel Okwi na Hilaly Echessa kutoka Kenya na kuiletea mafanikio makubwa, lakini aliachwa msimu uliofuata baada ya kuumia goti.
Baada ya kuumia, beki huyo mahiri alipelekwa India kupatiwa matibabu na aliporea nchini alijiunga na Azam FC, lakini alishindwa kuichezea kutokana na kukosa namba na kuamua kurejea Uganda.
Owino alionyesha umahiri mkubwa katika mechi mbili za kirafiki za kimataifa, ambazo URA ilicheza dhidi ya Simba na Yanga. Katika mechi hizo zilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, URA iliichapa Simba mabao 2-1 kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Yanga.
"Kimsingi tumeshazungumza na Owino na ameikubali ofa tuliyompa ili aweze kurudi tena Simba, lakini bado kuna masuala yanayohusu pesa, ambayo hatujayakamilisha,"alisema Hanspope.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili ya Simba alisema, kutokana na benchi la ufundi kuvutiwa na kiwango cha beki huyo, watafanya kila wanaloweza kuhakikisha anarejea Msimbazi na kucheza katika ligi kuu msimu ujao.
Wakati Simba ikiwa katika mikakati hiyo, Meneja wa URA, Sam Okabo amesema hawawezi kumruhusu Owino arejee Simba kwa sababu ampata ofa nzuri Marekani na Asia.
Okabo alisema jana kuwa, si rahisi kwa Owino kurejea Simba kama viongozi wa klabu hiyo wanavyotaka kwa vile mchezaji huyo ni lulu kwa sasa na anawindwa na klabu nyingi.
Kwa sasa, Simba imesaliwa na wachezaji wawili wa kigeni, Abel Dhaira na Hamis Tambwe baada ya uongozi kuvunja mkataba wa Mussa Mudde na pia kusitisha mpango wa kumsajili Robert Ssenkoom kutokana na benchi la ufundi kutoridhishwa na kiwango chake.
Katika hatua nyingine, Hanspope amesema mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Hamis Tambwe kutoka Burundi anatarajiwa kuwasili nchini Jumanne na kujiunga na timu hiyo kwenye kambi yake iliyopo Mbamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.

LIWAZO

Ajali ya treni yaua 78, wengine 140 Hispania

Watu 20 wamepoteza maisha


WATU zaidi ya 70 wamefariki na wengine 140  katika ajali mbaya ya treni inayoenda kasi ilitokea Kaskazini Magharibi ya Hispania.
Abiria hao walifariki wakati wakisafiri na treni hiyo kabla ya kupata ajali na kwamba baadhi ya majeruhi hali zao ni mbaya.
Moja ya mabehewa limeonekana likiwa linawaka moto na jingine kukatika katikati kwenye eneo la ajali hiyo karibu na Santiago De Compostela ambapo treni hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea Ferrol Northwest nchini humo.

Msondo yaingia studio, kula Idd Dar, Zenji

Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma wakiwajibika
BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' imetumia muda wake wa mapumziko kuingia studio kurekodi nyimbo zilizosalia za albamu yao, huku ikiweka bayana ratiba nzima ya Sikukuu za Idd el Fitri.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D' aliiambia MICHARAZO kuwa, wameona ni vyema kuutupia muda wa likizo ya mfungo wa Ramadhani kurekodi nyimbo za albamu yao ambayo inasubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wao.
Super D, alisema nyimbo zinazorekodiwa kwa sasa katika studio moja ya jijini Dar es Salaam ni Lipi Jema na Baba Kibebe zilizotungwa na Eddo Sanga, Kwa Mjomba Hakuna Urithi wa Huruka Uvuruge, Nadhiri ya Mapenzi wa Juma Katundu na Machimbo.
Wimbo wa Machimbo umeingia kwenye albamu hiyo baada ya kuondolewa kwa kibao kilichokuwa kimetungwa na aliyekuwa muimbaji wao, Isihaka Katima 'Papa Upanga' uitwao 'Dawa ya Deni' na kibao cha mwisho cha albamu hiyo kilichobeba jina wa Suluhu wenyewe ulishakamilika kitambo.
Aidha Super D aliweka wazi kwamba bendi yao katika shamrashamra za Sikukuu za Idd el Fitri, watatambulisha baadhi ya nyimbo mpya katika maonyesho yatakayofanyika kwenye ukumbi wa  DDC Kariakoo kwa onyesho la Idd Mosi na Idd Pili watakamua TCC Chang'ombe kabla ya kuvuka bahari kuelekea Zanzibar kwa onyesho la Idd Tatu pale Gymkhan.
"Idd Mosi tutakamua ngome ya zamani ya wapinzani wetu, DDC Kariakoo na siku inayofuata tutaila Idd viwanja vya TCC Chang'ombe kisha kwenda Zanzibar kumalizia sikukuu," alisema Super.

Kikosi kuweka Zogo lao videoni

Karama Masoud 'Kalapina'
KUNDI la Kikosi cha Mizinga kilichoadhimisha miaka 13 tangu kuanzishwa kwake hivi karibuni, kimekamilisha video ya wimbo wao unaotamba hewani wa 'Zogo la Mtaa'.
Kiongozi wa kundi hilo linalopiga muziki wake katika miondoko ya Hip Hop, Karama Masoud 'Kalapina' aliiambia MICHARAZO kuwa, video hiyo ipo mbioni kuachiwa wakati wowote.
Kalapina alisema mashabiki wa kikosi waliokuwa na hamu ya kuona video hiyo wajiandae kupata burudani.
"Kikosi kimekamilisha video ya wimbo wa 'Zogo la Mtaa' na hivi karibuni itaachiwa hewani, ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya miaka 13 ya Kikosi," alisema Kalapina.
Msanii huyo alisema mbali na video hiyo, pia kundi lao lenye maskani yake Kinondoni Block 41, linaendelea pia kuuza fulani na vifaa vingine vyenye nembo yao ya Kikosi.
"Pia tumefufua duka letu la Kikosi lililopo Block 41 ambapo tunauza t-sheti, na vifaa vingine," alisema Kalapina.
Kundi hilo la Kikosi cha Mizinga, lilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1997 baada ya kusambaratika kwa kundi lililomuibua Kalapina liitwalo School Face Gangster lililokuwa likiundwa na wasanii watatu.