STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 2, 2012

Yanga yakubali kwenda Zenji kushiriki Kombe la Urafiki

HATIMAYE timu ya soka ya Yanga imeamua kubadili msimamo wake wa kushiriki michuano ya Urafiki kwa kukubali kwenda visiwani Zanzibar kushiriki, ambapo inatarajiwa kuondoka leo sambamba na watani zao Simba. Awali uongozi wa Yanga 'ulichomoa' kushiriki michuano hiyo, lakini baada ya 'vikao' na waandaji wake, uongozi huo umelegea na kukubali kwenda kushiriki. Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa, alisema wamekubali baada ya kuridhiana na waandaaji na pia kwa vile michuano hiyo ina lengo la kudumisha urafiki baina ya timu za Tanzania Bara na Visiwani, hawakuona sababu ya kuigomea. "Tunaenda kushiriki, tutaondoka kesho asubuhi kuwahi michuano hiyo na tunaamini tutafanya vema na tutaaitumia kwa ajili ya fainali za Kombe la Kagame," alisema Mwesigwa. Mwesigwa alisema Yanga itaenda Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili ambacho Jumamosi iliitoa nishai Mabingwa wa Uganda, Express kwa kuilaza mabao 2-1 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa jijini Dar. Yanga ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo ya Kagame na itafungua dimba Julai 14 kwa kuumana na Atletico ya Burundi. Timu nyingine za Tanzania Bara zitakazoshiriki michuano hiyo ya Urafiki ni Simba ambao jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimba la Amaan kuumana na Mafunzo.

Hispania wabeba tena ubingwa wa Ulaya

WAFALME wa soka wa Dunia, Hispania usiku wa kuamkia leo iliweka rekodi ya aina yake kwa kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuisambaratisha Italia kwa mabao 4-0. Ushindi katika mechi hiyo ya kusisimua iliyokuwa ya kushambuliana mwanzo mwisho , imeifanya mabingwa hao wapya wa Ulaya kuwa timu ya kwanza katika historia kutwaa mataji mawili mfululizo, huku ikiwa pia na taji la Dunia iliyotwaa katika fainali za mwaka 2010 zilizochezwa barani Afrika. Hispania imefuata nyayo za Argentina iliyowahi kutwaa mataji matatu mfululizo kwa kutwaa ubingwa wa Copa Amerika wakati michuano hiyo ikichezwa kila mwaka kati ya a 1945 hadi 1947. Ikiwa na kiu ya kutaka kudhihirisha kuwa wao ni wababe wa kweli wa soka duniani kwa sasa, Hispania iliucheza mchezo huo kwa kushambulia mwanzo mwisho na kujiandikia bao la kwanza katika dakika ya 14 kupitia kwa David Silva aliyefunga kwa kichwa. Bao la pili la wakali hao wanaonolewa na Vicente del Bosque liliingizwa kimiani na dakika nne kabla ya mapumziko kupitia beki wa kushoto Jordi Alba baada ya kuwatambuka walinzi wa Italia na kumtungua kipa Gianluigi Buffon. Italia iliyokuwa ikijaribu kurejea tukio lililowashtua mashabiki wengi wa soka kwa kuikwamisha Ujerumani katika mechi ya nusu fainali, kwa kuilaza mabao 2-1 ilishindwa katika kufurukuta Kwa Hispania hasa baada ya kuumia kwa Thiago Motta wakati wakiwa wameshamaliza orodha ya wachezaji wa akiba na kucheza pungufu dimbani. Wengi wakiamini huenda mechi ingeisha kwa idadi ya mabao 2-0, Fernando Torres 'El Nino' alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga goli katika mechi mbili za fainali za Euro wakati alipopachika bao la tatu dakika ya 84. Torres, pia alifunga goli la ushindi katika fainali mwaka 2008 wakati walipotwaa ubingwa. Dakika mbili kabla ya kumalizika kwa pambano hilo kiungo matata wa Chelsea, Juan Mata aliifungia Hispania bao la nne lililoikatisha tamaa kabisa Italia ambao walitawala mchezo huo dakika za mwanzoni kabla ya kupoteana na kukimbizwa.