STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 1, 2014

Mtoto wa Rais wa zamani wa Misri anaswa na 'unga'

http://english.ahram.org.eg/Media/News/2012/8/13/2012-634804947670919459-91.jpg
Rais wa zamani wa Misri, Mohammed Mosri
SHIRIKA la habari la Misri linasema kuwa kitinda mimba wa rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi, amekamatwa akishukiwa alikuwa na dawa ya kulevya.
Shirika la habari la taifa linaarifu kuwa polisi walikagua gari walilokuwa na shaka nalo na ndani walimkuta Abdullah Morsi na rafiki.
Inaarifiwa kuwa ndani ya gari piya zilikutikana sigara mbili zilizokuwa na bangi.
Mtoto mwengine wa kiume wa Mohamed Morsi amelaani kukamatwa kwa ndugu yake, na kusema kuwa mdogo wake amesingiziwa tu.
Mohamed Morsi mwenyewe hivi sasa anakabili kesi nne za mashtaka ambayo adhabu yake inaweza kuwa kifo.
BBC

Chelsea, Newcastle zaua, Arsenal ikifa ugenini

Andre Schurrle
Schurrle akishangilia moja ya mabao yake matatu leo
Stoke City striker Peter Crouch has an attempt during the game against Arsenal
Arsenal walipokuwa ugenini leo
Romelu Lukaku
Lukaku akishangilia bao lake pekee lililoizamisha West Ham

MSHAMBULIAJI kinda wa Chelsea kutoka Ujerumani, Andre Schürrle amefunga hat trick na kuisadia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya England, huku Arsenal ikilala ugenini bao 1-0 mbele ya Stoke City.
Nayo Newcastle ikiwa ugenini iliifumua Hull City kwa mabao 4-1, huku Everton ikiiengua Manchester United katika nafasi ya sita baada ya kuifunga West Ham Utd bao 1-0.
Chelsea inayolewa na Jose Mourinho ikiongozwa na kinda hilo la Ujerumani Schurrle ilipata mabao yake katika kipindi cha pili baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika bila timu hizo kufungana.
Schurrle aliianza kuifungia Chelsea bao dakika ya 52 akimalizia kazi nzuri ya Eden Hazard na kuongeza jingine dakika ya 65 akitengenezewa pia na Hazard na kukamilisha hat trick yake dakika ya 69 baada ya Torres kumtengenezea bao hilo.Wenyeji walijipatia bao la kufutia machozi dakika ya  74 kupitia kwa John Heitinga.
Kwa matokeo hayo Chelsea imezidi kujikita kileleni ikifikisha pointi 63, nne zaidi ya Arsenal ambao jioni hii wamegongwa bao 1-0 ugenini na Stoke City kwa mkwaju wa penati iliyofungwa dakika ya 72 na Jonathan Walters baada ya Laurent Koscielny  kuunawa mpira laangoni mwake na mwamuzi Mike Jones kuamuru adhabu hiyo.
Katika mechi nyingine mabao mawili ya Mousa Sissoko na mengine ya Loic Remy na Vurnon Anita  yalitosha kuipa ushindi mnono Newcastle United wa mabao 4-1 dhidi ya wenyeji wao Hull City waliopata bao la kufutia machozi kupitia kwa  Curtis Davies
Everton nayo ilisubiri mpaka dakika ya 81 kujipatia bao pekee lililowapa ushindi nyumbani dhidi ya West Ham United lililofungwa na Romelu Lokaku na kuiengua Manchester United katika nafasi ya sita kwa kufikisha pointi 48 na kuipumia Tottenham Hotspur ye nye pointi 50 itakayocheza kesho.
Pambano la Sunderland dhidi ya West Brom imehairishwa na kwa sasa Liverpool ipo ugenini kuumana na Sputhampton.

Oljoro JKT yaibana Mbeya City ugenini

Oljoro JKT
Mbeya City iliyobanwa nyumbani
TIMU ya Mbeya City imeshindwa kuendelea kugawa dozi nyumbani baada ya jioni ya leo kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya maafande wa Oljoro JKT katika pambano pekee lililochezwa leo kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Licha ya timu zote kushambuliana kusaka mabao hakuna aliyeweza kujipatia bao lolote katika mchezo huo ambao Oljoro wamekiri pambano lilikuwa kali na lililochezeshwa vyema na waamuzi.
Kwa matokeo hayo timu hizo zimegawana pointi moja moja, Mbeya ikifikisha pointi 36 na kuendelea kusalia nafasi ya tatu na Oljoro imefikisha pointi 16 na kusalia nafasi ya 12.
Ligi hiyo intarajiwa kuendelea kesho kwa michezo kadhaa ambapo Simba watakuwa jijini Dar es Salaam kupepetana na Ruvu Shooting pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki baada ya timu zote kufungwa katika mechi zao zilizopita.

Yanga yavunja mwiko Taifa, yaidonyoa Al Ahly 1-0, Gor Mahia yafa nyumbani KCCA yaambulia sare ugenini

Mshambuliaji wa Yanga Mrisho Ngassa akichuana na mchezaji wa Al Ahly katika mechi yao leo uwanja wa Taifa (Picha:Habari Mseto)
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly waliokaa kwa Yanga 1-0 leo
Wanaumeeeeee! Yanga walioifumua Al Ahly na kuvunja mwiko wa unyonge kwa timu za Kiarabu Afrika
HATIMAYE mabingwa wa soka nchini, Yanga imekata mzizi wa fitina baada ya kuvunja mwiko kwa timu za Misri kwa kuwanyuka mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika , Al Ahly ya Misri wakielekea kufuata nyayo za watani za Simba walipointoa Zamalek mwaka 2003.
Bao pekee lililofungwa kwa kichwa dakika ya 82 na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' akiunganisha mpira wa kona iliyochegwa na Simon Msuva, ilitosha kuipa ushindi kiduchu Yanga na kuwa na jukumu la kulazimisha sare yoyote ugenini ili kufuzu hatua ya 16 Bora.
Hata hivyo Yanga hasa washambuliaji wao watajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga ambazo zilipotezwa kwenye vipindi vyote viwili ambapo kama zingetumiwa vyema timu hiyo ingeweza kuibuka na ushindi mnono na kuiweka pagumu Al Ahly.
Washambuliaji Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi walikosa mabao zaidi ya matatu ya wazi kipindi cha pili kabla ya kipindi cha pili kuendelea hata walipoingizwa Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi.
Yanga, ambayo ilikuwa haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri, imewapa burudani mashabiki waliofurika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ulishuhudia kikundi cha mashabiki wanaohisiwa wa Simba kung'oa viti kabla na baada ya Yanga kupata bao.
Haikufahamika sababu za mashabiki hao kuamua kung'oa viti na kusababisha askari wa FFU kuwa na kazi nyingine ya kuwaonya, lakini kwa hakika ni uhuni usiokubalika kwa sababu uwanja wa Taifa umegharamiwa na haikupaswa mashabiki hao kufanya kitendo hicho katika mechi ya kimataifa inayohusisha watani zao.
Kwa matokeo hayo Yanga imevunja mwiko kwa timu za Misri ikiwemo hiyo Al Ahly, na kuwa na kazi ya kusaka sare ugenini ili kuweza kusonga mbele na kurudia historia iliyowekwa na Simba mwaka 2003 walipoivua taji Zamalek waliowala bao 1-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa idadi kama hiyo ugenini na kushinda kwa mikwaju ya penati 3-2.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Gor Mahia ya Kenya imejikuta ikiloa nyumbani baada ya kulazwa mabao 3-2 na Esperance ya Tunisia, Dynamos ya Zambia ilitoka suluhu ya 0-0 na Vita Club ya DR Congo, nao mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, KCCA ya Uganda ilipata sare ya kuvutia ya mabao 2-2 dhidi ya wenyeji wao Nkana Red Devils ya Zambia.
Aibu! Kijana huyu kanaswa akiiba msikitini

* Ni mara ya nne anaswa bila kukoma
* Alishadakwa Kwa Mtoro, Manyema
* Mwenyewe adai njaa inamponza
Kijana anayesadikiwa kuwa kibaka wa kuiba viatu misikiti, aliyejitambulisha kwa jina la Abubakar Abuu (32) akijieleza mbele ya waumini wa msikiti wa Mwenge baada ya kunaswa kaiba sendoz za muumini.
Kijana anayesadikiwa kuwa kibaka wa viatu msikiti katika picha za matukio tofauti ikiwamo akiwa na viatu alivyoiba znazoonekana mwishoni kulia.Hiki ndicho kikosi cha 'mauaji' cha Yanga

KIKOSI cha Yanga kipo dimbani kwa sasa kikivaana na Al Ahly ya Misri huku Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi ameanza sambamba na kipa Deo Munishi huku Juma Kaseja akiwa benchi.

HIKI NDICHO KIKOSI KAMILI
1. Deogratias Munishi 'Dida' – 30
2. Mbuyu Twite – 6
3. Oscar Joshua – 4
4. Nadir Haroub 'Cannavaro' – 23 (C)
5. Kelvin Yondani 'Cotton' – 6
6. Frank Domayo 'Chumvi' – 18
7. Saimon Msuva – 27
8. Haruna Niyonzima 'Fabregas' – 8
9. Emmanuel Okwi – 25
10. Mrisho Ngassa – 'Uncle'17
11. Hamisi Kiiza 'Diego' – 20

Subs:
1. Juma Kaseja – 1
2. Juma Abdul – 12
3. David Luhende – 3
4. Athuman idd “Chuji” – 24
5. Hassan Dilunga – 26
6. Said Bahanuzi – 11
7. Didier Kavu

Ajali yaua mmoja, yajeruhi 38


AJALI zimeendelea kuua roho za wenzetu baada ya mtu mmoja kufariki na wengine 38 kujeruhiwa baada ya basi la Bunda kugonga kichwa cha treni wilayani Manyoni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ajali hiyo ilitokea kwenye njia ya makutano na reli na barabara wilayani Manyoni na mashuhuda wakiwemo walionusurika wanadai haraka aliyokuwa nayo dereva wa basi hilo kutaka kuvuka reli ndiyo iliyosababisha ajali hiyo.
Inaelezwa waliojeruhiwa walikimbizwa hospitalini kwa matibabu ambapo wengine walioruhusiwa na wachache wamelazwa kuendelea na matibabu zaidi.

Ratiba VPL, FDL yapanguliwa


BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya marekebisho madogo ya ratiba kwa mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na moja ya Ligi Daraja la Kwanza (VPL).

Mechi namba 143 kati ya Tanzania Prisons na Simba iliyokuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu sasa imesogezwa kwa siku moja hadi Machi 9 mwaka huu, kwa vile Machi 8 mwaka huu Mbeya City itautumia uwanja huo kwa mechi nyingine ya VPL.

Nayo Mgambo Shooting iliyokuwa icheze na Kagera Sugar, Aprili 12 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga sasa imesogezwa hadi Aprili 13 mwaka huu kwa vile Kituo cha Tanga kitakuwa na mechi mbili.

Kwa upande wa FDL, mechi ya Mkamba Rangers na Kimondo SC sasa itachezwa Machi 3 mwaka huu badala ya Machi 9 mwaka huu mjini Ifakara. Mechi hiyo imerudishwa nyuma ili kuipunguzia gharama Kimondo SC kwani Machi 1 mwaka huu itacheza na Burkina Faso mjini Morogoro.

YANGA 'CHINJA' WAARABU TUPATE RAHA

Jamani eeh hakuna kulala leo au mwasemaje? Kama wachezaji wa Yanga wakiambiana
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri yake kwenye mechi yake ya kwanza ya raundi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

Mechi hiyo inachezwa leo (Machi 1 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia 10 kamili jioni. Timu hizo zitarudiana Machi 9 mwaka huu jijini Cairo, Misri.

Maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika ambapo kamishna Abbas Sendyowa kutoka Uganda na waamuzi wanne kutoka Burundi tayari wapo nchini kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuvuta maelfu ya washabiki.
Milango yote katika uwanja huo itakuwa wazi, ukiwemo ule wa upande wa Uwanja wa Ndani (Indoor Stadium) wakati Barabara ya Taifa (Taifa Road) itafungwa kuanzia chuo cha DUCE hadi msikitini kuanzia saa 4 asubuhi.

Magari maalumu yenye sticker pekee ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani. Vilevile washabiki wanakumbushwa kuwa hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na silaha au vifaa vyovyote vya chuma.

Malinzi aunda Kamati ya Miaka 50 ya TFF


RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda kamati ya watu tisa kuratibu maadhimisho ya miaka 50 tangu TFF ilipojiunga na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

TFF ilipata uanachama wa shirikisho hilo la kimataifa Oktoba 8, 1964 ambapo itaadhimisha miaka hiyo 50 kwa kufanya shughuli mbalimbali za mpira wa miguu.

Kamati hiyo itaongozwa na Mhariri Mtendaji wa kampuni ya magazeti ya Serikali, Gabriel Nderumaki wakati Katibu atakuwa Lina Kessy ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA).

Wajumbe ni Ahmed Mgoyi, Hoyce Temu, Teddy Mapunda, Ruge Mutahaba, Richard Kasesela, Boniface Wambura na Meneja Biashara wa TFF anayetarajiwa kuajiriwa hivi karibuni.

Kamati itafanya kikao chake cha kwanza Jumatatu (Machi 3 mwaka huu) kwenye hoteli ya Courtyard iliyopo Upanda Seaview saa 7 mchana.

Twiga Stars siyo Riziki Afrika


TIMU ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imetolewa katika hatua za Awali za Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zambia katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii. Matokeo hayo yanaifanya Zambia, Shepolopolo isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, kufuatia awali kushinda 2-1 nyumbani katika mchezo wa kwanza.
Twiga inayofundishwa na Rogasian Kaijage, iliuanza vizuri mchezo wa leo na kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza bao 1-0, lililofungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika ya 39.
Asha Mwalala alifunga akimalizia pasi ya Vumilia Maarifa, ambaye naye alipokea krosi ya Nahodha Sophia Mwasikili aliyewachambua wachezaji wa Zambia kwanza.
Kipa wa Twiga Stars, Fatuma Omary aliokoa mchomo wa hatari wa Mupopo Kabange dakika ya 75, lakini hakuweza kuuona mkwaju wa mpira wa adhabu uliopigwa na Rachel Ilungu dakika ya 80 kuipatia Zambia bao la kusawazisha.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Fatuma Omary, Fatma Bashir, Deonisia Daniel, Fatma Issa, Evellyne Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Amina Ali/Zena Khamis dk86, Asha Rashid, Shelda Boniface/Fatma Mustapha dk 65 na Eto Mlenzi.

Yanga, Al Ahly hapatoshi leo, Jangwani waonywa

Yanga
WACHEZAJI wa klabu ya Yanga wametahadharishwa kucheza kwa umakini mkubwa na kushambulia kusaka mabao mapema katika mechi yao ya leo dhidi ya Al Ahly kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga wanavaana na mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika na washindi mara sita wa Super Cup kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, huku ikiwa na rekodi mbaya dhidi ya timu za Waarabu, licha ya kuweka rekodi hivi karibuni ya kushinda jumla ya mabao 19 katika mechi zao tatu ilizocheza ndani ya wiki mbili.
Kwa kutambua ugumu wa mpambano huo, nyota wa zamani wa timu hiyo, Edibily Lunyamila na Ramadhani Kampira wamewauma sikio wachezaji wa Yanga kwa kuwataka kucheza 'jihad' na kwa umakini mkubwa ili wasiwape nafasi wageni wao kupata mabao au sare ya aina yoyote.
Kampira, alisema anaamini vijana wa Johannes van der Pluijm wakishambulia na kupata mabao mengi katika mechi ya leo, nafasi yao ya kuiondosha Al Ahly na kuweka rekodi mpya kwao Cairo ni nyepesi.
"Wito wangu kwa mabeki kucheza kwa umakini mkubwa ili kutoruhusu Al Ahly kupata bao lolote au kulazimisha sare, na safu ya ushambuliaji inaonekena kuelewana, ihakikishe inafunga mabao mengi ya kutosha ili yaisaidie timu kwa mechi ya marudiano ambayo naamini itakuwa ngumu kama desturi za timu za Misri zikiwa kwao," alisema Kampira.
Naye Lunyamila alisema Yanga haipaswi kuichukulia kiwepesi wapinzani wao na badala yake washuke uwanjani kutafuta ushindi mnono huku wajilinda lango lao lisiguswe.
"Yanga ni timu nzuri, ina wachezaji wenye vipaji na wanaojua soka, lakini bado ina kazi ngumu kwa Al Ahly, icheze kwa umakini mkubwa hasa safu ya nyuma na viungo kuwazuia Waarabu hao wasipate mabao na washambuliaji nao wazitumie nafasi watakazopata kufunga mabao mengi ya kutosha ili kujiweka nafasi nzuri kwa mechi ya marudiano ugenini," alinukuliwa Lunyamila.
Lunyamila, winga nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema wachezaji wasibweteke na kauli za kutiana moyo kwamba watetezi hao kwa sasa wamechoka kwani jambo hilo siyo la kweli na wenzao wana uzoefu mkubwa na pia wanajua kufanya hila kwa mechi za marudiano wakificha makucha katika mechi za ugenini.
Yanga ambayo tangu ianze kushiriki michuano ya kimataifa ya Afrika haijawahi kuitoa timu yoyote ya 'Kiarabu' ilifika hatua hiyo baada ya kuitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 baada ya awali kuilaza mabao 7-0 na kwenda kuifunga kwao 5-2 na wiki iliyopita ilipata ushindi wa kishindo katika Ligi Kuu kwa kuicharaza Ruvu Shooting mabao 7-0.

Golden Bush Veterani kuwavaa waliosoma Jitegemee

Golden Bush Veterani
MABINGWA wa soka la maveterani jijini Dar es Salaam, timu ya Golden Bush inayonolewa na nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' na Wazir Mahadh 'Mandieta' leo wanatarajiwa kushuka dimba la Kinesi kupepetana na timu inayoundwa na wanasoka waliowahi kusoma Shule ya Sekondari ya Jitegemee JKT.
Kwa mujibu wa Mlezi wa Golden Bush Veterani, Onesmo Waziri 'Ticotico', mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa majira ya asubuhi kwenye uwanja huo wa Kinesi uliopo Ubungo, ikiwa ni wiki mpoja tangu walipoichakaza bila huruma Pugu Veterani kwa mabao 8-1 katika mechi ya kirafiki kwenye uwanja huo.
Ticotico, alisema kikosi chao kinachoundwa na wachezaji kama Salum Athuman, Herry Morris, Majuto Komu, Wisdom Ndlovu na wengine waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na klabu za Simba na Yanga wamejipanga kuhakikisha wanatoa kipigo kingine kwa wapinzani wao watakaoongozwa na Ally Mayay kiungo na nahodha wa zamani wa Yanga.
"Baada ya kuwakunyuga Pugu Veterans goli 8-1, jumamosi (leo) tunatarajiwa kushuka tena kwenye uwanja wa Kinesi maarufu kama St James Park, kuonyeshana kazi na vijana waliosoma Jitegemee wakiongozwa na kocha wao Ally Mayay," alisema Ticotico ambaye pia ni mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Golden Bush.

Ruvu Shooting kuivaa Simba kwa mbinu za JKT Ruvu

Ruvu Shooting
Simba
KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Mkenya Tom Olaba ametamba kuwa wataishukia Simba kesho kwenye uwanja wa Taifa kwa mbinu zilizotumiwa na 'kaka' zao baada ya kurekebisha makosa yaliyowapelekea kufumuliwa mabao 7-0 na Yanga wiki iliyopita.
Vijana wa Olaba walikumbana na kipigo hicho kwenye uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita siku chache baada ya 'ndugu' zao JKT Ruvu kufumuliwa mabao 6-0 na Prisons Mbeya, lakini wenzao JKT waliwaangukia Simba siku inayofuata (Jumapili) kwa kuilaza mabao 3-2.
Akizungumza na MICHARAZO, Olaba alisema kama JKT Ruvu waliweza kujiuliza baada ya kipigo cha jijini Mbeya ndivyo nao walivyojiuliza  na kurekebisha makosa na kwamba kwa sasa kikosi chake kipo tayari kuchochea zaidi 'machafuko' ndani ya Simba.
Oloba alisema vijana wake wapo fiti kwa mchezo huo licha ya kuwakosa Ibrahim Susan na George Osei ambao wanasumbuliwa na majeraha na watalikosa pambano hilo.
'"Nashukuru vIjana wangu wapo vyema na tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Simba Jumapili, kipigo cha Yanga hakijatukatisha tamaa, badala yake tumerekebisha makosa kama zinavyofanya timu nyingine ambazo kwenye duru la pili zimepoteza kama sisi na kupata mafanikio katika mechi zao zilizofuata," alisema Olaba.
Olaba alisema pamoja na kujiamini kuibuka na ushindi mbele ya Simba, lakini watashuka dimba la Taifa kwa tahadhari kubwa kesho ili wasitoe nafasi kwa wapinzani wao ambao klabu yao kwa sasa siyo shwari tangu walipopata matokeo mabaya katika mechi zao nne zilizopita ili kumalizia hasira zao kwao.
"Tunaijua Simba ni timu nzuri na inayotafuta mahali pa kumalizia hasira zao, hivyo tutacheza kwa tahadhari ilimradi tuhakikishe tunapata ushindi utakaoturudisha kwenye nafasi za juu kama ilivyokuwa kabla ya kufungwa na Yanga," alisema Mkenya huyo.
Simba inayonolewa na kocha Mcroatia, Zdrakov Lugarusic, itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-2 toka kwa JKT Ruvu ikiwa ni kipigo chao cha tatu msimu huu, huku ikiwa imepoteza pointi 10 kati ya 12 ya michezo minne iliyochezwa hivi karibuni.
Timu hiyo ilianza kwa kuambulia sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar kabla ya kulala 1-0 kwa Mgambo JKT na baadaye kwenda Mbeyana kupata sre ya 1-1 mbele ya wenyeji wao Mbeya City na kukumbana na kipigo hicho kilichoibua maneno toka kwa wadau wa klabu hiyo shutuma zikienda kwa uongozi wa Ismail Aden Rage kwamba ameshindwa kufanya kazi kwa kuitelekeza timu.
Hata hivyo uongozi wa Simba kupitia Katibu Mkuu wake, Ezekiel Kamwaga na manahodha Said Masoud 'Chollo' na Amri Kiemba wamewahakikisha wanasimba kwamba watarekebisha makosa na kuanza kuwapa raha kuanzia mechi hiyo ya kesho dhidi ya Ruvu.