STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 25, 2012

Ngassa atamani kucheza Simba

ACHANA na Mrisho Ngassa. Mshambuliaji nyota wa timu ya Moro United iliyoshuka kwenye ligi kuu ya Bara, Benedict Ngassa, amesema anatamani kuichezea Simba. Kama hatopata nafasi ya kucheza Simba, mabingwa wa mwaka jana, Ngassa amesema anatamani kusajiliwa Yanga. Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa, alisema kati ya ndoto anazoota kila siku ni ile ya kuja kuichezea ama Simba au Yanga, klabu anazozihusudu na anazoamini zitaweza kumfikisha mbali kisoka. Ngassa, alisema yeye hatakuwa mchezaji wa kwanza nchini kuziota timu hizo kubwa, ingawa alisema ni vigumu kupata fursa hiyo kirahisi kama hufanyi vitu vya kuzivutia. "Kwa kweli natamani kuichezea timu moja kati ya Simba au Yanga, ni klabu kubwa na zenye mafanikio makubwa nchini na zinazoweza kumfikisha mbali mchezaji kama ana malengo na kila kijana anatamani kuzichezea," alisema. Ngassa, alisema mpaka sasa wakati usajili ukiendelea bado hajasaini kokote licha ya kufuatwa na timu kadhaa. Ngassa ni mmoja wa nyota wa timu ya Moro iliyokuwa imerejea ligi kuu na kushuka msimu uliopita sambamba na Villa Squad na Polisi Dodoma. Nafasi za timu hizo tatu, mbili zikiwa za uraiani, zimechukuliwa na Mgambo Shooting, Polisi Moro na Mbeya Prisons.

Niombeeni kwa Mungu, naumwa-Omar Kapera 'Mwamba'

Kapera (wa tatu kushoto waliochuchumaa) akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga
NYOTA wa zamani wa kimataifa wa klabu za Yanga, Pan Afrika na Taifa Stars, Omar Kapera 'Mwamba' ni mgonjwa na amewaomba mashabiki wa soka kumuombea kwa Mungu. Beki huyo aliyewahi kuwa Afisa Michezo na Utamaduni wilayani Kinondoni na Temeke kabla ya kuiongoza Pan Afrika kama Katibu Mkuu, alisema hali yake si njema baada ya kupatwa na maradhi ya kiharusi. MICHARAZO ilimtembelea mchezaji huyo nyumbani kwake Temeke na kukumkuta katika hali isiyoridhisha, ingawa mwenyewe (Kapera) na mkewe Rukia Rashid walisema ni tofauti na alivyokuwa siku za nyuma. Kapera alisema alianza kuugua ghafla Oktoba mwaka jana kabla ya kuzidiwa hasa alipoanza kupinda mdomo na kupoteza hisia upande wake wa kulia kutokana na kiharusi. "Namshukuru Mungu naendelea vema kulinganisha na siku za nyuma, lakini bado naumwa kama unavyoniona na ninaomba watanzania waniombee nipate nafuu," alisema. "Japo kuugua ni ibada bado nawaomba wenzangu msinisahau kwa maombi na dua zenu." Kapera ambaye alikuwa mmoja wa waasisi wa Pan Afrika mwaka 1976 baada ya mgogoro ulioikumba Yanga mwaka 1975, pia aliwataka mashabiki watakaopenda kumjulia hali wawasiliane nae nyumbani kwake au kumpa pole kupitia simu yake ya mkononi ya 0713 636255. 

Hassani Kumbi: Kiungo mkabaji anayetesa na miondoko ya Mduara

AWALI ndoto zake tangu akiwa shuleni ilikuwa kuja kuwa nyota wa soka akimudu nafasi ya kiungo mkabaji na nafasi nyingine za mbele akitamba na timu kadhaa ikiwemo Ajax Mzamba ya Temeke alioshiriki nao Ligi ya Taifa. Hata hivyo kitendo cha kupigwa bisibisi katika mechi ya 'mchangani' ya Ligi ya kuwania Ng'ombe, Kiwalani, lilisitisha ndoto za Hassani Kumbi ' H-Kumbi au 'H-Kilakitu' na kujikuta akihamia kwenye fani ya muziki. Kumbi, alisema baba yake alimpiga marufuku kucheza soka baada ya tukio hilo lilomfanya alazwe hospitalini na alipopona aliamua kuingia katika muziki kwa vile alishawahi kuimba kaswida alipokuwa madrasa. Msanii huyo anayetamba baada ya kuibuliwa na kituo cha Mkubwa na Wanae kinachoendeshwa na Said Fella, alisema alipigwa bisibisi hiyo mbavuni na mmoja wa mashabiki wa timu pinzani iliyocheza na timu yake ya Young Stars. "Baba alinizuia kucheza soka baada ya kitendo cha kujeruhiwa uwanjani ndipo nikahamishia makali yangu kwenye muziki baada ya kupita usaili wa Mkubwa na Wanae," alisema. Kumbi alisema baadhi ya nyota aliocheza nao shuleni na kwenye timu kadhaa ni Abuu Ubwa, Nizar Khalfan, Adam Kingwande, Ramadhani Chombo, Juma Jabu na Ally Mustafa 'Barthez'. Mkali huyo anayetamba kwa sasa na kibao cha 'Vocha' alichoimba na Dogo Aslay waliopo naye kituo cha Mkubwa na Wanae, alisema licha ya kuimba kaswida, pia aliwapenda mno Banzastone na Zahiri Ally Zorro. "Nilivutiwa na Banzastone na Zahir Ally ambao hata leo wanawafuatilia ndio maana nimeweza kuinuka haraka kisanii," alisema. Msanii huyo, anayetarajia kuachia kazi mpya iitwayo 'Sindano' akiwa na video yake huku akikamilisha pia kibao cha Deni alichoimba na AT, alisema muziki kwa sasa nchini unalipa na una mafanikio makubwa. Alisema zamani ilikuwa vigumu msanii wa muziki wa kizazi kipya kuandaa shoo ya kiingilio cha Sh 20,000 au 50,000 lakini sasa inawezekana akitolea mfano tukio la Diamond alipofanya onyesho lake la 'Diamond Are Forever'. Kumbi, anayetamani kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa mara 'kijiwe' cha muziki kitakampomchanganyia, alisema licha ya muziki kulipa bado vipo vikwazo ikiwemo uharamia na unyonyaji unaofanywa dhidi ya kazi za wasanii. Alisema ni vema serikali ikawasaidia wasanii kwa kutunga sheria kali ili kuwatia adabu wezi wa kazi za wasanii, sambamba na kuvuna mapato yaliyopo katika fani hiyo, akidai fedha nyingi zinapotea mikononi mwa 'wahuni'. Msanii huyo anayependa kula wali kwa maharage au ugali kwa samaki wa kukangaa na mlenda pamoja na kunywa juisi ya Embe, alisema kama angekutana na Rais angemweleza jambo hilo sambamba na kumsihi aboreshe maisha ya watanzania hasa huduma za kijamii na kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za vyakula na bidhaa nyingine. Kumbi anayeishabikia Simba na Manchester United na kuwazimia wachezaji nyota wa timu hizo, Haruna Moshi 'Boban' na Javier Hernandez 'Chicharito', alisema kati ya matukio ya furaha kwake ni kukubalika kwa kazi yake ya kwanza ya 'Vocha' na pia kukutana kwa mara ya kwanza na kuzungumza na Zahir Ally Zorro anayemhusudu na kumsifia uwezo alionao. "Nilisisimka mno nilipokutana uso kwa uso na Zahir Ally na kujisikia faraja aliponieleza kwamba naweza, pia nilipoachia kazi yangu ya Vocha na kupokelewa vema na kwa huzuni ni msiba wa baba yangu Ally Kumbi na kuuguliwa na mama yangu hadi leo," alisema Kumbi. Mkali huyo aliyeoana na Aisha Soud na kuzaa nae mtoto mmoja aitwae Hawa (2), alisema matarajio yake ni kuhakikisha anafika mbali katika muziki, pia akiweka wazi kwamba yeye ni H Kila Kitu akimaanisha anaimba miondoko yote ya muziki ikiwemo taarab na dansi. Kumbi anayemshukuru Mungu na watu waliomsaidia katika muziki kama Said Fella, Yusuf Chambuso, Suleiman Daud 'Sulesh' na wasanii wenzake wa Mkubwa na Wanae, alisema kitu cha thamani anachokumbuka kununua kwa fedha zake za muziki ni kumuugizia mwanae. "Nakumbuka nilienda kufanya shoo Iringa na kupata fedha nyingi kwa mara ya kwanza katika maisha yangu bya muziki na niliporejaea Dar nilikuwa mwanangu Hawa mgonjwa hivyo nikatumia kumtibia pamoja na kumnunulia nguo za bei mbaya," alisema. Msanii mwenye ndoto za kuja kujitolea kuwasaidia wengine kama anavyofanya Mkubwa Fella, alitoa ushauri kwa watu matajiri kuwasaidia wasanii kuwaibua na kuwaendeleza badala ya kusubiri watu wengine wawaibue kisha kuwarubuni wasanii hao bila kujua walikotokea. "Wapo watu wenye fedha zao wamekuwa wakifanya hila kuwarubuni wasanii chipukizi baada ya kuona wameanza kutoka kwa kuinuliwa na watu kama THT, Mkubwa na Wanae au Tip Top Connection, hii sio haki kwanini wasitumie fedha zao kufanya kama wenzao?" Alihoji. Hassani Ally Kumbi, alizaliwa Juni 16, 1987 akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne na kusoma Shule ya Msingi Mabatini -Tandika Dar es Salaam kabla ya kuendelea na masomo ya Sekondari alipohitimu kidato cha nne mwaka 2006 Shule ya Twaybat pia ya Temeke. Alienda kusomea ufundi umeme wa magari mjini Morogoro kabla ya kuzama kwenye soka aliloanza kucheza tangu akisoma shule ya msingi, timu yake ya chandimu ikiwa ni Santiago Chile maarufu kama G Stiva akimudu namba 6 na nyingine zote za mbele. Timu nyingine alizozichezea kabla ya kutua kwenye muziki ni Good Hope, TMK Kids, DYOC na Ajax Mzamba aliyoitoa daraja la tatu hadi Ligi ya Taifa ya TFF. Mwisho

Kingwendu ajipanga kuachana na soka, kisa...!

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya African Lyon aliyewahi kutamba na timu za Ashanti Utd na Simba, Adam Kingwande amesema anatarajiwa kupumzika kwa muda kucheza soka ili arejee darasani kusoma. Kingwande, aliiambia MICHARAZO kama mipango yake ya kwenda darasani itatimia hivi karibuni, basi huenda asionekane tena dimbani hadi atakapomaliza masomo yake baada yaa miaka mitatu. Mchezaji huyo aliyekuwa msaada mkubwa kwa Lyon kabla ya kuumia na kuwa nje ya dimba hadi aliporejea mwishoni mwa msimu uliopita, alisema ameona ni bora arejee darasani kusoma kisha ndipo aendelee kucheza soka. Kingwande alisema anatarajia kwenda kusomea Sheria katika Chuo kimoja kilichopo hapa nchini na hivyo itamuwia vigumu kwake kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja. "Kaka huenda nisionekane tena dimbani kwa muda kidogo kwani natarajia kurudi darasani kusoma, si unajua soka la Bongo lilivyo kama mtu hujiwekei mipango mizuri unaweza kuumbuka mbeleni," alisema. Mkali huyo, aliyeibuliwa na kituo cha kukuza soka la vijana cha DYOC, alisema masomo yake yatachukua muda wa miaka mitatu na hivyo kipindi chote cha masomo hayo hataweza kucheza timu yoyote labda ya chuoni tu. Kingwande alisema mbali na chuo hicho, pia ameomba nafasi ya kusoma pia katika chuo kimoja kilichopo nje ya nchi hivyo anasikilizia kama akikubaliwa anaweza kuamua kujiunga na chuo kimojawapo kati ya hivyo. "Nimeomba pia katika chuo kimoja nje ya nchi, lakini ningependa kusoma hapa nchini, mradi tu nitimize ndoto zangu za kuwa mwanasheria," alisema. Mchezaji huyo anayemudu nafasi zote za mbele ikiwemo kiungo alisema anaamini kusoma kutamwezesha kulicheza soka lake kwa uhakika sambamba na kuwa na uhakika wa maisha baada ya kutundika daluga zake. Mwisho

Theresia Ojade, mshindi wa tuzo ya TASWA anaizimia Simba

MWENYEWE anakiri kuwa kiu aliyokuwa nayo tangu utotoni ya kutaka kuwa nyota wa michezo nchini, ndiyo iliyomfanya ajibidiishe, kujituma na kujifunza kwa wengine waliomtangulia na katika kipindi kifupi ameanza kuona matunda yake bila ya kutarajia. Moja ya matunda yanayomfanya mchezaji huyo mkali wa timu ya mpira wa wavu ya Jeshi Stars, Theresia Ojade kujivunia ni Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike wa Wavu aliyotwaa iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini, TASWA. Theresia, alisema tuzo hiyo ambayo hakutarajia kuipata licha ya kuwa mmoja wa nyota watatu walioteuliwa kuiwania sambamba na mchezaji wenzake wa Jeshi Stars, Zuhura Hassani na Evelyne Albert wa Magereza, imempa faraja kubwa na kumtia nguvu ya kujibidiisha zaidi. Mkali huyo aliyeanza kung'ara katika michezo tangu akisoma Shule ya Msingi akicheza netiboli, wavu na kikapu, alisema hakutarajia kama ndoto zake za kung'ara katika michezo zingeanza kutimia mapema kiasi hicho. "Kwa kweli namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuanza kutimiza ndoto zangu za utotoni za kutamba katika michezo baada ya kutwaa tuzo ya TASWA," alisema. Aliongeza tuzo hiyo haimvimbishi kichwa badala yake imemuongezea morali wa kuongeza juhudi ili aje kutamba kimataifa ikiwezekana kucheza mpira wa wavu wa kulipwa kama nyota wa nchi jirani za Rwanda na Kenya. "Natamani nifike mbali katika mchezo huu, hasa kucheza wavu wa kulipwa sambamba na kuisaidia timu yangu ya Jeshi Stars itambe kimataifa," alisema. MAFANIKIO Theresia, aliyeingia kwenye wavu kwa kuvutiwa na umahiri wa dada yake, Maria Daniel na Fausta Paul aliyestaafu kwa sasa, alisema mbali na heshima ya tuzo hiyo na kitita cha Sh. Mil. Moja, pia anashukuru wavu kumsaidia mengi. Alisema, mchezo huo umemfanya hafahamike, kutembea sehemu mbalimbali na kumwezesha kumudu maisha yake na kuisaidia familia yake licha ya kupata mafunzo ya kijeshi kama askariu wa kujitolea wa JKT. "Japo mchezo huu haulipi sana nchini kutokana na kutopewa kipaumbele na kudodora kwake, ukweli umenisaidia kwa mengi kiasi najivunia kuucheza," alisema. Alidokeza kuzimika kwa mchezo huo nchini kumechangiwa na Chama chao cha TAVA kukosa ubunifu na kuandaa mashindano mara kwa mara kuuhamaisha mchezo huo na kuutaka uongozi wake kuzinduka usingizini. Theresia alisema, pia 'ubaguzi' unaofanywa na serikali na wadhamini kwa kutupia macho soka tu, ni tatizo linalodidimiza wavu na michezo mingine na kudai angekutana na Rais angemlilia atupie macho michezo yote ili kuwasaidia wenye vipaji kunufaika nayo. "Ningemuomba Rais aitupie na kuiwezesha michezo mingine ili tunayoicheza tunufaike nayo kama kwa wanasoka na kama ningekuwa Rais ningewekeza katika michezo sambamba na kuboresha huduma za kijamii hasa Afya na Elimu," alisema. FURAHA Nyota huyo anayependa kula ugali kwa samaki na kunywa juisi ya Embe, alisema hakuna kitu cha furaha kwake kama kutwaa tuzo hiyo ya TASWA na kuhuzunishwa na kifo cha mjomba wake kipenzi, Ojade aliyefariki mwaka jana. Theresia aliyejaliwa umbo la kike na sura ya kuvutia, alisema licha ya kucheza mechi nyingi, hawezi kuisahau pambano kati ya Jeshi Stars dhidi ya Prisons ya Kenya katika fainali za michuano ya ubingwa wa nchi za Afrika Mashariki. "Naikumbuka kwa namna wapinzani wetu walivyotuzidi maarifa na namna tulivyocheza na kuambulia kipigo cha aibu cha seti 3-0," alisema. Theresia ambaye hajaolewa wala kuzaa mtoto, akitamani atakapoolewa awe na watoto watatu, ni shabiki mkubwa wa Simba na Manchester United akimzimia mchezaji mwenzake wa Jeshi Stars, Yasinta Remmy. Mkali huyo anayechishwa na nguo za rangi nyeupe na nyeusi na kupenda kutumia muda wake wa mapumziko kusikiliza muziki na kufuatilia maambo ya urembo na mitindo, aliwashukuru familia yake hasa wazazi, dada yake Maria Daniel na marehemu mjomba wake Ojade. ALIPOTOKA Theresia Sylvanus Abwao Ojade, alizaliwa Januari 8, 1988 Shirati mkoani Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Mbagala Kuu jijini Dar kabla ya kujiunga na masomo ya Sekondari katika Shule ya Mwanga na kukwamia kidato cha pili kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita katika michezo aliyoicheza tangu kinda. Klabu yake ya kwanza kujiunga kuichezea ni JKT Mgulani alipokuwa mmoja wa askari wa kujitolea wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa mkataba wa miaka mitatu. Baada ya kung'ara na timu hiyo na kumalizika kwa mkataba wake alijiunga na Jeshi Stars mwaka juzi na kufanikiwa kutwaa nao mataji mbalimbali ukiwemo ubingwa wa Ligi ya Muungano wa mwaka huu. Theresia anayewazimia wasanii Lady Jaydee na Ally Kiba wanaotamba katika muziki nchini, alisema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru wachezaji wenzake na makocha waliomnoa na kumfikisha hapo alipo. Mwanadada huyo alikiri kwamba amekuwa akipata usumbufu mkubwa kwa wanaume wakware, lakini kwa kujithamini na kutambua kuwa Ukimwi upo na unaua huepuka vishawishi jambo alilotaka wachezaji wenzake na jamii kwa ujumla nao kuwa makini kwa kuepuka tamaa. Pia aliwasihi wachezaji wenzake kupendana, kushirikiana na kujibidiisha na kujituma katika mazoezi na michuano mbalimbali ili wafike mbali. Mwisho