STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 3, 2012

Ngassa hatimaye akubali kutua Simba, wanachama wasubiri maelezo mkutano wa Jumapili

NYOTA wa kimataifa wa klabu ya Azam na Taifa Stars, Mrisho Ngassa ambaye juzi alinukuliwa kuigomea klabu yake kumpeleka Simba, hatimaye mchezaji huyo ameridhia kwenda mwenyewe Msimbazi baada ya kuahidiwa mambo mazuri katika klabu hiyo mpya. Hata hivyo kuna taarifa kwamba licha ya uongozi wa Simba kufanikiwa kumweka sawa mchezaji huyo, baadhi ya wanachama wamekuwa na mashaka na mchezaji huyo wakiamini ni mnazi mkubwa wa Yanga na hivyo watatoa hatma yake kwenye mkutano wa wanachama utakaofanyika siku ya Jumapili. Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliiambia MICHARAZO kwamba hawaamini kama Ngassa atacheza kwa mapenzi katika timu yao na pia kuhoji uongozi kitu gani kilichoufanya umchukue mchezaji huyo. Ngassa alinukuliwa jana kuwa yu tayari kuichezea Simba kwa vile yeye hana mapenzi na klabu yoyote zaidi ya kulitumikia soka na mchana huu alitarajiwa kutambulishwa rasmi na uongozi huo kwa waandishi wa habari. Winga huyo aliyewahi kung'ara na timu za Toto Afrika, Kagera Sugar na Yanga kabla ya kwenda Azam, ametua Simba kwa mkopo ikidaiwa kalipwa kiasi cha Sh. Milioni 30 na gari aaina ya Verosa na atakuwa kilipwa mshahara wa Sh Milioni2 kwa mwezi. Pamoja na sakata la mchezaji huo kuonekana limeisha baada ya Azam na Simba kumalizana kufuatia Yanga kushindwa katika mbio za kumwania kumrejesha Jangwani, wanachama wa Simba wamesisitiza kuwa uongozi wao unapaswa kuwapa majibu ya kuridhisha katika mkutano wao siku ya Jumapili. Mmoja wa wanachama hao ambao yupo kwenye baraza la wazee wa klabu hiyo (jina tunalo) alisema wameshangazwa na uongozi wao kumnyakua Ngassa kabla hata hawajalimaliza sakata la beki wao Kelvin Yondani aliyetimkia Yanga, huku ikidaiwa ana makataba nae. "TUnajua soka ndivyo lilivyo, lakini naamini Ngassa anaweza asicheze kwa kiwango chake kama alivyo kwa sababu ya watu kumhisini ana uyanga, ila viongozi wajiandae Jumapili kutueleza kilichotokea na namna Yondani alivyotukimbia," alisema mwanachama huyo. Kelvin Yondani, aliyekuwa akituhumiwa kuwa mnazi wa Yanga, aliitema Simba mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu msimu uliopita na kutua Yanga ambapo aling'ara kwenye michuano ya Kombe la Kagame. Pengo la Yondani lilionekana wazi kwenye kikosi cha Simba kilichotolewa hatua ya robo fainali kwa kunyukwa mabao 3-1 na Azam.

Okwi afuzu majaribio yake Austria

MSHAMBULIAJI tegemeo wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, Emmanuel Okwi amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Redbull Salzburg ya nchini Austria alikoenda kwa majaribio ya wiki mbili, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema jana. Hata hivyo, Okwi ambaye hakuwepo wakati Simba ikiishia robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), atarejea nchini wakati wowote ili kutibiwa malaria ambayo inamsumbua tangu alipotua Austria, alisema Kaburu. Aliongeza kuwa Simba inatarajia kulipwa Euro 600,000 kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Uganda (Cranes). Kaburu alisema kuwa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho huo na wamefurahi kuona Okwi anapata timu Ulaya na kutimiza ndoto zake. Alisema pia Simba tayari imemsajili beki wa APR, Mbuyi Twite na atatua nchini wakati wowote kabla ya tamasha la Simba Day ambalo litafanyika Agosti 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa Simba imeingia mkataba wa miaka miwili na beki huyo ambaye anachukua nafasi ya Lino Masombo aliyeachwa baada ya kiwango chake kutoridhisha. Wakati huo huo, taarifa kutoka Simba zinaeleza kwamba wachezaji wake wengine chipukizi watano wa Simba B ambao walikwenda Ujerumani na timu yao ya kituo cha soka cha jijini Mwanza wamepata timu mbalimbali za kuchezea za Ujerumani na Austria. Habari zinaeleza kwamba wachezaji hao watarejea nchini na klabu hizo zitaanza taratibu za kuingia nao mikataba. Wachezaji hao yosso waliong'aa ni pamoja na kipa Aboubakar Hashim, Said Ndebla, Miraji Athumani, Frank Sekule (washambuliaji) na Hassan Hassan. Mwaka jana Simba ilimuuza mshambuliaji Mbwana Samatta kwa TP Mazembe kwa dola za Marekani 150,000 na baadaye Patrick Ochan. CHANZO:NIPASHE

Mobby Mpambala ala shavu Pilipili

MKALI wa filamu za mapigano nchini, Mobby Mpambala amelamba dume katika kampuni ya Pilipili Entertainment baada ya kupewa shavu la kutengeneza filamu mpya iitwayo 'The Same Plan'. Akizungumza na MICHARAZO, Mpambala aliyedai sehemu kubwa ya mafanikio yake kimaisha na kisanii yamechangiwa na mkewe, Jasmine, alisema kampuni ya Pilipili imempa nafasi hiyo baada ya kukutana nao katikati ya wiki iliyopita ili kufanya nao kazi. Mpambala, alisema katika mzungumzo yao na kampuni hiyo waliafikiana kufyatua kazi ya utambulisho na kudai tayari yu mbioni kuandaa filamu iitwayo 'The Same Plan', aliyodai itawashirikisha wakali kadhaa wa fani hiyo nchini ambao hata hivyo hakuweza kuwataja majina. "Namshukuru Mungu, neema zinazidi kunifungukia baada ya Pilipili Entertaiment kunipa shavu la kufanya nao kazi na natarajia kutoa filamu ya kwanza iitwayo 'The Same Plan'," alisema. Aliongeza tenda hiyo mpya imekuja wakati akijiandaa kutoa kazi mbili kwa mpigo zilizokamilika kupitia kampuni yake ya Wazagi za 'Fuvu' na Anti Virus'. Mpambala, alisema hawezi kujivunia mafanikio yote aliyonayo bila kumshukuru mkewe Jasmine, ambaye alitoka nae mbali kabla hata hajapata umaarufu kama alionao, licha ya kukiri alishakuwa na mwanamke mwingine aliyezaa nae watoto watatu na kuachana nae na pia kuoa mke mpya, Zolla. "Hakuna siri siri ya mafanikio yangu ukiondoa baraka za Mungu na za wazazi, pia mke wangu ni sehemu ya haya yote, ndio maana nimefika hapa hata kupata tenda kama ya Pilipili," alisema. Mwisho

Klabu ya Azam yafafanua sakata la Ngassa

TAARIFA hii imetolewa na Meneja wa klabu ya Azam, Patrick Kahemela Klabu ya Azam FC inapenda kutoa taarifa ya ufafanuzi juu ya sakata la mchezaji Mrisho Ngasa ambalo linaonekana kupotoshwa 1. Azam FC ilitangaza kuwa biashara ya mchezaji Mrisho Ngasa ingefungwa siku ya Jumatano 1/08/2012 saa saba mchana na ilivitaka vilabu vyenye interest na mchezaji huyo kufika makao makuu ya Azam FC ofisi ndogo zilizopo kwenye kiwanda cha unga cha Azam-Mzizima zikiwa na pesa taslimu. Bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni Dola 50,000. Lakini katika mawasiliano ya email kwa makatibu wakuu wa Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei ya mauzo na ingemuuza Ngasa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya mwenzake. Kwa maana hiyo biashara ya mchezaji mrisho ngasa ilifanyika kwa uwazi. Lengo la Azam FC lilikuwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata huduma ya Ngasa. Pia tunaomba ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngasa alipewa taarifa kuwa anauzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake. Ngasa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na Azam FC yazingatiwe. 2. Hadi kufikia siku ya Jumatano 01/08/2012 saa saba mchana. Ni klabu ya Simba pekee iliyojibu kwa maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngasa. Yanga wao hawakuwahi kujibu email, ingawa kwa majibu ya simu Mjumbe wao wa Kamati ya usajili Bw Sefu Magari alitangaza kuwa Ngasa hana thamani ya zaidi ya milioni 20. Na Yanga haikuwa tayari kuboresha ofa yake. 3. Muda wa kufungwa kwa biashara ya kumuuza Ngasa ulipofika, ni simba pekee kupitia kwa makamu Mwenyekiti wake Bw Geofrey Ngange na Mhasibu wake ndiyo waliofika wakiwa na pesa taslimu shilingi milioni 25. Yanga hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana interest. 4. Kikao cha dharura cha Azam FC kilikaa na kuamua kuwa biashara ya kumuuza Ngasa ilishindikana kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000. Kwa maana hiyo Azam FC iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo kwenye klabu iliyofika na kuonesha nia ya kumhitaji (Simba) 5. Simba walipewa sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngasa mshahara wake kamili (TZsh 2,000,000) pamoja na stahiki zake nyingine zote za kimkataba 6. Sababu za kumpeleka Ngasa kwa mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam FC ingetoa kwa Ngasa kama angebaki. 7. Azam FC inapenda kuweka wazi kuwa haijamlazimisha Ngasa kwenda Simba kama inavyopotoshwa. Kama Ngasa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na dola 50,000 na Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo simba lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC 8. Tunaomba kuweka msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngasa na kuvunja mkataba wake na hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngasa hataki kwenda tunakompeleka Azam FC inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu. 9. Lakini Ngasa na washauri wake waelewe kuwa akiamua kubaki Azam FC atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba wake, kwani Azam FC haipotayari kumvisha jezi mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu. 10. Kwa kuwa Sakata hili limeanza kuhusishwa na sakata la Mchezaji ramadhani Chombo. Naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo. Redondo alipewa option tatu za kuchagua baada ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu timu ilipokuwa safarini Mwanza. a. Kupelekwa kwa mkopo Moro United? b. Kupatikana kwa mnunuzi mwenye shilingi milioni 40 c. Kukubali adhabu ya kufungiwa kwa miezi mitatu na kulipwa nusu mshahara wahati akitumikia adhabu. Redondo alithibitisha kuipenda Azam FC kwa kukataa kuuzwa au kupelekwa kwa mkopo. Alikubali kutumikia adhabu yake na ilipoisha alirudi na kuomba msamaha na sasa ni mmoja kati ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji kama Redondo na bila kupepesa macho wala kung’ata maneno. Azam FC inamchukulia Redondo kama mtu spesho na mwenye mapenzi ya dhati na klabu yake na inamtaka aendelee kuwa na moyo huo.