STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 12, 2012

Chelsea, Man City kufungua pazia la msimu mpya EPL leo

PAZIA la msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL)kwa mwaka 2012/13 linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo Jumapili kwa mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu England, Manchester City, na Mabingwa wa FA Cup, Chelsea, ambao pia ni Mabingwa wa Ulaya. Pambano la timu hizo mbili zitakazoshuka dimbani leo zikiwa na mabadiliko yanayotofautiana katika vikosi vyao unatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Villa Park, kuanzia saa 9 Alasiri kwa saa za Afrika Mashariki na Kati. Wakati Chelsea ikiwa na nyota wapya walionunuliwa hivi karibuni kwa ajili ya msimu mpya, Man City wao hawana mabadiliko yoyote. Chelsea itashuka dimbani leo ikiwa haina kinara aliyewapa mataji hayo mawili inayoyashikilia kwa sasa Didier Drogba, kutoka Ivory Coast aliyehamia katika klabu ya Shanghai Shenhua ya China akiungana na Nicolas Anelka. Vifaa vipya vilivyosajiliwa na ambavyo vimeanza kuonyesha makeke katika mechi za kujipima nguvu kujiandaa na msimu mpya utakaoanza mwishoni mwa wiki ijayo ni Eden Hazard, Marko Marin na Oscar lakini ni Hazard na Marin ambao wanaweza kucheza Mechi hii na Man City kwa vile Oscar atakuwa bado yuko na nchi yake Brazil kwenye Olimpiki. Msimu uliopita, Timu hizi ziligawana ushindi kwa Chelsea kuifunga Man City 2-1 Mwezi Desemba na Man City kuifunga Chelsea 2-1 Mwezi Machi. Katika Mechi zao za hivi karibuni, Mechi za kujipasha kwa ajili ya Msimu mpya, Chelsea imekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa kushinda Mechi moja tu kati ya 4 walizocheza na kufungwa zilizobaki wakati Man City wamecheza Mechi 5 na kushinda 3 na kufungwa mbili. Chelsea hawana majeruhi yeyote lakini Man City watamkosa Nahodha wao Vincent Kompany na Micah Richards ambao wameumia. Vikosi vinatarajiwa kupangwa kwa siku ya leo ni kama ifuatavyo: Chelsea [Mfumo 4-3-3]: Cech, Ivanovic, Terry, Cahill, Cole, Mikel, Meireles, Lampard, Ramires, Torres, Hazard Man City [Mfumo 4-4-2]: Hart, Zabaleta, Savic, Lescott, Clichy, Yaya Toure, De Jong, Nasri, Johnson, Tevez, Aguero

Rage adanganya Simba, alia akijitoa TFF Na Waandishi Wetu, Dodoma na Dar es Salaam

SIKU sita tangu awadanganye wanachama wa Simba kuwa mchezaji Emmanuel Okwi amefanya majaribio na kufuzu Ulaya, mwenyekiti wa klabu hiyo Isamil Aden Rage amelia hadharani akitangaza kujitoa uongozi wa moja ya kamati za TFF -- shirikisho la soka. Rage jana alitangaza kujivua nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, akituhumu baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kutoitendea haki timu yake. Mwenyekiti huyo wa Simba ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM) aliwaambia wanachama wa Simba katika mkutano Jumapili iliyopita kuwa Okwi alifanya majaribio na kufuzu katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria. Lakini akizungumza na Nipashe mapema wiki hii, Okwi alisema hakufanya majaribio yoyote Ulaya kutokana na kusumbuliwa na Malaria tangu awasili barani humo mpaka kurejea Uganda na kisha Simba. Alipoulizwa kama haoni kuwa aliwadanganya wanachama wa Simba alipowaeleza jambo ambalo linakanushwa na mchezaji husika jana, Rage ambaye alidai pia kuwa mchezaji huyo atakuwa akilipwa euro 300,000 kwa mwezi na Redbull alisema: "Okwi hakwenda kutalii kule... mimi ninasema kitu kilicho sahihi. "Alifanya majaribio na kufuzu. Haya maneno mengine ni ya magazeti tu... sasa kama hajafanya majaribio alienda kufanya nini kule kwa kipindi cha wiki nzima." Kwa mujibu wa taarifa za mtandao rasmi wa kompyuta wa Red Bull Salzburg, imesajili wachezaji wawili tu kati ya tarehe za Okwi kwenda Ulaya mpaka kurudi -- Valon Berisha kutoka Viking Stavanger na Havard Nielsen kutoka Valerenga Oslo. Zote za Norway. Akizungumza na waandishi wa habari Bungeni mjini Dodoma jana, Rage alisema amejitoa katika kamati hiyo baada ya kuchukizwa na kitendo cha Yanga kumsajili beki wa APR ya Rwanda, Mbuyi Twite ambaye Simba ilishaingia naye mkataba, na kwa baraka za TFF. Alisema TFF ina wajumbe wengi ambao ni wanazi wa Yanga na hivyo kushindwa kuitendea Simba haki. “Kama serikali na mamlaka za kusimamia soka zitaonekana zinapendelea timu moja, basi wapenzi na wanachama wa Simba wanaweza kuamua kuangalia kwingineko ambako wanadhani watapata haki zao za msingi,” alisema Rage na kulazimika kukatisha kwa muda mkutano wake baada ya kumwaga machozi. Rage hakufafanua Serikali inaingiaje katika suala la kuonewa kwa Simba huko anakodai, wala kama amepewa ridhaa na wanachama wa Msimbazi kuishutumu serikali yao kwa niaba yao. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwe, amesema kuwa wanasubiri muda ufike wamtangaze rasmi Mbuyi Twite atakayechezea timu hiyo msimu ujao wa ligi kuu ya Bara. "Hiko kitu kipo (usajili wa Mbuyi), lakini siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa," alisema. "Ngoja tusubiri wakati wake ufike na mchezaji ataonekana hapa kwa sababu hili sasa hivi limekuwa na mvutano kidogo." Chanzo:NIPASHE JUMAPILI

Pambano la watani wa jadi Msondo wajichimbia Dodoma, Sikinde wajificha

HOMA ya pambano la wapinzani wa jadi kwenye muziki wa dansi nchini kati ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' na Mlimani Park 'Sikinde' linalotarajiwa kufanyika Idd Mosi kwenye viwanja vya Leaders Club limechukua sura mpya baada ya bendi mmoja kukimbia mji na nyingine kwenda kusikojulikana. Bendi ya Msondo imelikimbia jiji la Dar es Salaam na kwenda kujichimbia mkoani Dodoma kujiandaa kikamilifu na pambano hilo la aina yake dhidi ya mahasimu wao. Meneja wa bendi hiyo Said Kibiriti amesema kuwa bendi iko Dodoma ikifanya mazoezi ya 'kufa mtu' ili kuwatoa nishai Sikinde na wasiwe na hamu tena ya kuomba pambano siku nyingine. "Tunataka tutoe dozi siku hiyo, tutawasambaratisha na waogope tena kupambana na sisi, mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi bendi yetu iko sawa na sasa inajifua na siku ya Idd El Fitri wajitokeze kwa wingi kuja kuishangilia Msondo," alisema Kibiriti. Kwa upande wa Sikinde, kiongozi wa bendi hiyo Habib Jeff amesema kuwa bendi yao ipo jijini Dar es Salaam, lakini akagoma kabisa kutaja sehemu ilipojichimbia. "Ndugu yangu sisi tupo hapa hapa Dar, ila siwezi kukwambia tupo wapi, tunaogopa hujuma, si unajua tena linapokuja suala la Msondo na Sikinde ni kama Simba na Yanga kwa hiyo mashabiki watatuona tu siku siku hiyo, wala hatusemi kwa sasa yuko wapi ila hapa hapa Dar," alisema. Kiongozi huyo amewataka mashabiki wake kujazana kwa wingi siku ya Idd Mosi kwenye viwanja vya Leaders Club kuipa sapoti bendi yao ili iibwage Msondo. Pambano hilo limeandaliwa na kampuni ya Keen Arts na kudhaminiwa na Konyagi. Bendi hizo zilipambana kwenye sikukuu ya Krisimasi mwaka jana kwenye ukumbi wa TCC. Mwisho

Ruvu Shooting yatangaza kikosi chake kipya, yasajili 26

KLABU ya soka ya Ruvu Shooting Stars inayojiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara imetangaza usajili wa wachezaji wao 26 kwa ajili ya msimu mpya wa ligi hiyo utakaoanza mwezi ujao. Miongoni mwa waliosajiliwa na kikosi hicho kinachonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa ni pamoja na waliokuwa washambuliaji nyota wa Kagera Sugar, Hussein Swedi na Said Dilunga. Msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO leo asubuhi kuwa, usajili huo ambao unatarajiwa kuwasilishwa kesho kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, umezingatia umri, kipaji na uwezo wa mchezaji kutokana na mapendekezo ya kocha wao. Bwire, alisema kati ya wachezaji hao 26 waliosajiliwa na klabu yao, sita ni wachezaji wapya na waliosalia ni wale walioichezea timu hiyo msimu uliopita. Aliwataja wachezaji wapya walionyakuliwa na timu yao kuwa ni Said Dilunga, Husseni Swedi, Mau Bofu aliyekuwa akiichezea Azam, Gideon Sepo, Kulwa Mobi aliyeichezea Polisi Dodoma msimu uliopita na Philemon Mwandesile aliyekuwa timu ya Toto Afrika. Wachezaji wa zamani waliobakishwa kikosi ni pamoja na kipa Benjamin Haule, Michael Norbert, Gido Chawala, Godhard Msweku, Liberatus Manyasi, George Assey, Mangasin Mbonosi, Paul Ndauka, Jumanne Juma, Shaaban Suzan, Said Madega na Nyambiso Athuman. Wengine ni Raphael Keyala, Frank Msese, Michael Aidan, Gharib Mussa, Ayuob Kitala, Ernest Jackson na Baraka Nyakamande. Bwire alisema wachezaji waliotemwa na kikosi hicho kutokana na sababu mbalimbali ni pamoja na Mohammed Kijuso, Emmanuel Mwagamwaga, Yusuph Mgwao na Kassim Kilungo.

Timu za Maafande wa JKT waandaliwa michuano maalum wazialika Coastal, Lyon

TIMU za soka za Coastal Union ya Tanga na African Lyon ya Dar es Salaam zinatarajiwa kushiriki michuano maalum ya 6 Bora zinazozihusisha timu za maafande wa JKT, kwa ajili ya kuziandaa vema na ushiriki wao wa Ligi Kuu. Michuano hiyo itakayokuwa ikifanyika kila mwaka kulingana na uwepo wa timu hizo za maafande inatarajiwa kuanza siku ya Jumatano na itakuwa ikichezwa kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Msemaji wa michuano hiyo itakayochezwa kama ligi hadi kupata mshindi wake, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO mapema leo kuwa timu nne za maafande wa JKT ndizo walengwa wakuu wa michuano hiyo ila katika kuipa msisimko zaidi wamezialika Coastal Union na African Lyon. Bwire alisema wamezialika timu hizo kwa imani itazipa changamoto timu zao ili kuanza kuhimili mikikimikiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu. "Katika kuziandaa timu zetu za JKT na kuhakikisha zinafanya vema kwenye Ligi Kuu msimu huu, tumeziandalia michuano maalum ya Sita Bora ambayo itaanza Agosti 15 na tumezialika Coastal Union na African Lyon, kutokana na kuonekana zina viwango bora," alisema Bwire. Alizitaja timu za JKT zilizolengwa kwa michuano hiyo ni wenyeji JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, JKT Oljoro ya Arusha na JKT Mgambo Shooting ya Tanga iliyopanda daraja msimu huu. Bwire alisema ratiba michuano hiyo itaanza kwa kuzikutanisha timu za JKT Ruvu na Ruvu Shooting siku ya Jumatano, siku inayofuata itakuwa zamu za JKT Oljoro dhidi ya Mgambo Shooting na Agosti 17 Coastal Union itavaana na Lyon. "Hizo ni mechi za awali na ratiba kamili inatarajiwa kutolewa kuanzia Jumanne ili kuwapa fursa mashabiki wa soka kuifuatilia na hatimaye kujua nani atakayeibuka mshindi wa michuano hiyo maalum," alisema. Mwisho