STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 4, 2013

FIFA yaifungia Cameroon kujihusisha na soka


SHIRIKISHO la Kandanda Duniani, FIFA limeifungia nchi ya Cameroon kwa muda usiojulikana nchi ya kufuatia serikali ya nchi hiyo kujiingiza katika maswala ya chama cha soka nchini humo.
Kwa mujibu wa tangazo la FIFA, hatua ya kufungiwa kwa nchi hiyo imetokana na maamuzi ya kamati ya dharura ya shirikisho hilo iliyokutana na kuamua kusimamisha kwa muda chama cha soka cha Cameroon FECAFOOT na uamuzi huo umeanza kutekelezwa mara moja kwa sababu serikali inaingilia maswala ya chama cha soka.

Tumuombeeni Mzee Mandela

Mzee Mandela akiwa hospitalini
TAARIFA zilizotangazwa na kituo cha runinga cha Al Jazeera zinasema kuwa hali ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela imezidi kuwa tete ikidaiwa anapumua kwa kutumia mashine maalum.
Inaelezwa Mzee Mandela ameshindwa kupumua yeye mwenyewe na hivyo kulazimisha madaktari kumvika mashine hiyo ili kumsaidia kupigania uhai wake na kusababisha simanzi kubwa kwa ndugu, familia na wananchi wa taifa hilo tajiri Afrika na duniani kwa ujumla.
Mzee Mandela aliyekimbizwa hospitali zaidi ya siku 25, ambako wakati hali yake ikiwa hivyo familia yake imekuwa katika mzozo wa kugombea mahali pa kumzikia.

Jumuika na Mapacha Watatu kuianza wikiendi yako

Brazili yarejea 10 Bora ya FIFA, Tanzania yaporomoka

Brazil waliorejea 10 Bora ya orodha ya viwango vya soka ya FIFA
Stars iliyoporoka toka nafasi ya 109 hadi 121

MABINGWA wa Fainali za Kombe la Mabara, Brazil imechupa hadi nafasi ya 9 katika orodha mpya ya viwango vya soka Duniani vilivyotolewa na Shirikisho la Kandanda Duniani, FIFA.
Brazil imechupa katika nafasi hiyo ikiwa imerejea kwenye 10 Bora baada ya awali kuporomoka kiwango siku chache baada ya kunyakua taji hilo kwa kuizodoa Hispania kwa mabao 3-0 katika fainali iliyochezwa kwenye ardhi yake ya nyumbani.
Hata hivyo orodha hiyo mpya ya viwango imeiacha kileleni Hispania, ikifuatiwa na timu za Ujerumani, Colombia,Argentina na Uholanzi zikikamilisha orodha ya timu tano bora za dunia.
Italia ambao walifika hatua ya nusu fainali kwenye kombe la Mabara wanashika nafasi ya sita mbele ya Ureno walio kwenye nafasi ya saba huku Croatia, Brazil na Ubelgiji  zikihitimisha 10 Bora
Vinara wa soka Afrika, Ivory Coast wameendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa orodha ya nchi za Afrika ikishika nafasi ya 13 duniani ikifuatiwa na wapinzani wa karibu Ghana waliopo nafasi ya 24 ulimwenguni na ya pili Afrika.
Taifa la Mali lenyewe lipo nafasi ya tatu ikikamata namba 28 duniani, kisha Algeria na Nigeria zilizohitimisha 5 Bora ya Afrika.
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda kama kawa wameendelea kukomaa kileleni huku kwa Afrika ikiwa nafasi ya
19 na dunia ya 80 ikiwa imepanda kwa nafasi 13 toka orodha iliyopita waliokuwa nafasi ya 93 duniani na Afrika ya 24. 
Ethiopia bado wamesalia nafasi ya pili kwa ukanda wa CECAFA ikishika nafasi ya  25 Afrika na 90 kwa dunia ilihali Tanzania ipo nafasi ya 35 Afrika ikipanda nafasi mbili toka 32 ya awali na duniani wapo nafasi ya 121 wakiporomoka toka 106 mwezi uliopita.

Temeke kupata kipusa wake kesho katika Redd's Miss Temeke 2013


 Mratibu wa shindano la Redd’s Miss Temeke Benny Kisaka akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu shindano la Redd’s Kanda ya Temeke linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa TCC Club Chang'ombe Julai 5. Kulia ni Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tz, Albert Makoye.Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tanzania, Albert Makoye akizungumza kuhusu fainali ya Redd's Miss Temeke. 
Na Mwandishi Wetu
MREMBO atakayetwaa taji la Redds Miss Temeke 2013, linalofanyika Ijumaa Julai 5, mwaka huu ataondoka na zawadi za jumla ya Sh. Milioni 3,250,000 ikiwa ni zawadi kubwa zaidi kutolewa katika mashindano yote ya urembo, yaliyofanyika mwaka huu.
Mshindi huyo, atapata ofa ya mwaka mzima kutoka RIO gym & Spa, iliyopo Quality Center, kutumia vifaa vyote ndani ya gym hiyo ambayo gharama yake ni Milioni 1,400,000, pia atajinyakulia simu ya kiganjani yenye thamani ya Sh 700,000 , dinner set kutoka AKO Catering yenye thamani ya Sh,150,000 sanjari na pesa taslim Sh. Milioni 1, hiyo jumla yake ni Milioni 3,250,000.
Mshindi wa pili katika mashindano hayo ambayo mgeni rasmi atakuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abas Mtemvu atajinyakulia kitita cha Sh.800,000 pesa taslim na dinner set ambayo thamani yake ilikuwa bado haijathibitishwa na mdhamni wa zawadi hiyo wakati mshindi wa tatu ambao wote kwa pamoja ni wawakilishi wa Miss Temeke, yeye atajipatia fedha taslimu Sh 700,000.
Sh , 400,000 zitakwenda kwa mshindi wa nne na atakayeshika nafasi ya tano yeye ataibuka na Sh 300,000. 

Washiriki wengine ambao hawatabahatika kuingia katika nafasi ya tano bora, wote watapewa Sh,200,000 kwa maana ya kifuta jasho. Tumelenga zawadi za fedha zaidi, hii ni kutokana na ugumu wa maandalizi kwa warembo ambao hugharamika zaidi, kiasi nasi kuona kuna kila namna ya kuwapunguzia maamivu hayo.
Shindano hilo, linatarajiwa kuwa na burudani ya kipekee kutoka kwa mshindi wa tungo bora ya Bongo Fleva ya Kili Music mwaka huu, Ben Paul sanjari na Twanga Pepeta ambayo mwishoni mwa wiki, ilizindua albamu yake ya 13 kwa mafanikio makubwa.

 Warembo watakaopanda jukwaani Julai 5 ni kutoka Kigamboni, Kurasini na Chang'ombe ambao wanawania taji linaloshikiliwa na Miss Tanzania namba tatu, Edda Sylvester walikuwa chini ya wakufunzi Suzy Mwenda na Shadya Mohamed wakati kwenye kucheza nako walikuwa na walimu wawili Super Bokilo na Charles.
Warembo hao ni pamoja na Axsaritha Vedastus, Darling Mmary, Esther Muswa,  Hyness Oscar, Irene Rajab, Jamila Thomas, Latifa Mohamed, Margreth Gerald, Margreth Olotu, Mey Karume, Mutesi George, Naima Ramadhan, Narietha Boniface , Stella Mngazija na Svtlona Nyameyo .       
Shindano hilo limedhaminiwa na kinywaji cha Redd's, Dodoma Wine, Gazeti la Jambo Leo, Cloud’s Media, Blogu ya Wananchi (Le Mutuz), Fredito Entertainment, CXC Africa tours & Safaris, RIO Gym & Spa, 100.5 Times FM na Kitwe General Traders. 

Mbali ya wadhamini hao pia Redds Miss Temeke imechangiwa katika ufanikishaji na Mbunge wa Jimbo hilo, Abbas Mtemvu na mwanamichezo maarufu nchini Geofrey Nyange Kaburu hasa kwa upande wa zawadi.
Temeke, imewahi kutoa warembo kadhaa miaka ya nyuma waliopata mafanikio katika mashindano hayo, mitindo na kazi nyingine hasa kupata uzoefu wa kujiamini katika njanja mbalimbali. Miongoni mwao ni Miriam Odemba(1997) aliyepata kuiwakilisha Tanzani katika fainali za mitindo zilizofanyika Nice Ufaransa na kupata mkataba wa Elite Model Look, baadaye kufakinikiwa kutwaa nafasi ya pili ya Miss Earth World, zilizofanyika China. 

Pia, Temeke ilimtoa Happines Millen Magesse(2001), na kutwaa taji la Miss Tanzania na kwa sasa anang'ara sana katika tasnia ya mitindo katika nchi za Marekani, Afrika Kusini na barani Afrika kwa ujumla. 
2003 Temeke ilimtoa Miss Tanzania, Sylvia Bahame na 2006 kuwatoa Jokate Mwegelo na Irene Uwoya. Jokate alitwaa taji la Miss Temeke mwaka huu na pia kushika nafasi ya pili Miss Tanzania na pia kushinda taji la ubalozi wa Redd's na gazeti la Citizen. 
Irene Uwoya ambaye alikuwa mshindi wa pili Temeke alishika nafasi ya nne kwenye Miss Tanzania mwaka huo. Genevieve Mpangala mwaka 2010 alitwaa taji la Miss Temeke baadaye kushinda taji la Miss Tanzania. 
Nafasi nyingine za juu zilizowahi kutwaliwa na warembo kutoka Temeke ni pamoja na Irene Kiwia, mshindi wa nne Miss Tanzania mwaka 2000, Regina Mosha mshindi wa nne Miss Tanzania mwaka 2002, Cecylia Assey mshindi wa pili Miss Tanzania 2004, Queen David mshindi wa tatu mwaka 2007 na Edda Sylvester mshindi wa tatu Miss Tanzania akiwa anashikilia taji la Redds Miss Temeke. 
BMP Promotions inayoandaa mashindano haya kwa mwaka wa 18 sasa, inatanguliza shukrani zake wadhamini wetu kwa miaka hiyo, sanjari na vyombo vyote vya habari kwa ujumla wake, kwani ndio waliofanikisha kuandaa Miss Temeke kwa ufanisi katika muda wote huo, shukrani sana.

Adhana kurushwa ktk runinga kwa mara ya kwanza UK


Waumini wa Kiislam wakiwa kwenye ibada ya swala

WAKATI mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikaribia kuanza, nchini Uingereza kituo kimoja cha runinga kimetangaza kuanza kurushwa hewani moja kwa moja adhana ya swala ya asubuhi.
Chaneli ya 4 ya televisheni nchini humo, imesema itaanza kurushwa hewani adhana hiyo ya asubuhi 'live' kuwaamsha waumini wa kiislam ili kuwahi swala.
Justine Bower mkurugenzi wa masuala ya umma wa chaneli ya 4 ya televisheni ya nchi hiyo amesema kuwa, kanali hiyo itakuwa ikirusha moja kwa moja adhana ya asubuhi kwa ajili ya wananchi wa Uingereza.  Ameongeza kuwa, waumini wa dini ya Kiislamu wapatao milioni mbili na laki nane nchini humo wataanza mfunguo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo. 
Bower amesema kuwa kanali hiyo pia itakuwa ikirusha hewani adhana kupitia mtandao wa kanali hiyo.
Alipoulizwa wamejiandaa vipi kukabiliana na ukosoaji kwa hatua hiyo, Justine Bower amesema kuwa, karibu asilimia 5 ya wananchi wa nchi hiyo wako katika pilika pilika za kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani. 
Amesema kuwa, mwezi wa Ramadhani hufungwa na waumini wa dini ya Kiislamu kila mwaka, na nitawashangaa watu watakaostaajabishwa na uwepo wa utambulisho huo wa kidini.
Mfungo huo ambao unatarajiwa kuanza kati ya Julai 8 na 9 ni kati ya nguzo tano za dini ya kiislam ambapo waumini hujizuia kula na kunywa mchana pamoja na kujikithirisha kufanya mambo mema kwa nia ya kutaka radhi za Allah Subhana Wataala.
 
(Radio Tehran  via  Wavuti)

Kaimu Rais mpya Misri aapishwa

Kaimu Rais Mpya wa Misri, Adly Mansur
KAIMU Rais mpya wa Misri ameapishwa kuchukua nafasi ya Rais Mohammed Mosri aliyeondolewa madarakani na jeshi la nchini kufuatia wiki kadhaa ya maandamano.
Jaji mkuu wa mahakama ya juu zaidi ya kikatiba, Adly Mansur, ameapishwa nchini Misri kuwa rais wa muda baada ya jeshi kumng'oa madarakani rais aliyechaguliwa na raia kwa njia ya kidemokrasia na kushinda kwa wingi wa kura, Mohammed Mosri.
Viongozi duniani wamepokea kwa tahadhari matukio yanayojiri huko Misri. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amewaambia waandishi kwamba anaangalia kwa umakini hatua iliyochukuliwa na jeshi la Misri.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza , William Hague, amesema Uingereza haiungi mkono uvamizi huo wa kijeshi lakini haina budi kuitambua hatua hiyo na kusogea mbele. Hata hivyo alikataa kulishutumu jeshi kwa kumpindua Morsi akisema ni uvamizi ulioungwa mkono na watu wengi. Mfalme Abdalla wa Saudia ametuma ujumbe wa hongera kwa kaimu rais wa Misri akisema kwamba uteuzi wake unajiri katika wakati muhimu.
Mkuu wa jeshi Generali Abdul Fattah al-Sisi alitoa tangaza hilo kupitia televisheini Jumatano jioni, katika kile Morsi, alisema ni mapinduzi ya kijeshi.
Generali Sisi alisema kuwa Morsi,ambaye ni rais wa kwanza kuchaguliwa amekosa kutimiza mahitaji ya watu.
Kaimu rais huyo mpya ameahidi kurejesha hali ya amani nchini humo wakati akielekea kuitisha uchaguzi mkuu hapo baadaye.
Ishara ya mapenzi iliyochorwa angani kwa kutumia ndege za kijeshi kuwataka wananchi kupatana
Hatua hiyo inakuja baada ya siku nyingi ya maandamano, dhidi ya rais Morsi wa chama cha Musolim Brotherhood, ambaye inaelezwa anashikiliwa katika kambi moja ya kijeshi nchini humo.
Waandamanaji walimtuhumu yeye na chama chake kwa kusukuma ajenda ya kiisilamu kwa taifa hilo na kukosa kusuluhisha matatizo ya kiuchumi yanayokumba taifa hilo.
Chama cha Muslim Brotherhood kimesema kuwa bwana Morsi pamoja na washauri wake wako chini ya kifungo cha nyumbani na hawana mawasiliano ya nje.
Hapo awali mkuu wa majeshi alisema kuwa katiba ya nchi hiyo imeahirishwa na kwamba jaji mkuu wa taifa hilo atachukuwa mamlaka ya rais.
Maelfu ya waandamanaji wanaompinga bwana Morsi mjini Cairo walisherehekea kwa shangwe na vifijo kufuatia taarifa hiyo ya jeshi lakini wale wanaomuunga bwana Morsi wanasemekana kubaki kimya huku wakisubiri matukio yatakayofwata.
Rais Obama amesema kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na matukio yaliyopo nchini Misri huku katibu mkuu wa umoja wa mataifa Banki Moon akitaka kuwe na utulivu.

BBC