STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 6, 2013

Aishi Manula achekelea ushindani Ligi Kuu

Kipa Aishi Manula
KIPA mahiri anayedakia timu ya Azam FC na timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Aisha Manula, amesema anafurahishwa na hali ya ushindani uliojitokeza mapema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Manula, miongoni mwa wachezaji chipukizi waliopo kikosi cha Kim Poulsen kinachojiandaa na mechi ya kukamilisha ratiba kati ya Tanzania na Gambia, alisema kwa mwendo ulianza kwenye ligi hiyo ni wazi msimu huu ni mgumu.
Kipa huyo aliyewahi kuwa kipa bora wa michuano ya Uhai Cup 2011, alisema matokeo ya kustaajabisha yaliyojitokeza katika mechi za raundi mbili za awali ni dalili za kuwa na msimu mgumu ulioweza kutabirika kirahisi.
"Nafurahishwa na namna ligi ilivyoanza, inaonyesha itakuwa ya aina yake msimu huu kwani timu zinaonyesha kupania kufanya vyema na ndiyo maana mechi mbili za awali za kila timu kumekuwa na matokeo yaliyostaajabisha, " alisema. Manula, alisema kwa upande wa klabu yake ya Azam anaamini huu utakuwa ni msimu wake wa kuweka rekodi kwa kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka nenda taji hilo kuzunguka klabu za Simba na Yanga.
Kipa huyo aliyekuwa dimbani wakati Azam ikizamishwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya Ngao ya Hisani, alisema haoni kitakachoizuia Azam isitimize ndoto ya kutwaa taji la Ligi Kuu mwaka 2013-2014.
Azam washindi wa pili wa misimu miwili mfululizo, ilianza ligi hiyo kwa mechi za ugenini ikipata sare ya 1-1 kwa Mtibwa Sugar kabla ya kuilaza Rhino Rangers  2-0 mjini Tabora na mechi ijayo itakuwa Kagera kuvaana na Kagera Sugar.

Mauaji ya kinyama! Waendesha Bodaboda wazidi kuuwawa Iringa

Edger Lalika akiwa  wodini kabla ya  kufariki dunia
 Francis Godwin na  Kayanda Mnyanya,Iringa 
 
ZIKIWA  zimepita  siku  chache  toka  mmoja kati ya madereva boda boda mjini Iringa kutekwa kisha  kujeruhiwa vibaya kabla ya kuporwa  pikipiki  yake ,unyama huo dhidi ya madereva  boda boda  umeendelea kutikisa mji wa Iringa baada kijana mmoja mkazi wa kihodombi kutekwa kisha kuuwawa kinyama.
Tukio hilo la kinyama  limetokea  usiku  wa  leo baada ya kijana  huyo aliyetambulika kwa  jina la Edger Lalika kukutwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani .
Mashuhuda  wa  tukio hilo  wameueleza mtandao  huu wa matukio daima .com kuwa tukio la kuuwawa  kwa  dereva  boda  boda  huyo liletokea eneo la  Tosamaganga wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Hata  hivyo kijana  huyo anayekadiliwa  kuwa na umri wa miaka 20,ameuwa akiwa anafanya shughuli zake za bodaboda baada  ya  kukodiwa na mteja  wake huyo ambae aliamua  kuitoa roho yake kabla ya kumpokonya boda boda.
Kutokana na tukio  hilo  baadhi ya madereva bodaboda wamelaani vikali kitendo hicho na kuwataka madereva bodaboda wengine kuungana na kushirikiana na jeshi la polisi kufichua vitendo hivyo  vya utekaji na mauwaji  dhidi ya madereva  boda boda.
Mazishi ya kijana huyo yanafanyika leo katika makaburi ya mlolo Iringa mjini
Jeshi la  polisi mkoa  wa Iringa  limethibitisha  kutokea kwa mauwaji  hayo.

Matukio Daima

Mhe. Ndugai atupiwa lawama vurugu za jana bungeni

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgbR2CeEeeh8aIgUAxVg23rr5e1DG0s7zx41yhCH6ZY0ziYoTLNSlZ-GP5_9Ea0yd37vWfoS1hBkiDketxjf3x7RCdF75YebSxZRnTJ2pZrrF6f6fURo2Bm3aA0BXX6bHz5R5_eUhGDKMDI/s400/_MG_0724+MBILI.JPG

Wanabodi, 
Mwaka mmoja uliopita niliwahi kuleta hoja hii humu Wito: Wabunge Badilini Kanuni Kuondoa Udikteta wa Spika/N.Spika!
Leo nimeikumbuka kufuatia vurugu za jana bungeni!.
Chanzo cha vurugu zile ni "Ukosefu wa Busara Ndogo Tuu toka kwa Naibu Spika!".
Tangu tumepata uhuru, Tanzania imekuwa nchi ya chama kimoja kwa kipindi kirefu, tulipoingia mfumo wa vyama vingi ile 1992, tulifanya marekebisho tuu ya kanuni, ila hatukuweza kufanya mabadiliko ya "mind set" toka mfumo wa chama kimoja hadi mfumo wa vyama vingi, hivyo hali hii imeendelea mpaka sasa kwa CCM ambayo ndio chama tawala, kuendelea kuonekana ni chama dola kwa sababu ndiyo inayoongoza dola, na nafasi ya vyama vya upinzani kuonekana vipo vipo tuu kwa vile vimeanzishwa kwa mujibu wa sheria!.
Kufuatia hali hii ya "CCM Supremacy" kunapelekea viongozi wa mihimili mikuu ya nchi, Bunge, Mahakama na Serikali, kutimiza wajibu wake kwa mlengo wa heshima kwa CCM kwa sababu M/Kiti wa chama tawala ndie head of Executive, ambaye ndiye rais wa nchi anaeteua kila mtu!.
Huku kujikomba komba kwa CCM, kumepelekea hata Spika na Naibu Spika ambao walipaswa kutimiza majukumu yao independently, wanajikuta wakiifavour CCM, kwa lengo la kujikomba komba huku wakiliangamiza taifa bila wao kujijua kwa kisingizio kuwa kwa vile CCM ndio chama tawala!.
Kwa mujibu wa uendeshaji wa mabunge ya vyama vingi, Mkuu wa shughuli za serikali bungeni, ambaye ni Waziri Mkuu, na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, KUB, ambaye ni Mhe. Freeman Mbowe, wana hadhi sawa kabisa ndani ya bunge!. Hakuna mmoja ambaye ni mkubwa zaidi ya mwingine wala hakuna aliyebora zaidi ya mwenzake!. Wako sawa sawa kabisa!.
Vivyo hivyo, hadhi za mawaziri na mawaziri vivuli ndani ya bunge ni sawa kabisa, tofauti pekee ni mawaziri wana means zaidi kutokana na uwezeshaji kiliko hawa vivuli!. Mfano Waziri Magufuli, akishakagua barabara au kuizindua, waziri kivuli alipaswa aifanyie ukaguzi na kutoa mawazo yake kama ni chini ya kiwango etc, etc.
Haki zote za Waziri Mkuu bungeni ndizo pia haki za KUB!. 
Japo haijaandikwa kwenye kanuni yoyote kuwa Waziri Mkuu akisimama, "ni lazima spika ampe ruhusa ya kusikilizwa" no matter what!. Spika hana mamlaka yoyote ya kuamua kutomsikiliza Waziri Mkuu anaposimama kwa hoja yoyote!. Vivyo hivyo, spika au naibu spika, "hana mamlaka!" ya kumzuia KUB kuzungumza!. 
Naomba wale wenye mapenzi mema na nchi hii, hebu tuwe wakweli toka ndani ya nafsi zetu, hivi kweli pale bungeni jana, angesimama Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, hivi kweli Naibu Spika angemwambia "Kaa Chini?!". Angeendelea kusimama hivi Naibu Spika angewaamuru askari wa bunge kumtoa nje?!.
Hadhi ya KUB ni sawa kabisa na Waziri Mkuu, kitendo cha Naibu Spika kumzuia KUB asizungumze, kumuamuru akae chini na kisha kuamuru atolewe nje, "that was provocation kwa wapinzani wote wa kweli!", kiliwatia hasira, na kilichofuata ni actions in provocation!. Chanzo ni ukosefu wa busara ndogo tuu wa Naibu Spika!.
Laiti Mhe. Naibu Spika, angelimruhusu KUB kuzungumza na kuisikiliza hoja yake!, naamini 100% kwa 100%, yote yaliyofuatia yasingetokea!.
Bungu letu lina mapungufu makubwa na ya msingi ya kikanuni za uendeshaji mabunge ya vyama vingi!. Kiukweli kila kunapotokea vurugu bungeni, mimi huwa namkumbuka sana Mhe. Samuel Sitta!.
Kiukweli huko nyuma nimewahi kulalamikia sana uendeshaji wa bunge wa Madam Spika, Mhe. Anna Makinda, lakini sasa sasa nakiri, pamoja na mapungufu yake yote ya kibinaadamu, Mhe. Anna Makinda is better of 100 times than Mhe. Job Ndugai!. This man is a disaster!. 
Wabunge tumieni kanuni namba 135-(1) Kutuondolea mtu huyu, japo najua wabunge wa CCM watautumia wingi wao vibaya kutoipitisha hoja hiyo, ile tuu process ya "kukataliwa!" ni funzo tosha!.
Mwaka mmoja uliopita nilitoa angalizo hili, na leo nalitoa tena! Wito: Wabunge Badilini Kanuni Kuondoa Udikteta wa Spika/N.Spika!

Wasalaam.
Pasco.

Chanzo : JamiiForums

Msikiti wa Answar Sunna wateketea kwa moto, kisa...!

 
MSIKITI mkubwa wa Answar Sunna  uliopo  barabara ya Saba mjini Dodoma  umewaka  moto  mchana  huu  ikiwa  ni  muda  mfupi  baada  ya  swala  ya  mchana  kumalizika.

Akiongea  kwa  njia  ya  simu  mmoja  wa  mashuhuda  walioshuhudia  tukio  hilo  amedai  kuwa  chanzo  cha  moto  huo  ni  moto wa  JIKO  la  wakazi  wa    ghorofa ya  juu  ya  jengo  la  msikiti  huo...

Hata  hivyo, shuhuda  mwingine  aliyeongea  na  mtandao  huu  amedai    kuwa  chanzo  cha  moto  huo  ni  hitilafu  ya  umeme  iliyoanzia  ghorofa  ya  juu  ya  jengo  hilo.

 
Kwa  mujibu  wa  mashuhuda  hao, moto  huo  umefanikiwa  kudhibitiwa  na  jeshi  la  zima  moto  na  kwamba  hakuna  mtu  aliyepoteza  maisha  kutokana  na  moto  huo.


  
MPEKUZI

Anko Kitime, Shigongo, Msama waula BASATA

Profesa Penina Mlama
Na Veronica Kazimoto – MAELEZO, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Profesa Penina Mlama kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.  
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari - MAELEZO, Uteuzi huo wa Profesa Mlama unaanzia mwaka 2013 na unatarajia kumalizika mwaka 2016.
Prof. Mlama ni Profesa wa Sanaa na Sanaa za Maonyesho Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  
Aidha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara ameteua jumla watu 12 kuwa wajumbe wa BASATA kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka huu.
Walioteuliwa ni pamoja na wawakilishi wa Vyama na Asasi mbalimbali wa Baraza hilo ambao ni Dkt. Vincensia Shule, John Kitime, Angela Ngowi, Dkt. Herbert Makoye, Erick Shigongo na Alex Msama.
Alex Msama
Wawakilishi wengine ni pamoja na Juma Adam Bakari, Daniel Ndagala, Michael Kadinde na Joyce Fisoo.
Wanaoingia kwa mujibu wa nyadhifa zao ni Prof. Hermas Mwansoko na Katibu Mtendaji wa BASATA.
http://www.bongocelebrity.com/wp-content/uploads/2012/06/John-Kitime.jpg
John Kitime 'Anko'
 
Katika hatua nyingine Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amemteua Bwana Ghonche Materego kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa). 
Kabla ya uteuzi huo Materego alikuwa amemaliza muda wake kama Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa.
Wajumbe wa Bodi hiyo walioteuliwa na Waziri Mukangara ni Dkt. Herbert Makoye, Prof. Emanuel Mbogo, Dkt. Lucy Mboma, Prof. Hermas Mwansoko pamoja na Katibu Mtendaji wa BASATA.
Wakati huo huo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara ameteua jumla ya watu 21 kuwa wajumbe wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2013 hadi 2015. 
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjoeAYpD19CUAPAApd52dHguEu911uTkpaFXAq9066MauQU5HEOi7C5LkQMpYFJQ0CXHPoiVJTGw5pvzB3-YujazwtVwQPuZQWhh4elz789G570CD39Q2Vvf-E15sj7DMO2jURIUcZW5jJy/s1600/eric.jpg
Eric Shigongo
Wajumbe hao ni Dkt. Shani Omari, Prof. Yohana Msangila, Ester Riwa, Dkt. Issa Zidi, Khadija Juma na Dkt. Martha Qorro.
Wengine ni Mmanga Mjawiri, Razia Yahaya, Richard Mbaruku, Selina Lyimo, Keneth Konga, Amour Khamis, John Kiango, na Shani Kitogo. 
Wajumbe wengine ni Ally Kasinge, Ahmed Mzee, Rose Lukindo, Shabani Kisu pamoja na Edwin Mgendera.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo la BAKITA atachaguliwa na wajumbe watakapokutana kwenye kikao chao cha kwanza.

Zantel yamleta Azonto, kuwasha moto kesho Dar

Mwanamuziki anayetamba na wimbo wa Azonto kutoka Ghana, Fuse ODG (katikati), akionesha manjonjo yake  wakati wa mkutano na waandishi wa habari, kuhusiana na onesho lake litakalofanyika Jumamosi katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam. Katikati ni Ofisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan. Mwanamuziki huyo ameletwa na Kampuni ya Simu za mkononi ya Zantel kwa kushirikiana na Times FM. (Picha na Francis Dande)
Mwanamuziki anayetamba na wimbo wa Azonto kutoka Ghana, Fuse ODG akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusiana na onesho lake litakalofanyika leo katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Ofisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan.

Wanaombeza bondia Francis Cheka someni hapa!

Francis Cheka (kulia) alipokuwa akimsulubu Mmarekani Phil Williams na kutwaa mkanda wa WBF
HIVI karibuni Mtanzania Francis Cheka ambaye alikuwa  bingwa wa IBF katika bara la Afrika uzito wa kati (Super Middleweight) alimshinda bondia kutoka Marekani Phil William na kutawazwa kuwa bingwa wa dunia anayetambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Dunia (WBF). Ushindi wa Cheka sio tu kwa Tanzania bali na kwa bara la Afrika na dunia yote kwa ujumla.
 
Cheka ameungana na mabingwa wengine wa dunia wa uziro wa kati (Super Middleweight) wanaotambuliwa na vyama na mashirikisho kadhaa kama ifuatavyo:
 
IBF    -  Carl Froch kutoka nchini Uingereza
WBC -  Andre Ward kutoka nchini Marekani
WBA -  Andre Ward kutoka nchini Marekani
WBO -  Robert Stieglitz kutoka nchini Ujerumani
WBF -   Francis Cheka kutoka nchini Tanzania
IBO   -  Thomas Oosthuizen kutoka nchini Afrika ya Kusini

Kwa uchache hao ni mabingwa wa uzito wa uzito wa kati (Super Middleweight ) wanaotambuliwa na vyama/mashirikisho hayo niliyoyataja hapo juu. Kati ya mabingwa wa dunia wa mashirikisho/vyama sita vikubwa duniani Afrika imetoa mabindia wawili tu nao ni Francis Cheka kutoka nchini Tanzania na Thomas Oosthuizen kutoka nchini Afrika ya Kusini.
 
Ubingwa alioupata Francis Cheka ni wa dunia na hautakiwi upingwe na mtu yeyote yule nje ya ulingo bali wanaotaka kumpinga na kuukebehi wanatakiwa wapande naye ulingoni au wamtafutie mtu wao apande naye ulingino ili apigane na Francis Cheka.
 
Kwa bahati mbaya, taratibu na sheria za mchezo wa ngumi haziruhusu mtu yeyote ambaye hayuko kwenye viwango vya ubora wa ngumi agombee ubingwa wa aina yeyote ule.
 
Mashirikisho au vyama vya ngumi vimeweka utaratibu maalum wa mabondia watakaoweza kugombea ubingwa wa dunia na mara nyingi ni wale tu walio kwenye viwango vya juu kuanzia namba moja hadi namba tano.
 
Tanzania sasa tuna bingwa wa dunia katika uzito wa kati (Super Middleweight) na ni Francis Cheka. Tunachukua fursa hii kumfagilia na kumpongeza Francis Cheka kwa kulitangaza vyema jina la Tanzania na kuliweka kwenye chati duniani.
Onesmo Ngowi
Rais wa IBF Africa, Ghuba ya Uarabu na Uajemi na mashariuki ya Kati
 

Stars watua salama Banjui, Kaseja kukaa golini kesho

Juma Kaseja
Na Boniface Wambura
KIKOSI cha Taifa Stars kimewasili salama hapa Banjul, Gambia tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji itakayochezwa kesho (Septemba 7 mwaka huu).

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imewasili hapa jana (Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni ikitokea Dakar, Senegal ambapo ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua kutumia usafiri wa barabara kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko kuingia Banjul badala ya kulala na kuchukua ndege nyingine siku inayofuata.

Wachezaji wako katika hali nzuri na leo jioni wanatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Independence ulioko Bakau ambao utatumika kwa mechi ya kesho. Timu imefikia hoteli ya Seaview iliyoko kandokando ya Bahari ya Atlantic.

Mechi hiyo itaanza saa 10.30 jioni kwa saa za hapa ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 1.30 usiku, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene Ndagijimana, Honore Simba na Issa Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka Liberia.

Washabiki na vyombo vya habari vya hapa wanaizungumzia mechi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia ikiwa imeita wachezaji tisa wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo imepata uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania kuhakikisha haimalizi mechi za mchujo ikiwa na pointi moja tu.

Kwa upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema nia ni kuona Stars yenye pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast ambayo tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho kutoka kundi hili la C.

“Mechi hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka matokeo mazuri ugenini. Lakini kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka katika nafasi ya kuwa wa pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi kwenye viwango vya ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi ya sisi kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim.

Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha.

Yanga yafafanua sakata la Katibu Mkenya

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga (kati) akifafanua jambo wakati wa mkutano wake na wanahabari leo kufafanua suala la ajira ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika leo. (Picha:Francis Dande)
UONGOZI wa klabu ya Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga ametoa ufafanuzi juu ya habari zilizokuwa zimeenea kuhusiana na taarifa za mabadiliko ya kaimu katibu mkuu Lawrence Mwalusako kuondolewa kwenye nafasi yake na kuchukukuliwa na mtu mwingine.
Akiongea na waandishi wa habari leo,  Sanga amesema taarifa hizo hazina ukweli kwamba tayari kuna mtu anachukua nafasi ya Mwalusako, bali kilichotokea ni kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri katika suala hilo kati ya viongozi na wazee.
Kilichopo ni kwamba uongozi wa klabu ya Young Africans upo katika mchakato wa kuhakikisha unajaza nafasi zilizopo wazi za mkurugenzi wa ufundi, mkurugenzi wa masoko, mkurugenzi wa fedha na zoezi hilo linaendeshwa na kampuni moja ambayo waliipa nafasi ya kuendesha zoezi hilo.
Zoezi likiwa ndani ya mchakato mmoja wa waombaji wa nafasi hizo Patrick Naggi aliwasili makao makuu ya klabu ya Yanga kwa lengo la kutaka kujua mazingira ya ufanyaji kazi yakoje na kufahamu baadhi ya mambo kuhusiana na klabu ndipo kulipotokea kutokuelewana na baadi ya wanachama wakiwemo wazee waliokuwepo eneo la klabu.
Kwa maana hiyo napenda kutoa taarifa kwa umma na wanachama wa Yanga kuwa uongozi bado haujatoa baraka za ajira kwa mtu yoyote katika nafasi hizo, isipokuwa ni muombaji aliwahi kufika makao makuu kabla ya mchakatao wa usahili kukamilika.
Lawrence Mwalusako anaendelea kuwa kaimu katibu mkuu wa Yanga mpaka hapo kutakapokuwa na taarifa nyingine zozote za mabadiliko kwa nafasi zote zilizopo wazi katika idara mbalimbali.
Uongozi unawaaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa soka kuwa kitu kimoja katika kuunga mkono harakati za kimaendeleo ili kuifanya timu iende katika hatua nyingine ya ushindani wa kimatifa.

Fundi Kinyambe fumbafu thana

Kinyambe (kushoto) akiwa na Mzee Jangala

MCHEKESHAJI mahiri nchini James Mohammed 'Kinyambe'  amefyatua filamu tatu binafsi ambazo amepanga kuziachia moja baada ya nyingine hivi karibuni.
Kinyambe anayetamba kwenye kipindi cha vichekesho cha 'Vituko Show' alizitaja filamu hizo kuwa ni 'Fundi Kinyambe', The Twins na ' Fumbafu Thana' kuanzia Novemba mwaka huu.
Akizungumza na MICHARAZO, Kinyambe alisema filamu hizo amepanga kuziachia moja moja kuanzia Novemba mwaka huu.
Kinyambe alisema filamu hizo za vyumba mbavu ameigiza na wasanii mbalimbali nchini wakiwamo wenzake wanaoigiza nao katika kipindi cha 'Vituko Show'.
"Ni kati ya kazi zinavyomfanya mtazamaji ashikilie mbavu zake mwanzo mwisho, nitaanza kuziachia rasmi Novemba nikianza na 'Fundi Kinyambe' kisha 'The Twins' na kumalizia 'Fumbafu Thana'," alisema Kinyambe.

Afande Sele kuzindua Novemba

Afande Sele

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Seleman Msindi 'Afande Sele' anatarajia kufanya uzinduzi wa albamu yake mpya iitwayo 'Kingdom wa Amani na Upendo' utakaofanyika Novemba mwaka huu mjini Morogoro na kusindikizwa a  wasanii mbalimbali nyota wa hapa nchini.
Akizungumza na MICHARAZO Afande Sele, alisema kwa sasa ni mapema kuwataja wasanii watakaomsindikiza kwa sababu anaendelea kumalizana na wadhamini wake.
Alisema kwa sasa anajipanga kuitambulisha albamu hiyo kwa kuachia video ya wimbo unaoendelea kutamba wa 'Dini Tumeletewa' alioimba kwa kushirikiana na Belle 9.
Mkongwe huyo alisema albamu hiyo itakuwa na nyimbo 10 na siku za uzinduzi itaachiwa 'audio' na video yake kwa mpigo ili mashabiki wake wapate vitu kamili kwa wakati  mmoja.
Alitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo ni pamoja na 'Dini Tumelewa', 'Amani na Upendo', 'Soma Ule', 'Mi Sielewi', 'Karibu Moro', 'Sukari na Chai', 'Simba Dume na 'Kingdom'.

Kinondoni yainyuka Pwani 7-0 Copa Coca Cola


MABINGWA mara mbili wa Copa Coca-Cola timu ya Kinondoni imewapa kipigo kikubwa wenyeji timu ya Pwani cha magoli 7-0 katika mashindano yanayoendelea ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya Copa Coca-Cola ngazi ya kanda kwenye uwanja wa Tumbi, Kibaha juzi jioni.
Kinondoni walipata goli lao la kwanza katika dakika ya 4 kupitia kwa Kidanga Hamadi baada ya kuunganisha krosi kutoka upande wa kulia. Hamadi kwa mara ya pili alitikisa nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 11 baada ya kuwapiga chenga mabeki wa timu ya Pwani na kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.
Magoli mengine yalifungwa na Alex Milanzi katika dakika ya sita, Oswin Nungu katika dakika ya 20, Ayubu M. Ayubu katika dakika ya 41, Majid Musa katika dakika ya 66 kwa njia ya penati na Aboubakari Mussa alihitimisha karamu ya magoli katika dakika ya 74.
Katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza, Geita waliifunga Mara 1-0 katika mechi iliyojaa ushindani.
Kigoma hawakuwa na bahati siku ya Jumatano baada ya kupoteza mchezo dhidi ya wenyeji timu ya Mwanza kwa kufungwa  2-1. Beki wa Kigoma, Hashimu Mussa alijifunga mara mbili katika dakika ya kwanza na ya 72. Kigoma walipata goli lao katika dakika ya 36 kupitia kwa Rashidi Bakari.
Mechi nyingine iliyochezwa katika uwanja huo wa chuo cha ualimu Butimba, Tabora waliilaza Simiyu 2-1. Tabora  walipata goli la kwanza katika dakika ya sita kupitia kwa Selemani Husein kwa njia ya penati kabla ya Rashidi Omary kuhitimisha katika dakika ya 54.
Mechi nyingine katika uwanja wa Butimba juzi iliwakutanisha Shinyanga na Kagera ambapo Shinyanga walishinda 3-0. Magoli ya Shinyanga yalipachikwa wavuni na Anwar Amada katika dakika ya 24, Jahid Nuru dakika ya 60 na Felix Rweyemamu dakika ya 74.
Katika uwanja wa Mkokotoni , Zanzibar , Timu ya Kaskazini Pemba na Kusini Unguja walitoka sare ya 3-3 wakati huo huo Tanga na Temeke nao walitoka sare ya 4-4. Na katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Singida  waliilaza Manyara kwa mabao 2-0.
Fainali za Taifa za Copa Coca-Cola zinahusisha timu 16 ambazo zitaanza kuchuana wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

Kaliza wa TRA afagilia masumbwi

Meneja wa Tanzania Revenue Authorithority 'TRA' Mkoa wa Dodoma Bw. Thadeo Kaliza katikati akiwa na promota na mdau wa masumbwi Mohamedi Bawazir kushoto Bondia Fransic Cheka na Fransic Miyeyusho wakati walipokwenda Dodoma kutembelea bunge la jamuhuri ya muhungano wa Tanzania baada ya Cheka kutwaa ubingwa wa Dunia wa WBF na kualikwa chakula cha jioni na meneja huyo mjini Dodoma
Baadhi ya wadau wa masumbwi na mabondia wakigongesheana grass na Meneja wa Tanzania Revenue Authorithority 'TRA' Mkoa wa Dodoma Bw. Thadeo Kaliza wakati wa kutakiana heri baada ya wadau hawo wa masumbwi kupewa heshima ya kutembelea bungeni kwa mara ya kwanza 

Baadhi ya wadau wa masumbwi na mabondia  wakiwa katika picha ya pamoja na  Meneja wa Tanzania Revenue Authorithority 'TRA' Mkoa wa Dodoma Bw. Thadeo Kaliza
Baadhi ya wadau wa masumbwi na mabondia wakigongesheana grass na Meneja wa Tanzania Revenue Authorithority 'TRA' Mkoa wa Dodoma Bw. Thadeo Kaliza wakati wa kutakiana heri baada ya wadau hawo wa masumbwi kupewa heshima ya kutembelea bungeni kwa mara ya kwanza  na kuarikwa kwa chakula cha jioni na meneja huyo
Baadhi ya wadau wa masumbwi na mabondia wakigongesheana grass na Meneja wa Tanzania Revenue Authorithority 'TRA' Mkoa wa Dodoma Bw. Thadeo Kaliza wakati wa kutakiana heri baada ya wadau hawo wa masumbwi kupewa heshima ya kutembelea bungeni kwa mara ya kwanza