STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 1, 2015

CHELSEA, SPURS KATIKA FAINALI YA KISASI

KLABU za Chelsea na Tottenham Hotspur zinatarajiwa kuvaana leo katika pambano la kisasi la fainali za Kombe la Ligi (Capital One).
Pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Wembley linarejesha mchezo wa fainali za mwaka 2008 ilizozikutanisha timu hizo kwenye uwanja huo na Spurs kuitambia Chelsea kwa mabao 2-1.
Katika pambano hilo lililochezwa Februari 24, 2008, Spurs ilinyakua taji hilo katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1 Chelsea wakitangulia kabla ya Spurs kurejesha.
Kadhalika pambano hilo la Fainali hizo za Kombe la Ligi limekuja ikiwa ni wiki kadhaa tangu Spurs walipoitoa nishai Chelsea kwa kuichapa mabao 5-3 katika pambano la marudiano ya Ligi Kuu ya England.
Awali Spurs ilicharazwa mabao 3-0 nyumbani kwa Chelsea mwaka uliopita na waliporudiana White Hart Lane waliwashughulikia Chelsea jambo linalofanya mechi ya leo kujaa visasi vitupu.
Chelsea chini ya Jose Mourinho itawakosa baadhi ya nyota wake akiwamo Nimanja Matic aliyefungiwa mechi mbili baada ya kupungiwa adhabu na FA kwa kadi nyekundu aliyoipata wiki iliyopita.
Hata hivyo timu hiyo inapewa nafasi kubwa ya kuwatambia wapinzani wao ambao wanauguza machungu ya kung'olewa kwenye michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya (UEFA Europa League) na Fiorentina ya Italia.
Ikiwa na wakali kama Ces Fabrigas, Diego Costa, Eden Hazard, Willian na wengine, Chelsea itapenda kutwaa taji hilo ili kuweka hazina kwa msimu huu baada ya awali kutolewa katika Kombe la FA.
Vinara hao wa Ligi Kuu wanapaswa kuwa makini na kinda linalotisha Harry Kane ambaye amekuwa wakiwaliza makipa hodari kama alivyoonya kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois.
Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimeshakutana mara 134, Chelsea ikishinda mara 57 na wapinzani wao mara 44 na mechi 33 zikiisha kwa sare na pambano la leo litakuwa la 135 kwao katika michuano yote.
Je, ni Chelsea au Spurs atakayecheka leo katika uwanja wa Wembley? Bila shaka ni suala la kusubiri kuona ila kwa hakika ni bonge la mechi.

Arsenal, Manchester City vitani tena EPL

WAKIWA na maumivu ya vipigo walivyopata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, klabu za Arsenal na Manchester City zitakuwa tena vitani leo kwenye viwanja tofauti katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Arsenal walikandikwa mabao 3-1 na Monaco ya Ufaransa itakuwa nyumbani kuumana na Everton, wakati Manchester City watakuwa wageni uwanja wa Anfield kupepetana na Liverpool.
Mabingwa watetezi hao walikumbana na kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Barcelona, na leo watakuwa na kazi ngumu mbele ya Liverpool ambayo imekuwa na matokeo ya kuvutia siku za karibuni.
Katika mechi nne zilizopita za ligi hiyo, Liverpool haijapoteza mchezo wowote, pia ikishinda katika Kombe la Ligi na Ligi Ndogo ya Ulaya.
Zilipokutana mara ya mwisho Agosti 25 mwaka jana katika mechi ya mkondo wa kwanza Liverpool ilinyooshwa na Manchester City kwa mabao 3-1 ugenini hivyo leo kulazimika kulipa kisasi kwa wageni wao.
Kocha wa Man City, Manuel Pellegrini amesisitiza umuhimu wa kupata ushindi katika mchezo huo wa ugenini ili kuweza kupunguza pengo la pointi dhidi ya Chelsea wanaoongoza msimamo wakiwa na pointi 60.
Katika mechi itakayochezwa Emirates, Arsenal itavaana na Everton ambayo katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Agosti 23 mwaka timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutosa sare ya mabao 2-2.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger aliyewashutumu vijana wake kwa kipigo cha Monaco atakuwa na kazi ngumu ya kuwaongoza kikosi chake kupata ushindi nyumbani ili angalau kuwafukuzia Man City.
Wenger anatambua ni michuano miwili tu mpaka sasa ndiyo wana hakika ya kutwaa taji kama watakomaa, Kombe la FA wanaotetea na watakaovaana naManchester United wiki ijayo na michuano ya ligi.
Nafasi ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ni finyu baada ya kipigo cha Monaco wakilazimika kuhakikisha wapate ushindi wa 3-0 wiki mbili zijazo nchini Ufaransa.
Everton wenyewe wamekuwa na mwenendo wa kuchechemea msimu huu, ingawa siyo timu ya kubezwa kwani inaweza kufanya lolote katika pambano hilo la leo.

Newz Alert! Chenge, Prof Tibaijuka wapigwa 'stop' CCM

WAJUMBE WA NEC NA VIOMNGOZI WAO WAKIWA KWENYE MKUTANO
http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2014/09/Anna-Tibaijuka.jpg
Prof Anna Tibaijuka

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgS27oyoYZIdbDtS0MoyijSDuiv-YrMjmoWZrojqWZkPwyqY_vw17QyE8ysEJ5E1Zc0kZ07135oIEJ1TkjFSxFGvTdXaxVJvwgpQdHdsMkac0L85zDaG5h_5MlobwaDS5lEnMj0GYtWSdc/s1600/chenge-june18-2013.jpg
Mzee wa Vijisenti, Chenge

KAMATI KUU ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetangaza kuwasimamisha Wajumbe wake wanaotuhumiwa kwenye sakata la wizi wa fedha za akaunti ya Tegete Escrow kuhudhuria vikao hivyo.
Taarifa rasmi iliyotolewa na CCM inasoma kama ifuatavyo;

KAMATI KUU ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo tarehe 28/8/2015, kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa kumi na moja alasiri, kimeazimia yafuatayo;
- Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, msanii wa Chama na Kada wa muda mrefu Mheshimiwa John Damian Komba.

Mwenyekiti wa CCM, Mhe Dr Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea kuwa msiba huo ni pigo kubwa kwa Chama hasa katika wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi na pengo ambalo ni vigumu kuliziba.

CCM imepata pigo na Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Kapteni John Damian Komba.

Kazi yake kubwa ndani ya Chama itaandikwa katika historia iliyotukuka ya Chama Cha Mapinduzi.

- Pia, kutokana na Kikao cha Kamati Kuu iliyopita iliyoiagiza kamati ya maadili kuwaita na kuwahoji wanachama na viongozi watatu waliotajwa kuhusika na kashfa ya Escrow.

@ Mheshimiwa Anna Kajumulo Tibaijuka
@ Mheshimiwa William Mganga Ngeleja
@ Mheshimiwa Andrew Chenge

Baada ya Kamati ya Maadili kuwahoji, Kamati Kuu imeazimia kuwasimamisha kuhudhuria vikao ambavyo wao ni wajumbe ikiwemo Kamati kuu kwa Mama Tibaijuka na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa Mheshimiwa Chenge na Ngeleja.,wakati ambapo kamati ndogo ya maadili ikiendelea na uchunguzi wa kuhusika kwao katika kashfa hiyo.

- Pia, Kamati Kuu imejadili suala la Adhabu iliyotolewa kwa wanachama sita ambao walibainika kuvunja Kanuni na sheria za Chama kwa kuanza Kampeni kabla ya wakati na imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuendelea kuchunguza mienendo ya wanachama hao katika kipindi walichokuwa wanatumikia adhabu zao. Na kisha taarifa hiyo ya Kamati ndogo ya maadili itawasilishwa kwa Kamati Kuu.