STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 29, 2012

Mapembe: Fundi 'mvunja mbavu' aliyejitosa kwenye muziki

TANGU utotoni, aliwavutia watoto na wanafunzi wenzake kwa kipaji cha kuchekesha, ila hakujitambua au kuota kama kipaji hicho kingemtoa kimaisha. Ndio maana mara alipohitimu darasa la saba katika Shule ya Kiwalala, Lindi alijitosa kwenye ufundi uashi na baada umakenika katika miji tofauti. Hata hivyo alivyotua Dar na kufanya kazi ya udereva wa daladala ndipo alipobaini alikuwa amechelewa mno, baada ya msanii Khalfan Ahmed 'Kelvin' kukitambua kipaji chake na kumshawishi kuingia kwenye sanaa. Wengi wanamfahamu kama 'Mapembe' ila majina yake kamili ni Ismail Makomba mmoja wa wachekeshaji mahiri nchini. Mapembe alisema wazo la Kelvin alilipuuza kwa kudhani angepoteza muda bure, lakini alipong'ang'aniwa aliamua kujiunga na kundi la msanii huyo la Simple Production na kuanza kuonyesha makeke. Mkali huyo aliyevutiwa kisanii na Abdallah Mkumbira 'Muhogo Mchungu' alicheza kazi yake ya kwanza mwaka 2003 iitwayo 'Sheria' kisha kufuatiwa na 'Lugha Gongana', 'Talaka ya Mdundiko', 'Msela Nondo' na 'Ngoma Droo' na nyingine. Alijitoa kwa ruksa Simple Production na kuanzisha kampuni binafsi ya Karena Production iliyozalisha filamu tano za Trafiki, Mdimu, Mbagala, Kiduku, Mpambano na sasa akijiandaa kuingiza sokoni 'Posa' akiwa pia ni muajiriwa wa kampuni ya Al Riyamy. Mapembe ambaye pia ni mwanaharakati anajishughulisha pia na muziki akiwa ameshatoa nyimbo kadhaa na kwa sasa yupo studio kukamilisha kibao kiitwacho 'Gesi ya Kusini'. Nyimbo zake nyingine zinazotamba hewani kwa sasa zikiwa katika miondoko ya Zouk ni Mwalimu, Nandenga, Usalama wa Raia, Muungano na Ubaya wa Mafisadi. Mapembe anayemshukuru Kelvin na kampuni ya Al Riyamy kumfikisha alipo, anajipanga kurudi 'darasani' Chuo cha Taifa cha Sanaa Bagamoyo ,TaSUBA, ili kuongeza maarifa. Mume huyo wa mtu na baba wa mtoto mmoja aitwae Makomba, alisema sanaa Bongo imepiga hatua kubwa, isipokuwa tatizo la wizi unaofanywa na watu wachache. Aliiomba serikali iwasaidie wasanii kunufaika na kazi zao kwa kuweka sheria kali za kuthibiti maharamia hao, huku akiwataka wasanii wenzake kupendana na kushirikiana. Pia aliwakumbusha wasanii wenzake wasijikite kutoa kazi zao katika nyanja za mapenzi na kusahau mambo mengine ikiwemo masuala ya kisiasa na kijamii, kama anavyofanya yeye kupitia muziki aliojitosa hivi karibuni. Mapembe alizaliwa Januari, 1972 Kiwalala, Lindi akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Kiwalala kabla ya kujishughulisha na kazi za ufundi uashi, magari na udereva na baadae kuingiza kwenye uigizaji.

Mobby Mpambala: Asiyeamini kama filamu zimempa nyumba, gari na kampuni

ALIPOSHAWISHIWA na nyota wa filamu nchini, Single Mtambalike 'Rich', aingie katika fani ya uigizaji, Mobby Mpambala, hakutilia maanani wazo hilo kutokana na imani aliyokuwa nayo juu ya sanaa ya Tanzania kwamba hailipi. Hata hivyo baada ya ushawishi wa muda mrefu na kuamua kujitosa rasmi mwaka 2000, msanii huyo amejikuta 'akiisujudia' fani hiyo kwa jinsi ilivyomwezesha kiuchumi na kimaisha tofauti na alivyofikiria mwanzoni. Mkali huyo wa filamu za mapigano na zile za kutisha, alisema kipindi kifupi cha kuweko kwake kwenye sanaa hiyo imemwezesha kujenga nyumba katika kiwanja alichokuwa nacho eneo la Gongolamboto, kununua gari na kumudu kuanzisha kampuni binafsi ya kuzalisha filamu ya 'Wizaga Entertainment'. Pia, msanii huyo anamiliki kundi la sanaa la Mtazamo Family linalojihusisha na sanaa za ngoma, maigizo na sarakasi huku akiendesha kiwanda kidogo cha kutengeneza masofa na samani nyingine za majumbani eneo la Amana-Ilala. "Sio siri kabla ya kuingia kwenye sanaa niliidharau fani hii kutokana na hali ya mambo ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wasanii hawakuwa na chochote cha kujivunia, lakini leo nakiri sanaa Bongo inalipa kutokana na mafanikio makubwa niliyoyapata katika kipindi kifupi," alisema. Mpambala alisema alikutana na Rich mwaka 1996 na kumtaka ajiunge kwenye sanaa baada ya kugundua kipaji chake na umahiri wake wa michezo ya Kungfu na utunisha misuli, ila alimpuuza kwa vile aliringia ujuzi wake wa ufundi seremala. Alisema hata hivyo shinikizo la Rich pamoja na ndugu na jamaa zake waliotambua kipaji alichonacho, ndipo mwaka 2000 alipojitosa kwa kushiriki filamu ya 'Kidole Tumbo' iliyozuiwa na serikali kutoka. Mpambala alisema Rich 'alimbeba' kwa kumshirikisha katika kazi zake kadhaa kama 'Swahiba', iliyomtambulisha kwa mara ya kwanza yeye na Rose Ndauka, 'Mahabuba' na 'Heshima ya Penzi'. Alisema kazi hizo zilimfungulia neema kwa kushirikishwa kazi nyingine kadhaa zinazofikia 30 kwa sasa, akizitaja baadhi kuwa ni; 'Kamanda', 'Jozani', 'Signature', 'Secretary', '007', 'Time to Fight, 'Zuadiswa', 'Before Death', 'Hii ni Tatu', 'Criminal', 'Jamal' na 'The Chase' aliyoitaja kama filamu bomba kwake. AMRI PURI Mpambala, alisema licha ya kwamba hakuwahi kuota kuwa msanii, lakini alimzimia mno nyota wa zamani wa filamu za Kihindi, Amri Puri 'Mzee Ashanti', ambaye kwa sasa ni marehemu. Alisema alivutiwa na Amri Puri, kwa aina yake ya uigizaji kama mbabe na jitu katili, kitu alichodai amekuwa akimuiga katika baadhi ya picha alizocheza kama njia ya kumuenzi mkali huyo wa Bollywood. Mpambala anayezishabikia Simba na Manchester United, akipenda kula ugali kwa dagaa na kunywa soda ya Pepsi, alisema hakuna kitu cha furaha kwake kama siku alipomuoa mkewe wa kwanza aitwae, Jasmine mwaka 2004 na ndoa nyake ya pili dhidi ya Zola mwaka 2011. "Kwa kweli siku nilipofunga ndoa na wake zangu hawa ndio tukio la furaha kwangu, na ninahuzunishwa na kifo cha baba yangu mlezi, Abdul Ally Kibena aliyefariki mwaka 1999," alisema. Mpambala, anayechizishwa na rangi ya bluu, alisema kingine kinachompa furaha ni kufanikiwa kufyatua kazi zake binafsi tano za filamu kupitia kampuni yake ya Wizaga. Alizitaja kazi hizo kuwa ni 'I Wonder', My Brother', 'Criminal' aliyoshirikiana na 'Carlos', 'Fuvu' na 'Anti Virus' anazotarajia kuziingiza sokoni hivi karibuni. SKENDO Mpambala anayemzimia 'swahiba' wake Haji Adam 'Baba Haji', alisema kati ya vitu vinavyomkera ni tabia ya baadhi ya wasanii chipukizi kupenda kujihusisha na skendo kwa nia ya kutafuta umaarufu. Alisema vitendo vinavyofanywa na wasanii hao wasiojitambua vinaidhalilisha fani yao pamoja na kuzichafua familia za wasanii hao, licha ya wenyewe kuonekana kutojali. Mkali huyo mwenye watoto sita, alisema ifike wakati wasanii watambue umaarufu hupatikana kupitia umahiri wa kazi zao na sio kujidhalilisha ovyo magazetini. Mpambala anayependa kutumia muda wake wa ziada kufanya mazoezi na kuendesha kazi za useremala katika kiwanda chake na kundi lake la sanaa lililotoa ajira kwa vijana 30, alisema kama angekutana na Rais au Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, angeomba sanaa isaidiwe. "Ningewaomba wasaidie iundwe kwa sheria kali ya kuthibiti wizi wa kazi za wasanii sambamba na kuwepo kwa mipango mizuri ya kutambuliwa kwetu kama ilivyo kwa watu wa kada nyingine wanaothaminiwa na kuenziwa nchini." ALIPOTOKA Mobbi Nassor Saleh Mpambala 'Mobby Mpambala', alizaliwa Novemba 28, 1965 katika wilaya ya Igunga,Tabora akiwa mtoto wa tatu kati ya nane wa familia yao. Alisoma elimu yake ya Msingi katika Shule ya Makurumla, jijini Dar kabla ya kurejea Tabora kumfuata mama yake aliyekuwa ametangana na baba yake na kujishughulisha na biashara ndogo ndogo huku akijiendeleza kwenye michezo ya sarakasi na kungfu aliyoicheza tangu utotoni. Mpambala anayewashukuru wazazi wake, Rich na mkewe wa kwanza Jasmine kwa namna walivyomsaidia kufika mahali alipo, amejaliwa kuwa na watoto sita watatu akiwapata katika ndoa yake ya kwanza nao ni Edo, 27, Mariam22 na Saleh,20. Watoto wake wengine ni Goodluck, 18, anayesoma Sekondari jijini Arusha, Zuwena, 13 aliyepo darasa la sita katika Shule ya Msingi Mapinduzi-Kigogo jijini Dar na Munira, 5 anayesoma chekechea.

TPBO yasitisha mapambano kisa....!

ORGANAIZESHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), imesitisha kwa muda mapambano yao yote ya ngumi ili kupisha mfungo wa Mwezi wa Ramadhani. Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema wamechukua uamuzi huo ili kuwapa nafasi mabondia na mashabiki wa ngumi kujikita kwenye ibada hiyo ya funga ambayo ni moja ya nguzo tano na muhimu kwa maisha ya waumini wa dini ya Kiislam. Ustaadh, alisema kusitishwa kwa michezo hiyo haina maana kwamba TPBO haifanyi kazi, kisha akafafanua kuwa ofisi zao zinaendelea kufanya kazi kama kawaida isipokuwa haitaruhusu pambano lolote katika kipindi hiki cha mfungo. "TPBO, tumesimamisha mapambano yote ya ngumi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuungana na waislam katika utekelezaji wa ibada yao ya funga, ingawa ofisi zetu zilizopo Temeke Mwembeyanga zinaendelea kufanya kazi ikiratibu mapambano yatakayofanyika baada ya mfungo huo," alisema Ustaadh Yasin. Aidha, alisema TPBO inawatakia mfungo mwema mabondia na wadau wa ngumi wenye imani na dini ya Kiislam ili waweze kufunga na kumaliza bila matatizo. Mwisho

YANGA KAMA KAWA KAMA DAWA YABEBA TENA KOMBE LA KAGAME

KLABU ya soka ya Yanga jana ilitwaa kwa staili ya aina yake ubingwa wake wa pili mfululizo na wa tano jumla wa Kombe la Kagame, la klabu bingwa ya soka ya Afrika Mashariki na Kati, kwa kuifunga Azam mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Ushindi huo si tu uliiwezesha kwa namna nyingi kulipa kisasi cha kudhalilishwa kwa mabao 3-1 na Azam kulikoandamana na kupigana uwanjani na kufungiwa wachezaji wake katika mchezo wa ligi kuu ya Bara Mei, bali pia ulikuwa wa kikatili. Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza katika dakika ya 44 likiwa la tano kwa mchezaji huyo katika michuano ya mwaka huu, baada ya kunasa pasi ya nyuma ya beki wa pembeni wa Azam Ibrahim Shikanda. Lakini goli ambalo lilinogesha ushindi huo, na ambalo litakuwa liliikata maini vibaya Azam ni la mshambuliaji mpya hatari Said Bahanuzi la dakika ya mwisho ya majeruhi. Zikiwa zimeongezwa dakika tatu za majeruhi, mpira mrefu uliopigwa toka nyuma na beki Kelvin Yondani katika dakika ya 93 ulimkuta Bahanuzi akikabiliana na Said Morad. Akitumia ubavu aliojaaliwa na Mola, pande la mtu Bahanuzi alimzungusha Morad kabla ya kumtoka na kuachia shuti kali lililotinga kwenye nyavu za juu za goli na kumfanya mfungaji-mwenza aliyeongoza kwenye Kombe la Kagame kwa pamoja na Kiiza. Tedy Etekiama wa Vita ya JK Kongo pia alifunga mabao sita lakini CECAFA, shirikisho la soka la ukanda huo, liliwatunuku wauaji hao wa Yanga kutokana na kuipa timu yao ubingwa. Tofauti na mechi zilizotangulia, Azam ambayo ilifika fainali ya Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza ikishiriki mara ya kwanza jana ilijenga mashambulizi yake taratibu kutokana na mpira wake wa pasi fupi fupi za kasi kuikauka. Kocha wa Yanga Tom Sentfiet aliwashukuru wachezaji wake kwa kumudu kucheza kwa "mbinu tulizopanga" na kwamba kufungwa kwao katika mechi ya kwanza kuliisadia kurekebisha makosa yaliyoipa ushindi wa mechi zote tano zilizofuata. Yanga ilikuwa pia bingwa wa Kombe la Kagame katika miaka ya 1975, 1993 na 1999 na mbali na kukata tiketi ya michuano hiyo tena mwakani imebakiza kikombe kimoja kufikia rekodi ya Simba ambayo ndiye bingwa pekee mara sita. Pia iwapo kama mwakani itafanikiwa kutetea taji hilo itakuwa timu ya pili baada ya AFC Leopard ya Kenya iliyowahi kufanya hivyo mfululizo wakati ikitamba katika soka la Afrika.
Katika vurugu za ushindi wa Azam Mei, wachezaji sita wa Yanga walitozwa faini zinazofikia jumla ya sh. milioni nane ambazo sasa zinaweza kulipwa kutoka katika zawadi ya sh. milioni 45 ya bingwa wa Kombe la Kagame. Azam inapata sh. milioni 30 wakati Vita imezawadiwa sh. milioni 15 kwa kushika nafasi ya tatu baada ya kuifunga APR ya Rwanda 2-0 mapema jana. Timu zilikuwa: YANGA: 'Barthez', Oscar Joshua, Stephano Mwasika, 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima, 'Chuji', Rashid Gumbo (Juma Seif dk.74), Hamisi Kiiza, Said Bahanuzi', David Luhende. AZAM: 'Dida', Ibrahim Shikanda (Samir Haji dk.68), Erasto Nyoni, Said Morad, Aggrey Moris, Jabir Aziz, Kipre Tchetche (Mrisho Ngasa dk.68), Salum Abubakar, John Bocco, Ibrahim Mwaipopo, 'Redondo'.

UBALOZI WA UAE WAFUTURISHA WAUMINI DAR

UBALOZI wa Nchi ya Falme za Kiarabu, UAE nchini kupitia taasisi ya kutoa huduma za kijamii ya Khalifa Bin Zaayid Al Nahyaan, umeamua kuwafuturisha waumini wa dini ya kiislam wa Msikiti wa Al Rahman wa Dar es Salaam kwa mwezi mzima wa mfungo wa Ramadhani. Msaada huo wa futari ulianza kutolewa tangu kuanza kwa mfungo wa mwezi huo siku 10 zilizopita na juzi MICHARAZO lilishuhudia ugawaji wake kwa waumini hao ambao imewafanya wapate fursa ya kuwa na uhakika wa kula baada ya funga zao. Imamu wa Msikiti huo wa Al Rahman uliopo eneo la Kinondoni, Sheikh Abdullah Salim Bahssany, akiwahutubia waumini wake wakati wakigawiwa futari hiyo, alisema huo ni msaada toka ubalozi wa UAE na utakuwa ukitolewa hapo kila siku hadi mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapomalizika mwishoni mwa mwezi ujao. Imamu huyo aliwaambia waumini hao kuwa wale waliokuwa na shaka na kupata futari katika funga zao, waondoe hofu kwani sasa watakuwa wakipata chakula hicho, huku akiushukuru ubalozi huo kwa ukarimu iliyouonyesha kwa waumini hao. "Jamani futari mnayokula leo imetolewa na ubalozi wa nchi za Falme za Kiarabu na msaada huu utakuwa ukitolewa kwa mwezi mzima katika mfungo huu wa Ramadhani hivyo msiwe na hofu katika funga zenu,"alisema Sheikh Bahssany. Nao baadhi ya waumini waliofuturishwa msikiti hapo waliushukuru ubalozi huo na kuomba watu wengine wenye uwezo kuiga mfano huo wakidai mwezi huu ndio wa waumini wa kweli kuonyesha upendo, ukarimu na kuhurumiana katika kutekeleza nguzo ya nne kati ya tano za Imani za Kiislam. "Wengine wetu tunafunga lakini hatuna hakika ya kupata futari, lakini kwa hili linalofanywa na ubalozi huu ambao hata mwaka jana walitusaidia tunashukuru na kuomba wengine wawe wanatukumbuka wanyonge kama sisi," alisema muumini mmoja aliyekataa kutajwa jina lake gazetini. Mwisho