STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, June 19, 2012

Waislam wadai hawahitaji upendeleo serikali, ila...!

AMIRI wa Vijana wa Dini ya Kiislam Tanzania, Sheikh Shaaban Mapeyo, amesema malalamiko wanayotoa waumini wa dini hiyo dhidi ya serikali haina maana ya waislam kutaka upendeleo bali kutaka haki na uadilifu utendwe kwa raia wote nchini. Aidha alisisitiza kuwa msimamo wa viongozi wa dini hiyo juu ya Sensa ya mwaka huu ni ule ule wa kuigomea mpaka kipengele cha dini kilichoondolewa kirejeshwe ili kuondoa utata uliopo na kusaidia kujua idadi ya wanadini nchini. Akiwahutubia waumini wa msikiti wa Mwenge, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mapeyo ambye pi ni Imamu Mkuu wa msikiti huo, alisema waislam hawahitaji upendeleo wa aina yoyote, isipokuwa wanapenda kuona haki na uadilifu unatendwa kwa raia wote. Sheikh Mapeyo alisema madai wanayoyatoa kila mara dhidi ya dhuluma na hujuma wanaofanyiwa ni kama njia ya kuikumbusha serikali ifanye shughuli zake kwa uadilifu ikiwatendea haki raia wake wote badala ya kupendelea kundi fulani na kuwapuuza wengine. "Waislam tunapolalamika na kupiga kelele kila mara hatuna maana ya kutaka upendeleo, tunachotaka ni kuona serikali inaendesha shughuli zake za usawa, haki na uadilifu kwa vile taifa hili ni la watanzania wote," alisema. Aliongeza, waislam wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu nchini licha ya kutambua kuna baadhi ya mambo hawatendewi haki, lakini kwa kupuuzwa kwao imewafanya wafikie kikomo na kuitahadharisha serikali iwe makini. "Kwa mfano kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika hujuma tunayofanyiwa katika elimu, ila majuzi imebainika hatulii ovyo baada ya kubainika madudu ya matokeo ya Baraza la Taifa la Mitihani, ambapo wenyewe wamekiri makosa." Alisema ni vema serikali ikazinduka na kuliona tatizo lililopo nchini ni kubwa kuliko wanavyofikiria, huku akisisitiza kuwa bila kuyrejeshwa kwa kipengele cha dini kwenye zoezi la Sensa waislam hawatashiriki. "Huu ni msimamo wetu na tumeanza kuwahimiza waumini wetu kuwa kama kipengele hicho hakirejeshwi basi wasishiriki Sensa na tumeshaiandikia barua serikali juu ya msimamo huo," alisema Sheikh Mapeyo. Alisema serikali iliwaita viongozi wa kidini mjini Dodoma kuzungumzia jambo hilo na kusisitiza hawaterejesha kipengele hicho na wao kuieleza wazi kwamba kama ni hivyo basi wapo radhi wahesabiwe watu wengine na sio waislam. Mwisho

Mcheza filamu wa Marekani kukimbia Mount Kilimanjaro

MCHEZA sinema maarufu duniani kutoka nchini Marekani Deidre Lorenz, anatarajiwa kushiriki mbio za kila mwaka za Mount Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika Jumapili ijayo mjini Moshi. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waratibu wa mbio hizo zilizoanzishwa na Marie France wa mji wa Bethesda, Maryland nchini Marekani mwaka 1991 na zitakazojulikana kama 7 Continental Races, muigizaji huyo wa filamu naye atakimbia katika mbio hizo. Taarifa hiyo iliyotumwa MICHARAZO na Afisa Habari Uhusiano wa mbio hizo, Grace Soka ni kwamba mcheza sinema huyu aliyecheza sinema kama Santorini Blue, Perfect Strangers, The Great Fight, ujio wake utaitangaza Tanzania katika macho ya dunia na kuwavutia watalii. Lorenz aliyewahi kuteuliwa mara tatu kuwania tuzo za Grammy, ataambana na wamarekani wengine na anatarajiwa kutua nchini Juni 21. Mbio hizo za Mount Kilimanajaro zitawashirikisha wakimbiaji wengine wa kimataifa pamoja na wa nyumbani na zitakuwa za umbali wa Kilomita 42 na washindi wake wakiwemo watoto watazawadiwa zawadi mbalimbali. Pia mbizo zitahusisha mbio za umabli wa kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5 kwa watoto na kwamba washiriki wake hawahitaji ujuzi wa kukimbia bali mradi mtu anayeweza kufanya hivyo. Deidre Lorenz alizaliwa katika jiji la Oregon nchini Marekani lakini alihamia katika jiji la New York City linalijulikana kama "The Big Apple" nchini Marekani akiwa na kampuni yake ya kutengeneza sinema inayoitwa Thira Films LLS. Lorenz alipatikana kushiriki mbio hizo katika bahati nasibu iliyochezwa wakati wa mbio za New York Marathon za mwaka jana.

Coastal Union yanasa vifaa vipya yumo Atupele

KLABU ya soka ya Coastal Union ya Tanga, imetangaza kuwanyakua wachezaji kadhaa wapya akiwemo kipa wa zamani wa Yanga na Azam, Jackson Chove. Afisa Habari wa Coastal, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO, Chove ni miongoni mwa makipa wawili wapya iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kumwembe alimtaja kipa mwingine iliyomnyakua ni Juma Mpongo aliyekuwa akiidakia Kiyovu Sports ya Rwanda. Afisa Habari huyo aliwataja wachezaji wengine iliyowanasa mpaka sasa kuwa ni mshambuliaji Nsa Job toka Villa Squad, mlinzi wa kushoto wa JKT Oljoro, Othman Omary, Atupele Green aliyekuwa Yanga na nyota wa timu ya taifa ya U20. Kumwembe aliwatraja wachezaji wengine kuwa ni Soud Mohamed kutoka Toto Afrika, Seleman Kassim 'Selembi' na Raraq Khalfan waliokuwa African Lyon. "Hao ni baadhi ya wachezaji tuliowanyakua na tunaendelea na usajili wetu kwa ajili ya kuziba nafasi za wachezaji tisa tuliowatema katika kikosi cha msimu uliopita," alisema Kumwembe. Aliongeza kuwa, mbali na wachezaji hao pia timu yao imeshamalizana na kocha wao wa zamani Rashid Shedu kutoka Kenya ambaye amechukua nafasi ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' waliyeachana nae mara baada ya kuiwesha Coastal kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tano. "Pia tumeimarisha benchi letu la ufundi kwa kumnyakua Rashid Shedu kuziba nafasi ya Julio tuliyeachana nae," alisema. Kumwembe alisema pia kwa sasa wanafanya mazungumzo na kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo ili zweze kuichezea timu yao kwa msimu ujao. Mwisho